Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ofisi ya Rais, TAMISEMI tukifanya vizuri tunamtendea haki mwenye jina mwenyewe; tukifanya vibaya hatumtendei haki mwenye jina mwenyewe, Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu muda ni mchache; ni aibu mpaka leo Bendera ya Taifa picha ya Mheshimiwa Rais kuwaambia shuleni wanunue. Wapeleke na inawezekana hatuhitaji Malaika Gabriel.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kuhusu upande wa TARURA. Ninaishukuru Serikali kwa kusikiliza Bunge kuongeza bajeti kwa miaka minne mfululizo; lakini bajeti hizo zinakwenda? Jimbo la Nkasi Kaskazini robo tatu ya barabara zake zipo chini ya TARURA. Pamoja na kuongezeka kwa bajeti waangalie maeneo yaliyoathirika zaidi wayapate kipaumbele au kuwe na programu maalumu ya kuweza kumaliza changamoto hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati ninazungumza hapa mwaka jana niliwaambia kuwa kuna kivuko kimoja ambacho kilikuwa kinapelekea vifo vingi vya wanafunzi, nikawauliza kwamba wanasubiri mpaka nani afe ndipo wachukue maamuzi? Ninashukuru wametoa fedha kidogo, lakini barabara ile haijakamilika. Hatutaki tena watoto wetu waendelee kufa pale hatujui wale wanafunzi watakuwa akina nani kesho. Tuheshimu ndoto zao, tujenge kivuko hicho kilichopo kati ya Kata ya Isunta na Kata ya Namanyele na tumalize kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, natambua uwekezaji ambao umefanyika kwenye Wizara hii upande wa elimu pamoja na upande wa Sekta ya Afya. Ushauri wangu ni kwamba, uwekezaji huo uendane na huduma zinazotolewa na siyo majengo yabaki kuwa sifa ya majengo; huduma hizo zitolewe kulingana na uwekezaji uliofanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa elimu; tuangalie sana kuna mikoa ambayo ilikuwa nyuma kielimu. Lengo, hii keki ya Taifa tuigawanye kote. Kwa hiyo, yale maeneo mengine yapewe kipaumbele zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Tulitumia shilingi bilioni 254, kutumia fedha siyo jambo baya, nini kilienda kufanyika? Mheshimiwa Mchengerwa ameshafanya kazi kwenye hizo Wizara nyingine vizuri kabisa na hata Wizara ya TAMISEMI maeneo mengine na usimamizi vizuri kabisa. Mimi ni Mkristo, Mkatoliki, ukweli utaniweka huru, mwaka jana mambo yalifanyika ya hovyo kabisa kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Kuanzia mwanzo kwenye kuwaengua wagombea, haiwezekani, tena mnaondoa mambo ambayo hayapo kisheria wala kikanuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ni Mwanasheria, eti mnasema fomu moja sehemu aliyojaza anajua kusoma Kiswahili kwamba eti alipiga tiki na sehemu ya pili kuwa anajua na Kiingereza kuwa alikosea kujaza fomu. Hilo jambo linamwondoa mgombea? Ninaomba niwaambie amani tunayoimba, amani ni tunda la haki. Tusipoiandaa haki, amani tutaimba haihitaji kutumia mtutu wa bunduki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ameanza vizuri, ametenda vizuri, yaliyotokea kwenye uchaguzi wa Serikali ya Mitaa bado maumivu ya Watanzania ni makubwa, imani imepotea juu ya kulinda haki yao kwenye kura zao watakazopiga. Ninaeleza hapa ninaipenda nchi yangu, niliwaambia wananchi wangu wasifanye fujo, sitaki ndugu zangu waumie wala wafe kwa ajili ya uchaguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna ajabu ilitokea, hata wale wachache waliotangazwa, siku wanakwenda kuapishwa kwa hakimu wanakutana na walioshindwa wanasema nimeagizwa na chama changu nije niape. Ni aibu ya Taifa. Amani hii tunayoizungumza leo ilitengenezwa na kutengenezwa kwake ni haki, tendeni haki. Mheshimiwa Rais amefanya mambo yake mazuri, asubiri wananchi waamue na haki za watu zilindwe, maamuzi yao yaheshimiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mmeona haya mambo yanayozungumzwa hapa, no Reform, no Election, hayaji tu. Ni mambo ambayo yamesababishwa na maumivu ambayo watu wanazungumza. Kuna majibu yatolewe, hakuna mtu ambaye anaweza kuvunja amani ya nchi hii, tukivunja tunaenda wapi? Taifa ni la kwetu sote. Yaliyojitokeza kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa tusione aibu kwamba tulikosea tujisahihishe, turudishe amani ya Taifa letu. Turudishe haki ya mpigakura, turudishe heshima ya mpigakura; viongozi wote wanatokana na maamuzi ya wananchi. Tukikosea leo tunatengeneza Taifa la namna gani? Tutasema sawa tumerudi na ninasema ni kweli mambo yamefanyika hata jimboni kwangu yamefanyika, ninataka nirudi kwa haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi waamue kwamba Aida tunakurudisha Bungeni siyo kwa sababu fulani amesema. Hao wananchi watakuwa wanaona Mbunge waliyemchagua… (Makofi)

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. AIDA J. KHENANI: … Diwani waliyemchagua, wanaweza kumkosoa kwa makosa anayoyafanya. Leo tukitumia mgongo wa nyuma tukatumia mamlaka, amani hii tunayoihubiri leo hatutatumia mtutu wa bunduki kuirudisha, tutairudisha kwa kutenda haki na haki ndiyo tunda la amani. Ndiyo ushauri wangu kwenye eneo hili bila hofu yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Mkristo nitakushauri…

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. AIDA J. KHENANI: …tumetoka huko na wote humu ndani tuna dini, makosa yaliyofanyika tukubali ni makosa. Tuilinde nchi yetu kwa kutenda haki na haki ndiyo tunda la amani. Ahsante.