Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa kuunga mkono hoja hii kwa kuchangia na niwapongeze sana Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kwa kazi kubwa na nzuri ambazo wanazifanya na kweli Wizara imepata mtu na ina watu na inafanya kazi. Hongereni sana kwa kazi nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana mwenye Wizara yake ambaye ni Mheshimiwa Rais. Katika kuitendea haki Wizara hii ameitendea haki sana. Tunajua TAMISEMI ndiyo imeshika maisha ya wananchi. Habari ya huduma za jamii zote zimelala katika Wizara hii, kazi kubwa ambayo Mheshimiwa Rais ameifanya tumekuwa tukiizungumzia hapa hata nilipochangia. Hata nilipochangia Ofisi ya Waziri Mkuu nilisema, sasa nisingependa kupoteza muda mwingi kuyarudia, lakini ninasema kwa kweli Mheshimiwa Rais anastahili maua yake katika namna bora alivyozitendea haki huduma za jamii kwa nchi nzima. Hatuna deni naye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hotuba ya Waziri ukurasa wa nane ilo paragraph ya 15 amezungumzia masuala ya namna ambavyo majukumu yalishushwa kwake na Mheshimiwa Rais tarehe 30 Agosti, 2023. Moja ya jukumu alilopewa ni pamoja na kusimamia utekelezaji wa sera ya ugatuaji madaraka (D by D) ili kuweza kuongeza kasi ya maendeleo katika miji na vijiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninataka kuzungumzia hapa suala la Wenyeviti wetu wa Serikali za Mitaa. Shughuli zote za maendeleo na changamoto na namna ambavyo tunakwenda kwa kasi Waheshimiwa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa wana nafasi kubwa sana katika kuhakikisha maendeleo yale yanakwenda, tunashukuru wanafanya kazi yao vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la posho kwao. elfu ishirini kwa Mwenyekiti Serikali iliangalie upya ni kidogo mno kwa kazi kubwa anayoifanya. Mwenyekiti huyu pia akimaliza miaka mitano hana hata kiinua mgongo. Hebu basi Serikali ione hata kama itawapa token, shilingi milioni tatu au tano kwa miaka mitano waliyofanya kazi ya maendeleo haya ambayo tunayasifia, Mheshimiwa Rais kafanya kila kitu na mambo mengi yamefanyika lakini wanaochakarika kule na kusimamia ni Wenyeviti wetu wa Serikali za Mitaa pamoja na Mabalozi katika kuhamasisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kuwaunganisha mabalozi hapa kwa sababu ndani ya Serikali hawapo wanatambulika kwenye chama. Kwa sababu tunawatumia sana katika shughuli za maendeleo, ninaomba basi tuone katika mfumo wa Serikali Balozi awe ni kiungo kikubwa kwa Mwenyekiti na atambulike kisheria. Balozi asiishie tu kwenye masuala ya chama kwa sababu kazi anayoifanya ni kubwa sana. Ninaomba sana hili kwa sababu wenyeviti wetu wanafanya kazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nizungumzie suala zima la TARURA, nimpongeze Mheshimiwa Waziri na nimpongeze Mkurugenzi Mkuu wa TARURA Ndugu yangu Mhandisi Seff. Katika watu ambao mmepata katika usimamizi wa masuala hayo Mhandisi Seff ni mtu ambaye kwanza ni mkarimu, msikivu na anamsikiliza kila mtu, ukipeleka hoja yako hata kama hakuna pesa lugha atakayokwambia utaelewa. Ninaomba sana mtu huyu tuendelee kumlinda afanye kazi yake vizuri kwa sababu ametuwezesha katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishukuru Serikali, niliuliza swali hapa kuulizia wakandarasi ambao walikuwa hawajalipwa, leo hii ninaambiwa wameshalipwa na wamekwenda site katika barabara zote tano wako site. Hoja yangu ya msingi, Mheshimiwa Mabula amezungumzia suala la bajeti, kwa kweli tunapoangalia bajeti ya TARURA pamoja na kwamba Serikalini imeongezeka