Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niipongeze sana hii Wizara ambayo pia ni Mjumbe wa Kamati ya Ardhi na Maliasili, kwa hiyo hii ni moja kati ya Wizara ambayo tuko nayo. Kwanza niunge mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri iliyoko mezani, lakini pili niunge mkono maoni ya Kamati yangu ambayo tunaisimamia yale ambayo tumeyatoa kwa ajili ya Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ninaomba niwapongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu kaka yangu Abbasi na viongozi wote wa Wizara hii, akiwemo Naibu Katibu Mkuu na Makamishna wote wanaoisimamia Wizara ya Maliasili kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya ya kumuunga mkono Mheshimiwa Rais na kwa kuhakikisha kwamba maliasili za nchi yetu na Sekta ya Utalii inaendelea kukua; kwa hiyo tunawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina jambo tu ambalo ninatamani nilizungumze; ni kwenye sekta ya hiki ambacho kimezungumza na Kamati kuhusu TDL. Niipongeze Serikali kwanza kwa kuwa na huu Mfuko wa Tozo, kwa maana ya Tourists Development Levy; ni Mfuko ambao kwa kweli umekuwa na manufaa, kwa maana ya upatikanaji wa fedha kwenye Wizara yetu. Pili, tunachokitamani ni kwamba fedha hizi zikafanye kazi ambayo Wizara inakusudia kufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme wazi kwamba, ukiangalia makusanyo ya kutoka mwezi Mei kama sikosei hadi mwezi wa Desemba ni karibu bilioni 33.4. Ni fedha nyingi na ni fedha ambazo tunatamani kwamba ziende kwenye utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninachokitamani ni nini; ni kwamba Sekta ya Utalii ni sekta ambayo ina changamoto mbalimbali. For instance, kuna kuna issue ya miundombinu ya barabara, mawasiliano na pia uelewa; elimu ya watu kuhakikisha kwamba Sekta ya Utalii inakua. Kwa sasa niombe sana Serikali na Wizara yetu, kwamba tunapopata fedha kama hizi tujikite kwenye kutatua changamoto zile ambazo tunatamani zihakikishe utalii unakuja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu TTB wanatangaza utalii, lakini hawawezi wakawa wanajikita kutangaza utalii bila pia kugundua ni changamoto zipi tuzitatue ili utalii wetu ukue? Kama changamoto ya kwanza ni miundombinu, kama wachangiaji wengine walivyosema, basi ni vema tukajikita kwamba fedha ambazo zinapatikana muda mwingine kwenye ku-support na kukuza utalii zijikite kwenye ku-support na kujenga miundombinu ambayo ni rafiki ili watalii waweze kuja kwa wingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nilikwishawahi kuzungumza hapa, kwamba kama tunatamani utalii pia ukue ni kuhakikisha kwamba tuna invest zaidi pia kwenye kutoa elimu na kuutangaza utalii wenyewe. Tunatamani kabisa kwamba kama fedha inapatikana Wizara ikiamua kwamba haya mambo matatu yanatatuliwa yawe yametatuliwa kuanzia mwanzo hadi mwisho yakaisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mathalani nilisema kwamba unaweza ukakuta mtalii ametoka nje amefika Dar es Salaam, amefika KIA, lakini wale watu wanaoanza kumpokea hadi anafika kwenye hifadhi mpaka anaondoka kuanzia kwenye huduma za hoteli. Je, hawa watu wana elimu kiasi gani na uzalendo kiasi gani kuhusu utalii?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kazi ambayo inatakiwa tuhakikishe kwamba Wizara hii ambayo inasimamia jukumu zima la utalii inatumia fedha hizi pia kuelimisha na kuwajenga Watanzania ambao wapo kwenye mnyororo wa kuhakikisha kwamba mtalii anaenda na kurudi, anapata ile taste, uzalendo na anapata vionjo vya eneo tofauti tofauti kabisa katika kuhakikisha utalii wetu unakua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme wazi unaweza ukakutana na watu ambao ni dereva tax wapo barabarani ambao wanabeba watalii wetu, lakini je, wana elimu kuhusu utalii wetu? Hawana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kwamba Wizara ione fursa wanapopata fedha kama hizi za TDL kujikita; kama wanajikita kwenye kuelimisha utalii, kuweka miundombinu sawa kwenye hifadhi, kujenga mahusiano mazuri kati ya sekta binafsi na Wizara. Basi wafanye hivyo ili ile fedha iweze kuleta tija kama ambavyo sisi Kamati tulitamani kwamba iendelee kuleta tija kwa ajili ya Wizara yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine unakuta hawa watu wa sekta binafsi ambao wanasimamia utalii, kwa sababu 90% ya Sekta ya Utalii inaongozwa na sekta binafsi. Wanatamani kuona pale ambapo wanatoa hizi tozo zinaleta return ya kutatua changamoto ambazo wanakutana nazo kwenye hifadhi au sekta yao ya utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri kazi nzuri ambayo wanaifanya pamoja na Makamishna wote wa NCCA, TANAPA na wengine wote wahakikishe kwamba fedha hizi ambazo zinapatikana kwa ajili ya TTB ziweze kufanya kazi husika ili ziweze kusaidia kwenye kukuza utalii wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwenye suala la orientation. Sisi kama Kamati nia na kilio chetu kama Bunge na ninalishawishi Bunge pia waendelee kuomba kwamba retention ya fedha kwa ajili ya TANAPA na NCCA ziweze kufanyika, ili wenzetu waweze kukusanya na kutumia wao wenyewe. Hii inaweza kutusaidia kabisa katika kutatua changamoto ambazo wamekuwa wakikutana nazo huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tumepata fursa ya kuzunguka kwenye hizi taasisi, maeneo ya Ngorongoro na hifadhi mbalimbali tunaona kabisa uendeshaji wa taasisi hizi muda mwingine unakuja kuwa ni mgumu, kwa sababu ya kusubiria fedha kutoka serikalini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tukirudi kwenye ule mfumo mwingine ambao unaweza ukaisaidia taasisi ikaendelea itakuwa kwetu ni nia njema na ni jambo zuri kwa Serikali kuhakikisha kwamba taasisi ambazo zinakusanya na kutumia fedha zinatumia vizuri. Ukitumia ule mfumo wa eyes on, hands off Serikali inaweza ikawasaidia wenzetu wakapata fedha na wakatumia vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwamba nilikuwa ninazungumzia hivi kwenye TDL. Pia, kwenye TDL kuna ule mradi tuliokuwa nao wa REGROW ambao ulileta changamoto kidogo na sasa Serikali imejiweka tayari yenyewe kwamba, sasa itatangaza utalii Kusini mwa Tanzania ambapo mojawapo ni Kitulo na maeneo mengine Kusini mwa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatamani kama hizi Fedha za TDL ambazo tunazipata kama wanaenda kuongeza kwenye effort ambayo REGROW ingefanya, basi wao waende kuweka hiyo effort kuhakikisha kwamba hatupati changamoto tena kuona utalii wa kusini umelala. Wanaenda kutumia pia fedha hii kuhakikisha kwamba wanainua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu sana Mheshimiwa Waziri kuhakikisha Utalii wa Kusini mwa Tanzania ikiwemo Kitulo kwa kweli wanatuunga mkono. Tuna uhitaji wa accommodation, barabara na kuhakikisha kabisa tuna airport ndani ya eneo la hifadhi yetu na tunashukuru kwamba walikuja eneo la Matamba wakapima eneo kwa ajili ya kujenga airport. Tunatamani vile vitu vitokee kwa sababu hii project ya REGROW imefika sehemu imesimama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia huu Mfuko wa TDL, Wizara wahakikishe kwamba wana-support ukuaji wa utalii Kusini mwa Tanzania na sisi watu wa kusini tujisikie afadhali na ahueni kuhakikisha kwamba tunaungwa mkono kwenye Taifa letu. Ukienda Mbeya, Rukwa, Njombe, Morogoro na maeneo mengine ya kusini yana vivutio vingi ambavyo vingeweza kuingiza fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Wizara yetu ya Utalii inakua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo ni maoni yangu kwa sababu ninatamani pia changmaoto kubwa Nyanda za Juu Kusini ni miundombinu ya barabara mvua zinanyesha sana. Kwa hiyo, watalii wakienda, wakirudi muda mwingine wanakuwa wakija hawawezi kurudi tena kutokana na changamoto ya barabara, wanasema kule kuna changamoto. Kwa hiyo, tunatamani wajikite kwenye kutatua changamoto ambazo zitafanya Bodi ya Utalii ukue, lakini changamoto ziweze kutatuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tofauti na hapo niseme wazi ninalishawishi Bunge waunge mkono bajeti hii na Serikali Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa na kusema kweli kabisa Dkt. Samia Suluhu Hassan, anastahili pongezi kwenye sekta hii ambayo sisi tunaisimamia. Wizara ya Maliasili wamefanya kazi nzuri sana. Mheshimiwa Rais amefanya kazi nzuri kuhakikisha kwamba utalii unarejea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukipita Arusha leo, Vijana wa Arusha wanasema Waheshimiwa Wabunge Rais alichotufanyia hapa ndani ya Arusha, imebadilika hatuna haja ya kuhangaika na mambo mengine kwa sababu uchumi umerejea. Wanaona kabisa uchumi umerejea na hifadhi zinaleta matunda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe Wabunge wenzangu wote tuunge mkono bajeti hii, tuiunge Serikali ikafanye kazi, pia niwaombe tu Waziri na…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Sanga muda wako umeisha.

MHE. FESTO R. SANGA: ….watumishi wa Wizara hii kwamba tunawatia moyo sisi kama Wabunge tunaunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana niseme wazi kwamba, ninaunga mkono hoja na ninawapa kila pongezi nikiamini wataenda kufanya kazi vizuri. Ahsante. (Makofi)