Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bagamoyo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi hii. Kwanza kabisa napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata wasaa huu wa leo kuchangia hii Wizara ya TAMISEMI. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mchango wangu utajikita zaidi katika kupongeza pamoja na kuisifia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mama yetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amefanya mambo makubwa sana. Leo hii katika majimbo yetu yale yote ya msingi ambayo tulikuwa tukiyaomba katika Serikali yake kwa asilimia kubwa tumefanikisha. Kwa kweli yapo machache yaliyobakia, lakini mengi yamefanikisha. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, Ndugu yangu Mohamed Mchengerwa (MMK - Mchengerwa Mtu Kazi). Kwa kweli, anafanya kazi kubwa sana katika hii Wizara na pia napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru na kumpongeza au kuwapongeza Manaibu Waziri wake Bwana Dugange pamoja na dada yangu Mheshimiwa Katimba kwa kazi wanayoifanya. Wamekuwa ni watu ambao wana ushirikiano mkubwa sana kwetu sisi Wabunge pale tutakapokuwa tunawafuata kwa ajili ya mambo mbalimbali. Kwa kweli nawapongeza sana kwa kazi kubwa wanayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nawapongeza viongozi wote wa Wizara, kuanzia Katibu Mkuu na timu yake kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya. Nichukue pia fursa hii kumpongeza Mkuu wangu wa Mkoa wa Pwani, Alhaji Abubakar Kunenge kwa kazi kubwa ambayo anaifanya. Kwa kweli, Mkoa wa Pwani sasa hivi umekuwa Mkoa ambao umepaa kimaendeleo kutokana na kazi anayoifanya pamoja na uongozi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia namshukuru Katibu Tawala wa Mkoa, ndugu yangu Mchata, naye anafanya kazi kubwa, anapambana kwa ajili ya kuineemesha Pwani. Nawashukuru sana. Hali kadhalika, napenda kutoa shukurani zangu za dhati kwa Mkuu wangu wa Wilaya ya Bagamoyo. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia natoa shukrani zangu za dhati kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo. Kwa kweli, huyu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo anastahili sifa sana. Namwomba Mheshimiwa Waziri amwangalie kwa jicho la pili Mkurugenzi huyu kwa namna anavyoisaidia Bagamoyo. Bagamoyo wakati anakuja mwaka 2022 mapato yetu yalikuwa shilingi bilioni 3.8. Leo hii Bagamoyo tumefikia hatua ya kukusanya mapato kiasi cha shilingi bilioni 7.6. Hii ni kazi kubwa sana ambayo anaifanya Mkurugenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nawapongeza sana Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Bagamoyo kwa kazi kubwa wanayoifanya chini ya usimamizi wa Mwenyekiti wetu Mohamed Usinga. Wanafanya kazi kubwa sana. Maendeleo haya yote yamepatikana kwa ajili yao, nasi pamoja na Mheshimiwa Rais ambaye anatu-support huko juu pamoja na ninyi viongozi wetu wa Wizarani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli kazi kubwa inafanyika. Nisisahau kuwashukuru pia viongozi wangu wa Chama cha Mapinduzi ngazi ya Wilaya pamoja na ngazi ya Mkoa, wanafanya kazi kubwa sana ili kuhakikisha kwamba Bagamoyo tunakuwa na maendeleo ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie mafanikio makubwa ambayo yamepatikana katika sekta mbalimbali. Nianzie sekta ya elimu. Wakati mimi ninaanza Ubunge baada ya Mama Samia kuingia madarakani, kuna baadhi ya kata hazikuwa na Shule za Sekondari. Leo hii Jimbo la Bagamoyo ndani ya kipindi cha uongozi wa Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan tumepata shule za sekondari mpya tano. Hii haijapata kutokea, kwa sababu kata kama Nianjema ambayo kimsingi haikuwa hata na shule moja ya sekondari, sasa hivi zimejengwa shule mpya za sekondari mbili kwa mpigo. Haya ni maendeleo makubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna sekondari mpya katika Kata ya Mapinga, ambapo hapo mwanzoni kulikuwa na sekondari moja, idadi ya watoto ilikuwa kubwa. Kwa hiyo, tukapatiwa sekondari nyingine pale. Kwa hiyo, ni mafanikio makubwa sana. Vilevile tuna Kata ya Makurunge ambapo watoto walikuwa wanatembea umbali mrefu, takribani kilomita 17 kufuata elimu. Leo hii Shule ya Sekondari Makurunge imejengwa na watoto wetu wanasoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haitoshi, katika Kata ya Yombo kulikuwa na Shule ya Sekondari na tumeongezewa shule nyingine ya pili ya sekondari katika Kijiji cha Chasimba. Ni juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali. Pamoja na hayo, nashukuru, kuna shule yetu moja ya Miembe Saba imepandishwa hadhi kuwa shule ya Kidato cha Tano. Pongezi kubwa sana kwa Serikali pamoja na Wizara ya Mheshimiwa Mchengerwa. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, tuna shule ya amali ambayo inaendelea kujengwa na muda siyo mrefu itamalizika. Hizi ni juhudi kubwa zinazofanywa kwa ajili ya kuwaandaa watoto wetu kwa ajili ya mafunzo mbalimbali katika taaluma ili waweze kuja kujitegemea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiachilia mbali shule za sekondari, tuna shule za sekondari takribani saba ndani ya kipindi hiki ambazo zimepatikana katika Jimbo la Bagamoyo. Kwa hiyo, ni juhudi kubwa ambazo zinafanyika na Mheshimiwa Rais pamoja na Serikali yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta ya afya, tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa mbayo anaifanya. Bagamoyo leo hii tumepata fedha zaidi ya shilingi milioni 900, hospitali yetu kongwe ya Bagamoyo sasa hivi inang’ara, imekarabatiwa, siyo ile hospitali ya mwaka 1957. Tumepata jengo jipya la EMD, tumepata ambulance mbili. Hizi ni juhudi kubwa ambazo zimefanywa na Serikali ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi katika suala la miundombinu ya barabara… 
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Muharami muda wako umeisha, tafadhali naomba hitimisho.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, basi naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)