Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Moshi Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika hoja hii muhimu. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Dkt. Pindi Chana na Naibu wake pamoja na watendaji wake wote. Kusema ukweli kazi wanayofanya inaonekana. Tunaona Sekta ya Maliasili na Utalii kuna mahali imetoka na kuna mahali inakwenda. Kwa hiyo, ninawapongeza sana kwa hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nianze kwa kusema Mungu alivyoiumba Tanzania alikuwa na makusudi yake. Aliiweka Tanzania hapa ilipo na akatupa 32.5% kama rasilimali za maliasili. Alikuwa na nia njema kabisa kwa ajili ya Watanzania na katika hizi rasilimali ambazo ametupa kuna vitu vingi vizuri ambavyo Mungu ametukabidhi; Mlima Kilimanjaro ukiwepo, mbuga za wanyama, na taja vitu vyote vizuri ambavyo Mungu ameviumba akaviweka Tanzania na vitu vyote hivi vinavutia utalii. Kwa hiyo, ni tegemeo langu kubwa kabisa hii 32.5% ya eneo letu utalii na maliasili zilizopo ziendelee kutupa faida na tija katika kukuza Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumeshauona utalii una faida nyingi sana. Waziri ametupa data nyingi nzuri na tumeona imechangia kikamilifu na vizuri kwenye pato la Taifa. Ukichanganya maliasili pamoja na utalii ni kwenye 21.5% ya pato la Taifa ambapo utalii umechangia 17.2%. 
Mheshimiwa Spika, hii ni hatua nzuri na idadi ya watalii imeongezeka kama ulivyosema kutoka kwenye 900,000 wale wa nje mpaka karibu milioni mbili na wale wa ndani pia wameongezeka kutoka laki ngapi mpaka milioni tatu. Kwa hiyo, lile lengo la kufikisha watalii 500,000 lililo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi tumelifikia. Hongereni sana, hapo ninawapongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niwe mkweli Daktari ninamsifu amefanya kazi nzuri, lakini bado nitampa changamoto. Sekta ya Utalii na Maliasili ina mchango mkubwa sana kwenye Taifa letu. Kwa hiyo, bado tunahitaji tujitathmini na tutafakari tuangalie ni kwa namna gani Sekta hii hasa Utalii inaweza ikachangia kwenye pato letu la Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninasema hivyo kwa sababu bado idadi ya watalii wanaokuja nchini kwa mawazo yangu bado ni wachache (ndiyo changamoto ninayokupa). Nilitegemea sawa tumeshafikisha 5.3 million; kwa hiyo, ndiyo tumefika au bado? Ninafikiri bado sana tulitakiwa twende mpaka kwenye milioni 10. Nina uhakika tukijipanga vizuri na kujitathmini tunaweza tukafikia watalii milioni 10 kwenye nchi hii na kama yule mchangiaji wa mwisho alivyoongea, watachangia kwa kiasi kikubwa kabisa katika pato la Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niseme kwamba ni vyema kuboresha vitu vifuatavyo ili tuweze kuchangia kikamilifu kwenye pato la Taifa letu hasa Sekta ya Utalii.
Mheshimiwa Spika, kitu cha kwanza ninachoomba tukiangalie tukiwekee mkazo ni kuweka mkazo kwenye kutangaza soko la watalii hapa nchini ili watalii waweze kuja. Bado idadi ni ndogo kwa mawazo yangu na tumeona mafanikio makubwa ambayo tumepata kutokana na filamu ya Royal Tour ambayo Rais ameshiriki na ile ya Amazing Tanzania ambayo pia Rais ameshiriki. 
Mheshimiwa Spika, sasa niwaombe kama Wizara, Serikali iendelee kufanya vitu kama hivi kutangaza masoko, kukamata nchi mbalimbali ambazo ni wateja wetu kwenye Sekta ya Utalii. Kwa mfano, tunaweza tukamshirikisha tena Rais, tukamwomba na nina uhakika hatakataa twende kwa Waarabu pale tucheze filamu inayofanana fanana na wao wataifurahia, watairusha kwenye dunia ya Waarabu na mambo yatakwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, twende kwa Wajapani, Wafaransa, turushe filamu kule kwa Kifaransa, tutumie wakalimani; tuipeleke kule kwa sababu, hizi ndiyo nchi ambazo zinashiriki sana kwenye Sekta ya Utalii dunia nzima. Pia, twende India, Australia tuoneshe vitu ambavyo tunavyo.
