Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia, lakini kutokana na muda nitagusa maeneo mawili suala la Nyatwali na uharibifu wa wanyamapori. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Mji wa Bunda ipo kwenye top ten ya halmashauri ambazo zinaathirika na wanyamapori, lakini tuna upungufu wa vifaakazi kwa ajili ya doria na hiyo inasababisha athari kubwa kwa wananchi kudhuriwa na wanyamapori hususani tembo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hivi ninavyozungumza hekari 5,398 za mazao mbalimbali zimeathiriwa na tembo. Hivi ninavyozungumza wananchi 1,483 mashamba yao yameathirika na hawajalipwa mpaka leo, hivi ninavyozungumza ng’ombe 800 wameuawa wananchi hawajalipwa, hivi ninavyozungumza ng’ombe 355 wameathirika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wanaoathirika hawa ni wananchi maskini kabisa, ni wananchi wa kawaida, lakini mpaka leo hakuna kifuta jasho, hii athari iko kwenye Kata mbalimbali za Halmashauri na Jimbo la Bunda Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niwatajie haya maeneo ili myafanyie kazi na mkitaka hata nyaraka nitawaletea. Kunzugu, Ichamu, Kiharagweta, Changuge, Bukore, Mashujaa, Nyamatoke, Tairo, Mitimirefu, Balili, Rubana, Mcharo, Utakare, Idara ya Maji, Nyasana, Guta, Makongeni, Stooni, Kunanga, Gushigwamala, Nyabehu, Kurugongo, Kunzugu, Bukore, Tairo, Ihale, Guta Mjini, Kinyambwiga na Guta B. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hawa wananchi wa maeneo haya wamekaa zaidi ya miaka miwili wananchi zaidi ya 1400 hawajalipwa hekari zaidi ya elfu tano mia tatu tisini na zimeteketezwa, ng’ombe zaidi ya 800 wameuwa, ng’ombe zaidi ya 355. Hivi Mheshimiwa Waziri tunataka wananchi wa Jimbo la Bunda Mjini waone kuwa na mbuga isiwe fahari tena?
Mheshimiwa Spika, ninaamini tukitengeneza mazingira mazuri ya kulinda wananchi wanaozungukwa na hifadhi, hifadhi hizi hazitahitaji zilindwe na mtutu. Hifadhi hizi zitalindwa na raia wema ambao wataona thamani ya mbuga yao na wao kunufaika. Dada yangu Mheshimiwa Pindi Chana na kaka yangu ninaomba watusaidie wananchi wa Halmashauri ya Bunda Mjini wapate haki yao, ninaomba sana hali ni mbaya! Huku kumesababisha njaa sasa hivi, watu wanalima, ngombe wanafuga, ng’ombe zinauliwa, zinajeruhiwa mashamba yao yanaliwa na tembo, wana zaidi ya miaka miwili hawajalipa fidia. Wapo akina mama, wapo vijana, wapo wazee wangu, tafadhali sana leo naongea kwa upole hili jambo ni kubwa mno. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hawa wananchi wameteseka sana wanahitaji fidia tumechoka sisi watu wa Mara hatupendi kuomba chakula, lakini hii njaa inasababishwa na wanyama wakali. Kama wameshajua kwenye halmashauri kumi hizi wanaathirika na wanyamapori kwa nini hawafanyi doria ya mara kwa mara? Leo hii mifugo ikienda hifadhini ni shida, mnyama akidhurika ni shida, lakini wananchi pia wanaathirika. (Makofi)
 Mheshimiwa Spika, tunapenda mbuga zetu tunajua zinachangia pato kwenye Serikali yetu, lakini lazima tu-balance wananchi walindwe, wananchi wahakikishiwe mazao yao, mifugo yao ili mambo yaende, kuwe kuna furaha kotekote kusiwe na furaha kwa upande mmoja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimemsikia Mheshimiwa Waziri amezungumzia suala la Nyatwali na amesema watu zaidi ya 3000 wamelipwa na amesema kuna makaburi yamehamishwa. Ni kweli kabisa malipo yapo, lakini malipo hayo ni yaleyale waliyokuwa wakilalamikia, leo wamewatoa kwenye eneo ambalo wanalipwa square meter 480 wamehamia kwenye eneo ambalo wameenda kununua square meter zaidi ya 2000. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, siyo sawa bado wananchi wa Nyatwali wanalia na wanalalamika na mimi leo wazee wangu wananchi wa Nyatwali wakiongozwa na Diwani wa Kata ya Nyatwali wanakuja Dodoma nitawaleta ofisini kwako. (Makofi)
 Mheshimiwa Spika, watu zaidi ya 384 vilevile hawajlipwa na kuna taarifa kwamba tayari fedha zimetokoa Wizara ya Fedha zimekwama Maliasili. Wale wengine wamewaondoa kwa kidogo na hawa watu bado wako pale, miundombinu wameshaibomoa, wamebomoa shule, wamebomoa mahospitali, watoto hawaendi shule. Siyo sawa, hata hayo makaburi wameyahamisha hawakuhamisha kwa staha, watu wameenda kwa mitutu ya bunduki wanafukua miili wanaichanganya na aliyefanya ni Mkuu wa Wilaya ambaye ninaona sasa hivi amehamishwa. Hatuwezi kuvumilia mambo kama haya tunataka kila mtu alindwe kutokana na utu wake. (Makofi)
 Mheshimiwa Spika, leo watu hawana sehemu za kuishi, wanafunzi wengine hawaendi shule, lakini kwenye huko kuhamisha Halmashauri yetu ya Mji ilikuwa imejenga majengo pale yamebomolewa, lakini kuna baadhi ya wale waliohama wamewahamishia kwenye maeneo mengine, fidia ya halmashauri yetu kwa ajili ya kwenda kuendeleza miundombinu kwa idadi ya watu wale ambao wamewapeleka kule ikoje? Maana watoto wameenda kwenye shule zingine wanahitaji madarasa! Kwa hiyo, hilo Mheshimiwa Waziri nilikuwa ninahitaji nipate majibu sahihi, wananchi wangu kwenye suala la fidia, wananchi wangu kwenye suala la Nyatwali na hili nililizungumza tangu nikiwa kijana kabisa mpaka sasa hivi mtu mzima na Brighton ana miaka 20 sasa. (Makofi)