Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Rufiji
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, katika kuanza hotuba hii, napenda kwa unyenyekevu mkubwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, kwa kutuwezesha kuja hapa kutazama tulikotoka, tulipo na tunakoelekea, kama Taifa lenye mwelekeo chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutulinda, na pia kwa kutupa jukwaa la majadiliano haya ambayo siyo tu tunapanga bajeti, bali tunachora hatima ya mamilioni ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama tunavyofahamu, Tanzania ni nchi huru, tutatetea bila hofu haki yetu ya kufanya maamuzi yetu wenyewe kuhusu utaratibu wetu wa kujitawala. Kama alivyosema Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwenye hotuba yake ya Tuwashe Mwenge ya Mwaka 1992, “na TAMISEMI ndio jukwaa la kujitawala kwa vitendo kwenye vijiji, kwenye mitaa, kwenye kata, kwenye halmashauri, kwenye shule zetu, kwenye barabara na kwenye hospitali zetu.” (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa heshima ya kipekee, namshukuru kwa dhati Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye katika kipindi kifupi ameonesha kwamba, maendeleo yanawezekana. Yanaweza kusimamiwa kwa upendo na yakafanyika kwa kasi bila kelele, lakini kwa matokeo. 
Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia, amekuwa mfano wa kiongozi wa kisiasa mwenye mapenzi na kona zote za nchi hii amehakikisha kwamba, mwenge wa maendeleo hautakiwi kuangaza mijini pekee, bali kuingia hadi kwenye mitaa ya pembezoni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sisi TAMISEMI tumepewa kibatari hicho kuusambaza mwanga huo wa matumaini. Pia, Mheshimiwa Dkt. Samia siyo tu anaongoza nchi, anawasha mwenge wa fikra za maendeleo jumuishi wa diplomasia yenye staha na mwelekeo wa kimaendeleo. Sisi TAMISEMI tumepewa mwenge huo, si kuutazama, bali kuupeleka kila kona ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, aidha, nitumie nafasi hii adhimu kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Amiri Jeshi Mkuu na Rais wetu wa Tanzania, kwa kuendelea kuniamini kuwatumikia wananchi wa Tanzania katika nafasi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI. 
Mheshimiwa Spika, naendelea kumuahidi kuwa, nitafanya kazi hii kwa bidii, kujituma na maarifa zaidi, ili kuhakikisha ndoto yake ya kuijenga TAMISEMI iliyo bora inatimia. Kwani mafanikio ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ni mafanikio ya Serikali kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, hii ni kwa kuwa, TAMISEMI ni maisha ya kila siku ya Mtanzania, ina jukumu katika maisha ya kila Mtanzania, ya kila mwananchi. 
Mheshimiwa Spika, kipekee kabisa nakupongeza wewe mwenyewe Spika wetu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Mabunge ya Dunia. Wanambeya, nitakwenda kuwaambia huko huko Mbeya tarehe 26 wiki hii, kwamba uwezo wako, nafasi yako na kazi kubwa ambayo umeifanya kwa taifa hili. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza viongozi wote wa Bunge hili Tukufu kwa kuliongoza Bunge letu hili kwa hekima na kwa weledi wa hali ya juu. Mmeonesha kwa dhati kuwa Bunge hili halisimamii tu bajeti, linajenga historia. 
Mheshimiwa Spika, mmejadili hoja hizi kwa uzito wa kitaifa, siyo kwa muktadha wa maeneo tu; na kama alivyosema Baba wa Taifa, tukiendeleza tabia ya kujadiliana bila kugombana, tutakuwa tumewasha mwenge wa ukweli wa demokrasi ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo hoja hizi zimekuwa taa ya kuangaza giza la changamoto za wananchi wetu. Mmeonesha uongozi bora kwa kuhakikisha kwamba majadiliano yenye tija yanakuwa msingi wa kujadili au Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali ikiwa Ofisi ya Rais TAMISEMI. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hakuna anayeweza kubeza, maoni, hoja na ushauri uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge kwa sababu ndani ya maneno yao kuna sauti za wananchi, kuna macho ya jamii na kuna mwanga wa mwelekeo. Maoni hayo siyo mapambo ya mijadala ya Bungeni, bali ni dira ya kusimamia kwa umakini utekelezaji wa mpango wa bajeti ya mafungu yote 28 ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kwa lengo la kuimarisha huduma kwa kila Mtanzania bila ubaguzi wa kijiografia wala hali ya kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, kama alivyosema Hayati Edward Sokoine akisimama kwa sauti ya wananchi, Serikali yoyote inayoshindwa kusikiliza kilio cha wananchi wake, basi haina sababu ya kuendelea kuitwa Serikali yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa msingi huu, hoja zenu Waheshimiwa Wabunge hazitapita kama taarifa ya kusikilizwa, bali kama mwanga wa hatua, kama mwenge wa utekelezaji, na kama alama ya dhamira mpya ya TAMISEMI inayojengwa kwa nguvu ya wananchi na misingi ya haki na usawa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI. Natumia fursa hii kuwathibitishia kuwa, maoni yao, ushauri wao, utazingatiwa na kuwa dira ya kuimarisha utendaji na utoaji huduma bora kwa wananchi. 
Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru na kutambua mchango wa viongozi wenzangu na wataalamu wa Ofisi ya Rais TAMISEMI. Kipekee, nawashukuru Manaibu Mawaziri, Mheshimiwa Dkt. Festo John Dugange, Mbunge na Mheshimiwa Zainab Athuman Katimba, Mbunge.
Mheshimiwa Spika, vilevile naishukuru Menejimenti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI ikiongozwa na Ndugu Adolf Ndunguru kwa kazi kubwa ya uchambuzi na ushirikiano walionipatia wakati wa kuandaa ufafanuzi wa hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge wakati wa kujadili mpango wa bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, imekuwa ni fursa adhimu kwangu kufanya kazi na timu hii yenye uadilifu, yenye watu wenye vipaji, uzalendo, ubunifu na kujitoa kwao kwa dhati kupigania maendeleo ya wananchi. 
Mheshimiwa Spika, leo sisimami kwa niaba ya Wizara tu, bali kwa niaba ya watu. Leo sijasimama kuhitimisha hoja tu, bali kuwasha mwenge; mwenge wa dhamira, mwenge wa matumaini, mwenge wa mabadiliko. Kama alivyosema Baba wa Taifa, mwenge huu siyo wa mashua/mshumaa bali wa kuangaza hata walio porini. Ndiyo maana ninasema, tuwashe mwenge wa TAMISEMI. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika zama ambapo Taifa letu linahitaji dira, tumaini na utendaji unaogusa maisha, wapo walio pembezoni. Leo siyo siku ya kutoa maelezo tu, bali ni siku ya kuwasha mwenge wa dhamira mpya ya TAMISEMI. 
Mheshimiwa Spika, kama alivyosema Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika hotuba yake ya kihistoria ya Tuwashe Mwenge ya Mwaka 1992, kuongoza ni kuonesha njia, lakini ni vigumu kuonesha njia gizani bila taa wala dira. Kwa hiyo, leo siyo mwanga wa takwimu, bali ni mwanga wa mwelekeo wa watu. Leo hatusemi tuwashe mwenge wa maneno, tunakwenda nao kwenye matendo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika Taifa letu TAMISEMI ni moyo wa maisha ya kila siku ya mwananchi. Hii ni kwa sababu, TAMISEMI ndipo ndoto huandikwa kwenye daftari la shule la kata, TAMISEMI ndipo maumivu hupona katika zahanati ya kijiji, ndipo fursa huinuka kupitia masoko ya mama lishe, na ndipo barabara za TARURA huunganisha vijana wa kijijini na soko la mjini. 
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, TAMISEMI siyo ofisi, bali ni mfumo wa maisha. Siyo Wizara tu pekee, ni tafsiri ya kiini cha utawala wa karibu. Kwa hiyo, nitende haki leo kwa kusema kwa sauti kubwa na ya faraja kwamba tuwashe mwenge wa TAMISEMI mpya, tusizime ndoto za walio mbali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wakati wa kujadili Hotuba ya Mpango wa Bajeti Ofisi ya Rais, TAMISEMI, mwaka 2025/2026, Waheshimiwa Wabunge 77 walipata fursa ya kuchangia ambapo Wabunge 73 walipata fursa ya kuchangia kwa kuzungumza na Wabunge wanne walichangia kwa njia ya maandishi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hoja za Waheshimiwa Wabunge zilijikita katika maeneo yafutayo: -
(a)	Ujenzi wa ukarabati wa matengenezo ya barabara;
(b)	Usimamizi na uendeshaji wa elimu msingi na sekondari;
(c)	Utaratibu na usimamizi wa huduma za afya ya msingi, ustawi wa jamii na lishe;
(d)	Usimamizi wa matumizi ya fedha za wajibu wa makampuni kwa jamii (CSR);
(e)	Kuongeza mapato ya ndani ya halmashauri;
(f)	Kuthibiti matumizi ya mapato ya ndani ya mamlaka za Serikali za mitaa;
(g)	Uwezeshaji wananchi kiuchumi;
(h)	Ujenzi wa masoko na stendi;
(i)	Upungufu wa watumishi katika sekta ya elimu na afya na;
(j)	Usimamizi wa utoaji wa fedha za mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia maeneo niliyoyataja hapo juu, napenda kutoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali ambazo zimeibuliwa na Kamati, pamoja na Waheshimiwa Wabunge wakati wa kujadili Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa mwaka wa fedha 2025/2026. 
