Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, kwanza, nakushurukuru sana kwa fursa hii ya kuchangia hotuba ya bajeti Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa mwaka huu 2025/2026. 
Mheshimiwa Spika, nianze kwa dhati kabisa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijalia afya njema na uhai na kuniwezesha kushiriki katika kupitisha bajeti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, mwaka 2025/2026. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, kwa dhati ya moyo wangu naomba nitumie fursa hii kumshukuru sana, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwanza, kwa kuniamini katika kipindi hiki cha miaka minne kuwa Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Heshima hii ni kubwa sana. 
Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa imani yake kubwa kwangu, na ninamuahidi katika kipindi hiki kilichobaki nitaendelea kuchapa kazi kwa uadilifu, kwa nguvu na kwa kujituma, kama ambavyo nilikuwa nikifanya siku za huko nyuma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri na kubwa anayoifanya ya kuliongoza Taifa letu. Sisi sote kama Wabunge na wananchi ni mashahidi. Mheshimiwa Rais katika kipindi cha miaka minne amefanya kazi ya kutukuka, amefanya kazi ya kupigiwa mfano, amefanya kazi ya kihistoria katika kuwekeza kwenye miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, katika kuwekeza kwenye miradi ya kiuchumi, amekuwa ni mfano ndani ya Taifa letu, pia nje ya Taifa letu. Kwa hakika Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anastahili kupongezwa, anastahili kupata nafasi nyingine ya kuliongoza Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kila Mtanzania mwenye nia njema aliposikia maamuzi ya Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi wa kumpitisha Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kishindo, kwa kauli, kwa kura 100%, kuwa Mgombea wa Urais wa Chama cha Mapinduzi, kila Mtanzania mwenye mapenzi mema na nchi hii, alifurahi na kupongeza sana, kwa sababu, Mheshimiwa Rais anastahili kwa kazi aliyoifanya. Kazi aliyofanya inaongea, tunatumia nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais na kumtakia kila la heri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, nampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Emmanuel John Nchimbi, Balozi, kwa kuaminiwa na Chama cha Mapinduzi kuwa Mgombea Mwenza wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tunamfahamu ni mchapakazi, kiongozi thabiti na tunaamini timu yetu baada ya uchaguzi itakuwa ni timu bora sana ya kuleta maendeleo katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tatu, nampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kupewa imani kubwa na Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi kuwa Mgombea Urais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Tunamfahamu ni mchapakazi na tunawaombea viongozi wetu hawa wote kila la heri, nasi watatukuta majimboni tukiwa tumeshinda kwa kishindo kura za maoni, tunatafuta kura zao na kura zetu na kura za Madiwani, ili Chama cha Mapinduzi kiendelee kuongoza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tatu, nitumie fursa hii kwa dhati kabisa kuwapongeza Viongozi wetu Wakuu wa Kitaifa. Wamefanya kazi kubwa ya kutuelekeza na kutuongoza Ofisi ya Rais, TAMISEMI, na pia wamefanya kazi kubwa ya kumshauri na kumsaidia Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 
Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nampongeza sana Mheshimwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ninampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati. Tunawapongeza viongozi wetu kwa kazi kubwa waliyoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nne, Waheshimiwa Wabunge katika michango yao wamepongeza kazi kubwa inayofanywa na Ofisi ya Rais, TAMISEMI na wamesema inakwenda kwenye direction sahihi. Kazi hii, sifa hizi na pongezi hizi zote zimrejee Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuwa, kwa mikono yake ndiye aliyeiunda Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ndiye aliyeweka Watendaji Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ndiye aliyekiweka chombo hiki katika maji kiweze kuelea kwenye direction ambayo inaleta matunda makubwa kwa Watanzania.
