Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema kwa kuturuzuku afya na siha njema na kuliwezesha Bunge lako Tukufu hili kujadili hoja ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026.

Mheshimiwa Spika, naomba nichukue fursa hii adhimu kuendelea kumshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuniteua kuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, hususan ninayeshughulika na masuala ya elimu. Kwa hakika, imani yake kwangu imeweka alama ya kipekee katika safari yangu katika kulitumikia Taifa langu.

Mheshimiwa Spika, kwa hakika ni fahari ya kipekee kuwa mnufaika wa malezi yake kwa viongozi wanawake wanaochipukia. Dhamana hii naitumikia kwa moyo wangu wote na ninamwomba Mwenyezi Mungu aendelee kuniongoza. Ahsante sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, natoa shukurani za dhati kwa viongozi wetu wakuu, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kwa miongozo yao mbalimbali na maelekezo ambayo wamekuwa wakitupatia ambayo imelenga katika kuboresha utekelezaji wa majukumu yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba pia nichukue nafasi hii kukushukuru wewe kwa kuliongoza Bunge hili kwa viwango vya hali ya juu. Kwa hakika viongozi wanaochipukia wanao mfano mzuri wa kujifunza uongozi wenye umakini, wenye uweledi na wenye viwango kutoka kwako. Tunakushukuru wewe na wasaidizi wako wote kwa ushirikiano ambao mmekuwa mkitupatia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee namshukuru Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa; ni kiongozi mahiri, kiongozi mchapakazi, mwenye uthubutu, ubunifu na ametuongoza na kutusimamia Ofisi ya Rais, TAMISEMI vema. Namshukuru sana kwa malezi yake kwetu, lakini kikubwa zaidi, namshukuru kwa kunipangia majukumu ambayo yamenipa nafasi ya kuendelea kujijenga katika utumishi wa Taifa langu. Kwa dhati ya moyo wangu, nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, aidha, namshukuru Naibu Waziri wa Nchi Mheshimiwa Dkt. Festo Dugange kwa ushirikiano ambao tumeujenga katika kutimiza majukumu yetu na kuwatumikia wananchi. Naishukuru Menejimenti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI ikiongozwa na Katibu Mkuu Ndugu Adolf Ndunguru kwa msaada wa kitaalamu ambao umeleta ufanisi katika majukumu yetu.

Mheshimiwa Spika, niendelee kutambua mchango wa kipekee kutoka Idara ya Elimu na Idara ya Miundombinu Ofisi ya Rais, TAMISEMI ambazo nimekuwa nikifanya nazo kazi kwa ukaribu.

Mheshimiwa Spika, pia nitambue mchango wa kipekee kutoka kwa wasaidizi wangu wote, Katibu wangu Wakili Frank Nkya, Karani, Waandishi wa Habari, bila kumsahau Dereva wangu Saidi Kimwaga, ambaye katika miezi 12 ambayo mimi nimehudumu kama Naibu Waziri, nimeweza kusafiri naye katika Mikoa 20, Halmashauri 56, Wilaya 49. Ahsanteni sana, natambua mchango wenu mkubwa katika kutimiza majukumu yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI ikiongozwa na Mwenyekiti, Mheshimiwa Justin Nyamoga na Makamu wake Mheshimiwa Jafari Chege kwa ushirikiano mkubwa ambao wamekuwa wakitupatia Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Maelekezo yao na ushauri wao umekuwa wa kujenga na kuboresha utekelezaji wa majukumu yetu.

Mheshimiwa Spika, nawashukuru wanawake wa Mkoa wa Kigoma kwa ushirikiano wao mkubwa ambao wamekuwa wakinipatia. Nawashukuru kwa kuniombea na kwa kunipa utulivu mkubwa ambao umeniwezesha kutekeleza majukumu yangu. Nathamini sana mchango wao, ahsanteni sana Mama zangu wa Mkoa wa Kigoma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge 73 wameweza kuchangia kwenye hoja hii na Waheshimiwa Wabunge wengi walijikita zaidi katika kutambua kazi kubwa ambayo imefanyika katika kuboresha sekta ya elimu, sekta ya afya, barabara ikiwa pamoja na utawala. Waheshimiwa wabunge shukurani zenu na pongezi zenu kwa Mheshimiwa Rais, tumezipokea na tutazifikisha. Maombi yenu mahsusi tumeyapokea na tayari tumeanza kuyafanyia kazi. Vile vile maoni na ushauri wenu pia wenye lengo la kuboresha tumeupokea na tutauzingatia katika utekelezaji wa majukumu yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sasa nizungumzie baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge, hususan zilizogusa kwenye sekta ya elimu. Waheshimiwa Wabunge walizungumza na wakauliza kuhusiana na hatua za utekelezaji wa Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la Mwaka 2023, lakini pia wakahoji kuhusiana na utekelezaji wa mtaala mpya wa elimu.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa taarifa kwa Bunge lako Tukufu kuwa Serikali tayari imeanza utekelezaji wa Sera Mpya ya Elimu ikiwa ni pamoja na mtaala mpya wa elimu. Kama tunavyofahamu, sera ya elimu imeboreshwa ili kuendana na mabadiliko ya kijamii, kisayansi, kiteknolojia na kukidhi mahitaji ya sasa ya Kitaifa na Kimataifa.

