Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Hai
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kwenye Wizara hii na Hotuba ya Waziri. Kabla sijatoa mchango wangu, Mheshimiwa Riziki Lulida amekuwa akisema sana kuhusu hilo jusi. Nnimsaidie, ifike mwisho sasa lirudi kwa sababu, faida ni kwa wote sisi Watanzania.
Mheshimiwa Spika, ninapenda nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, baada ya kufanya Filamu ya Royal Tour sisi watu wa Hai ni mashuhuda namba moja kwa sababu, Uwanja wetu wa Kilimanjaro, pale KIA, tumekuwa tunapokea ndege karibu kila siku. KLM wanaingia kila siku na mashirika makubwa ya ndege yanazidi kuongezeka. Hii idadi wanayoiona, tumetoka kwenye 992,000 mpaka 2,141,000 na bado ninaamini kule kwenye 5,000,000 tunaweza kufika, kama haya nitakayosema hapa yatazingatiwa na mengine waliyosema wenzangu.
Mheshimiwa Spika, kufikia idadi hii tunatakiwa kufanya maandalizi ya mazingira yote na hapa mchango wangu nitajielekeza kwenye Wizara mbalimbali ambazo Mheshimiwa Waziri anahitaji sana zimsaidie ili kutengeneza mazingira rafiki ya kuwezesha watalii, wakifika hapa, waende wao wenyewe kutangaza kwa watu wengine. Moja ya mazingira ni kuhakikisha kunakuwepo na hoteli za kutosha kwenye mazingira haya, ambayo kuna vituo vya utalii. Kwa mfano, sisi wa Ukanda wa Kaskazini, kuanzia Arusha mpaka kwenda Tanga, je, idadi hii ikifikiwa wameshafanya tathmini kujua hawa watu watapata sehemu za kukaa?
Mheshimiwa Spika, sasa nimwoneshe kona ambayo anaweza kupita ukapata hoteli. Sisi kule kwetu Hai tuna maeneo mazuri sana ya kuweza kujenga hoteli za vivutio vya kitalii. Niliwahi kuzungumza na Kamishna wa PPP - Ndugu David Kafulila, kumwambia atembelee eneo la Wilaya yetu ya Hai kwa mashamba yake ya ushirika, ili tuweze kuyatumia kwa kufanya tathmini na kutafuta wadau ambao wanaweza kujenga hoteli za kisasa kwa kushirikiana na vyama vyetu vya ushirika vilivyopo pale. Kwa hiyo, niombe Mheshimiwa Waziri, nimkaribishe apokee wazo hili. Tuna maeneo mazuri sana ambayo ukijenga hoteli za kitalii, mtalii akikaa pale, yeye mwenyewe anafanya utalii kwenye mazingira yale na vivutio vingine.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo ni barabara za kwenda kwenye maeneo ya utalii. Amesema Profesa Ndakidemi nami niseme, bahati nzuri nilishatembea na Mheshimiwa Waziri nikamwonesha barabara zile tatu ambazo zinaenda Mlima Kilimanjaro. Barabara zile zikipitika mwaka wote, kipindi cha jua na mvua, kwa maana ya Januari mpaka Desemba, zitatengeneza mazingira mazuri ya utalii kuweza kufikika, ikiwa ni sambamba na maeneo ya vivutio, hasa ya biashara. Pale Bomang’ombe, tunamshukuru Mheshimiwa Rais, zimejengwa barabara; kuna Barabara ya Cheki Maji – Bomang’ombe TPC.
Mheshimiwa Spika, pale katikati tukiweza kuweka vibanda vizuri vya utalii, maana yake ni mtalii anaposhuka KIA anaweza kuanza kupata huduma kuanzia pale Bomang’ombe, kuliko ilivyo sasa hivi, mpaka afike Moshi Mjini au aende Arusha, lakini pale angeweza kupata huduma. Eneo hili nimwombe Waziri alitazame, lakini pia, atushauri kwa sababu, Halmashauri ya Wilaya ya Hai tayari tumeshaanza mchakato wa kufanya pale, ni eneo la kitalii. Tupate wataalam wake watutembelee ili tuzungumze lugha moja inayofanana, sambamba na ujenzi wa hoteli pale eneo la KIA.
