Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbeya Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee, naomba kuungana na Watanzania wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutimiza vyema miaka minne kwa kuongoza nchi yetu akiwa Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tumeshuhudia mafanikio makubwa katika kuimarisha miundombinu hususan barabara, reli, viwanja vya ndege, bandari, huduma za kiuchumi na kijamii kama vile ujenzi wa madarasa, hospitali, zahanati na vituo vya afya, huduma za maji, utawala bora, pamoja na kuhamasisha uwekezaji na utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri iliyotukuka ya kumsaidia Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, kwa kuteuliwa kuwa Mgombea Mwenza wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa uzoefu na weledi wake, kama ilivyo kwa Watanzania walio wengi, nina imani kubwa kwa Mheshimiwa Nchimbi na kumtakia afya njema na kila la heri kwenye mchakato ujao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko, Mbunge na Naibu Waziri Mkuu, na Waziri wa Nishati kwa kutekeleza majukumu ya kumsaidia Waziri Mkuu, ikiwa na pamoja na jukumu la kuendelea kuisimamia ipasavyo Sekta ya Nishati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na uongozi wote wa Bunge kwa uongozi mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa, Mbunge na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Taifa letu katika ya ushindani wa Kimataifa (National competitiveness). Bajeti hii ambayo ni ya mwisho, inaenda sambamba na Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi chake akiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tathmini zinathibitisha mafanikio makubwa ya utekelezaji na usimamizi wa Mpango wa Kwanza na wa Pili na kupelekea Taifa letu la Tanzania kufanya vizuri mno kuinua uchumi katika kipindi hiki kigumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha miezi tisa ya mwaka huu wa bajeti, Serikali kupitia TAMISEMI imesimamia kwa uadilifu na ufanisi mkubwa mwendelezo wa ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya vituo vya afya na miundombinu ya shule za msingi na sekondari na pia ukarabati wa barabara za vijijini. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Mbeya Vijijini limenufaika kwa uboreshaji wa miundombinu ya shule kongwe za msingi na pia ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa shule za msingi na sekondari. Ujenzi wa miundombinu ya afya na elimu umeendelea kuweka historia ya kipekee katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya. Wananchi wana imani kubwa ya huduma nzuri zitakazotolewa ikiwemo kuwepo wa watalaamu bingwa, vifaa tiba vyote muhimu na dawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa ikiwemo utaratibu mpya wa mikopo kwa vijana, akina mama na watu wenye ulemavu kupitia kwenye taasisi za fedha. Huu ni mfumo mzuri siyo tu kulinda huo mfuko, lakini itakuwa ni sehemu ya kuboresha sera ya huduma ya fedha jumuishi (financial inclusion).
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio hayo makubwa, Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya bado ina changamoto za kumalizia miundombinu ya zahanati na vituo vya afya vilivyojengwa kwa nguvu za wananchi ikiwemo vituo vya afya kwa Kata ya Ilungu, Kata ya Isuto, Kata ya Ulenje, Kata ya Iwindi na Kata ya Bonde la Songwe, na zahanati kwa kila kijiji. Wananchi wamejitahidi kujenga maboma ya zahanati na vituo vya afya na wanategemea Serikali itawaunga mkono kumaliza kazi zilizobakia bila kuchelewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekamilisha ujenzi wa barabara za lami katika maeneo ya kilimo cha kahawa na mbogamboga. Barabara zilizokamilika ni Barabara ya Inyala – Simambwe ya kilometa zaidi ya 16 inayopita Kata za Inyala, Itewe, Maendeleo na Tembela. Pia kilometa 10 za Barabara ya Lupeta – Wimba - Izumbwe, inayopita Kata za Swaya na Igale. Barabara hizi zimeleta fursa nyingi kwa wananchi hasa wakulima kusafarisha mazao yao na hata kuleta unafuu wa usafirishaji wa pembejeo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio hayo makubwa, katika halmashauri zetu tumekuwa tunakabiliwa na changamoto hasa kwenye miundombinu ya barabara. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, barabara zinazohudumiwa na TARURA kwa zaidi ya 90% zipo kwenye hali mbaya sana kutokana na jiografia na hali ya hewa ya mvua nyingi. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengi ya vijijini, barabara hazipitiki kutokana na vivuko kusombwa na mafuriko. Naiomba Serikali ichukue hatua za haraka kunusuru hali hii ili wananchi waweze angalau kusafirisha mazao yao. Hali ya mtandao wa barabara wa zaidi ya kilometa 1,000 ni mbaya na hazipitiki kirahisi hasa kipindi cha mvua. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ambazo zipo kwenye hali mbaya sana ni pamoja na Mbalizi – Iwindi – Songwe Magereza, Shamwengo – Usoha Muungano, Itala – Wambishe – Mbonile, Nsenga – Swaya – Nzovwe, Ilembo – Isonso, Maganjo – I/Mapinduzi – Shisonta, Ilembo – Mbagala, Ilembo – Mwala, Iwowo - Igalukwa – Mlowo, Horongo – Igale, Songwe Viwandani – Jojo, Kawetere – Ikukwa, Mbalizi – Ilota, Nyalwela – Ngole, Nyalwela – Mbonile, Ilembo – Mbawi, Igawilo – Hatwelo, na Galijembe - Idunda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bajeti ndogo ambayo ni kilometa chini ya 100 kwa mwaka, ni vigumu kutatua changamoto za barabara hizi, kwa kiasi kikubwa zinabeba uchumi wa kilimo na madini kwa Mbeya na Tanzania kwa ujumla. Napendekeza Serikali iweke msukumo zaidi kwenye kuboresha miundombinu ya barabara kurahisisha usafirishaji wa mazao ya kilimo. Hii itasaidia kuimarisha uchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza kuwepo na msukumo wa kuhakisha halmashauri zinasimamia kikamilifu elimu ya kujitegemea kwenye ngazi zote za msingi na sekondari. Kwa shule za vijijini kushirikisha Maafisa Ugani wa Kilimo na Uvuvi kuanzisha mashamba darasa kwa kila shule za vijijini. Kwa shule za mijini kuna fursa pia kuweka msukumo wa elimu ya kujitegemea kulingana na mazingira ya shule ikiwemo elimu ya ufundi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na umuhimu wa mikopo kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, napendekeza Serikali iboreshe mfumo wa mikopo hii kuendana na madhumuni ya mikopo ya kuimarisha kundi hili kiuchumi. Kama ilivyopendekezwa kwenye hotuba ya Waziri, uendeshaji wa mikopo hii uwe na misingi ya huduma za kifedha jumuishi (financial inclusion) ikiwemo elimu ya matumizi ya mikopo na usimamizi wa kitalaamu wa mikopo. Kwa ukubwa wa mfuko huu Kitaifa kuna umuhimu wa kuunda taasisi ya kifedha kuusimamia kwa tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Halmashauri ya Mbeya, kuna Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mbalizi ambao una wakazi zaidi ya 100,000 na shughuli nyingi za kiuchumi ikiwemo viwanda, madini na hata uwanja wa ndege wa Songwe. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika Kata ya Utengule Usongwe kuna Kijiji cha Mbalizi ambacho mipaka yake haiungani na vijiji vingine vya kata hiyo. Napendekeza Serikali irekebishe mipaka ya Mbalizi na ipandishe hadhi kutoka Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mbalizi kuwa Halmashauri ya Mji wa Mbalizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo ya kugawa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya ni kilio cha muda mrefu, na Hayati Mheshimiwa Dkt. Magufuli mwaka 2020 aliagiza zoezi la kugawa lifanyike haraka na aliagiza kubadilisha jina la Jimbo la Mbeya Vijijini haraka iwezekanavyo. Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya ina sifa zote za kugawa ikiwemo uwezo kiuchumi ni mkubwa sana, idadi kubwa ya wakazi na pia changamoto za kijografia. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya inapakana na halmashauri zote za Mikoa ya Mbeya na Songwe kasoro Kyela na Tunduma, na pia inapakana na hata Mkoa wa Njombe. Vikao vyote vya kisheria toka ngazi za chini mpaka ngazi ya Kamati za Ushauri za Wilaya na Mkoa katika wakati tofauti vimepitisha mapendekezo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.