Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Nitaanza kwa kutoa pole kwa waumini wa dini ya kikatoliki ambapo pia mimi ni muumini kwa kumpoteza kiongozi wetu ambaye ametangulia mbele ya haki, tuendelee kumwombea pumziko jema ili naye atakapofika huko azidi kutuombea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee pia kwa kueleza kwamba ukisoma hotuba kuna maeneo ambayo ninajaribu kuya-quote, kwa sababu ya muda ninajua ni dakika tano. Mheshimiwa Waziri, amesema au ameandika: hapa alikuwa anaelezea lami “Tulipotoka kulikuwa na vumbi, lakini leo tunatembea kwenye lami, tulikotoka kulikuwa na miteremko isiyopitika, leo tuna barabara zinaunganisha ndoto na fursa, kuongezeka kwa barabara za changarawe kwa asilimia alizozitaja anasema hivi ni viunganishi vya matumaini.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, unavyosoma vyote alivyovisema katika Jimbo langu la Kyerwa ni kama havina uhusiano na wakati mwingine nikiwa ninasoma ninajiuliza hivi kuna Tanzania ngapi. Ninatambua kwamba resources zinaweza zisitoshe, lakini resource zitakuwa na maana kama zikimgusa mmojammoja, kama zikiigusa jamii, zikiigusa wilaya na kama zikiligusa jimbo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisemi hakuna kilichofanyika, lakini nikipata muda nikaeleza ramani ya Wilaya ya Kyerwa kuanzia hali ya zahanati, idadi ya watumishi, hali yenyewe iliyopo, vyumba wanavyotumia akinamama na maeneo ya kupumzikia. Nikaanza zahanati mojamoja, nikamtajia Songambele, nikatoka nikamtajia Nyakantuntu na maeneo mengine utasema kweli hii waliyoandika Mheshimiwa Waziri, haituhusu sisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukitoka hapa tukaenda kwenye changamoto ya vyumba vya madarasa ya shule za misingi, tukiongelea baadhi ya vyumba majengo yamechakaa, sawa maeneo mengine wamejenga, lakini ukijenga maeneo mengine na kwenye wilaya isiguswe wananchi hawawezi kuelewa unachokisema. Kwa hiyo, bado tuna vyumba vingi ambavyo ni chakavu kwenye maeneo yetu, nikianza kwenye Shule ya Msingi Songambele na maeneo mengine kadha wa kadha ambayo kwa sababu nina dakika tano sitayataja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wito wangu ninaotaka kuutoa, wananchi wametumia gharama zao kujenga magofu, tuna magofu ambayo yana wastani wa zaidi ya miaka 12 mpaka 15, tuinaomba Serikali iende imalizie hayo majengo, kwa sababu wameyajenga kwa maumivu makali, wamejenga kwa kufungiwa, lakini leo yameshindwa kuisha. Ninaomba tutie nguvu kuhakikisha haya majengo yanakamilika, lakini siyo hivyo tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu changamoto ya vyoo, leo katika karne ya 21, wakati ukijisifia kuna maeneo kadha wa kadha, shule za msingi kwenye maeneo yetu zinafungwa kwa kukosa vyoo, orodha ni ndefu, muda hautoshi, lakini Waziri akitaka nitampatia. Shule zinatishiwa kufungwa kwa sababu hazina matundu ya vyoo. Kuna shule moja ya msingi ambayo iko Kata ya Nyakantuntu ina matundu mawili ambayo matundu haya wanatumia walimu na wanafunzi, ambayo mengine yameshazama, hiyo tunaongelea karne ya 21.
Mheshimiwa Mwenyekiti, twende pia kwenye habari ya barabara, nyie wote mnajua nimekuwa nikiongelea changamoto ya TARURA kwenye Wilaya ya Kyerwa, kwamba wakati mwingine bajeti ya TARURA haitoshelezi kwa sababu ya nature ya kijiografia ya maeneo yetu. Kwa hiyo, ni lazima tunapokuwa tunaongelea hizi quick wins, quick wins zisambae kwenye maeneo yote na hasa kwenye maeneo ambayo ni ya kimkakati. Ukija kwenye wilaya zetu zina uchumi, zina rutuba na zina kila kitu, kama Serikali ikiwekeza, kama Serikali ikitoa maendeleo ina maana na sisi tutafika mbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba hayo niyaache, nije kwenye kazi ambazo Mheshimiwa Rais amefanya. Mheshimiwa Rais ni moja kati ya champion wa maridhiano. Mheshimiwa Rais amekuja na kitu kinaitwa 4R, sisi wengine tuliamini kwamba hii nchi ilihitaji mwanamke katika wakati sahihi kuiponya na akaja na 4R zake akasema kuna reconciliation, resilience, reforms, rebuilding, hizo ndiyo 4R ambazo zimem-define Mheshimiwa Rais duniani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa leo kinachotokea kwa watu wa Chama changu, CHADEMA, wanasema, no Reform, no Election, mnajua imetoka wapi? Kwenye ile 4R ya Mheshimiwa Rais ya tatu, wamesema wanataka reform, ni kwa nini wametaka reform? Ni kwa sababu ya past experience. Sisi wote humu ndani tumewahi kukiri, kuna wakati mambo yanaweza kwenda ndivyo sivyo, hivi watu wakisema wanataka reform ni kosa? Mheshimiwa Rais ameridhia kwamba hii nchi kama Taifa tuje pamoja, tujadili mustakabali wa maendeleo yetu ndiyo maana ameleta reform, ameongelea reconciliation, kuna shida ya reconciliation. Leo tunawaweka watu ndani kwa sababu ya kutaka reform, Tundu Lissu, ni sahihi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, amani ni tunda la haki, amani tuliyonayo leo, kuna watu wamefanya kazi kubwa mpaka tunayo leo, hatuwezi kukubali kuivuruga amani kwa sababu ya ubinafsi wa uchaguzi. Hatuwezi kutaka kuiumiza Tanzania, kwanza wanasiasa ni wangapi? Wabunge ni wangapi? Mawaziri ni wangapi? Kwa population ya Tanzania watu zaidi ya milioni 60. Ninadhani kama Taifa tunapaswa tukae chini tupate mustakabali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamekuwa wakitoa mfano, katika game ya Simba na Yanga, unamruhusije Referee wa Yanga kuchezesha hiyo game? Hayo maelezo mbona yako wazi. Nirudie kusema hiki chama kazi wamefanya, si wamejenga lami? Si wamepeleka zahanati? Si wamepeleka umeme? Kwani shida iko wapi referee akiwa neutral? Ninadhani hiyo ndiyo call ninapaswa kuitoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie na uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Aliyemaliza kuongea ameongea…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. ANATROPIA L. THEONEST:  Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dakika moja, kuna maeneo ambako kulikuwa na mgombea mmoja wananchi walipaswa kupiga kura ya hapana au ndiyo, hao wananchi walipiga kura ya hapana maeneo mengine kura zao hazijawahi kuhesabiwa mpaka leo na mshindi hajawahi kutangazwa. Haya mambo yanaliumiza Taifa, sisi tunataka Taifa letu la amani lenye viongozi wanaoheshimika waliopatikana kwa credibility, tudumishe hiyo itatufikisha mbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. (Makofi)