Mheshimiwa Spika, tuliambiwa tunapopisha eneo la KIA moja ya sababu ni kwamba, zitajengwa hoteli za five star. Tuombe basi na yeye atusaidie kusukuma huo mradi ukamilike, ili eneo lile la KIA liwe na hoteli za kujitosheleza, ni pamoja na Mradi wa Geopark. Mradi wa Geopark watalaam wako walitueleza kwamba, watapita kwenye vivutio vya utalii, vile vidogo vidogo, kule Mronga tuna vipepeo ambao Tanzania na duniani kote hawapatikani. 
Mheshimiwa Spika, tuna maeneo ya zamani, malikale nyingi. Afisa wetu wa Halmashauri alitembelea maeneo yale yote, ili mtalii anapokuja Mlima Kilimanjaro kuwe na package, aende Temka, aende kwenye hivyo vituo vingine, tutaboresha utalii wetu, tutawavutia zaidi na tutamuunga mkono Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Spika, ulinzi wa Mlima Kilimanjaro siyo wa Ofisi ya Makamu wa Rais peke yake na anayehusika na utalii aone. Walifanya tathmini ya kinachosababisha theluji ya Mlima Kilimanjaro kuyeyuka ni kitu gani? Mvua kubwa iliyonyesha, ya mawe, inasababishwa na kitu gani? 
Mheshimiwa Spika, tungeomba hii taarifa ya tathmini iliyofanyika itolewe kwa wananchi, ikiwa ni sehemu ya kuwajengea uwezo kujua mabadiliko ya tabia nchi, ili tutunze Mlima wetu wa Kilimanjaro huu. Sambamba na hilo ni upandaji wa miti, lisiwe ni suala tu la kupanda miti na kuiacha. Kumekuwa na utamaduni sasa hivi watu wanaenda wanasema taasisi fulani imetoa miche 100,000 wanapiga picha wanaondoka. Wanapanda ile miche inaliwa na mbuzi inaishia hapo.
Mheshimiwa Spika, nadhani tutengeneze kanuni, kama mtu anayetaka kutupa miti, apande, aitunze, ikifika angalau 30% au 50% ndiyo aite vyombo vya habari sasa kwenda kutukabidhi, kuliko hiki kinachofanyika sasa hivi. Tunapoteza hela na uoto wa asili bado unazidi kuteketea.
Mheshimiwa Spika, eneo lingine, pia, niombe kutengeneza mahusiano mazuri na sisi tunaotunza Mlima Kilimanjaro, CSR Mheshimiwa Waziri, alituahidi hapa. Ni kweli, kuna maeneo tumepata majiko ya gesi, ujenzi wa madarasa, lakini sisi tulioko kule Mlima Kilimanjaro, nilisema tena hapa mwaka jana, tunafahamu nchi yetu yote fedha zinakusanywa zinaenda kwenye central pool, lakini CSR maeneo mengine wanapata. Walioko kwenye migodi huku tunaona namna ambavyo wanapata CSR, inawasaidia wananchi wanaozunguka maeneo yale. Sisi CSR yetu ya Mlima Kilimanjaro mbona hatuioni na sisi ndio tunaotunza huu mlima?
Mheshimiwa Spika, moto ukiunguza, tunapanda kule kwa upendo kabisa, lakini tofauti na maeneo mengine ambapo wanakimbizana na watu. Sisi tunaupenda mlima wetu na tunautunza kwa upendo. Niombe fedha ya CSR tuletewe.
Mheshimiwa Spika, nimekuwa pia nikisema suala la vijana wanaopanda Mlima Kilimanjaro wasitoke tu maeneo mengine. Ni kweli, tunajua ni biashara huria, nchi yetu yote ni yetu sisi, lakini kutengeneza upendo, wale vijana wanaozunguka Mlima Kilimanjaro na wenyewe ni vizuri wakapewa kipaumbele kuliko tu mtu anakuja na watalii; kampuni inakuja inapanda mlimani moja kwa moja, hakuna hata mtu mmoja wa pale ameshirikishwa. Niwapongeze pia, kampuni zinazohusika na utalii, hasa Kampuni ya Alteza; tumeona imeongoza kwenye kampuni ambazo zinalipa kodi, tuendelee kuwatia moyo ili tushirikiane kwenye sekta hii kuhakikisha inainuka.
Mheshimiwa Spika, eneo lingine dogo sana; pale, Uwanja wetu wa Kilimanjaro umekuwa tembo wanaingia uwanjani. Sasa niombe, uwanja ule ni sensitive, waone namna ya kudhibiti jambo hili, tofauti kabisa na maeneo mengine, tusije tukapata taharuki pale.
Mheshimiwa Spika, nimekuona umeshawasha na ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)