Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kalambo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa ili nami niwe miongoni mwa wachangiaji wa hotuba yetu ya Wizara ya TAMISEMI. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema kwa kunijalia afya njema nami kusimama leo. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuunga mkono hoja, nisije nikasahau. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba kwa moyo wangu wa dhati nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi njema ambayo anaifanya kwa Watanzania. Kila mwenye macho anaona, na kama haoni, basi atahadithiwa na jirani yake. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi nyingine naomba nizipeleke kwa Mheshimiwa Waziri, Manaibu wake, Katibu Mkuu na Makatibu Wakuu kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya katika kuhakikisha kwamba maendeleo yanakwenda kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitaka kusema yaliyofanyika katika Jimbo na Wilaya ya Kalambo, ni mengi. Kwa uchache naomba nianzie na TARURA. TARURA imekuwa ikifanya kazi nzuri nasi sote tunaweza kushuhudia jinsi ambavyo TARURA imekuwa ikifanya kazi nzuri. Walipoanza na walipofikia sasa hivi, hakika hata maombi ambayo yanakwenda kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge wakiomba barabara zipandishwe hadhi ili zitoke kwenye TARURA, yanazidi kupungua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tafsiri yake ni kwamba TARURA imejiimarisha. Ninachoomba ni kuwa, Serikali iendelee kuiongezea fedha ili wafanye kazi nzuri. Katika Jimbo langu la Kalambo, kipindi kile Mheshimiwa Waziri alipokuja na Mheshimiwa Rais, katika maeneo ambayo wamefanya vizuri, ni kujengwa kwa daraja la mfano ambalo kwa bahati nzuri limejengwa na wakandarasi Watanzania. Kwa jinsi ambavyo limejengwa katika kiwango kile, unaweza ukadhani labda limejengwa na Wachina. Hongera sana TARURA. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Watanzania wanaweza wakiwezeshwa. Tuna kila sababu ya kuhakikisha kwamba tunaijengea uwezo TARURA ili waweze kufanya vizuri. Wamefanya katika Mto Kalambo. Pia daraja la pili ambalo limejengwa kwa kutumia mawe na matofali, ni mifano ambayo TARURA wamefanya vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kazi nzuri ambayo TARURA wameianza kwa ajili ya kufungua barabara kutoka Mpombwe kwenda Kipwa ambapo ni mpakani mwa Tanzania na Zambia kwa kupitia Ziwa Tanganyika. Wameleta fedha na kazi imeanza. Hata hivyo zimebaki kilomita kama 12. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ile tunaijenga kwa mawe, na nimekuja kwa Mtendaji Mkuu, Ndugu Seff, tafadhali sana naomba twende tukamalizie kipande kile ili fedha ambayo imeletwa na Serikali isije ikaonekana imetumika, lakini imeshindwa kufikia lengo ambalo tulitarajia ili wananchi wa Kipwa waweze kusafiri badala ya kutumia usafiri wa maji ambao siyo wa uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba niongelee suala zima la afya. TAMISEMI kwa upande wa afya wamefanya vizuri, hongereni sana. Sisi wananchi wa Kalambo tunajivunia uwepo wao na kazi nzuri ambayo wanaifanya. Hivi karibuni nimepata taarifa kwamba katika vile vituo vya kimkakati nimepata ku-confirm kwamba eneo ambalo nilikuwa nimechagua kama Mbunge kwa ajili ya kujenga Kituo cha Afya Katete, fedha zipo njiani zitakwenda, shilingi milioni 250. Hongera sana kwa TAMISEMI. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Pia ninaomba niunganishe hili na jambo zuri ambalo lilitamkwa alipokuja Waziri wa Mipango, kwamba sisi kama Taifa tuna kila sababu ya kuhakikisha kwamba tunatumia rasilimali zetu ili kusaidia Watanzania. Ni nini ninachomaanisha? Tuna kiwanda chetu pale Kibaha kwa ajili ya kuua mazalia ya mbu. Tukipigana na kuhakikisha kwamba tunamaliza mazalia yote ya mbu, maana yake ni kwamba tutakuwa tumemaliza Malaria Tanzania. Hili linawezekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati nzuri, namna pekee ya kuweza kujibu haya ambayo yanatoka kwenye Mataifa mengine ambayo tumekuwa tukitumia vyandarua, sasa fedha ile ambayo imekuwa inatumika kwa ajili ya kununua vyandarua na ambayo imekuwa ikitumika kwa ajili ya kuwatibu Watanzania wanaopata maambukizi ya Malaria, fedha hii yote naomba Mheshimiwa Waziri aelekeze halmashauri zetu zote kuhakikisha kwamba wanatenga fedha, wananunua dawa na tuhakikishe kwamba Tanzania inakuwa ni free zone, hakuna Malaria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana kiwanda kipo, majirani zetu wamekuwa wakitumia sana. Ni wakati mwafaka sasa, sisi Watanzania tuseme kwamba Tanzania tutahakikisha kwamba Malaria haitakuwepo kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo naomba nipongeze, TAMISEMI wameanzisha utaratibu mzuri, wana Mfumo wa TAUSI.  Sasa kumekuwa na majaribio, kuna kipindi kingine kodi kwa ajili ya nyumba (Property Tax) kuna kipindi imekuwa ikiondolewa pale ambapo TAMISEMI inaonekana kwamba uwezo wao wa kukusanya ni mdogo. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nawaomba, kutokana na utaratibu huu walionao na mfumo walionao waende wakahakikishe kwamba wanakusanya kodi ya majengo zaidi ya TRA, na kwa sababu wanayo mifumo mpaka chini, naomba jambo hili likafanyike. Wana watendaji wa vijiji na wana network ambayo iko kila mahali, ili Serikali Kuu wajue kwamba TAMISEMI inao uwezo mkubwa wa kukusanya pale ambapo wanaenda kukusanya Property Tax, na itumike kwa ajili ya kuleta maendeleo kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninaomba niwakumbushe, wakati Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuja katika Jimbo letu la Kalambo, mwaka 2020, alituahidi kujenga Kituo cha Afya Kasanga pale. Sasa jambo hili limekuwa likijirudia, na sasa hivi inafika miaka mitano. Sasa naomba, kwa kuwa tumeshatenga eneo kwa ajili ya kujenga Kituo cha Afya Kasanga kule, basi katika kutazama maeneo ya kupelekewa fedha hata kidogo, nasi tukumbukwe. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini wakati Mheshimiwa Mchengerwa alipofika Kalambo, alikuwa anapata upepo wa bahari, kwa maana ya Ziwa Tanganyika. Kule ndiko tunakotaka kikajengwe kituo cha afya ili kutimiza ahadi ya kiongozi wetu. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba msituchonganishe, jambo hili linawezekana. Naomba mjipigepige ili wananchi wa Kalambo wafurahie utendaji uliokuwa mzuri wa Mheshimiwa Rais, na Chama cha Mapinduzi kinaenda kushinda pasi na mashaka kwa sababu yanayofanyika hakuna mtu ambaye anauliza, yapo dhahiri shahiri. (Makofi) 
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niunge mkono hoja. Ahsante sana kwa fursa.