Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JANETH M. MASSABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kunijalia uhai na afya njema, pamoja na familia yangu na ndugu zangu wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kutoa salamu za pole kwa kuondokewa na Baba Mtakatifu, Papa Francis. Mwenyezi Mungu ampe pumziko la amani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema kwamba, amani inaanza kwenye nafsi ya mtu, nafsi ya mtu inaambukiza kwa watoto, nafsi ya watoto inaambukiza kwa jamii na baadaye inaenda kwenye nchi. Kwa hiyo, kila mmoja hapa tutafute nafsi za roho, tuwe na utulivu wa ndani na tufanye kazi kwa kuongozwa na Mwenyezi Mungu, tusipende kutumia akili zetu, tuongozwe na Mwenyezi Mungu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kumpongeza sana Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi nzuri anayoifanya. Nimpongeze Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Naibu Waziri Mkuu na hususan Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Kiujumla nawapongeza Mawaziri wote, Makatibu Wakuu na Watendaji wa Serikali, Ilani hii imetekelezwa kwa ushirikiano wa pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie pia, fursa hii kuwapongeza Wabunge, mawazo na maoni yao, Mheshimiwa Rais na watendaji wameyafanyia kazi na ndio maana tunaona maendeleo ambayo yanatokea kwenye nchi yetu. Hongera sana kwa Wabunge, wamechukua mawazo ya wananchi wakayaleta hapa hongera, Madiwani wamechukua wakayaleta yakachakatwa, yakafanyiwa kazi na Mheshimiwa Rais ni mwepesi sana wa kusikiliza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nipo Kamati ya Hesabu za Serikali, tumetembea sisi, tumeona kwa macho. Mambo tuliyokuwa tunayaona huwezi kuamini kama ni Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amechukua madaraka kutoka kwa Marehemu Mheshimiwa Dkt. Magufuli, Mwenyezi Mungu amrehemu. Amechukua wakati mgumu, na amepata mapingamizi makubwa sana, lakini Mwenyezi Mungu ameisimamia nchi hii na akamwongoza, akampa hekima akachagua viongozi wasaidizi wake ambao wamemsaidia kwa uaminifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kuwasema wachache. Makatibu Wakuu kwa ujumla nimewatamka, lakini nimzungumzie Msajili wa Kampuni, Ndugu Nehemiah Mchechu, ni mtu mzuri sana, ni mtendaji mzuri sana. Nije kwa Engineer Victor Seff; tuko kwenye hii bajeti ya TAMISEMI (TARURA). Amefanya kazi kubwa, ni msikivu na mnyenyekevu. Nasema, heri matiti aliyoyanyonya. Nampongeza mama yake na wazazi wake kwa kumlea katika maadili mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Prof. Ole Gabriel, Mtendaji Mkuu wa Mahakama Kuu. Huyu ni kati ya watendaji makini sana katika nchi hii. Wapo kadhaa, nashindwa kuwataja kwa kuwa muda sina, lakini wako watendaji wazuri katika nchi hii, wamefanya kazi njema na ya uaminifu. Mwenyezi Mungu awalinde. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na michango ya Waheshimiwa Wabunge, watu wamesema kwamba tunamsifia Rais sana kwamba yeye ndiye sijui amefanya. Waheshimiwa Wabunge lazima wamsifie kwa sababu wametoa mawazo na Mheshimiwa Rais amesikia, ametoa fedha na maendeleo yamepatikana. Ukitaka kumjua vizuri Rais Samia na kumwelewa vizuri, nenda kaangalie Bwawa la Mwalimu Nyerere. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitaka kumtambua Rais Samia, nenda kaangalie Daraja la Kigongo - Busisi, ukitaka kumjua kwa undani wake, nenda Daraja la Pangani; ukitaka kumjua Rais Samia, nenda kaangalie Barabara za Mwendokasi zinavyokwenda kasi katika Mkoa wa Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Daraja la Tanzanite, kuna madaraja mengi pale, yale madogo madogo kama vile Chang’ombe, Kurasini, daraja kutoka Bendera Tatu kwenda mpaka Gerezani; Dar es Salaam inabadilika. Nani kama Samia? Jamani, leo mimi nasema, kwamba kwenye utekelezaji wa Ilani mama huyu ametekeleza kwa kiwango kikubwa, anastahili kupewa nafasi tena na ana uwezo. Tunaomba tumpe heshima yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Bunge hili, namwomba Mwenyezi Mungu ampe Mama Samia kibali ili aweze kuendelea kushika usukani katika nchi hii, awe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mwaka huu wa 2025. Nawaombea Wabunge wote Mwenyezi Mungu akawatetee waweze kurudi. Tuiombee nchi yetu iendelee kuwa nchi ya amani, kwani hatuna mahali pa kwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mama Tanzania ndiyo nchi yetu, na tuendelee kuishi katika lugha ya staha, tusiende lugha ya kubishana. Twende kwa staha kwa sababu wanakwambia Mwenyezi Mungu huwa anaongea kwa utaratibu, nasi tukiwa tuna lugha kali tutakuwa hatuwezi kusikilizwa na Mwenyezi Mungu, lazima tuwe na utaratibu; tuvumiliane, tusameheane. (Makofi)  
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije na ombi kidogo. Pale Dar es Salaam eneo la Kitunda mpaka Kivule barabara yake ni chafu sana. Najua iko kwenye Mpango wa Ujenzi kwenye Mradi wa DMDP, lakini kwa sasa hivi angalau waweke changarawe ili watu waweze kupata kwa kipindi hiki ambapo Mkandarasi anafanya ujenzi, kwa sababu ujenzi utachukua kama miezi kadhaa, hivyo iwe katika kipindi hiki ili wananchi waweze kupita kwa usalama. Tunaomba ujenzi Mradi wa DMDP uanze kwa kasi katika maeneo ambayo yameainishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kupoteza muda, leo nilisema nitaongea kuhusu ilani tu. Kuna shule kongwe pale zipo Kata ya Mabibo zinaitwa, Shule ya Kawawa na Shule ya Amani Karume. Zile shule ni kongwe, na zimechukua majina ya waasisi wetu. Naomba zifanyiwe ukarabati wa haraka, na siyo vipande vipande, ili wanafunzi wetu na walimu waweze kufanya kazi kwa utulivu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia Kituo cha Magufuli kiweze kukamilika kwa ukamilifu kama kilivyopangwa na kiweze kutumika kwa kadri kilivyopangwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii tena kuwashukuru sana wanawake wa Mkoa wa Dar es Salaam ambao walinipa ridhaa. Nawaomba waendelee kuniombea kwa Mwenyezi Mungu. Mimi nipo pamoja nao, nawaombea wawe na afya njema na Mwenyezi Mungu awape haja ya mioyo yao. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nawashukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)