Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Stanslaus Shing'oma Mabula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyamagana

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kusema maneno machache juu ya bajeti iliyopo mbele yetu. Kwanza nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mungu wetu wa Mbinguni, kwa kuendelea kutupatia nafasi ya kuvuta hewa nzuri na pumzi ya Taifa letu na nafasi aliyotupatia ya kuwahudumia Watanzania wenzetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda wetu mchache, nami niungane na wenzangu kwanza kwa kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kwa namna ya kipekee katika kipindi hiki cha miaka minne hakika ameitendea haki Tanzania, hakika ameitendea haki Nyamagana, hakika amewatendea haki wananchi wa Jiji la Mwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri. Tunauona utulivu wa kiwango cha juu kwenye Wizara hii toka Mheshimiwa Mchengerwa alipopata nafasi ya kuhudumia nafasi aliyonayo sasa. Sasa tunafahamu maendeleo ni mchakato wa muda mrefu. Hata hivyo, ni maajabu makubwa sana tunaposema hakuna kilichosimama na hakika tumekuwa tukimaanisha. Tumekuwa tukimaanisha kwa sababu yale yote yanayojitokeza na tunayozungumza sasa, ni mambo ambayo yametokea kwa muda mfupi na yameleta tija na matumaini makubwa kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapompongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa watu wa Nyamagana na Watanzania wengine kwa kuongeza vituo vya afya, zahanati na kuboresha Hospitali za Wilaya na Mikoa, tafsiri yake tusiitazame kwenye majengo; tafsiri yake tuitazame namna ambavyo ameokoa maisha ya watoto, akinamama na maisha ya Watanzania ambao mara nyingi wamekuwa wakipoteza maisha wakihangaika kujifungua, kutembea umbali mrefu na kadha wa kadha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia uboreshaji wa Sekta ya Elimu Msingi na Sekondari, kila mmoja amesema hapa namna ambavyo shule za msingi zimeboreshwa, na namna ambavyo sekondari zimeboreshwa. Leo tunapozungumza kwenye uanzishwaji wa shule mpya za msingi zilizozingatia takwa maalum la watoto wadogo (kindergarten) kupata maeneo ya kujifunzia, tunaliona kama jambo dogo, lakini ninataka nikuhakikishie kuwa ni jambo kubwa sana lenye tija na linalowafanya watoto wetu wajione nao wanapita kwenye mazingira ambayo kesho na kesho kutwa yatawafikisha sehemu salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais. Wakati anaingia madarakani, Jiji la Mwanza tulikuwa na miradi mikubwa ya soko na stendi ambayo ilikuwa imetekelezwa kwa 15% peke yake. Hata hivyo, leo baada ya miaka minne ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, miradi imekamilika kwa 100% kwa zaidi ya shilingi bilioni 32. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili siyo jambo dogo. Pia, nimwambie kaka yangu Mheshimiwa Tabasam, alikuwa anaongea kuwa anataka miradi midogo. Kuna tofauti ya haya majimbo, hili nalo ni la kuzingatia sana. Unapozungumzia mradi wa shilingi bilioni tatu na shilingi bilioni mbili, kuna mazingira yake ya Sengerema unakubalika sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija Jiji la Mwanza, mradi wa shilingi bilioni 20 au 12 pale Nyamagana ndiyo mahali pake. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Tabasam, kila mtu atapata kulingana na urefu wa kamba yake. Hii ndiyo tafsiri ya miradi mikubwa ya kimkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nihame sasa niende kwenye miradi ya barabara. Namwona Mheshimiwa Tabasam amekuja kwa kasi hapa, hachelewi kuniharibia siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nianze kwa kumnukuu Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake. Amesema, “barabara ni miradi ya matumaini. Kila kilometa mpya iliyojengwa ni daraja kati ya masikini na maendeleo, njia ya mtoto kufika shule, mama kufika hospitali, mkulima kupeleka mazao sokoni na Taifa kusonga mbele.