Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nkenge
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nashukuru kwa nafasi ambayo umenipatia hii siku ya leo kuchangia katika Bajeti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuipongeza Serikali yetu ambayo inaongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, hasa kwa ongezeko la bajeti kama ambavyo imewasilishwa katika Hotuba ya Mheshimiwa Waziri ya kutoka shilingi trilioni 7.01 mwaka 2020/2021 kwenda shilingi trilioni 10.5 mwaka 2024/2025.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kwa huu mwaka wa fedha ambao tunajadili bajeti, tumeona kuongezeka kwa Bajeti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwenda shilingi trilioni 11.73. Ni pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa ni mwanamageuzi na mbeba maono wa nchi yetu kuhakikisha kwamba, anatatua changamoto zote ambazo zipo kwa wananchi kupitia hii Ofisi yake ya TAMISEMI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza pia wasaidizi wa Mheshimiwa Mchengerwa yeye akiwa ndio pilot na kinara mkubwa katika Wizara hii; Naibu Mawaziri wote wawili, Mheshimiwa Dkt. Festo Dugange, na Mheshimiwa Zainab Katimba ambao wamekuwa wakimsaidia kwa weledi mkubwa na wakati mwingine kufika katika maeneo yetu kuona kwa macho na kuweza kutatua matatizo au changamoto wakiwa site. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua hawa Viongozi wa Wizara hawawezi kufanya kazi peke yao. Nampongeza na kumshukuru Katibu Mkuu wa Wizara hii, kaka yetu Adolf Ndunguru na Naibu Makatibu Wakuu watatu tukiwa na Eng. Rogatus Mativila na Sospeter Mtwale na Ndugu yetu Atupele Mwambene. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mnyororo huu wa pongezi kwa viongozi wetu wakuu wa nchi, lakini siwezi kuacha kuwapongeza Wakuu wetu wote wa Mikoa Tanzania nzima ambao wamesimamia kazi hii kwa ukamilifu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mahususi, nampongeze Mkuu wangu wa Mkoa Mama yetu Hajat Fatuma Mwassa ambaye ameongoza Vikao vya RCC, Road Board na maeneo mengine kuhakikisha kwamba, Mkoa wake umesimama na ameweza kuleta na mambo mapya ya “Ijuka Omuka” kuhakikisha kwamba, anahamasisha Mkoa wetu unaendelea kuibuka kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, naipongeza Sekretarieti ya Mkoa ikiongozwa na Katibu Tawala Mkoa pamoja na Wakuu wa Wilaya wote, na mahususi Mkuu wangu wa Wilaya Mheshimiwa Kanali Hamis Maiga, Mkuu wa Wilaya ya Missenyi pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, kama unavyofahamu, halmashauri zetu zinaongozwa na Baraza la Madiwani. Nawapongeza Madiwani wetu wote wa Wilaya ya Missenyi, pia Mkurugenzi wetu Wakili Msomi John Paul Wanga, Wakuu wake wa Idara na watumishi wote wa Halmashauri hadi ngazi ya vijiji na kata, Watendaji wetu wa Kata na Vijiji, lakini mahususi wananchi wetu ambao wamejitoa kwa michango yao ya hali na mali kuhakikisha wamejitoa miradi ndani ya maeneo yao inasimama vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunasimama hapa mbele tukiwa Mheshimiwa Rais kwa mengi aliyotenda hasa kutuongezea bajeti na miradi hiyo, imeweza kufanyika kwa ufanisi katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mengi sana ambayo yametendeka ndani ya Wilaya ya Missenyi, lakini nitaweza kuongea machache kwa maslahi ya muda na niendelee kupongeza hasa kwa upande wa afya. Wananchi wa Wilaya ya Missenyi wanamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa upande wa Missenyi tumepokea takribani shilingi bilioni 2.02 katika miaka yake minne, mitano ya Serikali na tumeweza kupata Hospitali ya Wilaya mpya ambayo hapo awali haikuwepo. (Makofi)  
