Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sengerema
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. TABASAM M. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Sengerema. Leo nimekuja vizuri kidogo kwa maana hata taa za kijani barabarani zinaruhusu gari kupita. Kwa hiyo, leo Mheshimiwa Mchengerwa usiwe na hofu, niko vizuri sana, yaani leo hapa, ninakuja kupongeza, kushukuru na kushauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Rais katika uteuzi na mabadiliko aliyoyafanya ndani ya Serikali za Mitaa. Serikali za Mitaa ni sehemu imebeba maslahi ya wananchi na huduma za kijamii kwa wananchi wa hii Nchi ya Tanzania, likiwemo Jimbo la Sengerema. Sengerema tulikuwa tuna magumu mengi sana, tulikuwa tuna matatizo ya shule za sekondari, tuna matatizo ya shule za msingi, tuna matatizo ya barabara, hali haikuwa nzuri na pia, huduma za afya, tulikuwa tuna matatizo makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini huu muda wa miaka minne Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa sana kuhakikisha huduma za kijamii katika nchi hii zinaboreshwa kwa kiwango kikubwa sana; na hili linatutolea hofu kabisa sisi Waheshimiwa Wabunge. Hakuna Mheshimiwa Mbunge atakayekuwa na shaka jimboni kwake kwanini asirudi, labda kama ana hali mbali, damu imechafuka tu, lakini vinginevyo kama damu ipo vizuri Waheshimiwa Wabunge wote mnarudi humu ndani. Hapa sasa hivi ni kumwomba Mungu tu kuwa salama basi kura zifike. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yanayozungumzwa sijui namna gani, watu wanaangalia mifumo yote imebana. Ukipiga kelele kwamba barabara hazipo barabara zipo vijijini, ukipiga kelele kwamba kulikuwa hakuna huduma za afya huduma za afya zipo vijijini, ukizungumza habari za shule shule zipo vijijini zimejengwa za kutosha, sasa utakwenda kupumulia wapi. Lazima utafute njia nyingine tu mbadala ya kuanzisha sokosoko yaani hizi sokosoko hazikosekani hizi sekeseke hizi, tumeshazizoea lakini, kwa wanasiasa ndiyo moja ya kazi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kumweka pale kiraka. Katika hili Baraza la Mawaziri kuna mtu anaitwa kiraka hapa, anaitwa Mheshimiwa Mchengerwa. Hiki ni kiraka, yaani ni mchezaji kiraka uwanjani. Mheshimiwa Mchengerwa kazi aliyoifanya kwenye Jimbo la Sengerema bwana mimi ninampongeza sana leo, kabisa kutoka moyoni. Amekuja kama Mheshimiwa Waziri wa Nchi kule tulikuwa tuna matataizo makubwa ya TASAF. Tumezunguka naye vijijini na ameangalia hali ilivyokuwa. Wananchi hawakujua yeye ni nani amekuja kule. Walikuwa wanakuja kudai fedha za TASAF na wakati huo huo wakawa wanamwomba shule na vituo vya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake Mungu akampeleka tena kwenye Wizara nyingine tena, Wizara ya Michezo. Kule nako tena wakamwomba uwanja wa mpira na Sengerema tumemaliza uwanja wa mpira. Hii ninamweleza kabisa, kwamba tumemaliza ujenzi wa uwanja wa mpira. Bado, amekwenda wanyamapori kule nako tukatengeneza mipango mizuri sana ya kuvuna mamba waliokuwa wanasumbua kule. Fisi walikuwa wamezidi kule walikuwa wanachukua watu. Hata hivyo tena akaondolewa tena kwenye nafasi ile, Mungu akampeleka TAMISEMI. Huko amenijengea mimi hapa, nimemaliza shule 24 za sekondari. Hongera sana Mheshimiwa Mchengerwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna ujenzi wa mabweni, kuna shule tisa zimepandishwa hadhi kuwa advance, mabweni sasa yanakamilika, yapo mwishoni. Kwa hiyo Sengerema nitakuwa na jumla ya shule za advance 11. Hongera sana kwa Mheshimiwa Rais pamoja na timu yake ya TAMISEMI.  (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la afya; kwa upande wa huduma za afya pia nimepata vituo vya afya sita ndani ya miaka minne, ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa ajili ya jambo hili. Nimepata hospitali ya wilaya, nimerekebisha zahanati 19. Kwa upande wa barabara mimi nilikuwa na barabara za TARURA kilomita 1,701 na tumerekebisha safari hii kilomita 942; haijawahi kutokea tangu tumepata uhuru; na yamejengwa madaraja ya kutosha. Sasa pamoja na hizi kazi zote nzuri zilizofanyika tunaelekea mwisho na tumebakisha miezi miwili lakini kuna miradi ambayo inahitaji fedha ili ikamilike. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ninaomba sana kwenye bajeti ya Mheshimiwa Mchengerwa niweze kuona. Amekuja Sengerema, watu wamemsubiri hadi saa tatu usiku. Haijawahi kutokea Mheshimiwa Waziri anasubiriwa kwa muda mrefu kama huo. Akawaahidi kabisa kuhusu ujenzi wa soko na amekwenda hadi sokoni, akachuka na hati, akaniomba hati ya lile soko tukampatia. Tunaomba sana, sisi hatutaki masoko ya ghorofa kama haya wanayoyajenga sasa hivi; masoko ya ghorofa halafu yanakosa watu; sisi tunataka masoko yale ya kawaida tu; milioni 300, 400 utakuja uone soko hapa unaingia mle ndani. haya masoko ya bilioni nane, bilioni 21 ya kazi gani kwenye nchi hii? 
