Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru, dah! Anyway. Nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii ili nami niweze kuchangia kwenye bajeti hii muhimu sana ya TAMISEMI ambayo kwa kweli ndiyo backbone ya maendeleo ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ni uungwana, pamoja kwamba ni wajibu wa Serikali kupeleka maendeleo kwa wananchi, lakini pale ambapo unakuta pamefanyika kwa jitihada zaidi kidogo huna budi kupongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilivyokuwa Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini kuna miradi ambayo Halmashauri ya Mji wa Tarime tuliomba ikiwepo soko kuu ambalo sasa hivi limejengwa limekamilika na ni zuri linaongeza hata mandhari ya Tarime Mjini, tuliomba Stendi ya Kemange na tukaomba barabara za lami ambazo zinaenda kutekeleza pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa afya tumeona kabisa kwamba kuna jitihada zimefanyika. Nilikuwa ninajaribu kupitia takwimu mbalimbali; mathalani kwenye kuboresha miundombinu ya afya kumekuwa na ongezeko kutoka vituo 8458 mpaka 9826, takribani ndani ya miaka minne vimeweza kuboreshwa vituo 1,326, kwa hiyo ni ongezeko kubwa sana ambalo linapunguza pia vifo vya mama wajawazito.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vituo hivyo kumejengwa huduma za dharura za uzazi vituo 183 ambavyo pia vina-include upasuaji kwa mama wajawazito. Tumekuwa tukilia sana tukitamani Tanzania iwe na maternal death zero, sasa, hizi jitihada zinapunguza kwa kiwango kikubwa sana vifo vya mama wajawazito. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia pia uwepo wa ujenzi wa hospitali za wilaya 50, kukarabatiwa hospitali za wilaya hizi takriban 48; hizi nazo zinasogeza huduma karibu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka kabisa nizungumzie kuhusu ongezeko kwa utoaji wa huduma za magonjwa ya magonjwa ya dharura. Kwa mwaka 2020 tuliambiwa kulikuwa na MD saba tu, lakini mpaka sasa hivi tunavyoongea, ndani ya miaka minne kwenye hospitali tumejengewa emergency, ikiwepo Tarime Mjini MD zimekuwa 116. Ongezeko la hospitali ambazo zinakwenda kutoa huduma za magonjwa ya dharura 109, ndani ya miaka minne zaidi ya 1,558%. Kwa kweli haya yanatia tija na unaweza uka-justify kodi za Watanzania, pamoja na fedha ambazo unaweza ukakopa, unalinganisha maendeleo ambayo yanasogezwa karibu. Hapa nime-narrow tu kwa hii Wizara ya TAMISEMI. Kwa hiyo ni lazima tuone kama kuna kitu kimeongezeka na kwenye shule pia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu nina dakika tano, niende kwenye changamoto sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba wametusaidia kwa kupeleka fedha Tarime ambazo tumetumia kujenga maternity complex, mortuary ya kisasa pamoja na kichomea taka, lakini hospitali hii ya Mji wa Tarime ni kongwe sana. Hospitali hii imejengwa kuanzia mwaka 1966. Ilianza kama zahanati mwaka 1956 ikaja kituo cha afya mwaka 1962 na mwaka 1966 ikawa hospitali lakini jiografia ya Hospitali ya Mji wa Tarime inachukua watu zaidi ya watu wa Mji wa Tarime; wanatoka Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kwenye Kata za Bumela, Susuni, Silali, Mwema, Komaswa, Manga, wote wanakuja kutibiwa katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tarime.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa programu M-mama ambayo wanasajili, unakuta watu wamesajiliwa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, lakini wakiita gari lazima liwalete Mji wa Tarime kwa sababu wana-cross kwenda Nyamwaga. Tunaomba sana Serikali wazingatie na kuhakikisha kwamba dawa na fedha wanazoleta Hospitali ya Mji wa Tarime vizingatie uhalisia wa watu wanaotibiwa pale na si idadi ya watu ya Mji wa Tarime. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine tunaomba sana, ile hospitali ni kongwe, lile jengo la OPD limeshachakaa sana libomolewe, zipelekwe fedha ili lijengwe jengo lingine la OPD ili kuboresha huduma ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, kama ilivyo Kanda Maalum ya Tarime Polisi Rorya, tunaomba Hospitali ya Mji wa Tarime iwe kanda maalum ya Tarime – Rorya kwa sababu inapokea watu kutoka Tarime DC, Kutoka Rorya, kutoka kwa jirani wengine Wakenya na hata Serengeti; nimekuwa nikiongea sana, ikienda sambamba na ujenzi wa wodi ya VIP.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tarime ina watu wengi sana ambao wametumikia kwenye majeshi akiwemo George Waitara na wengine wengi; na Jaji Mkuu, Mheshimiwa Ibrahim Juma anatokea Tarime Mjini. Wakija kule wakapata dharura hatuna hata ward ambayo ni executive ya kulazwa watu hawa. Watu wanaotoka Kenya kuja kutibiwa pale Tarime wakiona wards zetu zile tunaweza kuwa na utalii wa kimatibabu. Tujenge wards ambazo ni executive ili tuweze kuwa-accommodate hawa watu wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye shule kwa haraka haraka. Huku nako ukiangalia kuna ongezeko kubwa sana la ujenzi wa shule na udahili wa wanafunzi. Hii inapelekea pia uhaba, kama walivyosema wenzangu hapa, wimbi la madawati. Nimekuwa nikiangalia hata kwenye vyombo vya habari kuna baadhi ya shule wanakaa chini; ningeweza kutoa tawimu, lakini muda hautoshi. Unakuta shule ina wanafunzi 1,500 ina madawati 50, wanafunzi wengine wote wanakaa chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba sana Serikali kupitia hata mfumo wa CIS ambao walimu wanasajili, tunavyotoa kipaumbe inaonekana dhamira ya dhati kabisa ya Serikali kuboresha elimu yetu ili kuweza kuongeza idadi ya Watanzania wenye weledi wa kufanya kazi kwenye sekta mbalimbali; tunavyojenga shule tuhakikishe tunapeleka na miundombinu ya madawati. Mtoto anayesoma akikaa chini kwenye sakafu na mtoto anayesoma ambaye amekaa kwenye dawati ni vitu viwili tofauti. Tunaomba sana wafanye utafiti wa kina kujua ni idadi gani ambayo ni mawimbi ambayo hayana shule ambayo hayana madawati kwenye shule walizojenga pamoja na shule kongwe ili wapeleke madawati kuhakikisha kwamba kweli tunakwenda kuboresha hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia pia nikaona kwamba Serikali imeongeza fedha kutoka bilioni 312 hadi bilioni 796 ya elimu bila ada na ninapongeza kwa hili lakini kuna changamoto....

