Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kyerwa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii muhimu. Kwanza, nimshukuru Mwenyezi Mungu, ambaye amenijalia na mimi kuwemo miongoni mwa wachangiaji.
Mheshimiwa Spika, ninaipongeza sana Wizara, Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na Watendaji kwa kazi nzuri na kubwa wanayoifanya kuhakikisha utalii wetu unasonga mbele. Pia nitumie nafasi hii kipekee kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa na nzuri aliyoifanya. Mheshimiwa Rais ana nafasi kubwa, ukiona Mheshimiwa Rais anaacha enzi yake pale Ikulu, anaacha mamlaka yake, anaenda kushinda msituni kutangaza utalii na kwa kweli, tumeona matokeo makubwa sana. Kipekee tunampongeza na tunaendelea kumwombea kwa Mwenyezi Mungu azidi kumpa nguvu na afya njema. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niombe sana Wizara ya Maliasili na Utalii. Tunajua wanafanya kazi kubwa na nzuri ya kumsaidia sana Mheshimiwa Rais.  Nianze na neno hili, Mheshimiwa Rais nia yake ni njema, niwaombe sana wazingatie ushauri na maoni ya Kamati. Pia, tuone nia njema ya Mheshimiwa Rais aliyonayo, kupitia utalii wetu, leo hii tunajivunia mafanikio makubwa, ambayo tumeyapata kutoka watalii 922,692 mpaka watalii 2,141,895 ni mafanikio makubwa. Pia, ukiangalia fedha ambazo tumeziingiza kutoka shilingi bilioni 1.3 mpaka kufika shilingi bilioni 3.9, saw ana 200%, haya ni mafanikio makubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niombe sana Wizara tujipange tuendelee kutangaza utalii wetu. Biashara ni matangazo, huwezi ukajifungia ndani ukasema biashara yako itajulikana. Kwa hiyo, niombe sana, kama tulivyoshauri Kamati, hiki kituo cha utangazaji, mambo ambayo yamefanyika, hatua zinazochukuliwa na huu uzembe ambao tumeuona ni sehemu ya kufifisha na kurudisha nyuma hatua ambazo Mheshimiwa Rais anazichukua. Kwa hiyo, tuwaombe sana, lazima wahakikishe kituo hiki kinafanya kazi ambayo imekusudiwa.
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wameongelea sana wanyama waharibifu pamoja na wanyama wakali. Tukubaliane, Tembo wanapopita wamekuwa wakiacha uharibifu mkubwa na umaskini, wananchi wengi wamekuwa walemavu na wengine kufa, lakini ukija kuangalia kifuta jasho, kwanza kinachelewa pia, kifuta jasho chenyewe ni kidogo sana. 
Mheshimiwa Spika, niwape mfano, kuna wananchi walikuwa kwenye kitongoji kimoja kule kwenye Kata ya Businde, kitongoji kizima wananchi hawa walikuwa ni wakulima, wana mashamba yao; wamehamishwa kabisa, tembo wameharibu mashamba yale na nyumba. Wale wananchi leo hii ni maskini wa kutupwa, lakini ndiyo waliokuwa wanazalisha ndizi, wanazalisha viazi, wanazalisha na mazao mengine ya kibiashara.
Mheshimiwa Spika, sasa lazima hili tuliangalie. Pamoja na juhudi za Serikali zinazochukuliwa, njia mbalimbali wanazotumia kuhakikisha wanadhibiti hao wanyama waharibifu na wakali, niombe sana, kama Kamati tumeshauri kujenga fensi hizi za umeme, zinaweza zikawa suluhisho. Tunaona maeneo mengine wamewekeza nguvu kubwa, lakini kwenye suala hili la fensi bado hawajawekeza nguvu kubwa. Kwa hiyo, tuombe sana Wizara hili waliangalie, vinginevyo tunaleta umaskini, tunaleta uharibifu mkubwa kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni, tumekuwa tunasema wananchi wanavamia maeneo ambayo ni ya wanyama. Hawa tembo walishapita, lakini huyu mwananchi anapokuja kwenye hili eneo, anapewa na kijiji, anafuata taratibu zote, hakuna alama inayomwonesha huyu mwananchi hapa alipita tembo, baada ya miaka 20 mpaka 30 huyu mwananchi ana shamba lake, ameshawekeza, tembo wanakuja kuvamia.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niombe sana, Serikali waweke alama waainishe maeneo yote ambayo bado wananchi hawajawekeza ili yajulikane. Mwananchi anapokuja kuomba eneo, kama ni kununua shamba, ijulikane kwenye kijiji, kitongoji na kwenye kata husika, maeneo haya walipita tembo, ili kuondoa uharibifu huu ambao unaendelea kwa wananchi wetu, tunaendelea kuwafanya kuwa maskini. Kwa hiyo, niombe sana Serikali hili iliangalie.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine tunaomba, kama Kamati, hizi fedha za TBL zisimamiwe vizuri, nia ya Mheshimiwa Rais ni njema. Sasa Mheshimiwa Waziri akae vizuri na wataalam wake waone namna ya kuzisimamia zilete tija kwenye Wizara.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, ninakushukuru. Ninawatakia kila la heri Wizara ya Maliasili na Utalii na Mungu awabariki. (Makofi)