Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Zuberi Mohamedi Kuchauka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Liwale

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi kukushukuru wewe jioni hii ya leo kunipatia nafasi nichangie Wizara hii muhimu ya Utalii na Maliasili. Nianze kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa namna anavyopambania maisha ya Watanzania kuhakikisha wanaishi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza mchango wangu kweli nifikishe shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya utalii, vilevile Naibu Waziri wake wa Utalii alishakuja Liwale, changamoto zetu tulimpatia na ametekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi hizi vilevile ziende kwa vijana wale Makamanda, Kamanda aliyepo pale Liwale wa TAWA pamoja na TANAPA wanafanya vizuri. Pamoja na changamoto kubwa tuliyonayo wanafanya vizuri wakiongozwa na Bi. Hadija, Mhifadhi Mkuu wa Kanda. Kwa kweli ni watu ambao ukiwapatia taarifa wanafanya kazi kwa wakati kwa maana wana-act kama inavyotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ninaomba nifikishe salamu, Mheshimiwa Naibu Waziri alipokuja Liwale moja ya changamoto alizopewa ni kuhusu kifuta machozi. Ni kweli tangu mwaka 2021 Liwale tulikuwa hatujapata kifuta machozi, lakini kilio hiki kimepata ufumbuzi baada ya mwezi uliopita. Watu takribani 2,496 wamepata kifuta machozi. Tunashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo wanavijiji walionituma nifikishe hizo salamu; Kijiji cha Ngumbu, Mirui, Ngunja, Mangirikiti, Mtawatawa, Mtawango, Nayuru, Kiangala, Kitogolo, Makinda, Ngorowele Nambinda Lilombe, Nanjegeja, Ngorowopa, Mihumo, Chimbuko, Kikuyungu, Kigwema, Namahonga, Nampigamiti, Namtungunyu. Hawa wote wamenipatia salamu wanashukuru, lakini kushukuru ni kuomba tena. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo limesababishwa na hao wanyamapori. Kuna dalili ya kuwepo kwa njaa kwenye vijiji hivi nilivyovitaja. Hili jambo ni mtambuka lipo kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu, Liwale tuna janga la njaa. Miongoni mwa sababu za njaa kwenye vijiji hivi nilivyovitaja, ziadi ya vijiji 34 hapa nimetaja vichache tu ni kwa sababu ya hawa wanyamapori. Kwa hiyo, tunaomba tusaidiwe vyakula kwa ajili ya wanyamapori.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kwenye uhifadhi tunashukuru kwamba sisi kule ndiyo waathirika wakubwa wa wanyamapori kwa sababu tuna ile Hifadhi ya Nyerere, Selous, Msitu wa Hangai, Msitu wa Nyela - Kipelele; hii sehemu yote ni makazi ya wanyamapori.

Mheshimiwa Waziri, nisikitike tu pale uliposema kwamba kuna ile fence ya umeme. Sikusikia ukitaja hifadhi hizi zote, hakuna hifadhi hata moja iliyotajwa kwamba itapata hii fence ya umeme kuzuia wanyamapori.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo vilevile ahadi ya Waziri aliyepita kwamba tutapewa vile vituo vitatu vya askari. Tukapata kituo kimoja cha Ngumbu, lakini bado tuliahidiwa kutakuwa na Kituo cha Lilombe na Kituo cha Ndapata. Ninaomba iwe kwenye kumbukumbu ya Mheshimiwa Waziri hivi vituo tuvipate, vitusaidie kuongeza idadi ya askari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati ninawashukuru wale Makamanda wetu pale Wilayani wanafanya vizuri, lakini wana changamoto kubwa ya usafiri. Unajua jiografia ya wilaya yetu imetawanyika sana, kwa hiyo gari lile walilonalo kama moja halitoshi. Kwa hiyo, suala la usafiri ni jambo la muhimu sana. Wanaweza wakapata lawama kwamba hawafiki kwenye matukio mapema, kumbe sababu ni usafiri na idadi yao vilevile ni wachache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule nina WMA yangu ya Magingo. Hapa napo ninaomba sheria