Mheshimiwa Spika, hoja za Kamati, moja ilisema, Serikali ifanye tathmini ili kubaini ukubwa wa tatizo la upungufu wa matundu ya vyoo katika shule zote nchini, shule za msingi na sekondari.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa sensa ya elimu ya msingi ya mwaka 2024, shule za msingi zina mahitaji ya matundu ya vyoo 429,599. Vyoo vilivyopo ni matundu 240,320, na upungufu ni matundu 189,279. Wastani wa uwiano uliopo kwa wavulana ni tundu moja kwa wavulana 47, badala ya tundu moja kwa wavulana 25. Kwa upande wa wasichana ni tundu moja kwa wasichana 43 badala ya tundu moja kwa wasichana 20.
Mheshimiwa Spika, upande wa sekondari mahitaji ni matundu 135,870 ya vyoo. Yaliyopo ni matundu 84,608 na upungufu ni matundu 51,262, ambapo wastani wa uwiano uliopo kwa wavulana ni tundu moja kwa wavulana 36 badala ya tundu moja kwa wavulana 25 na wasichana ni tundu moja kwa wasichana 35 badala ya tundu moja kwa wasichana 20.
Mheshimiwa Spika, ninakiri kwamba, bado tunakabiliwa na changamoto ya matundu ya vyoo katika shule zetu. Changamoto ambayo siyo ya miundombinu pekee, bali ni changamoto ya utu wa mwanafunzi, heshima ya elimu na uhai wa Taifa letu. Kwa TAMISEMI, choo siyo jengo tu, la hasha, ni sehemu ya usalama ya mtoto wa kike, ni ishara ya hadhi ya mwanafunzi wa Kitanzania, na ni kipimo cha thamani tunayoiweka katika elimu ya watoto wa maskini. 
Mheshimiwa Spika, kama alivyoona Hayati Mzee Abeid Aman Karume, kwa hekima na ujasiri wa kweli wa mwananchi, kama tunataka wananchi waishi kama binadamu, basi ni lazima tuanze kuwaheshimu kama binadamu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa mantiki hiyo, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, inatambua kuwa ujenzi wa vyoo siyo suala la kiufundi tu, bali ni jukumu la kimaadili. Tutaendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha kwamba kila shule nchini inakuwa na mahali pa staha, siyo kwa kusoma tu, bali pia kwa kuishi kwa heshima. 
Mheshimiwa Spika, choo cha staha ni haki ya mwanafunzi, ni chozi lisiloonekana, lakini lenye kuumiza. Kuuwasha mwenge wa heshima shuleni ili tuzime giza la aibu ya vyoo visivyofaa. Hii ndiyo dhamira mpya ya TAMISEMI inayojali uhai wa mwanafunzi kama inavyojali kitabu anachokishika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mkakati wa Serikali ni kuendelea kutenga kila mwaka fedha za ujenzi wa matundu ya vyoo kwa shule za elimu ya msingi na sekondari. Mkakati uliopo sasa ni kuhakikisha kuwa, kila darasa linalojengwa kunakuwa na ujenzi wa angalao matundu mawili ya vyoo. Aidha, mwaka 2025/2026 Serikali imepanga kujenga matundu 28,580 ya vyoo, yatakayogharimu zaidi ya shilingi bilioni 66.57 katika shule za msingi na sekondari. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema awali, Serikali haijalala katika hili. Lengo ni kuhakikisha shule zetu zinakuwa mahiri, salama pa kufundishia na kujifunzia. 