Mheshimiwa Spika, niipongeze Wizara, imeshaanza kampeni nzuri kwa kutumia mashirika ya ndege, tujiongeze zaidi, hapo wamefanya vizuri. Tuendelee kutumia vyombo vya habari vikubwa duniani kutangaza utalii wetu hapa nchini, tutumie watu maarufu. Kwa mfano, wachezaji wa mpira; ninajua wamesema kwenye ligi zile wanapeleka huko, lakini wachezaji maarufu wa mpira wakiwaleta hapa, hata wasipolipa; wamlete Lionel Messi hapa, wamlete Ronaldo au tutumie watu wengine maarufu duniani. Kwa mfano, wakimleta Bill Gates, ni rafiki yetu, akija hapa akionekana yupo kwenye mbuga zetu za wanyama ama Serena Williams na watu wengine wote maarufu, tukiwatumia wale nina uhakika tutakuwa tumeitangaza Sekta yetu ya Utalii vizuri na mambo yetu yatatunyokea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika matangazo ya soko letu pia, ninashauri tushiriki kwenye maonesho ya kimataifa na ya kikanda, tuoneshe vitu ambavyo nchi yetu inavyo. Kwa mfano, kule kwenye maonesho najua kuna kitu kinaitwa ITB Berlin, kwa Wajerumani kule, twende kwenye maonesho yao. Kuna kitu kinaitwa IFTM, ya Wafaransa, kuna kitu kinaitwa East African Tourism EXPO, vyote hivi tushiriki na ikiwezekana, ikitupendeza pia, tuwe na maonesho yetu ya ndani; tuite hawa giant waje washiriki waone vitu ambavyo tunavyo, tutakuwa tumelipanua soko letu na tutafanikiwa.
Mheshimiwa Spika, mchango wangu wa pili ni kuhusu kuboresha miundombinu ya barabara na usafirishaji. Kuna tatizo kubwa; kwanza niipongeze Serikali, mtalii anapotoka Ulaya mpaka Dar es Salaam mpaka KIA, mambo ni safi. Kutoka KIA kwenda mjini mambo ni safi, barabara ni safi, lakini hotelini kwenda kule site ambako kuna vivutio vyetu vya utalii, hali ni mbaya, barabara ni mbaya. Nitawapa mfano, kuna mti mrefu kuliko yote Afrika uko Kata ya Mbokomu kule Jimboni kwangu Moshi Vijijini, yaani sasa hivi ukisema unapanda kwenda kuuona ule mti haiwezekani.
Mheshimiwa Spika, kuna kupanda Mlima Kilimanjaro kupitia route ya Umbwe, haiwezekani, barabara ni mbaya. Sasa sisi tunahitaji pesa kutoka kwa hawa jamaa, lakini anapokuja, akipanda gari akienda kule, anarudi ameugua, hatarudi tena. Akifika kule tena atawaambia watu wengine wasije kwa sababu, hali ya barabara ni mbaya. Tukubaliane, hawa watu wametoka kwenye mazingira mazuri ambako barabara zao ni nzuri, anapokuja hapa akiwa subjected kwenye shida kama hizo na kuugua inakuwa siyo kitu kizuri.
Mheshimiwa Spika, niiombe Serikali tutumie hata ule mfuko wa kusaidia jamii, CSR. Badala ya kufanya vitu vingine, watengeneze hizi barabara ili tuendelee kupata kipato kutoka kwenye barabara zetu.
Mheshimiwa Spika, naona umeshaniwashia taa. Nilikuwa nina mengi, lakini nitawasilisha kwa maandishi.
SPIKA: Haya ahsante.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, nawapongeza sana. Naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)