Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukoba Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. STEPHEN L. BYABATO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa mimi na wengine wote uhai, afya na kuendelea kuyaona mema yanayoendelea kutokea hapa nyumbani Tanzania. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia, kumshukuru Daktari Samia Suluhu Hassan kwa kazi inayoendelea kufanyika, ambayo kila mmoja hapa amesema na kila eneo linahitaji kusemewa, lakini muda hautoshi. Kwa hiyo, kwa ujumla tuseme ameupiga mwingi na umemwagika, tumeukingia huku chini, ili usimwagike ukatuacha kwa sababu, bado tunauhitaji. Niipongeze Serikali yote kwa ujumla, ambayo anafanya nayo kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mahususi nimpongeze na kumshukuru kaka yangu Mheshimiwa Mchengerwa, pamoja na Manaibu Waziri wake wote wawili kwa usikivu na utendaji mwema. Nirudi nyumbani na kumshukuru sana Mkuu wangu wa Wilaya, Mheshimiwa Erasto Sima, Mkurugenzi wa Halmashauri kaka yangu Jacob Nkwera, Mstahiki Meya Godson Rwegasira Gibson pamoja na watendaji wengine wote tunaofanya nao kazi. Pia, upande wa chama kwa kuendelea kusimamia utekelezaji wa ilani na mpaka tukafikia sehemu Bukoba Mjini ya sasa siyo ile ya zamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengi ya kusema yatashindikana kwa sababu ya muda.  Nimeamua nichukue maeneo mawili ambayo ni ya kiuchumi na kiuwekezaji kwa sababu ya nature ya Mji wa Bukoba kuwa na mambo mengi mazuri. Nitapenda kusema mambo makubwa mawili; kila eneo TARURA, afya, elimu na maeneo mengine yote kama walivyosema wenzangu yameguswa, lakini ninaomba kwa leo nizungumzie mambo mawili makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, ninamshukuru sana Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuamua sasa ile ndoto ya muda mrefu ya ujenzi wa soko la kisasa kubwa kwa Bukoba Mjini, ujenzi wa stendi kubwa ya kisasa, ujenzi wa kingo za Mto Kanoni, ujenzi wa barabara zaidi ya kilomita 10 na uwekaji wa taa zaidi ya 400 katika Mji wa Bukoba Mjini sasa lifanyike. Dkt. Samia ametupatia fedha takribani shilingi bilioni 47, kwa ajili ya miradi hii kutekelezwa. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nimshukuru kaka Mchengerwa, nilimletea kilio na akanichukulia serious kama kawaida yake. Mwaka juzi, Desemba, akaja Bukoba Mjini kwa ajili ya kusaini mkataba wa kupata consultancy wa kusanifu miradi hii yote kwa upande wa Kanda ya Ziwa na maeneo mengine na baraka hizo tumeanza kuzipokea sasa kwa kuwa, wakandarasi wanakaribia kupatikana na miradi itaanza kujengwa. Hii ni miradi ya kihistoria na italeta faraja kubwa ya kiuchumi, italeta mabadiliko na mageuzi makubwa sana kwetu sisi. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kutumia nafasi hii kuwashukuru sana Wanabukoba kwa moyo waliouonesha katika kipindi hiki ambacho Dkt. Samia ni Rais, mimi ni Mbunge. Wananchi wakiongozwa na Madiwani kwenye maeneo yao wametoa ushirikiano mkubwa. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukisikia maeneo mengine wakitaka kujenga soko inabidi ndumba zifanyike, masoko yachomwe, watu wapigwe viboko, lakini kwa Bukoba Mjini ya safari hii, chini ya uongozi wa Dkt. Samia na mimi msaidizi wake, mambo ni shwari kabisa. Wafanyabiashara wa soko tumewaelimisha, tumewaomba, wamehama wenyewe, wametoka kwenye soko litakalojengwa, wameenda kwenye maeneo mengine. Ninawashukuru na ninawapongeza sana, nawaahidi tutaenda kusherehekea kuanza kwa ujenzi wa soko pia, kwa kupokea miradi mikubwa ya namna hii. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, lilikuwa ni jambo la ndoto kabisa kwamba, ipo siku Bukoba Mjini tutafikia sehemu miradi ambayo imesemwa, imeimbwa, imezaliwa kwa miaka mingi sana, haitofanyika, lakini sasa inafanyika na bila watu kutoana damu, bila watu kupigana ngumi, bila watu kufanya chochote. Akili za kisasa zimetumika na tumefanikiwa, wenzetu sasa wamehama na wako tayari kupisha ujenzi wa Miradi ya TACTIC. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwenye hili eneo nishauri jambo kwa Mheshimiwa Mchengerwa. Ninashukuru amekubali kuja kusaini mikataba ya wakandarasi watakaokuja kujenga miradi hii kwenye maeneo yetu. Ninamshukuru sana na namtarajia mwezi Mei, yeye au pengine kiongozi mkubwa zaidi, kuja kushuhudia utiaji wa saini wa miradi hii, lakini naomba atoe maelekezo mahususi ya namna ya utekelezaji wa miradi hii kwa best practice ambazo wamezipata, kama TAMISEMI, kutoka Tier one na sisi Tier two, ili watu wai-own na kuitekeleza vizuri kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine la pili, sisi Bukoba Mjini tumepata zaidi ya shilingi bilioni 10, kwa ajili ya kutengeneza mradi wa kimkakati wa kuwaweka wenzetu wamachinga. Mji wa Bukoba unakuwa machinga ni wengi sana na hizi kilomita kumi ambazo zitajengwa na Mradi wa TACTIC zitawafanya wakose maeneo ya kufanyia biashara, ambapo imezoeleka ni pembezoni mwa barabara. Kwa hiyo, tumeiomba Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, imekubali kutupatia zaidi ya shilingi bilioni kumi, kwa ajili ya ujenzi wa kitega uchumi cha wenzetu machinga katika eneo linaloitwa Kishenge na eneo la Machinjioni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari mambo mengine yameendelea kwa hatua za awali, tumezikamilisha, sasa ninaomba barua ambayo umewaandikia hazina kutupatia shilingi bilioni na milioni mia mbili, kwa ajili ya kuanza kazi za awali, tumeiona. Tunawaomba watu wa hazina mtusaidie kutupatia fedha hiyo katika mwaka huu wa fedha, ili hizi shughuli za awali ziweze kuanza. Kwa Mji wa Bukoba machinga ndio kipaumbele chetu kwa sababu, ni eneo la mjini tunahitaji kuwaweka katika maeneo mazuri ambayo watafanya biashara zao kwa kupata kipato na kuendeleza kukuza uchumi wa eneo letu. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine moja ambalo nimeona niliseme ni eneo la ajira. Tunafahamu kila eneo, wenzangu wameshasema, tuna upungufu wa watumishi, lakini ni kwa sababu ya ongezeko la miundombinu kwa maana ya elimu, kwa maana ya afya na maeneo mengine. Sasa naomba kushauri, ni eneo ambalo wenzetu wa utumishi watalifanyia kazi, lakini TAMISEMI pia, inahusika kwa sababu, ina waajiriwa wengi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kama ninayo shule kuna walimu wa kujitolea, wanajitolea kwenye eneo hilo, atakapopata ajira ninashauri na kupendekeza eneo la kipaumbele la kwanza la kupewa ajira liwe eneo lile ambalo alikuwa anajitolea. Hakuna haja ya kuwa anajitolea shule A halafu nikipata ajira napelekwa shule nyingine ambapo hapakuwa panahitaji mtu anayejitolea kwenye eneo hilo. Kwa hiyo, tuwabakishe watu kwenye maeneo ambayo walikuwa wanajitolea kwa sababu, eneo hilo lina uhitaji mkubwa wa kupata watu wa namna hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu, muda unakimbia, kama walivyotangulia kusema wenzangu, miradi hii ndiyo ambayo inatufanya sisi tutembee kifua mbele, tujidai na tuone kwamba, tayari mambo yamekamilika. Sisi kwa Bukoba Mjini hatuna uongo, hatuna deni, hatuna ugomvi na Mheshimiwa Daktari Samia Suluhu Hassan, kwanza, sisi Wabunge na wajumbe wengine wa Mkutano Mkuu tangu Januari, tulishamaliza. Sasa slogan ya kwetu, kama nilivyowahi kusema, wanasema wanaotaka kuwa Mbunge wa Bukoba Mjini mambo ya Dkt. Samia tumeshamaliza, atuambie miujiza gani atakayokuja kufanya hapa ambayo mtoto wetu Byabato imemshinda kwenye mazingira ambayo tuko nayo hapa. (Makofi).
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kusema tuendelee kutembea kifua mbele. Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, kaka yangu Balile, ameandika makala nzuri kabisa kwenye Gazeti la Jamhuri kueleza yale yaliyoshindakana, sasa yanawezekana na ni watu ambao wanaona changamoto tulizozipitia. Kwa hiyo, niwaombe tuendelee kumuunga Dkt. Samia mkono na sisi tujihimize wenyewe na kusimama imara tukiamini kabisa kwamba, ushindi unaokuja ni wa kishindo na ni kupiga kura za Daktari Samia, kupiga kura za Wabunge wa CCM na Madiwani wa CCM, halafu chama kiendelee kuisimamia Serikali, tuendelee kusonga mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa nafasi hii ndogo niliyoipata. Mambo ni mazuri, Mwenyezi Mungu atubariki sote tukutane hapa Mwezi Novemba, inshallah.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)