Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Korogwe Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kutoa mchango wangu kwenye hii Wizara muhimu kwa maisha ya wananchi wa Taifa letu. Nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, ambaye kwa neema na kudra yake ametujalia na ametuwezesha kuwa salama na kuwa kwenye hii nyumba tukiendelea kuifanya kazi waliyotukabidhi Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia mchango wangu niendelee kuungana na wenzangu wote kumpongeza kwa dhati kabisa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya kwenye Taifa letu, anayowafanyia Watanzania. Sitapoteza muda mwingi kwenye hilo eneo kwa sababu, Tarehe 24 Februari, 2025, Mheshimiwa Rais alifanya ziara Mkoa wa Tanga na tarehe hiyo alikuwa kwenye Wilaya ya Korogwe. (Makofi) 
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ule uwanja uliojaa maelfu ya Wanakorogwe tulikubaliana kwamba, kwa kazi kubwa na kazi nzuri aliyoifanya Mheshimiwa Rais, hatuna kujiuliza, hakuna kupepesa, ndiye Rais wetu anayestahili kupewa kura nyingi za ushindi mwezi Oktoba katika uchaguzi. Kwenye ule mkutano Wanakorogwe tulikubaliana, tukawaambia Watanzania wote kwamba, sisi Korogwe tunajua hii hadithi ya no Reform, no Election ni hadithi ya kusadikika isiyokuwa na uhalisia na isiyotekelezeka. Tunajua uchaguzi upo, Mgombea wetu ni Dkt. Samia na Rais wetu ni Dkt. Samia, tunaendelea kusonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kumpongeza Mheshimiwa Rais, nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI pamoja na Manaibu Waziri wake wote wawili. Kwa kweli, hii timu ya TAMISEMI imetimia, imefanya kazi nzuri, inawahudumia ipasavyo Watanzania.  Tunashukuru sana kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya, tunaendelea kuwatia moyo waifanye hiyo kazi, Mheshimiwa Waziri, Waheshimiwa Manaibu Waziri na timu yake nzima kule Wizarani, kuanzia Katibu Mkuu, Manaibu Katibu Mkuu, Wakurugenzi mpaka na Wakuu wa Taasisi ambazo ziko chini ya Wizara yako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mchango kwenye maeneo machache. Eneo la kwanza ni upande wa TARURA; kwanza nikubali, nikiri na kutambua kazi kubwa na nzuri inayofanywa na TARURA kwenye kurekebisha na kujenga barabara kwenye maeneo yetu. Kwa kweli, TARURA inastahili pongezi, inafanya kazi nzuri sana, sisi kama Wabunge, lakini kama Watanzania, tunaridhishwa sana na kazi inayofanywa na TARURA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ushauri kwenye maeneo machache. Eneo la kwanza ni, ukiangalia bajeti ya TARURA mwaka huu, iliyoletwa na Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake, haina tofauti sana na bajeti tunayoitekeleza kwenye mwaka ambao unaelekea mwishoni, karibu shilingi bilioni 850. Sasa ukiangalia changamoto za barabara tulizokuwa nazo, fedha hii kutokuongezeka siyo jambo zuri sana, lakini hainipi shida sana kutokuongezeka kwa bajeti mwaka huu kwa sababu, ninajua kuna fedha ambayo ilitengwa kwenye supplementary budget zaidi ya shilingi bilioni 350. Pamoja na bajeti ya TARURA kubaki kama ilivyokuwa kwenye mwaka wa fedha unaokwisha hela iliyotengwa kwenye supplementary budget, shilingi bilioni 350 ikipatikana, hakika itakwenda kuisaidia TARURA kufanya kazi zake vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuombe sana Serikali ituelewe, hatuna shida na TARURA, hatuna shida na utendaji kazi wao, wanafanya kazi nzuri. Tunaiomba Wizara ya Fedha wapelekeeni fedha TAMISEMI, wapelekeeni fedha TARURA, ili waweze kutatua changamoto tulizokuwanazo. Yako maeneo Wakandarasi wameanza ujenzi, lakini wamesimama kwa sababu, walikuwa hawajalipwa fedha zao. Fedha hii ikienda tunaamini changamoto nyingi zitatatuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kwenye eneo la TARURA tumeshuhudia kazi nzuri inayofanywa na TARURA kwenye kuboresha miji yetu kupitia miradi mbalimbali ya kimkakati ambayo ilipata ufadhili kutokana na harakati na jitihada za Serikali yetu kutafuta fedha, kwa ajili ya kuboresha miji yetu. Tunaitambua kazi hiyo, tunaithamini na tunaiunga mkono, lakini tuombe kutoa wito, pamoja na kazi nzuri inayofanyika kwenye maeneo ya mamlaka za miji tunahitaji kuwa na miradi mingine ya kimkakati, kama tunavyofanya kwenye mamlaka za miji kwenye maeneo ya vijijini, ambayo kwa sehemu kubwa maeneo haya ya vijijini ndiyo yanayofanya kazi kubwa ya uzalishaji. Wananchi wetu wanahitaji sana miundombinu ya barabara iendelee kuboreshwa, iendelee kufanya kazi nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ni maboma ya zahanati na madarasa. Tulikuwa na sera hii kwamba, wananchi wakiibua na wakianza ujenzi wa maboma ya zahanati na madarasa Serikali inakuja kuwaunga mkono kukamilisha kazi iliyofanyika. Kwa kweli, tuipongeze Serikali kwa kipindi cha miaka hii minne/mitano, tumefanya kazi kubwa sana na Serikali imeleta fedha nyingi kuunga mkono juhudi za wananchi ambao wameanza ujenzi wa maboma ya zahanati na madarasa. