Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlalo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi, nianze kwa kuwapongeza Mheshimiwa Waziri Pindi Chana pamoja na Katibu Mkuu, lakini na Wakuu wote wa Taasisi zilizo chini ya Wizara hii ya Maliasili na Utalii kwa kazi kubwa ambayo wanaendelea kuifanya.
Mheshimiwa Spika, nipongeze pia kwa hatua hii ya ukuaji wa Sekta ya Utalii kama ambavyo hotuba ya Waziri imesema. Kwa kweli tunafarijika sana na hasa tukiamini kwamba huu ni mchango mkubwa sana wa mwana diplomasia namba moja Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye dhamira yake ya dhati katika kukuza sekta hii kila Mtanzania anaiona na kwa kweli tunaendelea kumwombea kwa Mwenyezai Mungu basi aendelee kuboresha huduma na ustawi katika Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nina maeneo mahsusi kama matatu hivi niyachangie kwa haraka kutokana na changamoto ya muda.  Eneo la kwanza; pamoja na ukuaji wa Sekta ya Utalii lakini bado tuna changamoto ya wanyamapori hasa sisi ambao tunakaa pembezoni mwa hifadhi. Kule Lushoto tuko pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi na hifadhi hii inapatikana katika Mikoa miwili ya Kilimanjaro na Tanga, lakini kwa kweli wenzetu wa TANAPA sehemu kubwa sana wamelalia katika Mkoa wa Kilimanjaro kwa huku Tanga haionekani sana kiasi kwamba sisi tunakumbana tu na athari za hawa wanyama hasa ndovu na mbogo ambao wakikimbizwa maeneo ya Mkoa wa Kilimanjaro wengi wanakimbilia katika wilaya zetu hasa Lushoto.
 Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nitoe rai kwamba yale yote ambayo tumezungumza hapa kama mbinu za kwenda kuwadhibiti zifanyike kwa uwiano. Haipendezi sana kuona kwamba tunajenga vituo vya kuwakimbiza katika wilaya zingine halafu tunaacha wilaya zingine katika ushoroba uleule kiasi kwamba maana yake ni kwamba unapowafukuza eneo moja kwa njia rahisi tu ni kwamba wanaenda kwenye eneo lingine. Kwa hiyo, hilo ni muhimu sana kuliangalia.
Mheshimiwa Spika, mpaka sasa sisi tumepoteza zaidi ya wananchi wanne, wamevamiwa na ndovu na wamepoteza maisha na mwananchi mmoja yeye amevamiwa na mbogo. Kwa ujumla wananchi watano katika Halmashauri ya Lushoto Tarafa ya Umba.
Mheshimiwa Spika, hawa wananachi takribani 1728 wanaendelea kusubiri malipo yao ya fidia mbalimbali ambazo wamechukuliwa taarifa zao zote, lakini mpaka sasa hawajalipwa fidia na hili lilikuwa agizo la Mheshimiwa Rais alivyokuja kwenye Wilaya ya Lushoto tarehe 24 Februari, alitoa maelekezo mahsusi kwamba fidia hii ikalipwe kwa haraka ili wananchi hawa waweze kunufaika angalau na hayo malipo ya fidia.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, Sekta ya Kilimo imeathirika zaidi ya hekari 5,178 katika hiyo Tarafa ya Umba na sehemu kubwa hapa ni zao la mkonge, zimeathiriwa vibaya na wanyama hawa waharibifu na hii inasababisha umaskini watu wetu kwa sababu kilimo kama cha mkonge kupanda mpaka kuvuna ni zaidi ya miaka mitatu minne, sasa umeshapanda unafikia katika hatua ya kuanza kuvuna tembo wanakuja wanafyeka shamba zima hiyo kwa kweli ni kuwarudisha nyuma wananchi, tunaomba jitihada ziongezeke ili kuhakikisha kwamba wananchi hawa wananufaika na rasilimali zinazowazunguka.
Mheshimiwa Spika, hapa ninapozungumza nina barua ya Wizara ambayo ilikuwa inazitaka halmashauri zaidi ya 44 ambazo zinazungukwa na hifadhi zipeleke vijana wasiopungua watano ili wakapewe mafunzo maalum ya uhifadhi, lakini katika Mkoa wa Tanga kwa maana sisi tunaozunguka Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi kuna Wilaya ya Mkinga, Wilaya ya Korogwe na Wilaya ya Lushoto. Vijana wa Wilaya ya Mkinga na Wilaya ya Korogwe wamechukuliwa, lakini kule Lushoto vijana watano mpaka sasa hivi hawajachukuliwa na tumepeleka barua yetu na nakala yake ninayo hapa vijana hawa watano kutoka Kijiji cha Kivingo hawajaitwa kwenye yale mafunzo na wenzano sasa wanakaribia kukamilisha mafunzo. 
Mheshimiwa Spika, ninaiomba Wizara hili jambo imeomba yenyewe na imeenda kuwasaili hawa vijana ni muhimu sana kuleta usawa katika Taifa letu. Kama ambavyo nimetangulia kusema haitapendeza majirani zetu wao wanafukuza tembo maana yake wakiwafukuza watakuja kwenye maeneo yetu, sisi bila mafunzo tutawezaje kuwaondoa katika maeneo yetu? Kwa hiyo, hili ni jambo ambalo tungeomba sana lifanyike haraka vijana hawa na wenyewe wakapate mafunzo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la pili katika ziara ya Mheshimiwa Rais, hivyo hivyo aliahidi kutumegea eneo kupitia msitu/shamba la TFS pale Lukozi takribani ekari nne ambazo tumeomba. Barua zote tumezipeleka Wizarani tangu mwaka 2023, Katibu Mkuu nimewasilisha kwake, Waziri nimekutumia nakala Naibu Waziri nimekutumia nakala. Tunaomba sana Mheshimiwa Rais siku ile ameeleza kwa ufasaha sana kwamba ombi hili lishughulikiwe haraka kwa sababu kata hii ni kata ya kimkakati ambapo tunakusudia kujenga soko la Kimataifa la mbogamboga ili mbogamboga zote zinazotoka katika Wilaya ya Lushoto zianzie katika eneo. 
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tumeshafanya maongezi ya awali na wenzetu wa shamba wameridhia na wamezileta barua kwenye mamlaka zao ambapo ni ofisini kwako Mheshimiwa Waziri, basi tunaomba kwa msisitizo huu na ile ahadi ya Mheshimiwa Rais hili nalo liende likakamilike. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho, siyo kwa umuhimu ni jambo la uvunaji wa hewa ukaa (carbon). Kama Mheshimiwa Waziri utakumbuka Mheshimiwa Rais alitupongeza wananchi wa Lushoto kwa kuwa watunzaji wazuri wa mazingira. Kwa hiyo, nasi tungependa tunufaike na utunzaji ule na uhifadhi ule wa misitu kwa kuvuna hewa ya ukaa. Tunaiomba sana Wizara iwe msaada kwetu kutusaidia kupata elimu na mafunzo mbalimbali kwa sababu misitu tunayo ya kutosha na wananchi wako na utayari wa kutosha ili na sisi tuweze kushiriki katika fursa hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaomba kuunga mkono hoja, na ninakushukuru sana. (Makofi)