lakini kuna maeneo ambayo bado haijaongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano na ninaomba Waheshimiwa Wabunge mniwie radhi kwa mfano nitakaoutaja kama ni maeneo yenu. Ukiangalia Manispaa ya Ilala, tuseme ni Jiji, wanapata shilingi bilioni 29, Dodoma shilingi bilioni 20, Tanga shilingi bilioni sita, Mbeya shilingi bilioni nane, Nyamagana shilingi bilioni 4.6, Mabula aliisogeza juu tu na Ilemela shilingi bilioni tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Manispaa yenye mzunguko wa barabara 1,920, lakini inahudumiwa katika kilometa 875. Zinazobaki karibu 1,045 zote hazina huduma kwa maana hazina pesa. Tuzingatie barabara zile kwa kauli mbiu yetu ya ‘Ilemela ni yetu Tushirikiane Kuijenga’, wananchi walishirikiana na Mbunge wao kuhakikisha wanafungua kila kona ya mji ule, sasa hivi kokote unapita barabara zipo lakini tunaomba ziingie katika bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru kwamba kuna baadhi wameziweka lakini wameweka kilometa chache, ukiangalia Manispaa pamoja na mzunguko wote, lakini ina asilimia tano tu ya lami ambayo ni kilometa 43 katika hizo ninazozisema zaidi ya 1,900. Ninaomba tuangalie katika suala zima ambalo tunaweza kuona ni namna gani tutakuwa tunagawa bajeti hizi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakumbushia pia suala zima la ahadi ya Mheshimiwa Rais, alitoa ahadi tarehe 30 Januari, 2024 kujenga kilometa 12 za lami. Muda umekwisha hazijajengwa mpaka leo. Pasiansi – Lumala - Kiseke kilometa 3.7. Kahama – Isela – Ng’wang’wila kilometa 6.7. Barabara ya Mwika 0.5, Barabara ya Breweries 0.5, Barabara ya Kijiji Big Bite 1.2. zinaleta kilometa 12 hizi ni barabara ndogo ndogo sana ambazo zingejengwa zingeweza kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninamwomba tena Mheshimiwa Waziri pamoja na Mhandisi Seff na Waziri wa Fedha tuone namna bora ya kuweza kukamilisha jambo hili ili wale wananchi waone kwamba Mheshimiwa Rais alitoa ahadi na ahadi ile imetekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipongeza pia Serikali katika suala zima la uboreshaji wa miji. Manispaa ya Ilemela iko katika miji ambayo imepata bahati ya kuwa na miradi hiyo. Ninaishukuru tena Serikali imeweza kumlipa mkandarasi aliyepewa kujenga Soko la Kirumba pamoja na kilometa 2.9 za lami. Aliingia site mapema akawa hajalipwa, sasa hivi amepewa tunayo imani atarudi site. Ninaishukuru sana Serikali kwa hilo kwa sababu ni eneo ambalo ni la kimkakati na ni eneo ambalo lingeweza kuleta mapato ya kutosha katika Manispaa yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda kwenye ile miradi Green Smart Cities ambayo pia nasi tumebahatika katika suala zima la uboreshaji wa mialo ya Kirumba, New Igombe na Old Igombe. Upembuzi umeshafanyika toka mwaka 2022, lakini mpaka leo kazi haijaanza. Tukumbuke Soko la Kirumba ni Soko la Samaki la Kimataifa na ndilo linaiingizia Manispaa pesa nyingi, sasa upembuzi huo usiofikia mwisho lini kazi hii itafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi kubwa na nzuri inafanyika na Mheshimiwa Rais na Wizara, lakini tunapoacha mengine nyuma matokeo yake unakuta kwamba ile hali ya kuendelea kimaendeleo na kuwajaza wananchi mifukoni kwa sababu kwenye Wilaya yangu 87% ni maji na 23% tu ndiyo nchi kavu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo uchumi wa Ilemela unatagemea samaki, sasa tusipoboresha yale masoko wakaweza kufanya kazi yao vizuri Mheshimiwa Waziri tutakuwa pia tunawapunja hawa watu hatufanyi kazi yetu vizuri pamoja na yale yote mazuri wanayoyafanya. Ombi