Mheshimiwa Spika, Sera ya Elimu inataka mitaala ya elimu iendane na mahitaji ya soko la ajira, lakini imeweka mkazo katika elimu ya ujasiriamali, teknolojia na ubunifu ikiwa ni pamoja na kumwezesha mwanafunzi kupata stadi za kazi mapema zaidi. Katika utekelezaji wa sera hiyo, Serikali imefanya yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anajenga shule za amali 103 kwa jumla ya shilingi bilioni 88.8. Shule hizo ni shule za amali ya ufundi kama vile useremala, uwashi, umakenika, lakini kuna amali ambazo siyo za za ufundi, kama vile upishi, ususi, mapambo, ushonaji, kilimo na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, tafsiri yake ni kwamba mwanafunzi anapohitimu, atahitimu atakuwa ana cheti kile kinachojulikana cha Form Four ambacho kinatolewa na NECTA lakini mwanafunzi huyu atakuwa ana cheti cha pili ambacho kinatolewa na NACTVET ambacho kitakuwa kinatambua ule ufundi na ujuzi ambao ameupata akiwa shuleni.

Mheshimiwa Spika, tafsiri yake ni kwamba mwanafunzi huyu akiamua kuendelea na Kidato cha Tano na cha Sita atatumia cheti chake cha NECTA, ataendelea kusoma Kidato cha Tano na cha Sita kuendelea mpaka chuo kikuu, lakini kutumia ujuzi wake na ufundi aliyojifunza, anaweza kujiajiri yeye mwenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tafsiri kubwa ya uwekezaji huu ni kwamba ile changamoto ambayo tumekuwa nayo ya wahitimu wetu kukosa ujuzi wa kuweza kujiajiri wenyewe na kuwa tegemezi kwenye ajira rasmi, basi ndiyo tunasema unakuwa umefika mwisho. Haya ni mapinduzi makubwa sana katika sekta ya elimu na huyo ndiye Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Spika, vilevile Serikali imekarabati na kununua vifaa vya ufundi na amali katika shule 28 za amali zilizokuwepo na imetumia gharama ya shilingi bilioni nne katika kufanya hivyo. Hii ni kuendelea kuweka msukumo katika elimu ya amali kama vile sera mpya ya elimu inavyotamka.

Mheshimiwa Spika, halikadhalika ili kuwezesha utekelezaji wa mtaala mpya, Serikali imefanya mafunzo kwa walimu 181,777 wa elimu ya awali na msingi, walimu 103,000 wa sekondari na wasimamizi na wafuatiliaji wa utekelezaji wa mitaala 6008. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, aidha, katika utekelezaji wa mtaala wa elimu kwenye eneo la matumizi ya TEHAMA katika kujifunza na kujifunzia Serikali tayari imenunua na kusambaza vifaa vya TEHAMA vyenye thamani ya shilingi bilioni 8.9 vikiwemo computer za mezani 2,621, computer mpakato 431, projector 591, printer 360, Television janja kwa ajili ya ufundishaji mubashara 200, camera za kidijitali 200, camera za zoom 200 pamoja na UPS 662.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2025/2026 Serikali itaendelea na ununuzi wa vifaa vya TEHAMA katika shule 400 za Sekondari. Huu ni uwekezaji mkubwa uliyofanyika na Serikali ya Awamu ya Sita ili kuwezesha utekelezaji wa Sera Mpya ya Elimu ikiwa ni pamoja na mtaala mpya wa elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge walizungumza kuhusiana na ukarabati wa shule kongwe za msingi. Serikali inatambua kuna shule za msingi ambazo zilijengwa katika miaka 1940, na huko nyuma miaka mingi iliyopita, na kwamba shule hizo ni chakavu na zinahitaji ukarabati mkubwa.

Mheshimiwa Spika, Serikali katika kipindi cha mwaka 2021 mpaka 2025 imekarabati shule kongwe za msingi 840 kwa gharama ya shilingi bilioni 76.79. Aidha, madarasa 1,700 yamejengwa upya kwa gharama ya shilingi bilioni 33.12. Serikali itaendelea na utaratibu huu wa kutenga fedha kila mwaka wa bajeti kwa ajili ya kuhakikisha kwamba shule kongwe zinaendelea kukarabatiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge walizungumza kuhusiana na upungufu wa walimu katika shule za msingi na shule za sekondari. Sote tunafahamu kutokana na utekelezaji wa programu ya elimu bila malipo, udahili wa wanafunzi umeongezeka mara dufu na hivyo imetokea mazingira ambayo kuna uhitaji wa ongezeko la walimu.