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanataka wakafanyie biashara maeneo ambayo hayana matatizo; kwamba wasinyeshewe mvua, wananchi wafanye biashara wapate fedha. Masoko hayo ya bilioni nane, kumi hata watu maskini hawaingii. Sasa Sengerema sisi tunahitaji soko la milioni 500, 600, bilioni moja sisi tutajenga masoko mazuri tu, tunamwomba Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu stendi, Mheshimiwa Mchengerwa alikwenda pale stendi na akaliona lile eneo la stendi. Sisi hatuhitaji stendi za fedha nyingi. Kama kilomita moja ya lami ni shilingi bilioni moja sisi tuwekewe hiyo tu inatosha, sisi stendi yetu ikirekebishwa, kwa hiyo bilioni moja tutakuwa tumemaliza na mapato makubwa yatakuja. Hizi stendi za bilioni 17, bilioni 32 wapewe hao wanaotaka huko, sisi tunataka stendi tu ya gharama ndogo. Siku zimekwisha, wasukuma wanasema muda umeyoyoma, sasa tunaomba sana, yaani, anipokelee hili jambo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ambalo ninataka nimshauri Mheshimiwa Mchengerwa..., Mheshimiwa Mkumbo amwache kwanza, tunampa madini hapa. Mheshimiwa yaani atakuwa hanitendei haki. Mheshimiwa Mwenyekiti nilinde. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kuhusiana na hizi halmashauri zetu. Halmashauri zetu zinakusanya fedha za ushuru kwa wananchi, wananchi wanapeleka karanga, furu, mbuzi wake na ng’ombe, lakini fedha hizi matumizi yasiwe makubwa na ya anasa. Wananchi wanataka madawati kwenye shule za msingi inakuwaje halmashauri anaruhusu bajeti zinaletwa hapa za mabilioni wanafanya mambo makubwa? Kwa nini wasitenge angalau dawati 5,000 kila halmashauri? 
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye nchi hii kuna halmashauri 184, ikiwa kila halmashauri ikiweka dawati 5,000 tu watoto wote wa nchi hii wataacha kukaa chini. Haiwezekani hili suala la dawati nalo afuatwe Mheshimiwa Rais, hili liko ndani ya uwezo wa Mheshimiwa Mchengerwa, tunaomba kwenye hitimisho tuje tuone. Kwa sababu dawati moja ni shilingi 60,000 na kuna maeneo ambayo yana mbao, kama Mafinga, huko dawati haliwezi kufika shilingi 60,000. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa madawati shilingi 60,000 dawati 5000 ni sawa sawa na milioni 300 ambapo watakaa watoto 15,000 hadi 10,000. Sasa watoto 15,000 wakiwa wanakaa kila mwaka baada ya miaka mitano tayari tuna watoto zaidi ya 75,000 huko wanakalia dawati. Nchi imepata uhuru leo tunakwenda miaka sitini na kitu, lakini bado watoto wanakaa chini katika nchi yetu na bado ushuru unakusanywa? 
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili Mheshimiwa Mchengerwa asipokuja nalo vizuri kwa hili jambo nikamwona kwenye hitimisho lake, hapo tena nitageuka kuwa adui, nitakuwa mbabe wa kivita kwenye hii bajeti yake yaani pamoja na kuja vizuri na kupongeza tunafika mwisho sasa, hapo ndipo nakwenda kum-lock. Ninaomba sana nije nisikie ameliwekaje suala hili la madawati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo, ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)