Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Justin Lazaro Nyamoga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilolo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote ninachukua fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia uzima, afya njema na kuendelea kuwepo katika Bunge lako hili. Miaka hii mitano siyo michache na Mungu ametupa uzima tuko hapa ni kwa neema yake na hatuna budi kumshukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninaomba nichukue fursa hii kumshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri na kubwa sana anayoifanya kwa Jimbo letu la Kilolo. Nimetumwa na wananchi wa Kilolo kutoa shukrani zangu za dhati hasa kwa kipindi hiki ambacho Mheshimiwa Rais amekuwepo madarakani. Mambo mengi makubwa yamefanyika ambayo kwa kweli wananchi wanayaona na wanashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta mbalimbali zimepata mambo na miradi mbalimbali ambayo tulikuwa tumeiomba hasa kwenye maeneo ya miundombinu na barabara. Kilolo ilikuwa haijawahi kuunganishwa na barabara kuu lakini sasa imejengwa, barabara ya kilometa 33 inaendelea kukamilishwa kutoka Ipogolo hadi Kilolo, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara ya kwanza niliposimama hapa kuuliza swali langu la kwanza mwaka 2021 lilikuwa ni lini Kiwanda cha Chai Kidabaga kitajengwa? Ninachukua fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe pamoja na Wizara yake, wameweza kufanikisha ujenzi wa Kiwanda cha Chai Kidabaga na ujenzi huo unaendelea kukamika, ninawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo mengi yaliyofanyika katika Sekta ya Afya, Sekta ya Elimu, ujenzi wa shule za sekondari, vyuo vya ufundi na mambo mengi makubwa yaliyofanyika, kwetu wananchi wa Kilolo kwa sasa kwa kweli ni shukrani na kumuahidi Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwamba hatutamwagusha, wananchi wa Kilolo tumejipanga kwa ajili ya kumpa kura za kishindo kwa kazi kubwa sana aliyoifanya ambayo Wanakilolo wote wanaona. Hali tuliyoikuta na ilivyo sasa siyo sawa na haya yote ni kwa sababu Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya mambo mengi makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi hiki, tumepata fursa ya kuwepo kwenye Kamati mbalimbali, nami nimekuwepo kwenye Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na nimejifunza mambo mengi. Ninachukua fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mohamed Mchengerwa pamoja Naibu Mawaziri, Mheshimiwa Dkt. Festo Dugange na Mheshimiwa Zainab Katimba pia Katibu Mkuu Ndugu Adolf Ndunguru na wengine wote ambao tumefanya nao kazi vizuri sana katika kipindi hiki chote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo makubwa na mapinduzi makubwa niliyoyaona kwenye Wizara hii ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa katika kipindi hicho, pia yapo yatakayoacha alama ambayo haitafutika katika kipindi chote ikiwemo uanzishwaji wa Samia Infrastructure Bond ambayo lengo lake kwa kweli ni kupata fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya barabara. Jambo hili ni jambo kubwa kwa sababu linaenda kuleta ukombozi kwa watu wote ambao ni wakandarasi na walikuwa wanapata shida ya kupata mitaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachukua fursa hii kuipongeza sana CRDB Bank, TARURA, Engineer Seff na wenzake kwa ubunifu huu mkubwa walioufanya ambao pia umefanya Kamati ambayo mimi nimekuwa nikihudumu, kuweka alama ambayo haitafutika kwa sababu wale wakandarasi kila watakapokuwa wanapata fedha hizi watakumbuka kazi kubwa iliyofanywa na Kamati na Bunge hili katika uanzishwaji wa Samia Infrastructure Bond. Hili ni jambo kubwa ambalo nina hakika linapaswa kukumbukwa kwa kazi kubwa iliyofanywa na Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wito wangu kwa wakandarasi wazawa, wanapopata mitaji hii kuitumia vizuri hasa katika ujenzi wa miundombinu ya barabara ili ziweze kujengwa kwa kiwango ambacho kitafanya barabara hizi ziendelee kuwepo kwa kipindi cha muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge huwa tukiongea hapa, tunauliza maswali na kuzungumza, lakini nami nimepata uzoefu mkubwa sana wa kufahamu jinsi gani Wakurugenzi wetu katika halmashauri mbalimbali wanafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakurugenzi wetu katika Halmashauri mbalimbali wanafanya kazi kubwa sana katika kuhakikisha kwamba utekelezaji wa bajeti unafanikiwa. Kwa kweli katika kipindi hiki, tunayo haki ya kuwapongeza na kuwashukuru Wakurugenzi kwa kazi kubwa sana wanayoifanya ambayo pengine tukiwa huku Bungeni hatuioni lakini kule wanakofanya wanafanya kazi kubwa sana, wakiwemo pia watendaji wote katika halmashauri zetu mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ninachukua fursa hii pia kumshukuru Mkurugenzi wangu wa Jimbo la Kilolo ambaye anafanya kazi kubwa sana, si yeye tu ni pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri, Mkuu wa Wilaya na viongozi wengine wote kwa sababu wamefanya kazi kubwa sana katika kipindi hiki ambacho tumekuwepo hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo kubwa ambalo limekuwa ni changamoto kwenye Jimbo langu na ambalo nimelizungumzia mara nyingi lakini ambalo ufumbuzi wake umeenda kwa kiwango kikubwa sana, ni suala zima la miundombinu ya barabara. Jambo hili limetekelezwa kwa kiwango kikubwa kama nilivyosema, baadhi ya barabara ambazo zilikuwa ni kero zimeshughulikiwa. Kwa mfano, barabara kutoka Ipogolo kwenda Kilolo ambayo tayari ipo kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi hiki piatumepata zaidi ya kilometa 27 za lami kwenye maeneo ya vijijini kabisa ambazo zimejengwa na TARURA. Barabara ya kutoka Kidabaga kwenda Boma la Ng’ombe na sasa hivi kuna kilometa saba zinajengwa kwenda Mwatasi, ambapo lengo lake ni kuunganisha na Kibaoni pale Kilolo. Hii ni barabara ambayo ni kero kwa muda mrefu, lakini Serikali imeiona na imeifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haina faida nikitaja orodha ya barabara nyingi wakati ninafahamu bajeti yetu, lakini nina haki ya kushukuru kiwango cha kilometa 27 ambazo tumeshapewa huku nikifahamu kwamba Barabara ya kutoka Ilula kwenda Image hadi Ibumu ina fedha za Benki ya Dunia kwa ajili ya ujenzi wa kilometa 28 hadi Ibumu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni mafanikio makubwa ombi langu ni kwamba, ujenzi wa barabara ya kutoka Ilula kwenda Image ufanyike kwa haraka kwa sababu fedha zipo tayari na ninaishukuru sana Serikali kwa kutenga fedha hizo. Pia, kama barabara hiyo itajengwa, basi kwa kweli hayo ni mapinduzi makubwa sana katika kipindi hiki ambacho nimekuwepo hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, tumejenga vitu vingi vya afya ambavyo ninaweza kuviorodhesha, lakini kwa sababu ya maslahi ya muda sitaviorodhesha lakini vile ambavyo bado havijakamilika, nina uhakika Serikali ipo katika kuandaa taratibu za kuvikamilisha kwa ajili ya kutenga fedha. Hapa ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kutoa fedha kiasi cha shilingi milioni 600 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Ukumbi ambacho kilikuwa kimekwama kwa muda mrefu. Ninakushukuru sana Mheshimiwa Dkt. Dugange ambaye tulifanya ziara pamoja katika Kata ile, wananchi wa eneo lile wanashukuru sana na kwa kweli fedha zile zimefika, tumeshazipokea, taratibu za manunuzi zinafanyika ili ujenzi ule uweze kuanza na kura za eneo lile za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na za kwangu mimi mwenyewe ziko salama kabisa pamoja na Jimbo zima la Kilolo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapoelekea kuhitimisha mchango wangu, ninachukua fursa hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote ambao tumekuwa tukishirikiana hasa kwenye Wizara hii ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ambayo nilipata fursa ya kuhudumu kama Mwenyekiti. Baadhi yao wamekuwa na shaka kuhusu Jimbo la Kilolo, ninapenda tu kutoa kauli hii kwamba, hizi nafasi zote tulizonazo ni kudra na neema ya Mwenyezi Mungu na analolipanga Mungu mwanadamu hawezi kulipangua. Kwa hiyo, sisi sote tuendelee kuombeana dua ili iwe ridhaa ya Mwenyezi Mungu, kama itampendeza Mwenyezi Mungu tupate kurejea salama na tuendelee kutumikia wananchi ambao wana imani kubwa sana na sisi sote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja na ninaendelea kuwahakikishia Watanzania kwamba Kilolo ipo salama, kura za Mheshimiwa Dkt. Samia ziko salama, kura za Madiwani ziko salama na kura zangu mimi mwenyewe ziko salama pia. Ahsanteni sana kwa kunisikiliza. (Makofi)