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuajiri walimu ambapo katika kipindi cha mwaka 2021/2024 Serikali imeajiri walimu wa awali, msingi na sekondari 29,817. Katika kipindi cha mwaka 2025 Serikali imetoa kibali cha kuajiri walimu 15,925 ambapo mpaka wakati huu walimu 13,105 wamepangwa katika shule mbalimbali na wanaendelea ku-report.

Mheshimiwa Spika, endapo walimu wote wa ajira mpya hii ya mwaka 2025 wata-report tutakuwa tuna jumla ya walimu 45,742 waliyoajiriwa katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita. Aidha, Serikali itaendelea na mikakati ya kuajiri walimu kwa mikataba, na kutumia walimu wanaojitolea na pia kutumia teknolojia ya TEHAMA kufundishia kwa maana ya kuwa na madarasa au ufundishaji mubashara kupitia madarasa janja pamoja na mkakati wa kuwatumia walimu walio katika mafunzo kwa vitendo. Serikali itaendelea na jitihada hizi zote ili kuongeza walimu katika shule zetu za msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mambo ambayo yamefanyika katika kipindi cha Awamu ya Sita ni mambo mengi sana lakini naomba nizungumze kidogo kuhusiana na uwekezaji wa shilingi trilioni 5.1 kwenye upande wa miundombinu ya msingi na sekondari. shule zetu za msingi na sekondari, lengo la uwekezaji huo ikiwa ni kuhakikisha kwamba vijana wote, watoto wetu wote ambao wapo katika umri wa kwenda shule, basi wanapata nafasi ya kwenda shule, lakini wasiende shule tu, bali waende shule wakapate elimu iliyo bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha miaka minne...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Dakika mbili.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais amejenga shule mpya 2,441, amejenga vyumba vya madarasa 61,875, amejenga nyumba za walimu 1,792, amejenga mabweni 738, amejenga maabara 811 na amekarabati shule kongwe 906.

Mheshimiwa Spika, kipekee kabisa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amejenga shule 26 za wasichana za Sayansi za bweni, moja katika kila Mkoa wa Tanzania bara ili kutoa fursa kwa watoto wa kike kusoma masomo ya Sayansi ili kuwaepusha pia na vishawishi au mazingira ya vishawishi yanayoweza kukatisha masomo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule hizo zina maabara ya TEHAMA, zina maabara ya masomo ya Sayansi, zina maktaba ya kisasa na shule hizo kila moja imegharimu jumla ya shilingi bilioni 4.45. Huyo ndiyo Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hizi ni baadhi tu ya hoja za Waheshimiwa Wabunge, lakini hoja zote zitajibiwa kwa maandishi.

SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, dakika mbili malizia.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, ahsante. Hizi ni baadhi tu ya hoja za Waheshimiwa Wabunge, lakini hoja zote za Waheshimiwa Wabunge zitajibiwa kwa maandishi. Pia ushauri na maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI umepokelewa na tutauzingatia katika utekelezaji wa majukumu yetu.

Mheshimiwa Spika, ombi langu kwa Bunge lako Tukufu ni moja tu, Waheshimiwa Wabunge tembeeni kifua mbele. Kazi yenu ya kibunge mmeifanya kwa ufanisi mkubwa, mmeisimamia Serikali, mmeishauri Serikali na kwa namna ya kipekee mmewasemea wananchi wenu.

Mheshimiwa Spika, hili limekuwa ni Bunge lenye ufanisi mkubwa na ninyi Wabunge mna sifa ya kuendelea kuaminiwa na wananchi wenu kuwawakilisha katika Bunge hili. Kilichobaki tuungane kwa pamoja kuwaeleza wananchi mafanikio haya katika sekta ya elimu na sekta nyingine nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nawaomba Wabunge wote na Watanzania tuungane kumwombea Mheshimiwa Rais wetu afya, nguvu na uwezo wa kuendelea kulitumikia Taifa, na itakapofika Oktoba mwaka huu 2025 twende tukampe kura nyingi za ushindi Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Spika, nawaomba Watanzania tumpe Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan timu imara ya Wabunge na Madiwani watakaoenda kushirikiana naye katika kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Kwa kazi kubwa ya kishindo aliyoifanya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni dhahiri kabisa tukimwongezea muda atafanya mambo makubwa zaidi. (Makofi)

Mhshimiwa Spika, kwa muktadha huo, naomba Bunge lako Tukufu lipitishe bajeti hii ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ili Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan iende ikafanye kazi. Baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)