Mheshimiwa Spika, baada ya kufanya hivyo, alimweka nahodha Madhubuti, naye sio mwingine, ni Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Kwa hakika Mheshimiwa Mchengerwa, mtu kazi ni mtu kazi kweli kweli, siyo mchezo. Ni mchapakazi, ni mtu mahiri, ni kiongozi rahimu. Mheshimiwa Mchengerwa tunakushukuru sana kwa uongozi wako uliotukuka katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI na kwangu mimi, wewe ni zaidi ya Mwalimu.
Mheshimiwa Spika, sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tunajivunia kazi kubwa aliyoifanya ya kuiongoza Wizara hii ya TAMISEMI. Ninaamini Wananchi wa Rufiji hawatafanya makosa kwa sababu, wamempata kiongozi mwakilishi, na pia, kiongozi ambaye ni asset ya Taifa letu la Tanzania katika kutuhudumia Watanzania wote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kuwapongeza na kuwashukuru Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Ndugu Ndunguru, Naibu Makatibu Wakuu, Ndugu Mtwale, Ndugu Mwambene pamoja na Ndugu Mativila, kwa kazi kubwa wanayofanya, na pia timu nzima ya Wataalamu Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ngazi ya Makao Makuu. Ngazi ya Mikoa Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa tunatambua kazi yao kubwa sana wanayoifanya; Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi mpaka ngazi za Mitaa na Vijiji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa dhati kabisa, nitumie nafasi hii kukupongeza sana wewe mwenyewe kwa kazi kubwa nzito unayoifanya ya kuliongoza Bunge letu Tukufu. Umekuwa Mheshimiwa Spika wa mfano mzuri sana ndani na nje ya nchi yetu na Rais wa Mabunge ya Dunia. Umetuheshimisha katika kila sehemu uliyokwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunajivunia sana kazi yako nzuri, tunakuombea na kwa hakika ninaamini wananchi wa Jimbo la Mbeya hawatafanya makosa, kwa sababu, tangu dunia imeumbwa hawajawahi kupata Spika. Leo wana Mbunge, ambaye ni Spika. Ninaamini kabisa watatumia tunu hiyo kwa uhakika zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kwa dhati kabisa kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wenzangu. Mimi kwa miaka hii minne na nusu nimekuwa nikijibu hoja zenu hapa. Mmenipa ushirikiano wa hali na mali na ninawashukuru mmekuwa mkiridhika na hoja zangu. Nawashukuru sana kwa namna ambavyo mmenipa ushirikiano huu na niwaombe katika kipindi hiki kifupi kilichobaki mwendelee kunipa ushirikiano huu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nawashukuru sana familia yangu, mke wangu mpenzi Alafisa Moses Dugange. Nawashukuru sana watoto wetu Neema, Upendo na Christian. Vilevile nawashukuru sana Wapigakura wa Jimbo langu la Wanging'ombe, tumefanya kazi kubwa, Mheshimiwa Dkt. Samia ametuheshimisha. Miradi ambayo imetendeka katika Jimbo la Wanging'ombe haijawahi kutokea tangu kuumbwa kwa dunia, na ninaamini watanirudisha kwa kishindo kuja kuendelea kutumikia wananchi wa Jimbo la Wanging'ombe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wametoa michango mingi na mizuri. Kwa muktadha huu, naomba, nichangie eneo la sekta ya afya ya msingi. 
