Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Arumeru-Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na ufinyu wa muda, na idadi kubwa ya wachangiaji kwenye bajeti ya TAMISEMI kwa mwaka wa fedha 2025/2026, naomba nitoe mchango wangu kwa maandishi kama ifuatavyo kwa kifupi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri, lakini pia kwa kazi nzuri sana anayowafanyia Watanzania akishirikiana na Naibu Mawaziri Mheshimiwa Dkt. Dugange na Mheshimiwa Zainab Katimba pamoja na watendaji wote Wizarani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nitoe shukrani zangu za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia fedha nyingi jimboni Arumeru Mashariki mabilioni ya fedha za Kitanzania kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika sekta zote za maji, afya, elimu, barabara, umeme wa REA; kwa mfano kwenye elimu tumepata shule tisa mpya za sekondari ndani ya miaka minne ya uongozi wa Mheshimiwa Rais na madarasa mapya 265, Chuo cha VETA, lakini wakati huo huo akitekeleza kwa ufanisi mkubwa miradi mikubwa ya kimkakati ifuatayo:-
(i)	Ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme kwa nguvu za maji la Julius Nyerere (JNHPP) umekamilika;
(ii)	Ujenzi reli ya kisasa (SGR) section ya Dar/Morogoro/Dodoma kwa ajili ya abiria umekamilika;
(iii)	Uboreshaji Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) unaendelea na shirika lina ndege 16; na
(iv)	Madaraja makubwa yamejengwa kwa mfano Kigongo Busisi, Tanzanite na Wami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio makubwa hapo juu, jimbo langu lina changamoto kadhaa kama zifuatazo:-
(a)	Changamoto kubwa ni barabara na inasababishwa na hali ya kijiografia ambayo siyo rafiki kwa barabara za udongo na tiba yake ni barabara za lami au kwa teknolojia mbadala ya tabaka gumu;
(b)	Tunashukuru Serikali imeanza kutujengea kwa kiwango cha lami barabara ya Akeri kuanzia Sangis hadi Ndoombo japo ujenzi unaenda kwa kusuasua. Tunaomba TARURA waongezewe bajeti waweze kukamilisha mradi huu;
(c)	Barabara ya Kingori inayoanzia Malula Kibaoni hadi Ngarenanyuki ni ahadi ya Rais iliyotolewa mwaka 2020 kwamba ingejengwa kwa kiwango cha lami na hadi leo haijatekelezwa. Nashauri Serikali itenge fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii kwa sababu ni ya kimkakati; na
(d)	Tuna ahadi pia ya kilometa tano za barabara za lami katika mji wa Usa River iliyotolewa mwaka 2015 lakini hadi leo haijatekelezwa. Nashauri pia Serikali itenge fedha kwa ajili ahadi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo rahisi kumaliza changamoto za maendeleo, itoshe kusema kwamba tunapongeza Serikali ya Awamu ya Sita imefanya kazi nzuri sana katika kipindi cha miaka minne, na bila kumumunya maneno, naunga mkono hoja.