Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Abdallah Dadi Chikota

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyamba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili niungane na wenzangu, kwanza kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya na miongozo ambayo anaitoa kwenye Wizara hii ya TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kijana wetu Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa kwa kazi kubwa ambayo anaifanya na usimamizi mzuri, hongera kwake, lakini na Naibu Mawaziri, kuna Mheshimiwa Zainab Katimba na Mheshimiwa Dkt. Festo Dugange, ni Naibu Mawaziri ambao ni wasikivu, muda wote wanafikika na wanatoa ushirikiano kwa Wabunge. Kwa hiyo, hongereni sana na mwendelee na moyo kama huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze vile vile Katibu Mkuu wa Wizara hii Ndugu Adolf Ndunguru, Watendaji Wakuu wa Taasisi kwa kazi nzuri ambazo wanafanya kama Engineer Seff wa TARURA na watendaji wengine. Ninawapongeza sana kwa kazi nzuri wanazoendelea kuzifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba katika kipindi hiki tumeona kazi kubwa inafanyika TAMISEMI, tumeona miradi mingi ya kimkakati inafanyika TAMISEMI, tumeona fedha nyingi zinapelekwa katika Serikali za Mitaa na miradi hii inagusa jamii kwa kila eneo. Kwa hiyo, TAMISEMI hongereni sana na kazi wanazozifanya zinaonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu mazuri ni mengi, leo nitashauri baadhi ya maeneo. Ushauri wangu wa kwanza unaenda TARURA. Kama nilivyosema TARURA inafanya kazi nzuri chini ya Engineer Seff, inatatua changamoto zilizopo katika maeneo yetu, lakini nimwombe tu Mheshimiwa Mchengerwa na timu yako kwamba Mikoa mitatu ya Mtwara, Pwani na Lindi ni mikoa ambayo iliathirika sana na Kimbunga Hidaya mwaka jana na ni mikoa ambayo kazi inaonekana leo, Barabara ya Kibiti - Lindi pale Somanga basi hata barabara za ndani feeder roads katika maeneo haya vilevile zimeathirika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii nyongeza ya fedha ya TARURA basi katika hii mikoa mitatu waangalie jinsi ya kuongeza fedha ili zikatatue changamoto ambazo zipo katika barabara (feeder roads) ambazo zipo katika maeneo hayo ili kuhakikisha muda wote zinapitika na zinarejeshwa katika hali ya kawaida, kwa sababu Kimbunga Hidaya hakikuathiri main road tu kimeingia mpaka barabara za ndani, Kilwa, kule Kibiti na maeneo mengine, Mtwara, Lindi. Kwa hiyo, hawa wapewe special consideration wakati wa kutenga hizo fedha ambazo kuna ongezeko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, TAMISEMI imefanya kazi kubwa sana, kuna miundombinu mingi imeongezeka katika Sekta ya Elimu, Sekta ya Afya, lakini sasa miundombinu hiyo ambayo imeongezeka haitakuwa na athari kubwa kwa jamii kulingana na changamoto ya watumishi iliyopo kwa baadhi ya maeneo hususan mikoa ya pembezoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Ofisi ya Rais, TAMISEMI ifanye jitihada za makusudi kutoa kibali maalum kwa ajili ya mikoa ya pembezoni. Kwa mfano, Mkoa wangu wa Mtwara, nikitoa mfano, Sekta ya Elimu, ina upungufu wa 49% yaani tuna mahitaji 51% tu. Kwa hiyo tuna upungufu wa walimu 49%, ukienda Sekta ya Afya, kwa Mkoa wa Mtwara, tuna mahitaji ya watumishi 7,309 lakini waliopo ni 37% tu ya mahitaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi zote ambazo tumezifanya kwenye Sekta ya Elimu, kwenye Sekta ya Afya utakuta athari zake hazionekani kwa ukubwa wake kwa sababu tunayo miundombinu ya shule, tunayo miundombinu ya vituo vya afya, ya hospitali za wilaya, lakini kuna changamoto kubwa sana ya watumishi wa afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, katika jimbo langu tuna X-Ray Machine mbili, lakini hatuna mtumishi, tukawa tunachukua mtumishi wa Wilaya jirani ya Tandahimba na yule wa Tandahimba amehama, kwa hiyo hata tulipokuwa tuna azima sasa hatuna. Kwa hiyo, tuna Digital X-Ray za kisasa kabisa, lakini hazi-operate kwa sababu hatuna mtumishi na katika maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kwenye shule zetu, tuna majengo mazuri, tuna maabara za kutosha, lakini kwa sababu kuna upungufu wa walimu basi haziwezi kuwa na tija kama tulivyokuwa tunategemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa tatu, niungane na hoja ambayo alitoa Mheshimiwa Mnzava, suala la Sera ya Ugatuaji. Ugatuaji katika nchi yetu unaendeshwa kwa sera, Policy Paper ya mwaka 1998, kwa miaka mingi sana tumekuwa tunaongelea kuwa na Sheria ya Ugatuaji, lakini haipo na hii inakuwa ni vigumu sana katika utekelezaji wake. Leo huyu anakuja mtu, anaamua kwamba watumishi wa Sekta ya Afya waende Wizarani, kesho anakuja mwingine anasema watumishi wa ardhi waende Wizarani. Kesho atakuja mwingine atasema watumishi wa elimu waende Wizara ya Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tuwe na Sheria ya Ugatuaji, na sheria hii itaweka mipaka ni kitu gani kinagatuliwa, kitu gani kinafanywa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa na kitu gani kinafanywa na Serikali Kuu. Vilevile, ugatuaji utaelezea vyanzo vya mapato vinavyoaminika na vinavyotabirika, Serikali Kuu na Serikali za Mitaa lazima ziwe na share katika vyanzo vya uhakika vya mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vyanzo vya mapato vilivyopo sasa hivi kwenye Serikali ya Mitaa haviaminiki, halmashauri nyingi zinategemea produce cess, kilimo chetu kinategemea upatikanaji wa mvua. Kwa hiyo, mwaka kuna mvua tutapata produce cess ya kutosha, hakuna mvua hatuna produce cess ya uhakika. Kwa hiyo, lazima tuwe na Sheria ya Ugatuaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hii itaweka mipaka, itaweka vyanzo vya mapato vya uhakika na itaonesha demarcation, ni vitu gani vitafanywa na Serikali Kuu na vitu gani vitafanywa na Serikali za Mitaa. Hii haitabadilika badilika kulingana na maono ya mtu kwa sababu itakuwa imewekwa kwenye Katiba na TAMISEMI kila mwaka walikuwa wanaahidi wataleta hicho kitu bado hawajakamilisha. Mheshimiwa Mchengerwa, ninamwamini sana, yeye ni mchapakazi, ni mtu wa kuthubutu, hili linawezekana, litekeleze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya mabadiliko ya hili suala la Sheria ya Ugatuaji, twende kwenye uendeshaji wa halmashauri zetu. Sheria zetu ambazo zimeanzisha Mamlaka ya Serikali za Mitaa, ile Sheria ya Halmashauri ya mwaka 1982, ile Sheria ya Miji lakini na ile Sheria ya Fedha ya Mwaka 1989, sasa hivi tunahitaji mabadiliko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna masuala mengi inabidi tufanye tafakari, hivi je, katika uendeshaji wetu wa halmashauri kuna haja ya kumbadilisha Makamu Mwenyekiti kila mwaka? Hii ina tija au haina tija? Inaleta manufaa au inaleta migogoro? Kwa sababu kila mwaka, ni nini kinatufanya tuchague Makamu Mwenyekiti? Kwa nini tusichague Mwenyekiti wa Halmashauri au Meya na Makamu wake wa kudumu, kwa nini kila mwaka tunabadilisha? Tunasababisha migogoro ambayo siyo ya lazima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna knowledge gap kati ya watendaji na Madiwani. Je, tunavyokwenda kwamba Baraza la Madiwani lifanyike kikao kwa siku moja, Baraza la Madiwani kwa siku moja linajadili elimu, afya, maji na barabara, hii inawezekana? Wanapewa kabrasha asubuhi yake, wanajadili kwa masaa mawili wanaondoka