Mheshimiwa Spika, pili, Serikali isimamie fedha zote zinazotokana na CSR, zitolewe kwa wananchi kama sheria inavyotaka. 
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amewahi kusema, madini ni fursa na ni lazima tuyatumie kwa ajili ya maendeleo endelevu. Kutokana na usemi huo, Serikali inaendelea kusimamia mipango na fedha za wajibu wa makampuni kwa jamii zinazotolewa kwa wananchi. 
Mheshimiwa Spika, aidha, imeendelea kufuatilia utekelezaji wa miradi inayotekelezwa kupitia fedha hizo katika halmashauri husika. Ofisi ya Rais, TAMISEMI, imekubaliana na Wizara ya Madini kuendelea kujenga uelewa wa CSR kwa halmashauri, wamiliki wa leseni za madini na wananchi kuhusu wajibu kwa wamiliki wa leseni za madini kwa jamii, kama ilivyoelezwa kwenye Kifungu Namba 105 cha Sheria ya Madini Sura Namba 123 na Kanuni ya 18 ya Kanuni za Wajibu wa Wamiliki wa Leseni za Madini kwa Jamii ya mwaka 2023. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kuhakikisha kuwa CSR zinazotolewa na makampuni nje ya sekta ya madini nazo pia zinasimamiwa ipasavyo, Ofisi ya Rais TAMISEMI inakamilisha Mwongozo wa Usimamizi wa CSR Nje ya Sekta ya Madini. Maoni kutoka kwa wadau mbalimbali yameshakusanywa yakiwemo ya wanufaika wa CSR katika halmashauri 184, mikoa 26, kampuni na taasisi zinazotoa CSR 17, Wizara saba, Tume ya Madini na Tume ya Mipango na taasisi mbili zinazoguswa na makampuni yanayotoa CSR. 
Mheshimiwa Spika, aidha, baada ya kukamilisha uchambuzi na kuboresha rasimu iliyoandaliwa, itawasilishwa kwenye Kamati ya kudumu ya Bunge ya TAMISEMI ili kupata maoni yao kabla ya kukamilisha. Lengo ni mwongozo huo kuanza kutumika katika mwaka 2025/2026. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tatu, Serikali iunde Kamati ndogo itakayokuwa na jukumu la kufanya utafiti na kutoa maoni kuhusu namna bora ya utoaji wa matumizi ya fedha zinazotokana na CSR. Sheria inayosimamia utoaji wa matumizi ya fedha za CSR ipo chini ya Wizara ya Madini ambayo inatekezwa chini ya Kanuni za Wajibu wa Wamiliki wa Leseni za Madini na Wananchi kuhusu wajibu wa wamiliki wa leseni za madini, yaani CSR za mwaka 2023.
Mheshimiwa Spika, Kanuni ya 9 (2) ya kanuni hizo inatoa nafasi kwa Waziri mwenye dhamana kwa masuala ya Serikali za Mitaa kwa kushirikiana na Waziri mwenye dhamana ya masuala ya fedha kuunda kamati ya pamoja ambayo jukumu lake itakuwa ni kuwashauri Mawaziri husika kuhusu mpango wa CSR inayowasilishwa kwa ajili ya idhini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuimarisha Kamati za ushauri zinazopitia mipango ya CSR. Aidha, maoni ya Kamati ya kuunda timu ya utafiti yatafanyiwa kazi. 
Mheshimiwa Spika, nne, ni kuhusu usimamizi wa maeneo ya wazi ya mapumziko ya umma. Mamlaka ya Serikali za Mitaa hususan miji na majiji yote nchini, ziweke mikakati ya kutenga maeneo mahususi kwa ajili ya mapumziko ya wananchi, na Serikali iandae mwongozo wa utengaji, uendelezaji na ulinzi wa maeneo ya mapumziko ya wananchi ili yasipangiwe matumizi mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwongozo wa utekelezaji wa mipango kabambe wa mwaka 2022, unatoa maelekezo ya utengaji, uendelezaji na ulinzi wa maeneo ya mapumziko ya umma. Aidha, Ofisi ya Rais, TAMISEMI itazisimamia mamlaka za miji na wilaya zote nchini zihakikishe kuwa maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya mapumziko ya umma yanalindwa, yanaendelezwa na kusimamiwa kama yalivyopangwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tano, Serikali iweke mpango mkakati wa kupeleka vifaa vya maabara kwenye shule 26 za sayansi za wasichana za mikoa bila kuathiri mpango uliowekwa wa upelekaji wa vifaa vya maabara katika shule nyingine za sekondari nchini. 