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miaka minne katika historia hii ya Tanzania, haijawahi kutokea uwekezaji mkubwa uliofanywa katika miundombinu ya huduma za afya, ngazi ya msingi. Mheshimiwa Rais katika kipindi cha miaka minne ametenga zaidi ya shilingi trilioni 1.270, kwa ajili ya miundombinu ya huduma za afya. Amejenga hospitali za Halmashauri, amekarabati hospitali za Halmashauri, jumla ya hospitali 129. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi, katika maeneo yetu kulikuwa na kilio kikubwa cha hospitali za Halmashauri. Mheshimiwa Rais amemaliza kilio cha hospitali za Halmashauri katika nchi yetu ndani ya kipindi cha miaka minne. Hakika Mheshimiwa Dkt. Samia anastahili kupongezwa, amefanya kazi ya kupigiwa mfano. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, vituo vya afya. Kumekuwa na changamoto kubwa ya vituo vya afya. Tuliainisha kata za kimkakati na ndani ya miaka minne, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amejenga vituo vya afya vipya zaidi ya 367, vimeanza kutoa huduma. Amejenga zahanati 980 zinatoa huduma, lakini amepeleka vifaatiba vya kiwango, tuna digital X-Ray, tuna mashine za Ultrasound, tuna vifaa vya kisasa vya maabara, wananchi wetu wananufaika na huduma hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kwamba, Mheshimiwa Rais amefanya mapinduzi makubwa ya kihistoria kwenye sekta ya afya ya msingi na ndiyo maana tumeona katika kipindi cha miaka hii minne, vifo vya akina mama wajawazito vimepungua kutoka 556 kati ya vizazi hai 100,000 mpaka vifo 104 kati ya vizazi hai 100,000. Suala hili limeshangaza dunia nzima kwa sababu, kazi ya kupungua kwa vifo hivyo siyo ya kawaida, lakini imetokana na kazi nzuri na uwekezaji mzuri wa usimamizi mzuri wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hakika Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anastahili kupewa maua yake kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kusimamia sekta ya afya. Ndiyo maana dunia imemtambua kwa kumpa The Global Goal Keepers Award ambayo ni tuzo adimu na adhimu, lakini Mheshimiwa Rais wetu ndani ya miaka minne ameipata kwa kazi nzuri ambayo ameifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika sekta ya afya msingi, huko nyuma hatukuwa na msamiati wa ICU, Intensive Care Unit, katika huduma za afya msingi. Hatukuwa na msamiati majengo ya huduma za dharura (Emergency Medical Department), hatukuwa na msamiati wa mitambo ya kuzalisha hewatiba ya Oksijeni ngazi ya msingi. Huduma hizi zote zilikuwa zinapatikana ngazi ya Hospitali za Rufaa za Mikoa na ngazi ya Hospitali za Kanda na Hospitali ya Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo tunaongea hapa, Mheshimiwa Rais amejenga majengo ya huduma za afya ya dharura katika Hospitali za Halmashauri. Majengo 80 yamewekewa vifaatiba na yanatoa huduma. Amejenga majengo ya wagonjwa mahututi 30 katika ngazi za halmashauri na vituo vya afya, yanatoa huduma na amejenga mitambo 21 kwa ajili ya huduma za afya.
Mheshimiwa Spika, leo hatulazimiki kufuata hewa ya Oksijeni Hospitali ya Kanda wala Hospitali ya Taifa kwa sababu, Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa sana ya kimapinduzi ndani ya miaka minne. Kwa hakika Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuheshimisha na anastahili kupongezwa kwa kazi nzuri na kubwa aliyoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na changamoto kubwa ya magari ya wagonjwa, kulikuwa na changamoto kubwa ya magari ya usimamizi wa huduma za afya. Leo tunaongea ndani ya miaka miwili, uliongoza Bunge hili kugawa magari ya wagonjwa kila jimbo. Majimbo yote 214 yalipata magari ya wagonjwa.
