Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Riziki Saidi Lulida

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Mimi nianze kwanza kwa kuipongeza Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na timu yetu ya Mawaziri Dkt. Pindi Chana na Naibu wake Kitandula lakini bila kuwasahau watendaji wakuu wanaoongozwa na Katibu wetu Mkuu Dkt. Abbas. Kwa kweli, wanafanya kazi nzuri sana ya kuendeleza utalii.

Mheshimiwa Spika, siyo kidogo kutoka asilimia ambazo tulikuwa tunazipigia kelele huko nyuma kwamba sasa utalii Tanzania hauko vizuri leo tumefika asilimia 132, siyo kitu cha kawaida ni kwa sababu ya juhudi kubwa ambayo anafanya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia program mbalimbali ambazo Mheshimiwa Waziri amezisoma ikiwemo na Royal Tou. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais na sisi tutaendelea kumuunga mkono katika jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na mambo mengine mazuri ambayo Mheshimiwa Rais anafanya kwenye Sekta hii ya Utalii, kwa mara ya kwanza kabisa kuna maombi ambayo yapo hata kwenye taarifa ambayo Mheshimiwa Mwenyekiti wetu wa Kamati, Mheshimiwa Mnzava amewasilisha, kuna fedha ambazo alitoa Mheshimiwa Rais kwa ajili ya maendelezo ya utalii (TDL), fedha zile ni nyingi na zinahitaji umakini mkubwa sana halijaongelewa hapa hilo suala lazima niliongelee kidogo. Fedha zile zinahitaji umadhubuti na umakini mkubwa katika kuzitumia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, fedha zile Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan amezitoa kwa nia njema ili kuendeleza utalii, yako mambo mengi ndani mle kwa ajili ya kuendeleza utalii, lakini zipo taasisi ambazo zimeshaanza kutumia fedha hizo wanaendelea kuzitumia kwa ajili ya kuendeleza utalii, lakini zipo ambazo ninafahamu, karibu bilioni 17 bado hazijatumika na kuna baadhi ya maneno mengi ya mashaka kuhusiana na fedha hizo.

Mheshimiwa Spika, ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri kupitia Katibu wako Mkuu Dkt. Abbas wanafanya kazi nzuri sana fedha hizi kwa sababu mama amezitoa kwa nia njema ziende kutumika kwa nia njema hiyo hiyo. Maana kuna watu wakiishaona fedha zimetoka basi wanapeleka vitu vingine havijafanyiwa hata tathmini ya kutosha, uchambuzi wa kutosha, wanapeleka kuomba fedha zile. Zile fedha ni nyingi na huko ndiko kunaweza kukatokea upigaji, fedha hizi zilindwe ziende kwa madhumuni ambayo Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametarajia zitafanya kazi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninavyofahamu pia hizi fedha hazijakaguliwa bado na CAG, ikiwezekana CAG atakapoanza kufanya kazi basi apitie kuangalia hizi fedha alizoweka Mama za kuendeleza utalii je, zitatumika ama zinatumika kama ilivyokusudiwa? Ili yale malengo ambayo Mama anayatarajia katika Sekta ya Utalii ambayo tunafanya vizuri sana yaweze kutimia.

Mheshimiwa Spika, hilo lilikuwa la pili, katika hayo hayo mambo ya kitalii tulikuwa Arusha kama ripoti ya Kamati inavyosema kwenye mambo ya vyakula, tunafanya kazi au tuna sifa kubwa kwenye maeneo mengi, lakini kwenye chakula bado kidogo. Kwenye hoteli zetu za kitalii alikuwepo hivi karibuni Balozi wa India, alikuja kule Arusha na alikutana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha kuna baadhi ya vyakula hasa vya Kia sia nikichukulia mfano wenzetu Wahindi siyo wengi sana kama walivyo wazungu na mataifa mengine kwenye utalii wetu kwa sababu ya vyakula, kwa hiyo waangalie kuhusu vyakula wanafanyaje.

Mheshimiwa Spika, wanyama waharibifu wapo hata kule Tabora Igombe kule tunalo ongezeko kubwa la viboko wananchi wanaathirika, ninaomba sana kwenye kulipa fidia wasikawize fidia zao kwa sababu wanakuwa wamejeruhiwa na wengine wamepata madhara ya vifo, lakini tusisahau pia wapinzani wanatumiaga sana hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wanyama hawana uzazi wa mpango, kule wao wanazaliana na wamedhibitiwa ni wengi hata barabarani tunakutana nao, hata Arusha tulivyoenda tembo wako barabarani, tuangalie namna gani tutawavuna ili kupunguza makali yao kwa sababu wanaendelea kuongezeka na ni wengi kweli na ndiyo ilikuwa matarajio yetu kwamba waweze kuongezeka ili watu waweze kuwaona wanyama wakiwa wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati mwingine kuwasikiliza sana wapinzani hawa kunakuwa na shida, mimi huwa ninapenda kuwafananisha na mtoto mdogo wakati mwingine. Unajua mtoto mdogo huwa akianguka kwenye watu wengi hivi kanainuka kanaangalia huku na huku halafu kakiona mko kimya kanaendelea na shughuli zake, kosa useme pole, ukisema pole huwa kanaangua yowe. Ndiyo sawa na hawa wenzetu kila wanalotimiziwa na Mheshimiwa Rais wanalalamika, jamani hatuendi hata Ikulu wanakaribishwa mpaka chai, wengine hawa wengine wako sijui wamefungiwa wapi saa hizi, walionwa hata walipokuwa wagonjwa, lakini wao wanapenda kelele tu, uki-pay attention tu tayari wanapiga kelele kama yule mtoto mdogo na attention yao mojawapo saa hizi ndiyo hiyo wanaenda mpaka Bunge la Ulaya na kwingine, sisi kwetu kumetulia. Hawa wanapenda kelele, tusiwasikilize na Mama aendelee kukaa kimya.

Mheshimiwa Spika, ninaunga mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)