Mheshimiwa Spika, vifaa vya maabara kwa shule 486 vimeshanunuliwa katika awamu mbili. Usambazaji wa awamu ya kwanza unahusisha shule 231 zikiwemo shule 26 za sayansi za wasichana za mikoa. Hadi sasa, shule nane kati ya 26 za wasichana za mikoa zimepokea vifaa hivyo na usambazaji katika shule 18 zilizobakia unaendelea.
Mheshimiwa Spika, vifaa vya maabara na kemikali kwa awamu ya pili kwa ajili ya shule 255 zilizobaki zinatarajiwa kupokelewa na kusambazwa kabla ya tarehe 30 mwezi Juni, 2025. Aidha, Serikali imenunua na kusambaza kemikali za maabara katika shule za sekondari 231 za kata. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sita, Serikali ibuni chanzo cha kudumu cha fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya maabara kwa shule za sekondari nchini. Serikali imekuwa ikitoa fedha za ununuzi wa vifaa vya maabara kwa shule za sekondari nchini kupitia ruzuku ya uendelezaji wa shule.
Mheshimiwa Spika, ununuzi wa vifaa vya maabara vilevile hufanyika kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali, ikiwemo miradi ya kuimarisha elimu ya sekondari, mpango wa Lipa Kulingana na Matokeo na Michango ya Wadau. Hivyo, Serikali itaendelea kuimarisha mpango wa bajeti kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya maabara na kemikali za maabara ili kuhakikisha vinapatikana kwa uhakika na kwa wakati kwa ajili ya ujifunzaji na kufundishia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, saba, ni kuhusu usimamizi na uendelezaji wa shule za mchepuo wa kiingereza katika halmashauri. Tumeshauriwa halmashauri kuacha kabisa kujihusisha na ujenzi wa shule za mchepuo wa Kiingereza kwa kutumia fedha yoyote ile ya Serikali na kutoza ada kubwa, kuwa inakwenda kinyume na mpango wa Serikali wa utoaji wa elimu bila ada. 
Mheshimiwa Spika, pili, tumeshauriwa halmashauri zenye uhitaji wa kuanzisha shule za mchepuo wa Kiingereza, ziombe kibali kutoka Ofisi ya Rais, TAMISEMI; na tatu shule za mchepuo wa Kiingereza katika halmashauri zianzishwe zikiwa na utawala wake binafsi na zisitumie rasilimali za watu kutoka Serikalini. Serikali iwarejeshe katika shule zao za awali walimu waliochukuliwa kutoka shule za umma na kupelekwa kwenye shule za mchepuo wa Kiingereza Serikalini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, imepokea hoja hii na itafanya uchambuzi kwa kushirikiana na Wizara inayosimamia sera ya elimu ili kupata utekelezaji mzuri kuhusu hoja hii.
Mheshimiwa Spika, nane, Serikali ilipe kwa wakati madeni mbalimbali ya watumishi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa nchini ili kuondoa malimbikizo ya madeni. Serikali imeendelea kulipa madeni ya watumishi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa katika mwaka 2023/2024, shilingi bilioni 116.08 zimetolewa kwa ajili ya kulipa madeni ya watumishi, ambapo mishahara ni shilingi bilioni 32.22 na madeni yasiyo mishahara ni shilingi bilioni 83.85. 
