Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Prof. Patrick Alois Ndakidemi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Moshi Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa, Mbunge na Naibu Mawaziri wake Mheshimiwa Dkt. Festo Dugange, Mbunge na Mheshimiwa Zainab Katimba, Mbunge, pamoja na wataalamu wa Wizara kwa kazi nzuri wanazofanya kutatua changamoto za wananchi hapa nchini Tanzania katika sekta wanazohudumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukilinganisha na bajeti ya mwaka 2023/2024 ambapo Bunge lilipitisha shilingi 10,125,220,403,167, naomba nilipongeza Bunge lako Tukufu, kwani nina hakika litaidhinisha Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka 2025/2026 yenye jumla ya shilingi 11,782,984,202,000 kwa ajili ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI na taasisi zilizo chini yake: Fungu Na. 56 - Tume ya Utumishi wa Walimu, Fungu Na. 2 na Mafungu 26 ya Mikoa yakijumuisha Halmashauri 184.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii ya TAMISEMI imeongezeka kwa 13.4%. Fedha hizi ni muhimu, kwani zinakwenda kugusa mambo ya msingi ya maisha ya Watanzania wa vijijini na mijini ambayo ni elimu, afya, miundombinu ya barabara, ustawi wa jamii na uongozi katika ngazi ya vitongoji, vijiji, mitaa, kata, tarafa, wilaya na mikoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii kuipongeza sana Serikali kwa kutekeleza miradi mingi ya maendeleo katika sekta za elimu, afya, miundombinu ya barabara na ustawi wa jamii kupitia Wizara ya TAMISEMI katika Jimbo la Moshi Vijijini. Kusema kweli kipindi hiki cha miaka mitano ya Ubunge wangu, tumepata faraja kubwa ya miradi katika Jimbo la Moshi Vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu katika Wizara hii utajikita kwenye hoja mbili: kwanza ni umuhimu wa kukarabati barabara za jimboni kwangu, Moshi Vijijini; na pili, ni pendekezo kwamba Mbunge awe Meya wa Jiji au Manispaa au Mwenyekiti wa Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeze sana Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa kazi kubwa ya ujenzi, ukarabati na matengenezo ya miundombinu ya barabara mbalimbali hapa nchini kupitia TARURA. Katika bajeti hii ya 2024/2025, Ofisi ya Rais, TAMISEMI imepanga kutumia shilingi trilioni 1.18 kwa ajili ya ujenzi, matengenezo, ukarabati wa miundombinu ya barabara na usafiri na usafirishaji wa vijijini na mijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni tumaini langu kwamba kilio sugu cha ubovu wa barabara za jimbo langu la Moshi Vijijini kitapewa kipaumbele, kwani kuna changamoto kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Moshi Vijijini, maeneo mengi ya mlimani na tambarare ambako wananchi wake wanajishughulisha na uzalishaji wa bidhaa za mifugo, kahawa, ndizi, mpunga na kilimo cha mazao mbalimbali, kumekuwa na changamoto kubwa ya miundombinu ya barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika miaka yote, changamoto hizi zimekuwa na athari kubwa sana kwa wananchi baada ya mvua kubwa za masika kuanza kunyesha. Mwaka huu mvua hizo zilianza rasmi mwishoni mwa mwezi Machi, 2025 na bado zinaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mvua hizo zimesababisha barabara hizo zishindwe kupitika kwa vyombo vya usafiri kama magari, baiskeli na pikipiki. Katika ukanda wa tambarare kwenye Kata ya Mabogini na Arusha Chini, na upande wa Chekereni Weruweru katika Kata ya Kindi na Mandaka Mnono katika Kata ya Oldmoshi Magharibi, barabara hazipitiki kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha milimani kuishia maeneo ya tambarare na kusababisha mafuriko, kuziba mitaro na kupelekea maji kujaa barabarani pamoja na kutapakaa kwenye makazi ya watu, hali inayohatarisha usalama wa wakazi wa maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika Jimbo la Moshi Vijijini, kuna baadhi ya barabara zimeharibiwa vibaya na mvua. Kutokana na uharibifu uliojitokeza, tunaishukuru Serikali, kwani kuna baadhi ya barabara tayari wakandarasi wameshapatikana kwa ajili ya kufanya matengenezo ya sehemu zilizoharibiwa na mvua, na pia barabara nyingine TARURA Wilaya ya Moshi wanaendelea kuzifanyia tathmini ili ziweze kufanyiwa matengenezo ya haraka ili kuzuia uharibifu kuongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zifuatazo ni barabara ambazo tayari wakandarasi wapo site na wanaendelea na kazi ya marekebisho. Moja, Barabara ya Uru Mawela – Shimbwe KNCU na Mamboleo – Shimbwe tayari imetengewa kiasi cha shilingi 291,110,000 na sasa mkandarasi anajiandaa kuanza kazi kwa ajili ya kufanya matengenezo ya sehemu zilizoharibiwa na mvua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Barabara ya Fonga Gate – Mabogini – Kahe mkandarasi amefanya kazi ya kuchimba mitaro ya kuondoa maji barabarani yenye urefu wa kilometa mbili kwa ajili ya kuzuia maji ya mvua yasiendelee kuharibu barabara na pia kuingia kwenye makazi ya watu. Barabara hii inajengwa kwa kiwango cha lami. Tunaiomba Serikali iiweke kwenye mpango wa bajeti ya mwaka 2025/2026 ili kuendeleza ujenzi kwa kiwango cha lami, kwani eneo hili lina idadi kubwa sana ya wakazi, na lami inahitajika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba Serikali iendelee kufanya tathmini kuhusu uharibifu wa barabara zifuatazo na kuziingiza kwenye bajeti ya mwaka 2025/2026 ili kuendelea kuziimarisha:-

