Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Mrisho Mashaka Gambo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Arusha Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa fursa hii kwa ajili ya kuweza kuchangia kwenye Wizara yetu ya Maliasili na Utalii, Wizara ambayo tunajua kwa asilimia kubwa mapato wanayapata kutokana na Kanda ya Kaskazini na Arusha ikiwemo. Nitazungumza mambo yafuatayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, kilio chetu ni kile kile kama cha mwaka jana. Tumeona kuna changamoto kubwa sana tangu Serikali ilipoamua kuchukua fedha za Ngorongoro na TANAPA na kuzipeleka kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Fedha zinakwenda kule, lakini hazirudi kama ambavyo inavyotarajiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia taarifa tuliyosomewa hapa leo, tunaambiwa kwamba Serikali imeweza kurudisha 32.55% kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo. Hata hivyo, ukienda hali ya barabara ni mbaya, miradi mbalimbali kule inasuasua kwa sababu Serikali inakusanya fedha na hatimaye hairudishi kwenye taasisi husika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi ombi letu, tunaomba Serikali irudishe utaratibu wa zamani, Mamlaka ya Hifadi ya Ngorongoro na TANAPA pamoja na taasisi nyingine zote za Wizara ya Maliasili wakusanye wenyewe halafu warudishe gawio kama walivyokuwa wanafanya miaka mingine iliyopita. Kwa kufanya hivyo tutaweza kuboresha barabara zetu, miradi mbalimbali ya maendeleo, lakini pia tutaweka taswira nzuri zaidi kwa watalii wetu kwa sababu biashara ile ni biashara ya leisure. Mtu amesafiri anakuja ku-enjoy anakutana na makologesheni na vitu vingine. Ninadhani ni jambo ambalo haliendani na maono ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ameipigia debe Royal Tour akitegemea kwamba wageni wakija wanufaike na fursa ambayo ametutengenezea kama Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, tumekuwa tukisema kila siku, kwamba Sekta ya Utalii ni sekta ambayo lazima iwe predictable, ni sekta ambayo akitaka kuingiza tozo ni lazima uiandae jamii. Hata hivyo ni sekta ambayo tumeona inaonewa sana. Serikali kila ikikaa kutafuta fedha inakwenda kuangalia kwenye vilevile vya utalii. Badala ya kutafuta vyanzo vipya wanarudi kule kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, safari hii tumeona wameleta introduction of new environmental management ya fees and charges kwa wenzetu hawa wa NEMC. NEMC kupitia kanuni ya tarehe 14 Mei, 2021 walikuwa wana-charge kwa kupitia facility. Kama una hoteli unalipa kwa hoteli nzima. Kwa mfano hoteli ya nyota tatu mpaka tano walikuwa wanalipa milioni mbili kwa hoteli ambazo ziko ndani ya hifadhi au karibu na hifadhi. Kwa nyota moja hadi mbili ni milioni moja na nyota ambazo hazijawa graded ilikuwa ni laki saba na nusu. Sasa hivi wanataka na wao kulipa kwa kitanda. Yaani kila mtalii anapolala pale na NEMC naye pia anataka apate fedha. Kwa maana ya kwamba kila kwenye holeli ambazo ziko karibu na hifadhi au ndani ya hifadhi kila kitanda elfu hamsini, kama ni guest house kila kitanda ni elfu thelathini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninajiuliza yule mtalii akilala pale ndani kwenye kile kitanda yaani role pale ya NEMC inakuwa ni kitu gani? Ninadhani mwanzoni ile kufanya kwa facility ilikuwa angalau ina-make sense. Ni vizuri Wizara ya Fedha, Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na watu wa mazingira wakae chini waangalie. Tozo kama hivi zinawakatisha tamaa wale ambao wanamsaidia Rais Samia kwenye Royal Tour kwenye ku-boost utalii kwa sababu kila siku ni changamoto kubwa na zinakuwa ni nyingi zaidi. Kwa hiyo ninadhani hili jambo lina hitaji jicho la ziada la Serikali; na kwamba tozo kama hizi zinatakiwa ziondelewe na tubaki na kanuni ya zamani ambayo wala haikuwa na changamoto yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwenye upande wa matumizi ya dola, kwa maana ya fedha za kigeni. Sina tatizo na maelekezo ya Serikali kwamba tutumie shilingi yetu katika nchi yetu, lakini biashara ya utalii ni biashara ambayo ni very sensive. Leo