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2024/2025 hadi Machi, 2025 madeni yenye thamani ya shilingi bilioni 78.75 yameshalipwa. Kati ya fedha hizi, shilingi bilioni 16.32 ni madeni ya mishahara na shilingi bilioni 62.43 ni madeni yasiyo ya mishahara yanayojumuisha fedha za uhamisho, likizo na stahiki za watumishi. Ofisi ya Rais, TAMISEMI kupitia Ofisi za Wakuu wa Mikoa, imekamilisha zoezi la uhakiki wa madeni ya watumishi yasiyo ya mishahara kufikia mwaka 2023/2024. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nasisitiza kuwa, zipo halmashauri 36 zimeonekana zina uwezo wa kulipa zenyewe kutokana na mapato yao ya ndani, hivyo ninazielekeza zilipe mara moja, na zile halmashauri 145 zisizo na uwezo, taarifa ya uhakiki wa madeni imeshawasilishwa Wizara ya Fedha kwa ajili ya kuendelea na hatua zinazofuata. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali imedhibiti uzalishaji wa madeni mapya ya kimshahara kwa kuingiza kwa wakati watumishi wote wanaoajiriwa kwa mara ya kwanza katika payroll ya Serikali, kwa kuhakikisha marekebisho ya mishahara yanafanyika kabla ya mtumishi kupata barua ya kupanda daraja na kuingizwa kwenye payroll ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, posho za watumishi wanaokaimu madaraka, aidha uzalishaji wa madeni yasiyo ya kimshahara yamedhibitiwa kwa kutoa ruzuku kwa ajili ya gharama za likizo, uhamisho na stahiki za viongozi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tisa, utengaji wa fedha za mikopo ya vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani unatofautiana kati ya halmashauri moja na nyingine. 
Mheshimiwa Spika, kuna halmashauri ambazo zinatenga fedha kwa kutumia mapato ya ndani yote na kuna halmashauri ambazo zinatenga kwa kutumia mapato ya ndani yote na kuna halmashauri ambazo zinatenga kwa kutumia mapato ya ndani yaliyotengwa kwenye fungu la maendeleo. Serikali inashauriwa kuandaa mwongozo mmoja utakaotumika kwa ajili ya kutenga fedha hizo katika halmashauri zote nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumeipokea hoja hii. Mikopo ya vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu inatolewa kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa Sura Namba 290, Kifungu cha 37 na Kanuni za Usimamizi wa Utoaji wa Mikopo kwa Wanawake, Vijana na Wenye Ulemavu za mwaka 2024. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa sheria, mikopo hiyo inatengwa kutokana na 10% ya mapato ya ndani yasiyolindwa ambayo yanajumuishwa kwenye fedha za maendeleo za mapato ya ndani ya halmashauri. Aidha, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ilishatoa maelekezo mahususi na kuwafundisha wataalamu wanaohusika na utoaji wa mikopo katika halmashauri zote nchini. 
Mheshimiwa Spika, vilevile, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imeshatoa kwa mara nyingine maelekezo hayo kwa mikoa yote kwa ajili ya kukokotoa mikopo ya vikundi vya wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine ni kuhusu Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini ziendelee kubuni vyanzo vipya vya mapato, mbali na tozo za ushuru wa mazao na ambavyo havitawakandamiza wananchi. 
Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha imeandaa mwongozo ambao utawezesha mamlaka za Serikali za Mitaa kubuni vyanzo vya mapato vya ndani kulingana na fursa zinazopatikana katika maeneo husika. 
Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali inahimiza halmashauri kuendelea kujikita kwenye uwekezaji wa miradi ya uzalishaji ya vitega uchumi vyenye tija katika kuongeza mapato ya halmashauri kwa kutumia vyanzo mbadala vya kugharamia miradi. 
Mheshimiwa Spika, pia, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa inaendelea kutoa mafunzo kwa mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhusu namna ya uibuaji wa vyanzo vipya vya mapato, kuwezesha uandishi wa miradi ya kimkakati na matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika kuongeza ukusanyaji na udhibiti wa upotevu wa mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kutokana na hatua hizo, bajeti ya mapato ya ndani ya halmashauri imeongezeka kutoka shilingi bilioni 814 mwaka 2020/2021 hadi shilingi trilioni 1.35 kwa mwaka 2024/2025, sawa na ongezeko la 66%. Aidha, makusanyo ya mapato yameongezeka kutoka shilingi bilioni 757.05 mwaka 2020/2021 hadi shilingi trilioni 1.15 mwaka 2023/2024, sawa na ongezeko la 57%. Mwaka 2024/2025 makusanyo yanatarajiwa kufikia shilingi trilioni 1.35, sawa na 79% ambapo hadi Machi shilingi trilioni 1.04 sawa na 77% zimeshakusanywa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nilithibitishie Bunge lako Tukufu kuwa, ubunifu wa vyanzo vipya vya mapato ni moja kati ya vigezo mbalimbali vya kupima utendaji wa viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa. 
