Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Maida Hamad Abdallah

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii adhimu na kuchangia katika hoja hii iliyoko mbele yetu. Kwanza kabisa, ninapenda nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya kupitia Wizara au taasisi zote ikiwemo taasisi hii ya utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninampongeza pia Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa kazi kubwa ya kutuletea maendeleo wananchi wa Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninapenda nimpongeze vile vile Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya hadi kuhakikisha kwamba mapato ya nchi yetu kupitia sekta hii yanaongezeka mara dufu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Sekta ya Maliasili na Utalii inachangia katika pato la Taifa kwa 17% na zaidi. Awali kabla ya kipindi cha Royal Tour cha Mheshimiwa Rais, Sekta hii ya Utalii ilikuwa inachangia dola za Kimarekani bilioni moja, lakini kutokana na juhudi za Mheshimiwa Rais, Sekta hii imeweza kukua na sasa hivi tunajivunia kusema kwamba inachangia dola bilioni 3.9 katika mapato ya nchi. Hongera sana Mheshimiwa Rais na watendaji. Hongereni sana kwa kazi kubwa wanayoifanya kuhakikisha kwamba mapato ya nchi yanaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika kuendeleza Sekta hii ya Utalii, taarifa ya Wizara na Kamati zimesema. Ninaungana na Kamati kwamba Mfuko wa TDL lengo lake ni kutangaza vivutio vya utalii na kuimarisha utalii Tanzania. Kama ni hivyo, ni lazima tuangalie vigezo vya nchi ambazo zimefanya vizuri kupitia Sekta hii ya Utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, miongoni mwa nchi zilizofanya vizuri, moja ni Nchi ya Singapore ambayo imefanya vizuri katika Sekta hii ya Utalii. Nchi ya Singapore ina Bodi ya Utalii kama ya kwetu, lakini kila mwaka inaingiza dola bilioni 22. Pia Bodi hiyo hiyo imesambaa katika nchi tofauti zinazofanya vizuri. Katika masoko ya Kimataifa imefungua ofisi 19 kila nchi. Pia, ina watumishi 514. Bodi yetu sisi ya Utalii hatujaipa nguvu ya kisheria. (Makofi)




Mheshimiwa Spika, ninamwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kufanya majumuisho, ninaomba sana kwa sababu Bodi yetu bado ni tegemezi. Hatujaipa mamlaka ya kisheria kuweza kutangaza vivutio vya utalii Tanzania. Tuipe mamlaka bodi, siyo kila sekta tu itangaze vivutio. Bodi hii ina uwezo wa kutangaza vivutio, ina uwezo wa kujenga miundombinu na ina uwezo wa kutangaza na kukaribisha uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Bodi hii kama tutaiimarisha na tukasema kwamba fedha za TDL zielekee moja kwa moja kwenye Bodi ya Utalii, matokeo yake watayaona. Ninaomba sana Mheshimiwa Waziri kuleta Bungeni hapa mabadiliko ya Sheria ya Bodi ya Utalii. Bodi yetu bado ni tegemezi, inategemea fedha za OC za Wizara. Mpaka Wizara iseme sijui ni kiasi gani, hawana uwezo wa kufanya kazi wala kuweka watumishi wenye weledi na walio bora.

Mheshimiwa Spika, Bodi hii kama tutaiimarisha vizuri na tukafuata vigezo kama vile, Mheshimiwa Waziri wewe unajua vizuri tu, tutaweza kuongeza mapato ya nchi kuliko. Fedha zinazotokana na utalii katika nchi hii zitaweza kuendesha mapato yote ya nchi kwa mwaka mzima kwa sababu nimesema kwamba dola bilioni 22 zile za Kimarekani ni sawa na shilingi trilioni 64, ambapo sisi tunaweza kutumia na kubaki ziada. Sisi tunataka twende mbele zaidi hatutaki tuwe nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumefika hatua nzuri, tunampongeza sana Mheshimiwa Rais. Tumsaidie Mheshimiwa Rais ili tuweze kwenda vizuri. Tuongeze mapato kwa kupitia Sekta hii ya Utalii. Wizara zote zilizopo nchini zitashindwa na utalii kutokana na ukubwa wake na kutokana na sasa hivi wasafiri walivyo wengi kwa sababu wakipitia kwenye mitandao wakiona mwenendo wa nchi ulivyo, wakiona amani na utulivu wa nchi ulivyo, wakiona miundombinu, huduma mbalimbali na mambo mengine kupitia mitandao wataweza kuongezeka zaidi na zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninamwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kufanya marekebisho ya Bodi ya Utalii aje atoe majibu kwamba ni lini tunafanya marekebisho ili Bodi iweze kuwa na nguvu na mamlaka ya kusimamia na kuendesha utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwaka 2011, Nchi ya Singapore ambayo ninasema imeendelea katika masoko ya Kimataifa, ilileta mikataba mitatu ya kibiashara ya utalii ambayo lengo lake ni kufanya biashara na nchi ya Tanzania kupitia Sekta ya Utalii, iwe miundombinu, uwekezaji au vitu vingine, lakini mpaka leo mikataba hiyo haijasainiwa. Tatizo ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumekwenda kuona, kule ukiingia unakwenda sehemu moja tu ya utalii. Kila mtu analipa dola 20, lakini angalia ni watu wangapi wanaingia katika eneo moja la utalii? Watu 4,000 kwa siku. Kila mmoja analipa dola 20 au 15 na sehemu nyingine unakwenda hadi dola 35. Maendeleo yamekua sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wao wenyewe wametushangaa wanasema: “Ninyi mna uwezo, mna vitu artificial na mna kila kitu.” Yaani sisi tunashangaa tumetembea Tarangire, Ngorongoro na kwingineko; ninyi mna vitu natural kabisa. Ndiyo maana sisi tukasema tuingie mkataba na ninyi. Leo wanakuja kufanya nini? Hivi mlirogwa wapi? (Makofi)

SPIKA: Haya ahsante sana.

MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja kufanya majumuisho atupe matokeo ya mabadiliko ya Sheria ya Bodi ya Utalii. Pia, atuambie mikataba hii imekwama wapi iweze kusainiwa ili tuweze kuingia mkataba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)