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna changamoto ambayo imeongezeka.

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Dakika chache sana Waheshimiwa Wabunge. Mheshimiwa Mbunge ninakuruhusu.

TAARIFA

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Matiko mchango wake ni mzuri sana na anaonesha kwamba ameridhika na kazi anayoifanya Mheshimiwa Rais. Sasa, ni kwa nini asijiunge na Chama Cha Mapinduzi sasa hivi ili amuunge mkono vizuri Mheshimiwa Rais?

MWENYEKITI: Mheshimiwa Tarimba ahsante kwa taarifa, Mheshimiwa Esther Matiko unapokea taarifa ya Mheshimiwa.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wajibu wa Waheshimiwa Wabunge pale ambapo Serikali inafanya vizuri, kwa sababu sisi tunaisimamia na kuishauri Serikali, ikifanya vizuri objectively unaishauri Serikali, inapofanya vibaya lazima uishauri kwa sababu ni fedha za Watanzania walipakodi, kwa hiyo niongezewe dakika zangu. Nilikuwa nasema kwamba...

MWENYEKITI: Mheshimiwa Tarimba alitumia sekunde 30 tu, tafadhali. Hujapokea taarifa.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa ninashauri, kwamba Serikali ni lazima ihakikishe kuwa inavyokuwa inajenga shule hizi, ipeleke miundombinu toshelezi ili kuhakikisha kwamba hata watoto wanaosoma kule vijijini wasome wakiwa wamekaa vizuri kwenye madawati, wawe na walimu toshelezi ili waweze kupata elimu bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho; Serikali imewekeza na nimeona hapa wamejenga nyumba za walimu. Ukifanya correlation, kwa mfano nilikuwa ninaangalia shule za msingi, zimejengwa 3,000 na kitu lakini nyumba za walimu shule ya msingi zimejengwa 500 na kitu. Kwa hiyo inaonekana kuna shule zinajengwa bila kuwa na walimu. Tunaomba sana, walimu wakikaa, kwa mfano nje ya mji, kwa miundombinu ya barabara hizi mvua ikinyesha hawawezi wakafika kule. Kwa hiyo wanapojenga shule hizi wahakikishe kwamba kunakuwa na administration block, viwanja vya michezo na nyumba za walimu toshelezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nizungumzie kuhusu shule chakavu na ambazo ni hatarishi Tanzania nzima na nimekuwa nikiongea, hata kule Tarime; kwa mfano Shule ya Susuni Kata ya Susuni, Shule ya Nyabilongo Kiongela pamoja na shule za pale mjini ambazo ni chakavu, za miaka ya 70, miaka ya 60. Tunaomba sana, tumeona wamewekeza kwenye miundombinu ya shule, sasa wawekeze kwenye kujenga, shule zile waboreshe, pace iwe kubwa zaidi ili kila mtoto wa Kitanzania ambaye yuko hata kule Chini aweze kufaidika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamalizia kuhusu michango shuleni. Ada wameongeza lakini michango shuleni imekuwa mingi...

MWENYEKITI: Mheshimiwa, hitimisha.

MHE. ESTHER N. MATIKO:... michango ya rim, mchango sijui wa uzio, mchango sijui wa mlinzi, masomo ya ziada, walimu wa ziada inakuwa zaidi unakuta mzazi anatoa zaidi ya 10,000, 15,000...

MWENYEKITI: Mheshimiwa Esther...

MHE. ESTHER N. MATIKO:... hadi wanahisi labda ada irudi waondoe, wapeleke waraka ili iwe uniform kwenye michango hii ya shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, lakini mwisho, uungwana ni vitendo. Tunaona kabisa comparison mpaka 2020 mambo yaliyofanyika 59 years na hii miaka minne ni mingi sana kama alivyosema baba yangu pale Mheshimiwa Shigongo. Mama anajitahidi sana kwa sababu anaishi matatizo ya wananchi, mwanamke anayaishi matatizo ya wananchi. Tumuunge mkono, tuwaunge mkono wagombea wote wanawake kwenye majimbo na madiwani. Ninashukuru sana. (Makofi)