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, meseji hii unaweza kutazama uzalendo wa hali ya juu ndani ya Mheshimiwa Waziri, lakini akitumika kwenye Wizara ambayo inasimamiwa na Mheshimiwa Rais. Tafsiri yake tunaiona kwa vitendo na Waheshimiwa Wabunge wote hapa ni mashahidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunazungumza tunajenga barabara yenye urefu wa kilometa 14.47 kutoka Buhongwa – Lwanima – Kanido – Kishili – Igoma. Barabara hii tumeipigania kwa zaidi ya miaka 10. Tangu ameingia Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, barabara inajengwa na tayari iko zaidi ya 80%. Mheshimiwa Mchengerwa, tafsiri yake ninataka nimhakikishie; pale tuna shule takribani nne, kupitia mradi huu zimejengewa fensi ambayo nimesikia wenzangu hapa wanaomba kwenye maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka niseme, unapojenga barabara ni kweli kabisa wala haujakosea kwani unaboresha maisha ya Watanzania, unaimarisha uchumi wa nchi hii na unatia tija kwenye miji yetu ili iweze kupata maendeleo zaidi ambapo tafsiri yake tunaiona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana Mheshimiwa Waziri, watu wa TARURA tuwasaidie. Tumekuwa na mfumo wa kutangaza tender 60% na zile 40% zinabaki. Zinaleta mkanganyiko tunapokwenda kukamilisha ujenzi wa mradi wenyewe. Kwa hiyo, tuombe sana na hili ndilo ombi langu kubwa. Mheshimiwa Waziri, ni bora tukatangaza kazi 100% yote, halafu tukabaki kutafuta fedha ili miradi yote tuliyoikusudia kwa mwaka husika iweze kukamilika. Tusipofanya hivyo, tutakuwa na miradi viporo mingi. Mheshimiwa Mchengerwa, nimwombe sana. Sasa hivi pale Mwanza tuna miradi mikubwa miwili ya barabara na miradi miwili mikubwa ya madaraja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajenga Daraja la Mkuyuni kwa zaidi ya shilingi bilioni tano na tunajenga Daraja kubwa la Mabatini kwa zaidi ya shilingi bilioni sita. Mheshimiwa Mchengerwa, shida tunayoipata na niliuliza swali hapa asubuhi kuhusu Barabara inayotoka Mkuyuni – Tambukareli – Nyanguruguru – Mahina kutokea MWATEX (Nyakato). Barabara hii tumeiomba kwa muda mrefu. Mheshimiwa Mchengerwa, madhara yake ni nini? Bahati nzuri ulikuja Mwanza wakati unasaini mkataba wa kujenga soko la kisasa la mazao ya majini na nchi kavu pale Mkuyuni. Ulielekeza na kuagiza barabara ianze kujengwa mara moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa tunalolipata; sasa hivi wakazi wa Jiji la Mwanza, wana adha kubwa sana kwenye Barabara ya Kenyata na Barabara ya Nyerere kwa sababu mvua zinanyesha, maji yanajaa kwenye madaraja kwa sababu mkandarasi yuko kazini. Tunafahamu kila neema inakuja na changamoto zake. Ombi langu, ni lazima sasa tukubali kujenga barabara mbadala ambazo zitasaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais anakuja kuzindua Daraja la Busisi. Likishazinduliwa Daraja la Busisi msongamano na foleni itakayokuwepo kwenye Jiji la Mwanza itakuwa ni mara 10 ya sasa; kwa sababu ule muda wa magari yanayosubiri pale ferry haitakuwepo tena. Magari yote yatakuwa yanatoka kule kwa kaka yangu Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa Shigela (nimemwona pale), Geita na maeneo mengine kule yatakuwa yana-flow kwa kasi ya ajabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tuwe na hizi njia mbadala za pembeni zitakazojengwa kwa ubora ili barabara kubwa (Barabara ya Mkuyuni, Barabara ya Kutoka Nyakagwe – Masongwe inapita Buhongwa na inakwenda mpaka Daraja la Busisi itakuwa ni msaada mkubwa sana wa kusaidia upumuaji na matumizi bora na sahihi ya Barabara ya Kenyata na Barabara ya Nyerere. Mheshimiwa Waziri, nimwombe sana, maelekezo yako tunafahamu amesema kwenye bajeti hapa kwa mwaka ujao wa fedha ambao tunauzungumza sasa umetupatia tuanze na kilometa mbili kati ya kilometa 10. Ninamwomba aziongeze angalau zifike kilometa tano kwa mwaka wa kwanza unaoanza kwa sababu bila kufanya hivyo hatutawasaidia wakazi wa Jiji la Mwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema hapa, leo tuna Barabara ya Buhongwa inakwenda Igoma kupitia Lwanima na Kishili. Hii ni barabara moja muhimu sana. Pia, hii ndiyo tafsiri ya njia zitakazokuwa mbadala kwenye hii barabara kubwa ambayo tunaijenga leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa madaraja haya yanaendelea kujengwa, lakini ukweli ni kwamba kati ya kilometa na niwapongeze sana. Mheshimiwa Mchengerwa, kitendo cha kuongeza bajeti kutoka shilingi bilioni 886 mpaka shilingi 1,108,000,000,000, ni hatua kubwa sana itakayosaidia TARURA kupeleka fedha. Vilevile, Mheshimiwa Mchengerwa, kwa Jiji la Mwanza kulipelekea shilingi bilioni tano kwa mwaka ni fedha kidogo sana na haiwezi kutosha kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuongeze walau tupate shilingi bilioni 10 kwa mwaka ili tuweze kufikia malengo ya kuwasaidia wananchi yaendane na ile kauli uliyoisema, “Barabara zinapojengwa ni matumaini, kila kilometa iliyojengwa, ni daraja kati ya masikini na maendeleo, ni daraja la mtoto kwenda shule, mama kutibiwa, kuokoa maisha ya watu na kadhalika.” Tunakushukuru sana kwa kazi nzuri, endelea kupiga mwendo. Pia, watoto wa mjini wanamwita mtu kazi. Hatuna shaka mtu kazi na kazi tunaiona kwa vitendo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)