ukiangalia BOT pale wanatumbia dola moja unaweza ukanunua kwa 2,670 unaweza ukauza kwa 2,697, lakini mtalii anayekuja Tanzania leo ana book one year in advance wengine hata miaka miwili kabla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa leo ume-quote umeambiwa dola moja ni 2,670, umebadilisha hiyo fedha ukamtumia kule mtalii wako akalipia leo halafu anakuja baada ya mwaka mmoja, pengine dola imefika 2,900 au 3,000 au 2,800. Sasa, ile tofauti inayojitokeza pale itakwenda kumuathiri mfanyabiashara wa utalii wa ndani. Sisi tulikuwa tunadhani, kwa sababu hii biashara ni ya kimataifa inasaidia pia kuleta forex ni vizuri wakaruhusiwa kuendelea ku-quote kwa dola wakapokea fedha kutoka nje huko kwa dola na mwisho wa siku hata mtu akibadilisha vile hata baada ya miaka 10 ijayo bado dola moja itabaki kuwa ni dola moja tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiigawa kwa shilingi mabadiliko yoyote yakitokea changamoto itakuwa ni kubwa zaidi, kwa hiyo tuinaomba Wizara, kwa sababu kwenye ile kanuni hawajatoa ufafanuzi kwenye Sekta ya Utalii hili jambo linakwenda kuangaliwa kwa namna gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipongeza sana Serikali kwa kweli, wameweza kufuta tozo ile kwa wale ambao wanaongoza utalii. Hata hivyo wamesahau kitu kimoja, wafanyakazi wa Sekta ya Utalii ambao wanaingia ndani ya hifadhi kila siku wanachajiwa fedha na Serikali. Kwa hiyo tulikuwa tunaomba, pamoja na kufuta tozo hii kwa wale wanaoongoza utalii na wafanyakazi wote ambao wanafanya ndani ya hifadhi, pamoja na yale ya magari na wenyewe pia wakafute tozo zao kwa sababu wao si watalii, wao ni wafanyakazi, wameajiriwa; na ule mzigo wote hauendi kwa wafanyakazi peke yake, pia unakwenda kwa mwenye kampuni ya utalii. Kwa hiyo tunaomba Serikali ikaangalie uwezekano pia wa kufuta na hii ili wafanyakazi wale Tanzania ambao wamepata fursa ya ajira wasipate changamoto kama hiyo ya kulipishwa wakati wanatumikia ajira zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tozo nyingine wanasema ya kupanga hoteli nyota tano, tatu, nne wamepunguza kutoka dola 2,500 kwa nyota tano hadi 1,500. Hii tozo ni kufuta kabisa; hii ni kazi ya Serikali kuzi-grade hoteli zetu kwamba hii ni nyota tano, ni nyota nne, nyota ngapi. Kwa nini wakam-charge mtu ambaye anafanya kazi ya utalii? Sasa wanakusanya kodi, kodi kazi yake ni nini? Wanalipwa mishahara, kazi yake nini? Sasa si wakafanye kazi kama hiyo ya kwenda ku-grade hizo hoteli na vitu vingine? Isiwe kila kitu kwenda kuwakamua tu hawa watu wa Sekta ya Utalii, kitu ambacho kwa kweli kinarudisha nyuma jitihada za Rais Samia za masuala ya Royal Tour.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kwenye upande wa wale wanaofanya biashara ya kuwapandisha watalii mlimani, tumeona na wenyewe pia wamepunguza kama Serikali kutoka dola 2,000 hadi milioni tatu; ya nini yote hiyo? Hiyo ni leseni tu ya biashara. Leseni inakusaidia kumtambua huyu mfanyabiashara ukishamtambua; ana kodi nyingine zaidi ya 53 hapa ambazo anazilipa. Sijui analipa huko TRA, analipa concession fee, wanalipa sijui bed night levy; wanalipa conservation fee, sijui digit services, wanalipa kodi kibao zaidi ya 53.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hiki kileseni cha kumtambua tu kwa nini kinakuwa na gharama kubwa namna hiyo? Kwa hiyo ninashauri na hii yenyewe kama tunataka ku-charge basi angalau kwa kampuni ndiyo angalau milioni moja ambao wanapandisha utalii; lakini kwa mtu binafsi ingekuwa angalau shilingi elfu hamsini ili vijana wengi wa Kitanzania ambao hawana ajira waweze kupata fursa ya kupata ajira na hatimaye fedha isiwe kikwazo cha kuwaingiza sekta hiyo rasmi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante…

MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kumalizia…

MWENYEKITI: Muda wako tayari Mheshimiwa Mrisho Gambo.

MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana…

MWENYEKITI: Sijui kama umeunga mkono hoja?

MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja nimezitoa, ninadhani nikipata ufafanuzi wake nitakuwa na fursa nzuri zaidi ya kuweza kuunga mkono.