Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Priscus Jacob Tarimo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Moshi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Spika, ninashukuru sana kwa nafasi hii na kwa sababu muda umekwenda, niende tu moja kwa moja. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na staff wote pia, Kamati ya Kisekta kwa mchango mzuri sana.

Mheshimiwa Spika, nitaanza na eneo lile la OC na retention, hapo hapo niguse miundombinu. Mwaka jana nilichangia, niliongelea barabara na katika barabara niliongelea, hasa, hii Barabara ya kutoka Ngorongoro kwenda Serengeti, ambayo sasa imetengenezwa vizuri, lakini barabara, zile feeder roads kule kwenye mbuga kwa kweli, zina hali mbaya sana, sana. Hebu tusaidieni.
Mheshimiwa Spika, hili tatizo limeonekana, ukiangalia ripoti ya CAG ya Mwaka wa Fedha 2023/2024 imeonesha kabisa kwamba, ile OC ambayo ilikuwa inatakiwa ije; kwa mfano, Ngorongoro, OC ya maendeleo ilikuwa ije shilingi bilioni 28, lakini kwa mwaka huo ilienda zero. Kwa TANAPA, kwa ujumla wake, ilikuwa iende shilingi bilioni 23, lakini ilienda bilioni moja tu.

Mheshimiwa Spika, wanasema ng’ombe anayekamuliwa hachinjwi, ng’ombe anayekamuliwa analishwa vizuri, anapewa molasis. Sasa hawa ng’ombe ambao tunawakamua, lakini kwenye retention, kwenye hizi OC hatuwapelekei! Pamoja na kwamba, kwenye Taarifa ya Kamati wameonesha kwamba, kutakuwa na retention, lakini inaonekana uendaji wake hauendi na hawapati hizi fedha. Sasa hii kwa kweli tunawaua.

Mheshimiwa Spika, tuangalie tu unapokuwa na barabara mbovu, zile siyo tu kwamba, unamtesa mtalii, lakini hata mfanyabiashara, magari yake yale yanakuwa yanachoka kwa haraka na magari haya yanayokuja, model mpya, hayana ugumu kama yale ya zamani, kwa hiyo, niombe sana. Kwenye Ripoti ya CAG wameelezea kabisa, kuanzia ukurasa wa 156 mpaka 158 na kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Waziri ameongelea, ukurasa wa 20, Kamati pia, kwenye ukurasa wa 16, ninaomba sana.

Mheshimiwa Spika, lazima tukubaliane hii OC inayoenda ya mshahara peke yake, tukumbuke pia, kwenye OC ya Maendeleo kuna miradi imesimama, ipo imekuwa listed pale, lakini mbele zaidi kuna suala la ulinzi ambao rangers wako pale wana mahitaji mengi. Kwa hiyo, ninaomba hilo niliongolee kwa uzito wake kwa kweli na ninajua pengine siyo la kwako moja kwa moja, Mheshimiwa Waziri, lakini ni la Serikali kwa sababu, hii inatakiwa irudi kutoka Hazina.

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ni, eneo la manpower. Manpower kwenye eneo la uhifadhi na ma-guide tumepiga hatua sana na nikipongeze sana Chuo cha Mweka Wildlife, kimekuwa kina standard za Kimataifa, lakini fedha tuliyoweka kwenye Chuo cha VETA, kwa ajili ya watumishi wa hoteli ninaona haijaweza kutupa tija. Kuna haja ya Serikali ku-review, aidha mitaala au attitude peke yake, tuna shida kubwa sana kwa watumishi wa hoteli. Kuna mzungumzaji mmoja amesema, hata kwenye chakula; chakula ni eneo moja, lakini customer care na namna ya ku-handle wageni, pamoja na lugha za kigeni, tuna shida sana.

Mheshimiwa Spika, kazi zetu nyingi zimechukuliwa na majirani hapa na hawa majirani wana chuo kimoja tu, kama cha kwetu. Sisi tunakuwaje tunashindwa na tuko karibu kupata watu watakaotoa elimu bora, hasa kwenye hoteli? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna suala la ma-guide na ma-porter, nimeliongelea kwa muda mrefu. Sasa ninaomba tuwe na mechanism, Mheshimiwa Waziri anaifahamu ile Kilimanjaro Porters’ Association Program, ni kama NGO, inaweza ika-endorse kampuni za tours ambazo zinawalipa vizuri wale porters, kuendana na mwongozo wa Serikali, lakini inatumia hiyo hiyo website kwa kampuni ambazo zime-default kuwafanyia marketing, ambayo ni negative kule na wanapoteza utalii.

Mheshimiwa Spika, sasa tunashindwaje, kama Serikali, kuwa na chombo cha kusimamia hayo maslahi ambacho kitakuwa badala ya kwamba, huyu ame-default, unatangaza dunia nzima kwamba, huyu hafai, halipi hawa vizuri; kukawa kuna makubaliano, watu wakarekebishwa, badala ya kuharibu biashara kwa sababu, unapokuwa umesha-recommend negatively mtu kuja ku-recover tena hiyo market inachukua muda mrefu. Kwa hiyo, ningeomba tuangalie namna ya kufanya.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Saashisha ameongelea suala la hoteli na ametaja maeneo mengi. Mimi nitoe tu mfano, ni kweli kwamba, Serikali imeshindwa kuwa na bailout mechanism kwa kampuni kubwa kipindi zinaposhindwa kujiendesha, kwa ajili ya ku-rescue kodi, ambayo tunapata pale na zile ajira?

Mheshimiwa Spika, mfano, nimetolea Hoteli ya Ngurdoto. Juzi nimepita tena pale kulikuwa kuna mkutano wa airport zote Afrika, ulikuwa unafanyika pale. Kuna eneo zuri, ni sehemu pekee Marais wanaweza wakaenda wakalala, zaidi ya 10, 20, inaingia kwenye mchanganyiko, Serikali kweli, inashindwa ku-bailout hata kwa kununua share au kutafuta mbia wa kuiendesha, mwisho wake inaenda inakuwa mabweni ya wanafunzi?

Mheshimiwa Spika, hebu tuangalie namna, kama Serikali kwa sababu, yule naye ni ng’ombe ambaye tunamkamua, ni vizuri akatunzwa. Hii iwe ni kwa biashara nyingine zote ambazo zimeshakuwa kwa kiwango kikubwa kama ile Hoteli ya Ngurdoto.

Mheshimiwa Spika, kuna fee mpya ambazo ziliwekwa kwenye scenic flight, zile ndege ambazo zinapita karibu na mlima na maeneo yenye mandhari nzuri, kwa ajili ya watu kuangalia na kupiga picha. Kumekuwepo na kodi zilizowekwa mpaka wadau walikuja mpaka hapa na ninashukuru baadhi ya watendaji Wizarani walinisaidia kuangalia kuzirekebisha. Zile scenic flight ni aina mpya ya utalii, sasa inapokuwa imewekewa kodi kubwa inaua mandhari nzima ya kuwa na product nyingi za watalii. Ninaomba sana tuangalie namna ya kurekebisha zile kodi, ili watu hawa waweze kufanya biashara yao vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa niendelee kukumbusha lile la ku-integrate mikutano, ku-integrate michezo na utalii wetu. Nilishatoa ile tournament ya golf, ilikuwa ifanyike kule Kili Golf, ambayo ni PGA tour, ni ya Kimataifa, ingetuweka kwenye ramani ya dunia, lakini watu pia, wangeweza kwenda kwenye vivutio vyetu.

Mheshimiwa Spika, ninaomba kuunga mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)