Mheshimiwa Spika, jumla ya magari 382 ya wagonjwa yamegawiwa katika majimbo yetu katika halmashauri zetu na yanatoa huduma, lakini jumla ya magari 210 ya huduma za usimamizi yamepelekwa katika majimbo yetu, mikoa yote 26 pia imepata magari ya usimamizi. Hii ni kazi kubwa. Tunafahamu bado kuna mahitaji ya vituo vya afya, bado kuna mahitaji ya magari na Serikali hii ya Awamu ya Sita ni Serikali sikivu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ndiyo maana leo kuna ahadi ya Serikali ya majimbo yote 214 kupata vituo vya afya. Leo wakati naongea na Mheshimiwa Waziri, tayari Serikali imeshatenga shilingi bilioni 30 kwa awamu ya kwanza, kwa ajili ya majimbo 120 ya vijijini na majimbo haya yatapata fedha wakati wowote kuanzia sasa. Wizara ya Fedha ipo hatua za mwisho za ukamilishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, ahadi ya Serikali hii sikivu ni ya vitendo, na mtaona hivi karibuni mnapata fedha katika kata zile ambazo mliainisha wenyewe. Hatufanyi mabadiliko ya kata yoyote, kila kata iliyoainishwa na Mbunge ndiyo ambayo itapelekewa kituo cha afya na tutahakikisha tunapeleka mapema iwezekanavyo awamu hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, majimbo yale ya mijini na mengine yatapata fedha awamu ya pili, nazo zitakuwa ndani ya muda mfupi kwa maana ya kuhakikisha kwamba, majimbo yote 214, kama ilivyo ahadi ya Serikali yanapata vituo vya afya. Kwa hiyo, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, wawe na amani, mambo hayo yanakwenda kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wakati wa kuchangia hapa, Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum, Mheshimiwa Anatropia, alitoa hoja kwamba, mafanikio haya hayajaigusa Halmashauri ya Kyerwa. Naomba nimpe taarifa kwamba, Halmashauri ya Kyerwa katika kipindi cha miaka minne, sekta ya afya peke yake, imepewa zaidi ya shilingi bilioni 17.629 ambapo tayari imejenga Kituo cha Afya cha Rutunguru shilingi milioni 500, Mabila shilingi milioni 500, Murongo shilingi milioni 410, Nkwenda shilingi milioni 36, jengo la X-Ray na mortuary shilingi milioni 18.
Mheshimiwa Spika, kama haitoshi, Serikali hii pale Kyerwa peke yake imepeleka fedha za kujenga zahanati 11. Zahanati hizo tayari saba zimekamilika, jumla ya shilingi milioni 674 zimetumika katika kujenga zahanati zile. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nyumba mpya za watumishi zimejengwa saba katika Jimbo la Kyerwa. Pia Mheshimiwa Rais amepeleka fedha za dawa na vifaatiba kwa Halmashauri ya Kyerwa zaidi ya shilingi bilioni 7.470 katika kipindi cha miaka minne na wananchi wa Kyerwa wanaendelea kupata huduma. Amepeleka watumishi 110 na kadhalika orodha ni ndefu. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Anatropia kwamba, Serikali hii inafanya kazi yake ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wakati naelekea kuhitimisha, naomba nitumie fursa hii niwahakikishie wananchi wote wa Tanzania kwamba, Serikali hii sikivu ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeonesha kazi yake kwa vitendo na kila mmoja, kila Mtanzania, ana kila sababu ya kuiunga mkono Serikali ya Awamu ya Sita. Mimi ninaamini mafanikio haya makubwa kabisa yanatokana na kazi nzuri iliyofanywa na Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaamini, kama ambavyo pacha wangu amesema kwamba, kazi hii ya mikono ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, sisi tulikuwa vidole vyake kuhakikisha majimbo yetu yanapata miradi na inakamilika kwa wakati. Ninaamini Waheshimiwa Wabunge wote kwa hakika Mwenyezi Mungu atatujalia tutarejea kwa ajili ya kuendelea kujenga Taifa letu na kuwahudumia Watanzania wenzetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya, nitambue kabisa mchango na ukaribu wa pacha wangu, Mheshimiwa Zainab Athman Katimba, Naibu Waziri. Tunafanya kazi vizuri sana, kama mapacha, na kwa hakika nakupongeza sana kwa kazi nzuri unayofanya. 
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya, nakushukuru sana. Nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge, nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri. 
Mheshimiwa Spika, naomba Waheshimiwa Wabunge tupitishe bajeti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kwa kishindo, kwa ajili ya miradi hii tuliyoisema na mingine ambayo ipo kwenye kitabu hiki. 
Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, naomba kuwasilisha na ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)