Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kupata nafasi ili niweze kutoa mchango wangu. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunafahamu kwamba kwa sasa Taifa letu tupo kwenye maandalizi ya kuelekea kwenye uchaguzi mkuu, sote tunafahamu kwamba zinapofika nyakati kama hizi huwa kunakuwa na vuguvugu nyingi sana za kuanza kudai Katiba mpya, pia kwa miaka mingi iliyopita tumeshuhudia mabadiliko mbalimbali yakifanyika juu ya kufanya marekebisho ya Katiba mpya. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na Katiba ya Uhuru ya mwaka 1961, tulikuwa na Katiba ya Jamhuri ya mwaka 1962, tulikuwa na Katiba ya Muungano ya mwaka 1964, tulikuwa na Katiba ya muda ya mwaka 1965, vilevile tulikuwa na Katiba ya kudumu ya mwaka 1977, Katiba ambayo tunaitumia mpaka sasa lakini ni Katiba ambayo imeendelea kufanyiwa amendments za kutosha ikiwemo amendment ambayo imefanyika mwaka 1992 ya kuruhusu mfumo wa vyama vingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi mpaka sasa Katiba yetu tunayoitumia imeshafanyiwa mabadiliko mara 14. Tafsiri yake ni nini?  Tafsiri yake ni kwamba, Serikali ya Chama Cha Mapinduzi ambayo ndiyo inayoongoza Nchi yetu ya Tanzania tangu tupate uhuru, hata siku moja haijawahi kuogopa kufanya mabadiliko ya Katiba kwa madai ya kwamba, itaenda kushindwa kwenye uchaguzi kama ambavyo wenzetu, akiwepo Mheshimiwa Tundu Lissu, walikuwa wakidai. Kwamba, Serikali ya Chama Cha Mapinduzi ni waoga wa kufanya mabadiliko kwenye Katiba kwa sababu, watashindwa uchaguzi. Jambo hilo siyo kweli na limedhihirisha namna ambavyo mara kwa mara Serikali imekuwa ikifanya mabadiliko katika Katiba yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nitumie nafasi hii kidogo niweze kuwakumbusha ndugu zetu ambao wanadai kwamba, no Reform, no Election.  Mwaka 2012 katika Serikali ya Awamu ya Nne, Rais wetu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete aliweza kuwasikiliza madai yao na akaasisi mchakato wa kuanzisha Marekebisho ya Katiba Mpya. Rais alianza kwanza kwa kuteua tume na Mwenyekiti wa Tume alikuwa Jaji Warioba na Wajumbe wengine walikuwa ni mzee wetu Butiku, Dkt. Salim, pamoja na mzee wangu Profesa Baregu, ambaye kwa sasa hivi pia, ni marehemu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tume hiyo ilipoteuliwa mtu wa kwanza kuja kuipinga, tume iliyoteuliwa na Mheshimiwa Rais, alikuwa ni Tundu Lissu, ambaye alisimama hadharani akasema kwamba, Wajumbe walioteuliwa na Mheshimiwa Rais wote ni CCM, hivyo moja kwa moja Watanzania wasitegemee kwamba, watapata Katiba Mpya.  Hawa wenzetu wakaenda mbali zaidi, wakamtaka Profesa Baregu, ambaye alikuwa ni Mwanachama wa CHADEMA na Mjumbe wa Kamati Kuu aweze kujitoa kwenye huo mchakato, lakini Profesa Baregu alisimama akasema kwamba, nikiambiwa nichague chama changu na Taifa langu, mimi nitachagua nchi yangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi kwamba, kwa CHADEMA tuliyonayo sasa hivi ni ngumu sana kuweza kumpata mtu kama Profesa Baregu, ambaye alijua kabisa ni wakati gani wa kuchagua maslahi ya chama na ni wakati gani wa kusimama na maslahi ya nchi. Hiyo ni mifano midogo ya kuonesha kwamba, ni namna gani ambavyo Serikali ya Chama Cha Mapinduzi imekuwa na dhamira ya dhati ya kuhakikisha inaleta Katiba mpya, kama ambavyo Watanzania na watu wa upinzani wamekuwa wakidai. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunafahamu baada ya hapo mchakato uliendelea, lakini Rais aliteua Bunge dogo la Katiba. Bunge lile lilipoteuliwa kazi ilianza humu Bungeni, katikati ya mchakato wale ndugu zetu walisusia huo mchakato, wakatoka nje na wakakataa kuendelea kujenga Katiba ya Nchi yetu, lakini leo wanakuja na Sera kwamba, no Reform, no Election, ni jambo ambalo linafikirisha kwamba, ni reform zipi ambazo wao wanazitaka? Wakati tayari walishagomea mchakato wa kuandaa Katiba Mpya ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwaombe tu Watanzania kwamba, hawa watu ni kawaida yao. Sasa hivi wamekuja na Sera kwamba, no Reform, no Election, lakini ukiangalia hakuna jipya ambalo wanalidai, ambalo halikuwepo kwenye ile Tume ya Jaji Warioba. Ndiyo maana hata baadaye walikuja kusema kwamba, tunaomba mapendekezo yale ambayo yalikuwepo kwenye Tume ya Jaji Warioba yaweze kuzingatiwa na Serikali, wakasahau kabisa kwamba, mwanzoni walisema ile tume ni Tume ya CCM na haiwezi kufanya kazi yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Wizara ya TAMISEMI, tunajua kwamba, tunaenda kwenye uchaguzi na kipindi kama hiki huwa kinakuwa na mavuguvugu mengi sana. Kwa hiyo, niwaombe mwendelee kusimama mfahamu kwamba, nchi yetu inategemea Chama Cha Mapinduzi na wale wenzetu hawana dhamira ya dhati ya kujenga nchi yetu, wao ni watu ambao wamekuwa na siasa za kuleta matukio mara kwa mara. Ndiyo maana wanafahamu kwamba, endapo Katiba Mpya ikipita wao watakosa ajenda ya kusema. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, niwaombe kuendelea kusimama kuhakikisha tunafanya uchaguzi, lakini hata wao ambao wamesema kwamba, hawatashiriki kwenye uchaguzi kwa sababu, ni watu ambao wana siasa za ndumila kuwili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata wakisema kwamba, wanataka kushiriki, niiombe Wizara ya TAMISEMI iweze kuwaruhusu kufanya uchaguzi kwa sababu, sisi kama Chama Cha Mapinduzi, wala hatuwaogopi. Sasa hivi CHADEMA hawana ajenda, wala hawana jambo ambalo, sisi Chama Cha Mapinduzi, tunawaogopa. Wakishiriki tutashinda, wasiposhiriki tutashinda kwa sababu, Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi nzuri katika nchi yetu, ambayo Watanzania wameiona.  (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ilipofika mwaka 2022, tunafahamu Rais wetu alipounda kikosi kazi maalum, kwa ajili ya kuweza kufanya marekebisho ya sheria, lakini kwenye kile kikosi kazi wao waligoma kwenda kushiriki. Baada ya hapo wakaanza kukosoa tena kwamba, kulikuwa hakuna haja ya Mheshimiwa Rais kuunda kikosi kazi kwa sababu, kuna yale maoni ambayo yalitolewa na Jaji Warioba wakasahau kwamba, walishaiponda hiyo Tume ya Jaji Warioba. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakaendelea mbele wakasema kwamba, wanahitaji kujua fedha ambazo zimetumika kwenye kuandaa hicho kikosi kazi. Wakasahau kwamba, walishalitia hasara Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kugomea mchakato wa kuanzisha Katiba mpya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe wote kwa pamoja tushikamane na tufahamu kwamba, hawa watu ni ndumila kuwili. Walianza kwa kusema kwamba, Uchaguzi wa 2022 hawautambui, lakini kadri siku zinavyoenda wakazunguka, wakaenda kuomba Serikali iweze kuwapa ruzuku. Tafsiri yake ni nini? 
Mheshimiwa Mwenyekiti, tafsiri yake ni kwamba, yale matunda na mazao ambayo yanatokana na Uchaguzi Mkuu, kwa maana ya Madiwani, Wabunge, pamoja na ruzuku, wao wakasema kwamba, wanatambua zile ruzuku, lakini Wabunge walioko huku ndani ambao pia, ni zao la uchaguzi wakasema kwamba, hawawatambui.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa watu ni ndumila kuwili na tumeshuhudia wakiendelea kuwaita hawa Wabunge majina mbalimbali wakasahau kwamba, kama wanatambua mazao ya uchaguzi, ilibidi watambue ruzuku, lakini vilevile waweze kuwatambua na Wabunge ambao wako ndani. Tunawafahamu vizuri, wamekuwa na utaratibu wa kuwasifia marais wakishatoka madarakani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tunafahamu hakuna Rais ambaye alitukanwa kama Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, lakini ilivyofika Serikali ya Awamu ya Tano, ndiye mtu ambaye walimsifia na wakampongeza sana. Ilivyoingia Serikali ya Awamu ya Tano alitukanwa, kudhalilishwa na kuitwa majina mbalimbali, lakini ilivyoingia Serikali ya Awamu ya Sita, walianza kwa kumsifia mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, baadaye walivyogundua kwamba, kuendelea kusifia kazi za Mheshimiwa Rais kutaendelea kuwapotezea malengo yao ya kisiasa wakamgeuka na kuanza kumsema vibaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimtie moyo Mheshimiwa Rais kwamba, aendelee kuchapa kazi. Watanzania tumeona kazi yake na tunamuahidi kwamba, kwenye uchaguzi ujao Chama Cha Mapinduzi kitashinda kwa kishindo, kama ambavyo tumeshinda katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ambayo Rais amefanya katika nchi yetu ni kubwa sana. Nikizungumzia tu kwenye Mkoa wangu wa Songwe, ndani ya miaka minne ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, tumepata hospitali ya mkoa, tumepata hospitali tatu za wilaya. Tulikuwa na kilio cha mradi mkubwa wa maji, sasa hivi tumepata mradi mkubwa wa maji, haya ni matunda makubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita. Kwa hiyo, Watanzania wanathamini na kuona kazi ambayo Mheshimiwa Rais wetu amefanya. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Wanasongwe tunasema kwamba, tuko pamoja naye, tutatembea kifua mbele, wala, asiogope, yeye achape kazi. Hawa ambao wanasema kwamba, no Reform, no Election, ngoja tuwaache waendelee kutaka hizo reforms ambazo tayari Serikali ilishazifanya na wao ndiyo wakawa wakwamishaji wa kwanza, lakini wanasema kwamba, Serikali ya Chama Cha Mapinduzi inaogopa mabadiliko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninaomba niwatie moyo, Mheshimiwa Waziri, endeleeni kufanya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu, lakini mkijua kwamba, Chama Cha Mapinduzi kitaenda kushinda kwa kishindo. Nakushukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)