Mheshimiwa Spika, naomba sasa nije kwenye hoja za Waheshimiwa Wabunge zilizotolewa kwa kuzungumza. Katika mjadala wa hoja za bajeti, Mheshimiwa Mrisho Gambo, Mbunge wa Arusha Mjini, aliwasilisha tuhuma nzito kuhusu miradi miwili mikubwa inayotekelezwa na Halmashauri ya Jiji la Arusha, yaani ujenzi wa jengo la utawala la Halmashauri na ujenzi wa Soko la Semunge. 
Mheshimiwa Spika, katika yote mawili, Mheshimiwa Mrisho Gambo aliibua hoja zinazodai kuwepo kwa upotevu mkubwa wa fedha za umma, matumizi mabaya ya madaraka na mchanganyiko wa vipimo uliopelekea malipo yasiyo halali. 
Mheshimiwa Spika, kwa heshima kubwa ya Bunge hili na kwa maslahi ya Taifa, nina wajibu wa kuweka bayana ukweli wa mambo haya. Taarifa ya uchunguzi na ufuatiliaji imekamilika. Kwa kibali chako, tutakuwa tayari kuiwasilisha mbele ya Bunge lako hili Tukufu kwa namna utakavyoona inafaa. 
Mheshimiwa Spika, pia, kwa unyenyekevu mkubwa, niruhusu niseme maneno ya mwisho kabisa. Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ni wananchi na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ni Serikali hasa. Niwathibitishie Watanzania, hakuna senti ya Watanzania iliyopotea katika miradi yote hii miwili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni muhimu tutofautishe hoja za kujenga, na lugha za kuchomea. Tuhuma zisizo na mzizi, siyo hoja. Ni cheche za siasa ambazo hazifai kuwekwa ndani ya taasisi zenye misingi ya sheria. Miradi ya maendeleo haijengwi kwa maneno, bali kwa mchakato. Tuhoji kwa hoja na tusihukumu kwa jazba. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa itaendelea kulinda uwazi, kuchukua hatua za uwajibikaji na kuhakikisha taasisi zake haziingii katika hofu kwa sababu ya siasa za majukwaa. Kama kuna jambo la kuchunguzwa tutalifuatilia hasa, lakini kama ni juhudi za kuwaza visasi kupitia minong’ono ya kisiasa, Serikali hii haitatoa nafasi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara, natambua uwepo wa changamoto za ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara katika maeneo mbalimbali nchini. Katika kushughulikia changamoto hiyo, Serikali imeendelea kutenga fedha kupitia TARURA kwa ajili ya ujenzi, matengenezo na ukarabati wa barabara, ambapo bajeti imeongezeka kutoka shilingi bilioni 275 kwa mwaka 2020/2021 hadi shilingi bilioni 772 mwaka 2024/2025, sawa na ongezeko la 180.8% ya fedha ya ndani. 
Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali kwa kushirikiana na Benki ya CRDB imeratibu uanzishwaji wa hatifungani ya miundombinu iitwayo Samia Infrastructure Bond iliyolenga kukusanya shilingi bilioni 150, ambapo hadi dirisha la ununuzi wa hisa lilipofungwa, shilingi bilioni 323, sawa na 215.33% zimekusanywa na zitatumika kuwakopesha kwa masharti nafuu wakandarasi watakaoingia mikataba ya kazi za TARURA. (Makofi) 
Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kupitia TARURA iliidhinishiwa fedha za dharura shilingi bilioni 71.46 kwa ajili ya kugharamia matengenezo ya miundombinu ya barabara zilizoathiriwa na mafuriko ya maji ya mvua. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 50 ni nyongeza ya bajeti kwa mwaka 2024/2025, ambapo hadi Machi, 2025, shilingi bilioni nane zimepokelewa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwaka 2025/2026, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imepanga kutumia shilingi trilioni 1.18 kwa ajili ya ujenzi, matengenezo na ukarabati wa miundombinu ya barabara, usafiri na usafirishaji wa vijijini na mijini. 
Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa itahakikisha inaendelea kutoa fedha za ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara. Hii inatokana na ukweli kuwa, kila kilometa mpya ya barabara inayojengwa ni daraja kati ya umasikini na maendeleo, njia ya mtoto kufika shuleni, mama kufika hospitali, mkulima kupeleka mazao sokoni na Taifa kusonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu usimamizi na uendeshaji wa elimu msingi na sekondari. Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, inatambua umuhimu wa kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia ambapo imeendelea kujenga na kukarabati miundombinu ya elimu pamoja na kuendeleza mazingira ya maeneo hayo. 