(i) Barabara ya Rau Madukani – Mamboleo – Materuni (hii ujenzi wake ni wa kiwango cha lami;

(ii) Kiboroloni – Mbokomu (barabara hii hupeleka watalii kwenye mti mrefu kuliko yote Afrika);

(iii) Barabara ya Sango – Kimochi;

(iv) Barabara ya Mjohoroni - Shia – Kimochi;

(v) Barabara ya Mtakuja – Chekereni;

(vi) Barabara ya Kidia – Kimochi;

(vii) Barabara ya Uru Seminari - Okaseni – Kifumbuni;

(viii) Barabara ya Mto Umbwe – Nyamaa;

(ix) Barabara ya Tema - Mengeni – Olimo;

(x) Barabara ya Kwa Saraki - Kindi Kibaoni;

(xi) Barabara ya Oldmoshi - Mdawi – Kisaseni;

(xii) Barabara ya Kombo - Geti la Umbwe (kupandia mlima kilimanjaro);

(xiii) Barabara ya Mwasi Kusini - Mwasi Kaskazini - Mruwia hadi Materuni;

(xiv) Barabara inayounganisha kijiji cha Mandaka Mnono na kata ya Mabogini;

(xv) Barabara ya Chekereni – Weruweru;

(xvi) Barabara ya Kibosho Sokoni - Kibosho Hospital - Singa Juu;

