Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Donge
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia hii Wizara ya Maliasili na Utalii. Shukurani zangu za dhati kuwa mchangiaji wa mwanzo jioni hii. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanza tu nimshukuru Allah Subhanahu wataala kwa kutujalia uzima na uhai, lakini hali kadhalika nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Dkt. Hazara Pindi Chana kwa utekelezaji wake mzuri wa bajeti, uwasilishaji ulikuwa mzuri. Hali kadhalika Mheshimiwa Naibu Waziri amefanya kazi nzuri amekuwa akijibu maswali yetu hapa kwa ukakamavu na ufanisi mkubwa. Pia nimpongeze Katibu Mkuu na timu yake kwa ujumla kwa utekelezaji mzuri na uandaaji wa taarifa hii ambayo leo tumewasilishiwa hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kwa moja niende kwenye mchango wangu na kwanza nimshukuru Allah kwa sababu katika kipindi changu cha mwaka wa tano hapa Bungeni toka mwaka 2020 nimekuwa nikichangia hii bajeti ya maliasili na utalii. Hali kadhalika taarifa zote za Kamati nimekuwa vilevile nikichangia. Kwa hiyo, kuna mambo ambayo nimeyaona ambayo tumekuwa tukiyazungumza hapa yametekelezwa vizuri na yale ambayo ni changamoto na kwamba bado hazikupata ufumbuzi ni mategemeo yetu kwamba katika bajeti ya awamu hii basi Wizara itajitahidi kuweza kuzishughulikia na kuweza kuleta ufanisi na utekelezaji wa ilani uwe mzuri zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyojua, changamoto ya kidunia ya upoteaji wa misitu inazikabili nchi nyingi kwa sababu sasa hivi dunia nzima inapoteza takriban hekta milioni 23 za misitu kila mwaka. Katika upoteaji huo sisi Tanzania tunachangia karibu hekta zaidi ya laki nne kwa mwaka zinazopotea kutokana na ukataji na utumiaji mbaya wa misitu yetu. Sababu kubwa za upoteaji wa misitu kwa Tanzania, kwanza ni uvamizi wa maeneo kwa sababu za kilimo pamoja na ujenzi. Sababu nyingine kubwa ni utumiaji mbaya kutokana na ukataji wa shughuli za kuni, makaa pamoja na harakati za mifugo. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, upoteaji huu wa misitu umekuwa na athari kubwa sana na kama Wizara, zile ambazo ni Wizara mtambuka hazikukaa pamoja zikazishughulikia kwa pamoja basi tutaendelea kupoteza misitu na tutafika wakati basi Zanzibar na Tanzania kwa ujumla itakuwa ni jangwa. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ningeziomba tu zile Wizara, kwa sababu tukiangalia ukataji wa misitu huu tusiiangalie Wizara ya Maliasili na Utalii peke yake, tuziangalie Wizara za Maji; kwa sababu misitu ikipotea maana yake vyanzo vya maji vinapotea; misitu ikipotea vilevile maeneo ambayo yanazalisha nishati kama vile Bwawa la Mwalimu Nyerere nalo linakuwa ni hatarini. Vilevile misitu ikipotea vyanzo vya utalii ambavyo tunahangaika hivi sasa kuhakikisha kwamba watalii wanaongezeka navyo vilevile tunaenda kuvurugika. 
Mheshimiwa Spika, kuna bajeti kubwa ya kilimo imetengwa nayo kama tukiendelea hivi hivi misitu kupotea, mabwawa, mito na hata ile reserve yetu ya maji ya chini nayo inakwenda kuathirika kwa sababu kilimo cha umwagiliaji nacho kitakuwa vilevile, kazi ni bure kwa sababu inategemea maji ambayo yanapotea kutokana na uharibifu wa misitu. Hata Sekta ya Mifugo nayo itaathirika kama misitu itaendelea kupotea kwa sababu na wao wanategemea maji kuweza kunywesha mifugo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu sasa, ni lazima sekta hizi zikae kwa pamoja, wasiangalie sekta zao tu wakajifungia kwenye Wizara zao au ofisini kwao wakasahau kwamba na wao tatizo la uharibifu wa misitu pia linawaathiri. Sasa, mapendekezo yangu, la kwanza ningemwomba sana Mheshimiwa Waziri tukajitahidi kwanza kuangalia uwezekano wa kuhakikisha sana utawala wa sheria unaimarika. Kwa sababu Tanzania tunasifika kwamba tunatunga sheria vizuri, lakini shida tuliyonayo ni kwamba utekelezaji wa sheria hizi ndiyo mgumu. Kwa hiyo ningeliomba hili nalo tukalitia maanani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kwamba, tuweke mfumo madhubuti wa kitaasisi wa kuweza kushughulikia suala la uharibifu wa misitu. Kwa sababu tumekuwa tukizungumza hapa TFS (Tanzania Forest Service) itapandishwe iwe mamlaka; lakini nalo hili kwa mwaka wa tano nalo limeshindikana pia. Sasa na hili pia linakuwa gumu? Tunataka tuweke umadhubuti wa uhifadhi wa misitu yetu. TFS kuipandisha hadhi ni suala la usiku mmoja tu wakatuletea sheria hapa tuhakikisha hili linakamilika. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la Jeshi la Uhifadhi, tumezungumza kwamba Jeshi la Uhifadhi kuna vijana wengi wanamaliza chuo kule Olmotonyi pamoja na Chuo cha Mweka; tuongeze idadi ya Jeshi la Uhifadhi, lakini pia maslahi yao tuyaangalie. Kwa sababu sasa hivi TANAPA wanalipa kivyao, TFS wanalipa kivyao na WMA wanalipa kivyao. Sasa, tuangalie haya maslahi ya Jeshi la Uhifadhi ambayo vijana wetu hawa wanapata athari za uharibu, wanaumia, wanauliwa lakini hatimaye ukiangalia maslahi yao si mazuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine vilevile ni kuongeza wigo wa elimu na ushirikishaji wa jamii. Tukiongeza wigo wa elimu kuhusu uhifadhi wa jamii; na Mheshimiwa Rais amekwishatupa dira kwa sababu yeye amekwenda kwenye ku-act ule mchezo wa Royal Tour pamoja na Amazing Tanzania kama kutupa dira kuhusu tunashughulikia masuala ya kutoa elimu kwa jamii. Sasa twende na sisi tuongeze wigo wa elimu, tuielimishe jamii. Tutumie vipindi vya redio na TV; Hali kadhalika twende kwa jamii kama vile zamani ambapo kulikuwa na cinema maalum zinakwenda vijijini kuweza kufanya shughuli hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ningeliomba tu, suala la uharibu wa misitu na ni suala nyeti ni suala la kushughulikiwa haraka ili Tanzania iwe endelevu katika sekta zake mbalimbali za uzalishaji pamoja na za uhifadhi. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)