tulishapitisha kwamba zile fedha za WMA ziende moja kwa moja kwenye jumuiya hii. Jambo hili halijatekelezwa. Miongoni mwa maombi yetu ni maombi ya hizi fedha. Fedha za WMA zinachelewa kufika na zinapochelewa wale kule wahifadhi na wao wanashindwa kulipwa mafao yao. Wasipolipwa askari wale kwa wakati maana yake hawaendi ku-patrol kule hifadhini. Kwa hiyo, ili fedha zile zije mapema ziweze kusaidia uhifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati ule fedha za Covid, Hifadhi ya Mwalimu Nyerere walipata milioni 700 kwa ajili ya kutengeneza barabara ya ulinzi. Ninaomba sana hii barabara ya ulinzi ambayo imetajwa ndiyo barabara ambayo mimi siku zote nimeipigania ndiyo inatuunganisha na watu wa Morogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, niombe kila ukiuliza watu hawa wa ujenzi wanakwambia mpaka waongee na watu wa Maliasili. Ninamwomba Mheshimiwa Waziri wafanye hayo mazungumzo yaishe ili ile barabara yetu ya Mkoa wa Lindi na Morogoro ipatikane pamoja na kwamba inapita hifadhini. Inaonekana kikwazo kikubwa ni kwa sababu tu inapita hifadhini, lakini zipo barabara nyingi tu zinapita kwenye hifadhi zetu mbalimbali kama vile Serengeti na Mikumi huko zipo barabara zinapita. Kwa nini hii Barabara ya Liwale – Morogoro ishindikane eti kwa sababu tu inapita hifadhini? Ninaomba jambo hili lifike mwisho wajadiliane, wakubaline ili barabara hii ya ulinzi iweze kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, jambo lingine la TFS, nayo tunawashukuru kwamba wanafanya vizuri wanatulindia misitu yetu. Hapa ninaomba nichangie mchango mmoja waone namna TFS wanaweza kushiriki kwenye ile Biashara ya Hewa Ukaa kwa sababu miongoni mwa sisi halmashauri tumeshatenga baadhi ya misitu kwa ajili ya kuingiza kwenye hii Biashara ya Hewa Ukaa lakini misitu mingi inayomilikiwa na TFS pale Liwale kwa mfano, kama huo Msitu wa Nyela – Kipelele au Mahangai wameweka mabango mengi. Sasa, sijaelewa ushiriki wao kwenye hii Biashara ya Hewa Ukaa, TFS wana nafasi gani? Ushauri wangu hawa watu wangeweza kufika huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho siyo kwa umuhimu, kuna hii Idara ya Malikale. Sisi pale Liwale ukizungumzia Vita vya Majimaji lipo Jengo la Mjerumani lina ghorofa moja. Lile jengo lina historia kubwa sana na ukifika pale kwa wazee watakuelezea historia ya hili jengo. Mawe waliyojenga lile jengo ni matumbawe yanapatikana Kilwa kilomita zaidi ya 250, babu zetu walibeba na unaona na picha kabisa pale babu zetu wamebeba yale mawe kutoka Kilwa kwa ajili ya kwenda kujenga lile boma. Juzi nimeuliza swali hapa tukaambiwa kwamba kuna mazungumzo halmashauri na Idara ya Malikale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwenye hili hebu tuharakishe hili jambo ili nalo liwemo kwenye vivutio vya utalii. Kwa kweli kama tukiamua kweli kujikita kwenye kuibua utalii kwa Kanda ya Kusini. Kusini kuna vivutio vingi mno, lakini ni vivutio ambavyo vimelala kwa sababu vingi havijaibuliwa. Kwa hiyo, hapo mchango wangu ni kuhakikisha kwamba Idara ya Malikale, waende Liwale waangalie lile boma namna ya kutushauri nini tufanye ili boma lile nalo liingie kwenye urithi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu biashara yoyote ya utumwa ukiizungumzia kabla ya wale watumwa hawajafika Kinyonga ina maana walikuwa wanakusanywa pale Bomani Liwale. Wakishakusanywa pale wanabebeshwa wanapelekwa Kilwa kwenye Soko la Watumwa. Kwa hiyo, Biashara ya Utumwa na Vita ya Majimaji huwezi kuitenganisha na lile Boma la Mjerumani lililopo pale Liwale.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Kuchauka.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja, ahsante sana kwa kunisikiliza. (Makofi)