Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Buhigwe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru kwa kunipa fursa hii ili kuchangia kwenye Bajeti hii ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu, muumba wa mbingu na nchi kwa kunijalia afya ya roho na mwili na kunifikisha siku ya leo na kusimama mbele ya Bunge hili Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nitoe pongezi na kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wa Rais Dkt. Philip Isdor Mpango kwa miradi mingi ambayo wametuletea katika Wilaya yetu ya Buhigwe. Shukrani za pekee zimfikie Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa, Waziri wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI na wasaidizi wake wawili, Mheshimiwa Zainab Katimba na Mheshimiwa Dkt. Festo Dugange, tunawashukuru sana kwa ushirikiano na kwa miradi mingi ambayo wametupa Wilaya yetu ya Buhigwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, shukrani nyingine za pekee ziende kwa Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wetu wa Kigoma, Thobias Andengenye, kwa kazi kubwa ambayo anaifanya kusimamia miradi katika Wilaya yetu ya Buhigwe. Nitumie nafasi ya pekee kumshukuru Mkuu wangu wa Wilaya, Kanali Michael Masara Ngayarina na Ndugu Mbilinyi, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya yetu ya Buhigwe, kwa kusimamia miradi yote na kufanikiwa kukamilika. Hakika Wilaya yetu ya Buhigwe tunasonga mbele, tunashukuru sana na ninawashukuru watendaji wote walioko katika Wilaya ya Buhigwe kwa mshikamano na utendaji mzuri wa kazi za ujenzi wa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuchangia kwenye Idara ya Afya. Kwanza nitumie nafasi ya pekee kushukuru katika miaka hii mitano tumefanikiwa, Serikali imetujengea vituo vitatu vya afya, Kituo cha Afya cha Mwayaya, Kajana na Lusaba. Bado tuna vituo ambavyo havijapata fedha ambapo tuna kata za kimkakati za Mkatanga, Muhinda, Kilelema, Kinazi na Mnyegela. Tunashukuru kwa miradi hii mitatu ya vituo vya afya, ambayo imekamilika na tunashukuru kwa ujenzi wa zahanati saba ambazo zimekamilika. Huduma zimeshaanza kutolewa, tumepata watumishi, tumepata dawa na vifaa tiba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo bado tuna changamoto na ninaomba Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa anisikilize na anisaidie. Kwenye Hospitali yetu ya Wilaya ya Buhigwe hatuna kabisa wataalam wa mionzi pamoja na kupata vifaa tiba. Tuna x-ray na ultrasound hizi ambazo tumeletewa kwenye hospitali ya wilaya na kwenye vituo vitatu vipya vya afya, lakini hatuna mtaalam hata mmoja. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tuna x-ray mbili, hospitali ya wilaya na Kituo cha Afya cha Mwayaya, mpaka muda huu hatuna mtaalam hata mmoja na x-ray hii haitumiki. Tuna ultrasound nne, hospitali ya wilaya moja, Kituo cha Afya cha Janda moja, Munzeze moja na Muyama moja, lakini hatuna mtaalam hata mmoja hizi ultrasound mpaka dakika hii hazitumiki. Ninaomba kwa moyo wa dhati tupatiwe kwa haraka sana wataalam wa mionzi, ili ultrasound na x-ray tulizozipata ziweze kutoa huduma katika wilaya yetu. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo tunao upungufu mkubwa sana wa nyumba za watumishi kwenye vituo vya afya na zahanati hizi saba ambazo zimekamilika. Kwa ujumla tuna uhaba mkubwa sana wa watumishi kwenye afya na ustawi wa jamii. Tuna upungufu wa watumishi 476 katika ajira zitakazoendelea kutolewa. Tunaomba sana kwa dhati na kwa moyo mmoja watuletee watumishi, ili waweze kutoa huduma katika zahanati hizi zilizokamilika na vituo hivi vitatu vya afya vilivyokamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye Idara ya Elimu. Tunashukuru sana tumepata miradi mikubwa na tumefanikiwa kujenga sekondari saba ndani ya miaka hii mitano. Tunamshukuru sana Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo ameifanya. Tumepata fedha za ujenzi wa madarasa katika shule za msingi, tunashukuru sana. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio bado tunazo changamoto, tunao upungufu wa watumishi idara ya elimu. Kwa ujumla idara ya elimu ya awali na msingi tuna upungufu wa watumishi 1,025 na kwa upande wa elimu ya sekondari tuna upungufu wa watumishi 119. Tunaomba kwa jicho la huruma tupatiwe watumishi wa shule ya awali, msingi na sekondari ili waweze kuja kutoa huduma hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo wilaya yetu inayo changamoto ya kuwa na shule nyingi ambazo ni shule kongwe zinazohitaji ukarabati. Tunaomba kwa moyo wa dhati kabisa shughuli zifuatazo ziangaliwe kwa jicho la huruma, zipatiwe fedha, kwa ajili ya ukarabati, ni shule ambazo zina umri zaidi miaka 50. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, shule zifuatazo zinahitaji ukarabati wa haraka; Shule ya Msingi Muhinda, Kibande, Nyamugali, Nyamasofu, Kitambuka, Nyakimue, Musagara, Kirungu, Kibwigwa, Mwayaya, Nyaruboza, Songambele, Mbanga, Kajana, Murela na Katundu. Tunahitaji fedha za ukarabati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nihamie kwenye upande wa TARURA…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Felix muda wako umeisha. Tafadhali hitimisha.
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Ninaunga mkono hoja iliyoko Mezani, ahsante. (Makofi)