Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Manyoni
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nachukua nafasi hii kukushukuru wewe kwa kunipatia nafasi hii. Kipekee namshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ambayo ameshaifanya Tanzania, hususan katika Jimbo la Manyoni Mashariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza na kumshukuru sana ndugu yangu, Mheshimiwa Mchengerwa, Waziri wa TAMISEMI. Siku moja niliwahi kumwambia, kuna siku utakuja kuwa Waziri wa TAMISEMI. Kazi yako tumeiona, vilevile unao Naibu Mawaziri wawili wanyenyekevu sana. Daktari mwenzangu Dugange na dada yangu, Mheshimiwa Katimba pale wanafanya kazi kubwa sana. (Makofi)  
Mheshimiwa Mwenyekiti, TAMISEMI imepata timu ambayo inafanya kazi kwa kweli. Mheshimiwa Mchengerwa, mimi niseme ukweli, umeitendea haki TAMISEMI na sisi tunaendelea kukuombea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema, Rais amefanya mambo makubwa sana. Sisi kule Manyoni upande wa elimu, unajua kuna wakati fulani tukiongea, watu wanasema kwamba ni uchawa, lakini mimi nimekuwa kwenye taasisi hizi na nimefanya kazi na TAMISEMI kama mshauri nikiwa UNICEF. Kwa kweli mambo yaliyofanyika Manyoni upande wa elimu unaweza ukasema hii nchi ilikuwa wapi zamani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, sisi tumepewa shilingi 4.5 billion kujenga Shule ya Wasichana ya Kitaifa ambayo sasa hivi tuna watoto pale zaidi ya 500 wa kike wa Kidato cha Kwanza hadi cha tatu. Pia wa Kidato cha Tano wanatoka Tanzania nzima. Haya ni mafanikio makubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na ndugu zangu Wasukuma, wao wanakimbia kwao Shinyanga wanakuja Ugogoni, wanakaa huko mbali wakawa wanajenga shule za tope. Mheshimiwa Rais alitoa fedha za UVIKO tukajenga Shule za Msingi zaidi ya 20 na zote zimeshasajiliwa. Hivi vitu huko nyuma hatujawahi kusikia, eti kwamba Serikali imejenga shule 20 ndani ya miaka minne. Ndiyo maana nimesema haya ni mafanikio makubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, upande wa sekondari, tulikuwa na sekondari, zimejengwa, zimekaa miaka 15. Kwa mfano, Shule ya Sekondari ya Mkwese haijakamilika. Vilevile, tulikuwa na kata tano, zilikuwa hazina sekondari kabisa. Mheshimiwa Rais alitoa fedha, tumejenga zaidi ya sekondari saba mpaka sasa hivi. Hii yote ni ndani ya miaka minne. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, Manyoni tuna ujenzi wa Shule ya VETA, tumepewa ziadi ya shilingi milioni 900 tunajenga Shule ya VETA. Pia, Manyoni tunajenga Shule ya Amali, tumepewa 1.6 billion, awamu ya kwanza tumeshapewa shilingi milioni 500. Haya yapo ndani ya miaka minne ya Mheshimiwa Rais. Ndiyo maana nilisema tukiyaongea haya, watu wakati fulani wanasema uchawa. Sasa mimi na Ph.D yangu nitakuwa chawa? Huu ni ukweli usiopingika, haya mafanikio ameyafanya Mheshimiwa Rais. Tumekua, tumesoma Tanzania, tunajua tumefanya kazi Tanzania, haya, mambo hayakuwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, lazima tumpe maua yake Mheshimiwa Rais kwa kweli. Mimi huwa nawaambia watu, kwanza nina bahati kufanya kazi na Mheshimiwa Rais. Inawezekana Mungu alinipangia niingie kipindi hiki ili nilete mabadiliko makubwa sana katika Jimbo la Manyoni Mashariki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nimshauri Mheshimiwa Waziri upande wa TAMISEMI. Ule upungufu wa walimu shule za msingi siyo wa kuilaumu Serikali. We have to be creative. Kwa nini usiielekeze halmashauri zako katika yale mapato ya ndani watenge percent fulani waweze kuajiri walimu wa mkataba. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kusubiri kila kitu kitoke Central Government (Serikali Kuu), no. Wakurugenzi wanahitaji kuwa wabunifu, na hilo Mheshimiwa Mchengerwa nina uhakika unaweza ukalisimamia. Hiyo itasaidia kupunguza tatizo la ajira huko mtaani. Kwa hiyo, hilo nilikuwa ninashauri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kuhusu shule chakavu, Mheshimiwa Waziri, alikuja na mpango mzuri sana wa zile shule kongwe. Kule kwangu alinijengea shule kongwe takribani tatu. Ule mradi uli-phase out. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshauri Mheshimiwa Waziri, huu ulikuwa ni ubunifu mzuri sana. Naomba tu-revive ule mpango. Mimi nina shule kongwe pale kwa mfano Shule ya Majengo Manyoni, Shule ya Iseke na Shule ya Udimaa, hizi zote ni Shule Kongwe. Ningetamani ule mpango wake aliokuwanao auendeleze, a-revive, atasaidia sana, na kwa kweli alisaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni yale maboma. Wenzangu wamesema, wananchi waliweka nguvu kubwa kwenye maboma. Nashauri, abuni mradi wa kimkakati wa kuhakikisha kwamba ile nguvu iliyotumika na wananchi, tunaenda kui-support ili iweze kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa afya, nashukuru, lakini nampongeza Mheshimiwa Rais. Pale Manyoni tulikuwa na Hospitali ya Wilaya kongwe, tumepewa 1.9 billion shillings. Ukifika Manyoni kwenye ile Hospitali ya Wilaya, utafikiri ni Benjamin Mkapa. Haya yote ni mafanikio makubwa sana. (Makofi) 
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tumefanya mambo makubwa upande wa zahanati na kwenye vituo vya afya. Nina ushauri. Kwanza, vile vituo vya afya vya kimkakati wenzangu wamesema, mimi nilikuwa nina Kituo cha Afya cha Mkakati cha Makanda ambacho kimsingi nilishaleta jina na nina uhakika tutapata fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Kituo cha Afya cha Kintinku, kinahudumia halmashauri tatu; Halmashauri ya Chemba, Halmashauri ya Bahi, na Halmashauri ya Manyoni. Pia, kipo kwenye mainroad, ajali zote zikitokea, wagonjwa wanapelekwa pale. Kile kituo hakina wodi, hakina OPD, lakini ni kituo cha kimkakati na tayari kilishajengwa. Nashauri vilevile tukiangalie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, Hospitali ya Wilaya hatuna ICU. Ninyi ni mashahidi, Manyoni ipo katikati ya barabara inayoenda Mwanza. Hatuna ICU. Kwa hiyo, tukipata ajali, tunapata shida sana kwa ajili ya kuwa-manage wale majeruhi. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri, nakuangalia hapo, nawe unaniangalia, suala la ICU kwenye Hospitali ya Wilaya ya Manyoni nalo utuangalie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa TARURA wenzangu wamesema. Eng. Seff, kwa kweli ameweka maajabu makubwa sana Manyoni. Mimi niseme, nampongeza sana Mheshimiwa Rais. Kulikuwa kuna madaraja ya kihistoria Manyoni, Daraja la Ngonjigwe walitoa huko zamani shilingi milioni 100 likaanguka. Mheshimiwa Rais ametoa shilingi milioni 600, tunajenga daraja la kisasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ndumbi walikuwa hawategemei kupata daraja. Mheshimiwa Rais ametoa shilingi milioni 500, tunajenga daraja la Ndumbi. Chikola walikuwa hawana uhakika wa kupata daraja, lakini walipewa shilingi milioni 300 daraja lilishajengwa. Haya yote ni mafanikio makubwa yamefanyika ndani ya miaka minne. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri anisikie hapo. Kata ya Muhalala kuna eneo linaitwa Daraja la Kapiti, tunahitaji takribani shilingi milioni 100 kulijenga. Lipo katikaki ya kijiji, linagawa shule na mji. Wakati wa masika watoto hawaendi shuleni. Sasa, hili naomba shilingi milioni 100; hazikushindi Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, tuna barabara ya kutoka Chikuyu kwenda Itetema. Hii ni barabara ya kimkakati, inaunganisha tarafa mbili. Inahitajika shilingi bilioni moja tu kuhakikisha ile barabara inapitika wakati wote. Hili nalo utusaidie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho Mheshimiwa Rais alikuja Manyoni, tukamwomba kilometa 10 za lami Manyoni Mjini. Alimwagiza Waziri kwamba afanye usanifu na afuatilie. Kwa hiyo, nami namkumbusha Mheshimiwa Waziri, zile kilometa 10 za lami Mheshimiwa Rais alizoahidi, naomba sasa azifuatilie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, pale Manyoni mji wetu unakua, lakini hatuna stendi ya kisasa wala hatuna soko la kisasa. Ninyi wenyewe mnajua Dodoma inapumulia Manyoni sasa hivi, lakini hatuna stendi ya mabasi ya kisasa wala hatuna soko la kisasa pale Manyoni Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naendelea kukushukuru lakini nampongeza sana Mheshimiwa Rais. Pia, nakipongeza Chama changu cha Mapinduzi kwa maajabu makuu ambayo yamefanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)