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia kwenye hii bajeti, hatujaweka fedha nyingi zaidi kwenye eneo la maboma ya madarasa pamoja na zahanati, lakini Mheshimiwa Waziri ninatambua, hii hainipi shida kama ilivyokuwa kwa TARURA. Kwenye supplementary budget kuna fedha nyingi iliwekwa, kwa ajili ya kwenda kupeleka kwenye maboma ya zahanati na madarasa. Tuwaombe Wizara ya Fedha kama bado hawajapeleka hizi fedha TAMISEMI, hizi fedha ziende zikatusaidie kutatua changamoto hii, zikatusaidie kuunga mkono jitihada hizi za wananchi, tuendelee kuwapa moyo wananchi na mambo yaendelee kuwa mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Korogwe nina maboma ya zahanati zaidi ya 28 ambayo wananchi wamejenga kwa nguvu zao, mengine mpaka imefika hatua wameshapaua. Tunasubiri Serikali ituletee fedha, kwa ajili ya kuunga mkono hizi jitihada za wananchi, tutatue changamoto, lakini wananchi waweze kupata huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine, tumeimba sana kwa muda wa miaka miwili au mitatu kuhusu vituo vya afya vya kimkakati. Mheshimiwa Waziri tuna imani kubwa sana na wewe na tunajua leo unahitimisha hoja yako, tunatamani unapokuja kuhitimisha tupate majibu fedha, kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya vya kimkakati, lini zitafika kwenye maeneo yetu, kwa ajili ya kufanya kazi iliyokusudiwa? Wananchi wa Korogwe, maeneo ya Vugiri na Mashewa, tuliwaahidi muda mrefu, tunasubiri fedha, tunaomba Mheshimiwa Waziri utuambie hizi fedha zinakuja lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni ugawaji wa maeneo mapya ya kiutawala. Siku chache zilizopita tumesikia Tume ya Taifa ya Uchaguzi imetoa tangazo la kugawa, kubadilisha na kuboresha majina ya majimbo. Tangazo hili au jukumu hili Tume inalifanya kwa mujibu wa Katiba, Ibara ya 75. Ukisoma Ibara ya 75(4) inaipa tume mamlaka ya kufanya mabadiliko na kugawa majimbo mara kwa mara kadiri itakavyoona inafaa, lakini Katiba inasema angalau kila baada ya miaka 10. Nikatafakari, kwa nini kila baada ya miaka 10?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jibu jepesi ni kwamba, miaka 10 ni muda wa kutosha kutafakari upya kwa sababu, ni muda ambao tunaamini jamii zetu zitakuwa zimepata maendeleo na zimepiga hatua kubwa. Ombi langu kwa upande wa TAMISEMI, muda mrefu tumekuwa tukizungumza kuhusu maeneo mapya ya utawala, tumeusikia msimamo wa Mheshimiwa Rais kwamba, tunaboresha maeneo ambayo tayari tumeshayaanzisha. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri, kipindi hiki ambacho wenzetu tume wanakwenda kugawa majimbo mapya na ninyi mkatafakari kuongeza maeneo mapya ya utawala. Ninajua kuna gharama kubwa, hasa kuongeza mikoa, kuongeza wilaya na kuongeza halmashauri, huko sipataki sana, tuna maeneo ya vijiji; Mheshimiwa Waziri tumepeleka madaraka kule chini kwa wananchi, yapo mambo mengi ambayo wananchi wanayafanya wenyewe kwenye vijiji vyao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yako maeneo ambayo tangu tulipogawa vijiji miaka 10, 15 iliyopita yamekuwa makubwa yanahitaji kupata vijiji vipya. Kule Korogwe sisi tuna maeneo zaidi ya sita ambayo ni maeneo ya sehemu ya vijiji vilivyopo, lakini wamejenga shule zao, zimesajiliwa, watoto wanasoma. Maeneo yana zahanati, lakini hawana kijiji, kumekuwa na mivutano ya kufanya shughuli za maendeleo kati ya hilo eneo na eneo la makao makuu ya kijiji. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Korogwe, Kijiji cha Mwenga, eneo la Kwaluma, wana mpaka shule yao, wanajiendesha wenyewe, wanafanya shughuli zao, kwa nini tusiwape Kijiji? Ukienda eneo la Mkameni wana shule na zahanati yao, maisha yanaendelea, lakini kwa nini hatutaki kuwapa Kijiji? 
