Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Ahmed Ally Salum

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Solwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. AHMED A. SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii. Kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu, kwamba Bunge hili ni la Bajeti, tunakamilisha miaka mitano ambapo tumefika salama salimini na kwa afya njema wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, namshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa sana aliyoifanya katika kipindi chake chote ambacho amekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza pia na niunge mkono hoja ya TAMISEMI kwa maana ya bajeti hii ikiongozwa na Mheshimiwa Waziri Mchengerwa. Mheshimiwa Mchengerwa anafanya kazi kubwa sana, na kwa kweli mimi kama Mbunge wa Jimbo la Solwa, awamu zangu nne leo siwezi nikasema zaidi ya kumshukuru Mungu, Mheshimiwa Rais na Waziri wa TAMISEMI kwa kazi kubwa mno na fedha nyingi sana anatuletea katika maeneo ya Tanzania hasa katika Jimbo la Solwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru pia Mkuu wa Mkoa wetu wa Shinyanga, namwona yupo hapa, Mheshimiwa Anamringi Macha. Amefanya kazi kubwa sana na anaendelea kufanya kazi kubwa sana. Shinyanga yetu ipo salama na anafanya kazi kubwa hasa kufufua zao la pamba. Mimi kama Mbunge, naamini wananchi wote wa Mkoa wa Shinyanga tupo pamoja kuendelea kufanya kazi katika suala hili la kufufua zao la pamba ili wananchi waendelee kufaidika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na elimu, tulikuwa na maboma mengi sana. Maboma zaidi ya 130 yalikuwa hayajajengwa, lakini kutoka 2023 mpaka sasa hivi 2025, zaidi ya maboma 48 katika shule za msingi tumeyakamilisha zaidi ya shilingi milioni 450, kazi kubwa mno imefanyika. Maana yake kwa spirit hii ya Mheshimiwa Rais, tunayokwenda nayo, tunamrudisha tena Ikulu, anaendela kuchapa kazi, 2025/2026, 2026/2027, sidhani kama tutafika 2028 maboma ya nchi nzima ikiwemo Jimbo la Solwa yatakuwa hayajakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutoka 2005 tangu niwe Mbunge sijawahi kupata fedha nyingi kama ambavyo nazipata kwenye hii Awamu ya Sita. Fedha ni nyingi za kutosha na unaona kabisa kwamba maendeleo sasa yanawagusa wananchi kule vijijini kabisa; wakulima, wafugaji, shule za msingi hizo, afya, pamoja na zahanati, tunakwenda kukamilisha miradi mingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ninapoongea, namshukuru kwanza Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Mchengerwa ninakushukuru sana umeniletea shule za msingi mpya mbili ambazo tuliweka katika Kata ya Salawe na tukajenga kwenye Kata ta Mwakitoryo kutokana na idadi ya watu iliyopo kule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee namshukuru Mheshimiwa Mchengerwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ameniletea shule nyingine, sasa hivi tunasubiri fedha kwa ajili ya shule mpya tutakayoenda kuijenga kwenye Kata ya Tinde, Kijiji cha Nyambui. Niliwahi kuongea hapa, Mheshimiwa Rais amekuwa msikivu, Mheshimiwa Mchengerwa nakushukuru sana, ulisikiliza, fedha hizo umeniletea, tumezisubiri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo shule ya msingi wakati ule nilisema tutaijenga huku ili wanafunzi wale wanaokata barabara, wanaotaka kuvuka barabara kutoka eneo la Shule ya Msingi Tinde A na Tinde B, walikuwa wanavuka kwenye wakati mgumu sana, tunakuwa tunahatarisha sana maisha yao. Barabara ya Tinde nyie mnaijua ilivyo, ukivuka pale ovyo ovyo unaweza ukapoteza maisha. Watoto wale walikuwa wanapoteza maisha. Sasa hivi mwarobaini umepatikana, watoto wa maeneo ya huku tukijenga shule ile zaidi ya milioni 500 maana yake watasoma vizuri, watapata elimu vizuri na tutakuwa tumetatua tatizo kubwa sana kwenye Kata ya Tinde na hasa Kijiji cha Nyambui. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala hili la walimu wanapopata likizo. Tulifanya marekebisho mwaka 2015 katika fedha kwa ajili ya kukidhi likizo kwa ajili ya walimu. Walimu wanafanya kazi kubwa sana, nawasemea hivi kwa sababu ya kazi kubwa mno wanayofanya na wanafundisha watoto wetu vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezunguka kwenye Jimbo la Solwa, nimejaribu sana kuongea nao. Ukiongea na Watoto, wanatoa shukrani kubwa sana kwa namna ambavyo walimu wanafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tufanye marekebisho mengine, kuna fedha ambazo zinahitajika ili walimu wanapochukua likizo wapate fedha zao, waende likizo salama salimini. Fedha ambazo zinatakiwa kwa sasa, naongelea katika Halmashauri ya Shinyanga DC, ni shilingi milioni 231. Walimu wamekwenda likizo, lakini bado hawajapata fedha hizo. Sasa, Mheshimiwa Mchengerwa mimi nakuamini, utalichukua hili ukalifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu sekondari, tuna sekondari za kutosha kabisa, na pia kipekee nashukuru nimepata sekondari mbili mpya ambazo tumejenga kwenye Kata ya Usule na Kata ya Puni. Shule za Sekondari zina thamani ya shilingi milioni 600 kila moja. Sasa, tatizo kubwa linalojitokeza hapa ni madawati, ni tatizo kubwa kweli siyo dogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri alichukue hili kwa uzito wake, na ninamshukuru sana kwa kazi kubwa anayofanya. Vilevile, naomba sasa aje atembelee Halmashauri ya Shinyanga DC na Jimbo la Solwa ili tumwonyeshe yale ambayo atakayoweza kuyachukua, akatusaidie katika miradi ya Jimbo la Solwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye afya, hapa napoongea sasa hivi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ahmed muda wako umeisha, tafadhali hitimisha.

MHE. AHMED A. SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika kumi zimeisha! Dah!

MWENYEKITI: Tafadhali hitimisha Mheshimiwa.

MHE. AHMED A. SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Tunamwombea sana Mheshimiwa Rais afya njema, tuingie 2025 tukiwa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, nawaombeeni sana Bunge hili tumalize salama wote turudi salama tukiwa na afya njema. Nakushukuru sana na ninaunga mkono hoja, ahsanteni. (Makofi)