langu ni kuhakikisha kwamba haya yote yanafanyika katika utaratibu ili tuweze kusonga mbele katika hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii pia imefanya kazi moja kubwa na nzuri sana katika suala la ujenzi wa stendi. Stendi ya Mwanza nimekuwa nikiisema hapa ya Nyamhongoro ni stendi ambayo ni ya mfano. Kwanza, ni stendi ya mabasi, pili, ina hostel ya wasafiri wanaweza kulala, tatu ina gereji kwa ajili ya malori na nne ina storage kwa ajili ya mizigo. Stendi ile ni kama haitumiki vizuri kwa sababu inakuwa inatumika ndivyo sivyo katika ule uwezo wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo stendi pia ya Nyegezi ambayo nimekuwa nikizungumza sana, kwa sababu suala la usafirishaji mijini na kwenda katika mikoa mingine ni namna ya uratibu tu, kwa hiyo, ninaomba sana katika hizi stendi zote mbili basi tuone pesa ya Serikali, pale imekwenda zaidi ya shilingi bilioni 24, sasa return yake ni lazima ionekane katika kuona kwamba ile stendi zinafanya kazi kulingana na namna ambavyo Serikali ilikusudia kufanya. Ninaomba sana hili lifanyike kwa sababu nimekuwa nikilirudia mara kwa mara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la wafanyabiashara wadogo wadogo, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri pia amezungumzia hilo katika suala zima la kuratibu shughuli za wafanyabiashara wadogo wadogo katika kuwajengea mazingira mazuri. Serikali ilishaagiza halmashauri zote nchini na sina uhakika ni halmashauri ngapi mpaka sasa zimeshatenga maeneo kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo wadogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika yale pia kulikuwa na masuala ya kuweka industrial park ambapo ungeweza kuwaweka mafundi wa welding pale, watu wa kuchonga furniture na mambo mengine unawakuta katika centre moja, lakini sasa hivi unakuta wako maeneo mbalimbali. Pia, utulivu haupo, leo anaweza akahamishwa na kesho akafanywa hivi. Ninaomba sana hii itekelezwe kwa sababu ni sera ya Serikali kuhakikisha inawaweka mahali ambapo inaweza kuwahudumia kwa pamoja, basi hili litekelezwe kwa sababu wengi bado wanahangaika leo yuko hapa, kesho yuko hapa na hajui hatma yake ataishia wapi. Ninaomba sana hilo kwa sababu ni suala la Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru na kupongeza sana kwenye suala la mikopo ambayo kwa kweli ilikuwa imesimama kwa kipindi na sasa hivi imeboreshwa na watu wanatumia mfumo. Ninaomba sana bado elimu kwa wakopaji haijakaa sawa na bado masharti ya vikundi bado yanawabana. Kama mtu umeshamtambua ni mfanyabiashara mdogo na anajulikana alipo, kwa nini asipewe yeye kama yeye na akafanya shughuli zake? Habari za kuwaunganisha wengine wanaogopana kwa sababu wengine wamekuwa na tabia siyo nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata wale walioko kwenye vikundi wanapeleka maombi yao, lakini hawapati mikopo kwa wakati au pesa inakuwa haiutoshelezi kwa sababu tu hatujaweza kuwapa elimu wakajua. Wengine wanashindwa kujaza kwenye mifumo ile. Kwa hiyo, ninaomba sana elimu bado inatakiwa kwa watu hawa ili waweze kutumia ule mfumo vizuri na waweze kupata kwa sababu ni eneo ambalo tunaweza kuwafanya wanawake wengi na vijana wengi waweze kufanya kazi zao vizuri katika suala zima la kutii na kuweza kufuata taratibu za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala zima la kuona ni jinsi gani mambo yanakwenda vizuri katika Serikali za Mitaa, chaguzi zimefanyika ni kweli na tumekwenda vizuri na watu wameshinda vizuri, lakini sasa hivi ninataka kusema kwa sababu tuko kwenye mwaka wa uchaguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo Wabunge wengine wamesema, ninawaomba Wabunge tutulie kazi iliyofanyika ni kubwa na ya kutosha na ndiyo maana hata wanaokwenda kushughulia majimbo yenu hawakusemi wewe Mbunge hujafanya lipi kwa sababu kila kitu kiko site. Atatumia mbinu ya pesa na vizawadi vidogo vidogo lakini watu hawataki pesa na vizawadi wanataka kuona site kuna kitu gani na wote mmefanya kazi kubwa, hakuna ambaye hajafanya kazi kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Wabunge ni viungo wachezeshaji, tunacheza nane na sita, unapokea kutoka kwa Mheshimiwa Rais unawashushia huku chini mambo yanakwenda na Madiwani wanachukua wanashusha kule. Kwa hiyo, tusiogope kwa sababu tunajua tutarudi hapa Bungeni 2025 mwezi Oktoba sote tutakuwa hapa kwa kazi kubwa na njema ambayo Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita ameifanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais. Katika ile miradi ya kimkakati hususan iliyoko Kanda ya Ziwa ukiacha hayo maeneo mengine nchi nzima, lakini ninazungumzia ya Kanda ya Ziwa. Ukiangalia SGR sasa hivi ni karibu inaingia, iko 75%. Ukija kuangalia maeneo ambayo yalikuwa yamewekwa kwa ajili ya kusogeza huduma Sengerema kwa mwenzetu Mheshimiwa Tabasam, daraja lile limekamilika na mwezi Mei nadhani Mheshimiwa Rais anakwenda kulizindua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lile kwa TAMISEMI ni eneo la kimkakati kwa sababu maeneo yale yanahitaji kuboreshwa ili kuweza kufungua uchumi wa maeneo ya ng’ambo ya Ziwa ambako tayari barabara kiungo kitakuwepo kupitia njia ya maji, daraja la kilometa tatu ambalo halijawahi kutokea. Ni daraja refu katika suala zima la urefu wa madaraja kwa maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu, miradi hii yote ikiwa ni pamoja na ya Ziwa Victoria ninaiongea kwa sababu inaleta uchumi zaidi kwa Jiji la Mwanza na Mwanza ni hub ya Maziwa Makuu, tunahitaji kuona miradi hii inafanya kazi kwa tija ili iweze kuona kwamba namna gani tunaunganisha nguvu ambayo tayari Serikali imeiweka, lakini tunaiunganisha na uchumi wa wananchi wetu katika suala zima la kujiletea maendeleo. Miradi ile imekuja kimkakati lakini tayari inakwenda katika kuboresha maisha ya Watanzania kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho japo siyo kwa umuhimu, pamoja na kwamba hili ni la Wizara ya Maji, lakini ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais katika suala zima la uboreshaji wa maji katika Manispaa ya Ilemela. Nililisema hili wakati ninaongea kwa Waziri Mkuu, sasa hivi watu wako site wanakwenda kutengeneza tena miundombinu mingine kwa maana ya kuwa na chanzo kingine cha maji eneo la Kabangaja, Mkandarasi ameshapatikana kwa sababu watu walikuwa wanashangaa maji yako Ziwa Victoria, lakini hawayapati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona nichukue fursa hii kuishukuru Serikali kwa namna ambavyo imeendelea kuboresha huduma za jamii katika maeneo yetu, mambo ya shule na afya sikutaka kuyarudia kwa sababu tayari tulishayasema, lakini kwa suala la maji lililokuwa na changamoto ninaishukuru sana Serikali kwa sababu tayari huduma ile inaanza kufanyiwa kazi na wananchi tayari watakwenda kufaidika nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kuunga mkono hoja na kuipongeza sana Wizara. Mtu kazi Mjukuu wangu tembelea Ilemela uone namna ambavyo Serikali imefanya kazi nzuri na pengine ninaweza kuwa nimependelewa kuliko wengine. Karibu uje uone kazi ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia, ahsante sana. (Makofi)