Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ludewa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Nami naungana na Wabunge wenzangu wote waliompongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kwa kweli miaka hii mitano kazi zilizofanyika majimboni kwetu ni kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia tena kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mchengerwa pamoja na wasaidizi wake wote kwa kazi nzuri. Kwa kweli mnatupa heshima kubwa sana kule majimboni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, halikadhalika, nampongeza sana na kumshukuru Mkuu wangu wa Mkoa, nimeona anatambulishwa hapa, Mheshimiwa Anthony Mtaka. Kwa kweli anatusaidia sana Wabunge Mkoa wa Njombe. Mambo mengi yanaenda vizuri. Naomba tu Mheshimiwa Waziri aiwezeshe ofisi yake ili iweze kwenda kukagua miradi mara kwa mara kule Ludewa kwa kushirikiana na Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tunaye RAS mzuri na Mkuu wa Wilaya, na timu ya Mkurugenzi na wataalamu. Nawashukuru sana, kazi wanayoifanya ni kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka hii mitano kwa kweli Halmashauri yetu ya Wilaya ya Ludewa ilikaa vizuri. Tulikuwa na Mkurugenzi, yuko vizuri. Ukusanyaji wa mapato umefanyika vizuri. Wakuu wake wa idara, safu imekaa vizuri sana. Kwa hiyo, hata mimi Mbunge iliniwia wepesi sana kufanya kazi pamoja na Waheshimiwa Madiwani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na shukurani, nikianza na sehemu ile ya elimu, naungana na Wabunge wenzangu wengine kuishukuru Serikali, imetupa heshima kubwa sana kule majimboni. Miundombinu mingi imeboreshwa, ila tunaomba tu kwenye eneo hili la Elimu ya Msingi, lile tangazo la Mheshimiwa Simbachawene la uhamisho wa watumishi kufuata ndoa zao, bahati mbaya sisi kule Ludewa tulikuwa hatujaoa maeneo mengine; tungejua kama Mheshimiwa Simbachawene ataruhusu watumishi wa kule kufuata ndoa zao, nasi tungeoa walimu wa maeneo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ile imetuathiri sana. Shule nyingi walimu wamehama na wengine wamestaafu. Kwa hiyo, naomba sana mtusaidie kutupa walimu wa kutosha. Kuna shule walimu wamebakia wawili, na walimu wengine unakuta mmoja akiwa maternity leave, shule inabakia na mwalimu mmoja. Kama mwingine yuko masomoni ndiyo inakuwa tatizo kabisa. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, namshukuru sana Mheshimiwa Rais, miaka hii mitano kila mwaka tumekuwa tukishuhudia akiajiri walimu. Kwa hiyo, tunaomba na hao walimu walioajiriwa mwaka huu, Ludewa nayo iweze kupata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikwenda Shule ya Msingi Kingole nikaona ina upungufu mkubwa sana wa walimu. Shule ya Msingi Lifuma na shule nyingine za Mwambao kule Ziwa Nyasa, nazo zina upungufu sana wa walimu. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, katika ajira hizi basi Ludewa tuweze kupewa kipaumbele kwa sababu walimu wetu wengi sana walihamishwa, lakini ni kwa nia njema. Siyo kwamba tunamlaumu Mheshimiwa Simbachawene. Hata mimi ukinihamishia mke wangu akaenda eneo lingine sitajisikia vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo naomba tuweze kusaidiwa ili tukae vizuri zaidi kwenye elimu ya msingi, ni kuboresha miundombinu ile ya madarasa. Ziko shule ambazo kwa kiasi kikubwa zilijengwa kwa nguvu za wananchi. Kwa hiyo, tukipata fedha, mambo yatakuwa mazuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, naomba wale walimu ambao wanajitolea kama ambavyo Wabunge wengine wamesema, waweze kufikiriwa. Halmashauri iweze kutenga fedha, hasa elimu ya msingi. Wale wana certificate, wana diploma, hata graduates wale wawe wanapewa walau nauli, tuwapunguzie mzigo wananchi ambao wanachangishwa fedha kwa ajili ya kulipa walimu wa kujitolea. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda mrefu walimu wametusaidia sana. Jitihada hizi tunazozisema ambazo Mheshimiwa Rais amezifanya, kule Ludewa, matokeo yake tumeyaona. Kwa kweli kwenye elimu, tumepanda sana. Nilipofika, tulikuwa wa mwisho kimkoa, namba sita, sita sita, lakini kutokana na hizi jitihada na safu nzuri tuliyonayo pale Ludewa, kwa kweli tumeweza kupanda sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeweza hata kutoa shule ya kwanza kimkoa, kata, kwa Kidato cha Sita, Shule ya Sekondari Chifu Kidulile. Vilevile, Kidato cha Pili kwa shule za Serikali; Shule ya Sekondari Ludewa Kwanza nayo ilifanya vizuri, tuliweza kuongoza kimkoa. Hata Kidato cha Nne, kiasilimia tumepanda sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hizi jitihada ambazo Mheshimiwa Rais anazichukua, kwa kweli matokeo yake yanaonekana dhahiri. Walimu ambao ametuongezea, tunaomba tu hao waliohama tuweze kupata walimu mbadala ili wananchi kule wasihangaike sana kulipa walimu wa kujitolea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo naishukuru sana Serikali ni eneo la afya. Tumeweza kujengewa zahanati zaidi ya 25, na kuna nyingine ambazo zilikuwa zimetelekezwa zaidi ya miaka 20. Tulikwenda pale Kijiji cha Ndowa Kata ya Makonde, tulikuta kuna zahanati ina miaka 20. Wananchi wameianza, haijakamilishwa. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali hii sasa, iliweza kupeleka fedha, leo wale wananchi wanapata huduma pale. Halikadhalika Zahanati ya Nsele, Kimata, Chanjale pale, naomba tu watumishi waweze kupelekwa. Serikali ilishapeleka fedha, bado wananchi wanatembea kilometa 17. Ninaamini wakipeleka fedha kwa ajili ya kumalizia zahanati ile tutaweza tukawasaidia sana wananchi wale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la mwisho ambalo napenda kushukuru sana, ni eneo la miundombinu ya barabara vijijini.
(Hapa, kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa, naomba uhitimishe.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, ila tunazo barabara zetu kama nne. Kusema uzito wa mwisho tani 10, zile za vijijini, tuongezewe ubora wa madaraja, mitaro, ili malori mazito zaidi yaweze kwenda kubeba nguzo kule Ilininda, Ludende, na maeneo mengine. Kwa hiyo, kuna barabara ambazo tutazichagua, tunaomba Serikali ituboreshee ili magari yenye uzito zaidi ya tani 10 yaweze kuruhusiwa, kwa sababu kule ndiyo kwenye uzalishaji mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
MWENYEKITI: MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Ahsante sana.