na mjue kuna knowledge gap kati ya madiwani na watendaji. Hiki kitu lazima TAMISEMI ikiangalie upya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, kwenye ukaguzi wa miradi yetu, Madiwani wanapewa masaa manne wakague miradi, halafu kesho inaenda kwenye baraza na sasa hivi tuna uwekezaji mkubwa tunafanya kwenye Sekta ya Elimu, Afya, Barabara na Maji. Miradi yote hii inaweza kukaguliwa kwa siku moja, lazima haya mambo tubadilishe. Madiwani wapewe muda wa kukagua miradi yao ili wakiingia kwenye baraza waweze kujadili uendeshaji wa halmashauri yao. La sivyo, wanaingia pale wanapitisha mambo yanabaki kama kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, muundo wa Kamati zetu ambazo tumeziweka kwenye halmashauri unatosheleza katika uendeshaji wa halmashauri kwa muda tuliyonao sasa hivi? Maana pale tumejiwekea Kamati za Kudumu ambazo lazima tuzifanyie review tuangalie zinakidhi kwa mahitaji ya sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo ni machache kati ya mengi. Mheshimiwa Mchengerwa, ninamwamini sana, wanaweza wakaunda timu ya wataalam. Huko nyuma zipo research zilifanywa na akina Profesa Ngwale wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam walifanya, wameandika mambo mazuri sana kuhusu local government reform tuyapitie yale. JICA wamepeleka Wakurugenzi Japan mara nyingi tu, wana mawazo mazuri ya kufanya reform kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Mheshimiwa Mchengerwa ninaamini ukiyafanyia kazi hayo tunaweza kuboresha uendeshaji wa halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe ushauri vilevile katika Mradi wa TACTIC. Huko nyuma tuliambiwa kwenye Mradi wa TACTIC hasa ule wa tier two na tier three kutakuwa na maboresho ili mharakishe utekelezaji wa hii miradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ya halmashauri ambazo ziko kwenye tier three bado ni ya kusuasua. Pia, kumekuwa na timu nyingi sana za ufuatiliaji kabla ya utekelezaji. Mheshimiwa Mchengerwa, ninaomba sana, wewe ni mtu wa kuthubutu, tuangalie sasa namna ya kuanza kutekeleza hii miradi hasa kwenye halmashauri ambazo zipo kwenye tier three ili kazi hiyo sasa ianze kuonekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na timu, leo inakuja timu hii inafanya mabadiliko haya, inakuja nyingine tena kesho inafanya mabadiliko haya, lakini hakuna utekelezaji ambao umeanza katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho niungane na wenzangu ambao wamesema Mheshimiwa Waziri wakati wa kuhitimisha hii hotuba yako utuambie hili suala la vituo vya afya vya kimkakati. Tunaomba hiyo orodha iwekwe wazi na tuambiwe hizo fedha zinapatikana lini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwangu nina Kituo cha Afya Namtumbuka. Wakati wa ziara ya Mheshimiwa Rais ilitamkwa mbele hadharani na wewe mwenyewe ulikuwepo pale, kwamba tutawaletea fedha hivi karibuni na Wanamtumbuka wameshaandaa eneo. Pia, kule Nanyamba kura zipo za kutosha. Zipo za kutosha, tunasubiri tu Mwezi Oktoba tumpe Mama Samia kura zake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule atakuja kusalimia tu. Mkoa wa Mtwara tumekwishajipanga kwamba, kura zote kwa Mama Samia na sisi tunataka tuwe miongoni mwa mikoa mitatu ya kwanza kwa kutoa kura nyingi kwa Mheshimiwa Rais. Kwa hiyo, ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri wakati wa kuhitimisha atuelezee hivi vituo vya kimkakati fedha zinapatikana lini ili wananchi wetu waweze kujua kwamba wanaanza utekelezaji lini na ujenzi unaanza lini ili huduma inayokusudiwa itolewe kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja na ahsante sana kwa kunisikiliza. (Makofi)