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda sehemu inaitwa Magoma, Kijiji cha Makangara, eneo la Songea, ukienda sehemu ya Kalalani, eneo la Kigwasi, haya maeneo yote yamekuwa makubwa. Wananchi wameweka miundombinu yao, wana shule zao na zahanati zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tafsiri yake ni kwamba, hata ukiwapa Kijiji, gharama zitakazoongezeka haziwezi kuwa kubwa kwa kiasi ambacho tunakiogopa, kama nchi. Tunaiomba Serikali, ni wakati sasa, zaidi ya miaka 10 hatujafanya kazi hii tukaifanye ili mambo yawe mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la mwisho nililokuwa ninataka kuchangia siku ya leo ni eneo la Sera yetu ya Ugatuaji wa Madaraka. Tulikubaliana, kama nchi, kuingia kwenye Sera ya Ugatuajia wa Madaraka (Decentralization by Devolution (D by D). Sera hii ilikuwa inalenga kwenye maeneo makubwa manne; tulikuwa na eneo la Political Decentralization, Administrative Decentralization, Physical Decentralization na Central and Local Relations.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ubora wa hii sera, imekumbana na changamoto kwamba, sera hii haijajengwa kwenye mfumo wa kisheria. TAMISEMI walituahidi kwamba, mnafanya maboresho na mapitio ya hii sera na tarehe 3 Aprili, 2023 Waziri wa Nchi, TAMISEMI, akimkaribisha Waziri Mkuu kwenye Mkutano wa Kumi na Tatu wa Mamlaka za Serikali za Mitaa alisema, hii sera iko kwenye hatua za mwisho. Mheshimiwa Waziri anavyokuja kuhitimisha ninatamani kujua, atuambie Sera mpya ya Ugatuaji wa Madaraka imefikia wapi? Kwa nini ninauliza? 
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, maisha yamesonga, maboresho yamekuwa makubwa, maendeleo yamekuwa makubwa... (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mnzava.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika moja nimalizie.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mnzava, muda wako umekwisha. Ninakuongezea dakika moja ya kumalizia, tafadhali.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Maboresho yamekuwa makubwa na ndiyo maana tumeleta TARURA, inafanya kazi nzuri. Kumeibuka RUWASA, lakini leo Watumishi wa Ardhi wamekwenda Wizarani, kuna wakati ilikuja move ya Watumishi wa Kilimo na Watumishi wengine. Mheshimiwa Waziri, lakini kwa nini haya yanatokea?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu, bado hatujaweka clear Sera yetu ya Ugatuzi wa Madaraka. Tusipoangalia tunapokwenda tutarudi nyuma badala ya kwenda mbele. Ninatamani TAMISEMI wailete hii sera, lakini ninatamani wawe na wivu na ugatuaji wa madaraka kwa sababu, ndiyo wana jukumu la kusimamia na kuzilea hizi halmashauri. Tutoe miongozo, tuone ni namna gani ya kufanya kazi pamoja kati ya Wizara moja na nyingine na sekta moja na nyingine, bila kuathiri madaraka ya wananchi ambayo tumeyashusha kule chini, ili kuwaongezea nguvu wananchi kwenye kupanga na kuamua mambo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninakushukuru sana na ninaunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri. (Makofi)