Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ilemela
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuunga mkono hoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio makubwa sana ambayo Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hususan ni katika maeneo ya huduma za jamii kama vile afya, elimu, maji, kilimo, mifugo na uvuvi na kadhalika. Kazi kubwa sana imefanyika na jamii kwa ujumla inashukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio mengi tuliyoyapata Jimboni Ilemela, Mkoa wa Mwanza na Taifa kwa ujumla, kuna changamoto kadhaa ambazo naomba Serikali isaidie, hususan madai ya fidia za wananchi, utekelezaji wa ahadi ya Rais na malipo kwa wakandarasi wa barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mchengerwa na Naibu Mawaziri wake, Mheshimiwa Dkt. Dugange na Mheshimiwa Zainab Katimba na timu nzima ya management ya Wizara ya TAMISEMI chini ya Katibu Mkuu, Ndugu Ndunguru. Kazi yao hakika ni ya kutukuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uchache, naomba kutaja changamoto chache ambazo zinahitaji Serikali izifanyie kazi: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni changamoto inayohusu deni la fidia ya ardhi shilingi 6,388,973,372.29. Halmashauri inakabiliwa na deni la fidia ya ardhi lipatalo shilingi 6,388,973,372.29 ambapo kati ya deni hilo, shilingi 3,774,221,795.43 ni deni la fidia ya ardhi lililorithiwa kutoka Jiji la Mwanza wakati wa mgawanyo wa mali na madeni. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, shilingi 2, 614,751,577.29 ni deni la fidia ya ardhi lililotokana na uhitaji wa maeneo ya umma kwa ajili ya shule, vituo vya huduma za afya, maeneo ya wazi, masoko, eneo la Maonesho ya Nane Nane, maeneo ya makaburi, maeneo ya barabara na upangaji wa mji kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muhtasari, madeni haya yamegawanyika kama ifuatavyo:-
(a)	 Deni la fidia kwa ajili ya maeneo ya Shule 2,492,337,433.30;
(b)	Deni la fidia kwa ajili ya maeneo ya vituo vya afya na zahanati shilingi 403,808,037.85;
(c)	Deni la fidia kwa ajili ya maeneo ya barabara shilingi 1,255,800,132.57;
(d)	Deni fidia kwa ajili ya maeneo ya masoko shilingi 76,412,419.25;
(e)	Deni la fidia kwa ajili ya maeneo ya wazi shilingi 56,360,742.50; na
(f)	Deni fidia kwa ajili ya maeneo ya Maonesho ya Nane Nane, Mradi Kiseke, Buswelu na Nnyamhongolo shilingi 2,104,254,607.25
Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla ni shilingi 6,388,973,372.72.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela imekuwa ikitenga fedha za kulipa fidia katika bajeti za kila mwaka ambapo kwa mwaka 2024/2025 imetenga shilingi 1,300,000,000 kwa ajili ya ulipaji wa fidia. Hata hivyo, fedha inayotengwa haitoshelezi deni kubwa lililopo ambalo limekuwa likiongezeka riba kwa mujibu wa Sheria ya Utwaaji Ardhi ya mwaka 1967, Sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999 na Sheria ya Uthamini Namba 16 ya Mwaka 2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Manispaa ya Ilemela, naomba Serikali isaidie fedha shilingi 6,388,973,372.72 kwa ajili ya ulipaji wa madeni ya fidia ya ardhi kutokana na sababu zilizoainishwa hapo juu, kwani imekuwa ni kero kubwa sana kwa wananchi ambao maeneo yao yalitwaliwa na Serikali kwa manufaa ya umma. Madeni haya mengi ni ya mwaka 2007 jambo ambalo wananchi sasa wameanza kukosa imani kwa kupewa ahadi nyingi zisizotekelezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine ni utekelezaji wa ahadi ya Rais ya kujenga barabara kwa kiwango cha lami kilometa 12, ahadi aliyoitoa tarehe 30 Januari, 2024 wakati akiongea na vijana uwanja wa Nyamagana, Jijini Mwanza. Barabara hizo ni kama ifuatavyo: Barabara ya Pansias - Lumala - Kiseke yenye kilometa 3.7, Barabara ya Kahama - Isela – Ngwag’wila yenye kilometa 6.7, Barabara ya Mwika yenye kilometa 0.5, Barabara ya Breweries - Bwiru Junction yenye kilometa 0.5, na Barabara ya Kijiji - Bigbite yenye kilometa 1.2. Barabara hizi zote zinatengeneza kilometa 12 ambapo Mheshimiwa Rais aliahidi kuzijenga kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho japo siyo kwa umuhimu, naiomba sana Serikali iwalipe wakandarasi ambao tayari walishakabidhiwa site, lakini hawajaanza kazi kwa kuwa Serikali bado haijawalipa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.