(xvii) Barabara ya KDC Office - KKKT Kiwalaa; na

(xviii) Ujenzi wa daraja katika barabara ya Samanga - Chemchem.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba barabara hizi zimefanyiwa ukarabati wa mara kwa mara, lakini bado kuna changamoto kubwa ya ukosefu wa mitaro katika baadhi ya barabara. Niishauri Serikali kwamba, wakati wa ujenzi wa barabara, ni vyema kutoa kipaumbele kwenye kujenga mitaro kwanza ili kulinda miundombinu ya barabara hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa inatenga fedha nyingi kujenga barabara, lakini zinadumu kwa muda mchache kutokana na maji ya mvua kuingia barabarani na kuharibu hizi barabara. Kuweka kipaumbele kwenye mitaro kutanusuru gharama za kila mara zinazotumika kukarabati barabara kwa sababu tu hakuna mitaro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali kuandaa mpango wa kuhakikisha kuwa barabara hizi za Moshi Vijijini zinapitika muda wote ili kuondoa hii kero. Pia naomba fedha itengwe ili kufanya ujenzi wa daraja katika barabara ya Samanga - Chemchem.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changarawe zinazotumika kutengeneza barabara hizi zinapatikana katika maeneo mengi ya Jimbo la Moshi Vijijini, chanzo kikiwa ni changarawe za volcano ya Mlima Kilimanjaro. Hivyo basi, ikiwa Serikali itajipanga vyema, kazi hii itatekelezeka kwa gharama za kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ya pili ni pendekezo kwamba Mbunge awe Meya wa Jiji au Manispaa au Mwenyekiti wa Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kufanya tafiti binafsi na tafakari, nimewiwa kushauri kwamba kuna umuhimu wa kufanya mageuzi ya muundo wa utawala wa uongozi wa halmashauri, manispaa na majiji hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nchi yetu, kuna viongozi wa kuchaguliwa na wananchi kuanzia ngazi ya kitongoji/mtaa (Mwenyekiti), Kijiji (Mwenyekiti), Kata (Diwani), Jimbo (Mbunge) na nchi (Rais). Katika muundo wa uongozi uliopo, viongozi hawa wana majukumu makubwa ya kuongoza maeneo yao. Kwa mfano, Mwenyekiti wa Mtaa/Kitongoji/Kijiji ni Mkuu wa Serikali ya Kitongoji/Mtaa/Kijiji; Diwani wa Kata ni Mkuu wa Serikali ya Kata; Rais ni kiongozi wa nchi; na Mbunge wa kuchaguliwa na wananchi wote ni mwakilishi wa wananchi Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mbunge huwakilisha matatizo au mahitaji ya watu Bungeni, lakini hana rungu la kusimamia maendeleo katika Jiji, Manispaa au Halmashauri inayoundwa na jimbo/majimbo husika. Badala yake, msimamizi wa miradi ya maendeleo huwa ni mmoja; Diwani anayechaguliwa kuchukua nafasi ya Umeya au Mwenyekiti wa Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiuhalisia, kiongozi huyu hana mizizi kwa wananchi wa jimbo lote kama alivyo Mbunge. Katika hili, uongozi huu una dosari, kwani hauna uhusiano wa kuchaguliwa na wananchi wote wa jimbo moja kwa moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uchambuzi niliofanya, ni vyema kabisa Mbunge wa kuchaguliwa na wananchi awe ni mkuu wa shughuli za maendeleo katika jiji/manispaa au halmashauri inayoundwa na jimbo/majimbo husika. Hili likikubalika, litaondoa mkanganyiko ulipo sasa katika eneo hili la kiutawala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muundo wa sasa, kuanzia kitongoji/mtaa/kijiji/kata kuna Serikali za kuchaguliwa na wananchi ambazo zinafanya kazi moja kwa moja na wananchi hao. Kitendo cha hii nafasi ya kisiasa kwa ngazi ya jiji/manispaa/halmashauri kuongozwa na mwanasiasa ambaye hajachaguliwa na wananchi wote kunaondoa muunganiko muhimu wa uongozi katika mfumo mzima, kwani inakata uwakilishi wa Mbunge kama mwakilishi aliyechaguliwa na wananchi na msimamizi wa maendeleo ya wananchi waliomchagua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maoni yangu, nafasi hii inatakiwa ishikwe na kutumikiwa na Mbunge wa kuchaguliwa na wananchi. Kwenye jiji/manispaa au halmashauri zenye zaidi ya Wabunge wawili, vipindi vya uongozi vigawanywe ili kutoa fursa ya wote kuongoza jiji/manispaa au halmashauri. Kwa kufanya hivyo, Mbunge atasimamia vyema idara hii muhimu inayohusika moja kwa moja na maendeleo ya wapigakura katika jimbo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hoja zangu mbili hapo juu, naunga mkono hoja. (Makofi)