Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kyela
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi. Kwanza kabisa ninaomba nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa mambo makuu mawili. Jambo la kwanza ni kwa kunipa uhai, baraka na neema hii ya kwamba leo ninasimama Bungeni na kuzungumza machache kwenye Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili; ninamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunifanya niwe Mbunge wa Jimbo la Kyela, katika kipindi ambacho Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hili ninamshukuru sana Mwenyezi Mungu.  Kwa nini ninashukuru? Ninamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa sana ambayo ameifanya. Amefanya kazi kubwa, lakini siyo kubwa tu; ni Rais mwenye mapenzi mema kwa Watanzania, Rais mpole, Rais anayesikiliza watu, Rais ambaye anaongozwa na maono ya Mungu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, anaongozwa na maono ya Mungu na hili linadhihirishwa pale ambapo anaunda timu ambayo ni bora kabisa na imeweza kumsaidia. Leo hii tuko na Mawaziri kwenye TAMISEMI ambao ni bora sana wakiongozwa na Mheshimiwa Mchengerwa.  Ahsante sana na Mungu ambariki Mheshimiwa Mchengerwa, akisaidiwa na Ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Dugange na Dada yangu Mheshimiwa Katimba, wanafanya kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais hajaishia hapo, ameweka timu nzuri inayomsaidia kuanzia kwa Katibu Mkuu, ndugu yetu Ndunguru. Pia, wapo wanaomsaidia ndugu yetu Ndunguru ambao ni akina Mwambene na Engineer Seff. Ninakushukuru sana Engineer Seff, tumefanya kazi nzuri kwa siku hizi mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pesa za maafa (emergency shilingi milioni 200) zilikuja kule Mbeya, lakini nilinyimwa (sikuletewa) na wakati huo mimi ndiye mwenye mafuriko. Hata hivyo, ninakushukuru sana Engineer Seff, ameli-solve hili, ameniletea shilingi milioni 200, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ogopa sana mtu ambaye ana-invest kwenye maisha ya watu. Mheshimiwa Rais ameamua ku-invest kwenye maisha ya watu. Mtu ambaye anashughulika na elimu ya watu, afya ya watu na miundombinu anawagusa moja kwa moja wananchi wake. Jambo hili siyo dogo. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiona watu wanaleta slogan zao hapa, huko pembeni wanalialia, siyo kwamba wanapenda; ni kwamba hawajaona mahali pa kutokea.  Mheshimiwa Rais anashughulika na SGR, Miradi Mikubwa ya Maji, Bwawa la Mwalimu Nyerere, kuna watu leo hii walidhani huku kutalala, wamekosa uchochoro na ninawaomba Wabunge, tuache. Kwa vile wamekosa uchochoro, wameamua kutafuta njia ambayo ni rahisi ya kutoingiza timu uwanjani, sisi tuwaache wasiingize timu uwanjani. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi hata ungekuwa wewe au hata ningekuwa mimi, kwa mambo ambayo ameyafanya Mheshimiwa Rais, nisingethubutu kuingiza timu uwanjani kwenda kwenye uchaguzi kwa sababu nina uhakika tungepigwa tu na wataendelea kupigwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikupe mifano michache, pale Kyela kwenye upande wa elimu tumejenga shule za sekondari tisa katika miaka hii minne, siyo jambo dogo. Tumejenga shule za msingi 12, tumejenga shule kubwa ya wasichana ya shilingi bilioni nne, utawaambia nini wananchi? Leo wananchi wameacha kuchanga michango ya kujenga madarasa. Huko nyuma, Watanzania na wananchi wengi katika wilaya yangu walikuwa wanashinda mitoni kwa kuogopa michango. Mgambo na watendaji kazi yao ilikuwa ni kufukuza wananchi wachangie ujenzi wa madarasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan akasema hapana, wananchi wangu mmechoka michango, nitaleta pesa na nitajenga madarasa. Hapo siyo padogo ndugu zangu, ni jambo kubwa. Hivi ungekuwa ni wewe mtu anawaambia watu wasichange michango, nitajenga mimi madarasa, unaingizaje timu kwenda kupambana na mtu wa namna hiyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amepambana na amejipambania. Kura zake zimejaa kwa sababu anafanya kazi kubwa. Mheshimiwa Rais, kule kwangu amejenga Hospitali kubwa. Tangu uwepo wa Kyela tulikuwa na kituo cha afya kimoja tu. Leo tunaongelea kujenga vituo vipya vya afya saba. Kazi kama hiyo huko nyuma ilikuwa haifanyiki. Leo tunajenga vituo vya afya saba, siyo kazi ndogo.  Ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo ningependa kushauri, ninaomba sana kwenye jambo la vituo vile vya afya ambavyo tuliahidiwa (Kituo cha Afya Matema na Kituo cha Afya cha Busale) Mheshimiwa Waziri, ninaomba sana pesa zije.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi pia wa Hospitali yetu kubwa ya Kyela ambayo tumepewa shilingi bilioni tano, tumejenga ghorofa mbili ambazo ziko pale nzuri na zinapendeza kwa ajili ya mama na mtoto. Tunaomba ile shilingi bilioni 1.1 kwa ajili ya hospitali yetu ninaomba sana ije ili tuendelee na hospitali yetu iendelee kutoa huduma zilizo bora kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri hapa amesema kwamba tumetoka kwenye vumbi tumeenda kwenye lami, maneno haya yanasadifu kabisa mambo ambayo yametokea Wilayani Kyela. Tangu uwepo wa Wilaya ya Kyela tulikuwa na kilomita 2.18 za lami, leo tunaongelea kilometa saba za lami. Katika kilometa hizo nataka niseme zimetokea kipindi hiki cha miaka minne, leo hatuwezi tukabeza. Ndiyo maana ninataka niseme hata uchaguzi mkuu hatutakuwa na shida kwa sababu hata kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa Mheshimiwa Waziri katika sehemu aliyofanya vizuri na wananchi wanampongeza ni Kyela. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka niombe msamaha, Sheria ya Uchaguzi inasema mtu anayekwenda kugombea anatakiwa awe easily identified, awe na uwezo wa kutambulikia, sisi tulikubali hata wale ambao walisema wamezaliwa mwaka 2024 tuliwaambia waingie mtaani, waliingia kwenye uchaguzi. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mtu alisema amezaliwa mwaka 2024 tukasema aingie kwa sababu tulikuwa na uhakika kazi tulizofanya ni kubwa tumewatandika wote na tunawaambia kipindi kijacho tunaenda kuwatandika pia. Mheshimiwa Waziri naomba utembee kifua mbele kama kuna mtu anasema uchaguzi haukufanyika vizuri Kyela ulifanya vizuri na hakuna manung’uniko. Hata wenyewe walisema Kyela tunashukuru mmefanya uchaguzi tumekubali matokeo.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, dakika zake zimeisha.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mbunge upo nje ya muda tafadhali hitimisha.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ninaomba tu niseme tunakoelekea ni kuzuri na tulikotoka nako kulikuwa kuzuri, lakini kwenye kipindi cha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan mambo ni mazuri na ahadi ya asali na maziwa tunaenda kuipata. Twendeni tuungane tuzungumze lugha moja. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja na ahsante sana.  (Makofi)