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuwekeza katika utoaji wa elimu msingi na sekondari ambapo mpango wa elimu msingi bila ada umeongezewa bajeti kutoka shilingi bilioni 249.66 mwaka 2020/2021 hadi shilingi bilioni 510.96 mwaka 2025/2026. Hii ni sawa na ongezeko la shilingi bilioni 261.30, sawa na 104.66%. 
Mheshimiwa Spika, Serikali imeboresha na kuzipatia vifaa shule 330 zikiwemo shule 28 za mchepuo wa elimu ya ufundi wa amali, shule 274 za mchepuo wa kilimo na shule 28 za mchepuo wa biashara. Hii ni kuhakikisha watoto wa Tanzania wanapata elimu yenye ujuzi na maarifa yatakayowawezesha kujiajiri na kujitegemea. Vilevile, Serikali imeajiri walimu 45,808 wakiwemo walimu 477 wa elimu maalum na 127 wa lugha za alama. (Makofi) 
Mheshimiwa Spika, kwa nafuu ya muda, naomba nitumie nafasi hii kulithibitishia Bunge lako kuwa, hoja zote zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge zimepokelewa na nimetoa maelekezo ya kuandaa mpango kazi wa utekelezaji na taarifa yake itawasilishwa kwa maandishi. 
Mheshimiwa Spika, nawahakikishia Waheshimiwa Wabunge kuwa tunathamini sana michango yao na kila hoja iliyotolewa itapatiwa majibu au ufafanuzi. Ndiyo maana tunasema tumewasha mwenge. Siyo mwenge wa siasa tupu, bali ni mwenge wa dhamira na matumaini kwamba hakuna mtoto anayepaswa kukatishwa masomo kwa kukosa dawati, hakuna mkulima anayepaswa kuozewa na mazao yake shambani kwa kukosa barabara, na hakuna kijana anayepaswa kugeuka mwizi kwa kukosa fursa. 
Mheshimiwa Spika, kwa maneno ya Mwalimu, “Tanzania ni nchi huru, tutatetea bila hofu haki yetu ya kufanya maamuzi yetu wenyewe kuhusu utaratibu wetu wa kujitawala”, na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa niaba ya Serikali ya Awamu ya Sita, tupo mstari wa mbele kutekeleza dhamira hiyo. 
Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, ni nani anayetaka Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuwa gulio la kisiasa badala ya kuwa chombo cha mabadiliko halisi? Kama alivyosema Mwalimu, “CCM isiyo na itikadi itakuwa ni soko huru la wanaotafuta vyeo.” Hali kadhalika Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa isiyo na dira itakuwa ni orodha ya mafungu ya bajeti na taasisi na siyo mabadiliko. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo siyo tu tunahitimisha hoja ya kibajeti, bali tunaanza ukurasa mpya wa utendaji. Ninatamani sana baada ya bajeti hii wananchi waseme, Bunge la Mwaka 2025 liliandika historia ya mabadiliko ya kweli. Tuwashe mwenge huu, tuuwashe kwa wengine. Tusikubali mwanga huu uzimike kwa sababu ya hofu, uzembe au ukosefu wa dhamira. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia, napenda kutumia nafasi hii kutoa maelekezo mahususi kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya wajikite kikamilifu katika kulinda amani, mshikamano wa Kitaifa na ufanisi wa utendaji wa Serikali katika maeneo yao. Wakuu wa Mikoa hamtakiwi kuwa watazamaji wa migogoro, bali wazima moto wa chokochoko na walinzi wa misingi ya haki, maendeleo na umoja wa Kitaifa. 
Mheshimiwa Spika, utulivu wa nchi unaanza pale ambapo viongozi wa chini wanatimiza wajibu wao bila kusubiri maagizo kutoka juu. Tuwashe mwenge wa ulinzi wa jamii, tuzime cheche za migogoro midogo inayoweza kuwa ni moto mkubwa katika Taifa hili. 
Mheshimiwa Spika, sasa naomba Bunge lako likubali kuidhinisha Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka 2025/2026 yenye jumla ya shilingi 11,782,984,202,000 kwa ajili ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na taasisi zote zilizo chini yake Fungu namba 56; Tume ya Watumishi wa Walimu, Fungu namba mbili; na mafungu 26 ya mikoa yakijumuisha halmashauri 184. 
Mheshimiwa Spika, ninaomba kutoa hoja. (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, ninaafiki.