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, ndani ya Wilaya ya Missenyi tumepata vituo vya afya vipya viwili ambapo tunaona Kakunyu na Kanyigo na kimoja kikiwa kimejengwa kwa fedha za mapato ya ndani ambayo ilikuwa ni jambo kubwa katika eneo letu. Kwa hiyo, wananchi wa Missenyi wanaendelea kushukuru pamoja na zahanati nane ambazo zimeongezewa fedha kumalizia maboma katika eneo letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tunaendelea kushukuru, kwani kwa upande wa watumishi wameendelea kuletwa, lakini bado tuna uhitaji. Ninaamini Wizara yetu hii kwa umakini wao wataendelea kuongeza watumishi. Pia, tumeweza kupatiwa vifaatiba katika zahanati zetu na vituo vya afya pamoja na Hospitali ya Wilaya. Siyo hiyo tu, hata magari ya wagonjwa tumeyapokea. Kwa hiyo, tunatoa shukrani za dhati katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maombi katika eneo hili kwenda kwa Mheshimiwa Waziri ni kuomba katika orodha ambayo tuliomba vituo vya afya, nami niliomba kituo cha afya katika Kata yetu ya Mutukula ambayo ni kata ya kimkakati, ipo mpakani mwa nchi ya Uganda. Kwa kweli ina wakazi wengi sana ambayo inastahili kupata kituo cha afya na eneo Wanamutukula wameshaliainisha. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kama Mbunge, nilikuwa Jimboni tarehe 17, tuliweza kukagua eneo hilo kwa vigezo vyote ambavyo vinatakiwa. Hilo eneo linakidhi vigezo vyote. Basi naomba Mheshimiwa Waziri, kwa sababu kwenye orodha nimejiona, basi hizo fedha ziende hapo Mutukula tujenge kituo cha afya ambacho kitaweza kuhudumia kimsingi Kata yetu ya Mutukula na Minziro. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nataka kuishukuru Serikali ya Dkt. Samia, ni upande wa elimu ya sekondari ambapo Wilaya ya Missenyi tumepokea takribani shilingi bilioni 5.6 na hapo tumeshapata shule mpya tatu za Kitobo, Kanyigo na Kasambya. Pia tumepata mabweni, madarasa, mabwalo, matundu ya vyoo na maeneo mengine ambayo kwa kweli yote yameendelea kujengwa kwa umakini mkubwa mno.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili, bado kama Mbunge niliweza kuleta maeneo ambayo ni ya kimkakati hasa kwenye Shule za Sekondari yenye changamoto kubwa hasa kutokana na umbali wa watoto kwenda umbali mrefu, pia wingi wa watoto katika shule hizo. Nashukuru katika maeneo hayo, ndiyo niliyotaja takribani sehemu tatu sasa shule zimejengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa sehemu inayofuata pale Mutukula tuweze kujenga shule ya sekondari ambapo eneo limeshaainishwa, na kwa kweli kuna mwingiliano wa watu. Pia, watoto wa ule Mji wa Mutukula wanatoka hapo takribani kilometa 15 mpaka 20 kwenda kijijini kwa ajili ya shule. Kwa hiyo, naomba kwa kweli katika eneo hili pia sekondari inayofuata tuiweke pale Mutukula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa upande wa elimu, Wizara hii imetutendea mema mengi Wilaya ya Missenyi, tumeweza kupata shule mpya moja, na pia madarasa yamejengwa katika maeneo yetu, na tunaona madarasa mengi. Katika eneo hili pamoja na kazi nzuri, bado tuna uhitaji na maombi maalumu. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo la Wilaya ya Missenyi sisi wote ni mashuhuda upande wa missionary shule na elimu zilianzia sana katika maeneo yetu. Kwa hiyo, shule zilijengwa enzi za mkoloni. Kwa hiyo, ukiangalia katika Tarafa ya Kiziba, shule nyingi katika kata mbalimbali ni shule kongwe mno ambazo kimsingi naishukuru Serikali, kuna baadhi tumeweza kupata vyumba baadhi vya madarasa na nyingine zimebadilishwa, lakini bado tunazo shule kongwe mno. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia Bugandika, kuna Shule za Butulage, Ukilembo, lakini ukiangalia Kitobo kuna Shule ya Kayanga bado ni shule ambayo kwa kweli ni kongwe mno ambayo watoto wetu wapo pale kwa sababu hatuna namna nyingine. Shule nyingi katika Kata ya Kanyigo zimekuwa kongwe mno. Naomba sana, Wizara hii kwa umakini wake, katika hii bajeti inayokuja angalau tuweze kupata kwanza kidogo kidogo, lakini hizi shule ziweze kuwekewa mazingira mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye elimu msingi, niendelee kuomba, pamoja na kazi kubwa iliyofanyika, naomba shule shikizi katika maeneo ambayo ni magumu kufikika. Nashukuru Wizara hii imeweza kutujengea shule shikizi katika eneo la Bulembe ambalo ni lazima usafiri kwa mtumbwi kufika katika kisiwa hicho. Pia, Rugongo, Bushelegenyi na Rushenyi. Naomba shule shikizi katika eneo la Rugongo. Kwa hiyo, katika maeneo haya tukiweza kutatuliwa hii changmoto, naamini wananchi kwa kweli watakuwa wamepata nafuu katika eneo hili.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, sijui kama ni kengele ya kwanza au ya pili, lakini niseme katika eneo lingine la barabara…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Florent, muda wako umeisha.
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nashukuru kwa yote ndani ya wilaya yetu, naunga mkono hoja. (Makofi)