Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipatia nafasi nami niweze kuchangia. Kwanza, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa kazi nzuri waliyoifanya, tumeona mapato yameongezeka, hongera sana kwa Waziri pamoja na wataalam wake, Katibu Mkuu na Wasaidizi wake. Hongera sana kwa kuifanya Wizara hii kuwa rafiki na Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatokea Geita, ninaomba kuchangia. Geita ninayo hifadhi inaitwa Rubondo. Hii Hifadhi ya Rubondo ni ya kihistoria ipo katikati ya Ziwa. Umri wangu wote Makao Makuu ya hifadhi ile mlango wa kuingia ulikuwa upo sehemu moja inaitwa Nkome, wahifadhi wanafahamu. Kuna majengo, ofisi na kila kitu cha ku-park boat na kila kitu. Miaka miwili au mitatu iliyopita nyuma Wizara iliamua kuhamisha mlango wa kuingia kwenye hifadhi na kuupeleka Chato Muganza. Cha ajabu zaidi Mheshimiwa hifadhi hii inapiga kura kwenye Jimbo la Geita maana yake ipo Kata ya Jimbo la Geita haipo Chato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, ninachotaka kujiuliza ni kwa nini kilitokea hicho kitu watu wa Wizara wanafahamu, sitaki kupingana na maamuzi waliyoyafanya lakini ombi langu kwanza; tunachezea vitu vya Serikali. Pale tuna ofisi za kutosha kabisa, kila kitu kipo mpaka na magari, lakini vimekuwa vikichakaa baada ya kuhama watu wote kwenda Muganza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu ni kwamba vivutio vyote vya ile hifadhi vipo kilomita nne tu kutoka kwenye Mlango wa Nkome, lakini ukiingilia Muganza inabidi uzunguke zaidi ya kilometa 30 ndiyo uje ukutane na hivyo vivutio.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, ninaomba Mheshimiwa Waziri anisaidie hatuna sababu ya kuufunga ule mlango na sina sababu ya kuufunga Mlango wa Muganza kusema mhame, hapana! Kwa sasa kwa sababu utalii umeongezeka na hilo eneo lipo kwenye Jimbo la Geita, ninaomba ule Mlango Mkuu wa zamani wa Nkome ufunguliwe. Kama kutakuwa na milango miwili sawa, sidhani kama Wizara inakosa wafanyakazi wawili au watatu wa kuanzia kurudisha ile heshima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hawapatumii basi ninaomba sisi pale Nkome tuna upungufu wa Shule za Msingi. Ninaomba yale majengo na lile eneo basi Waziri aturudishie tuweze kugawa tuwapatie watoto waweze kukaa pale walau wapate kusoma kuliko kuteketeza yale majengo, hakuna mtu anafanyia kazi, watumishi wote wamehamishwa, radio call zipo pale hazifanyi kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana na hakuna sababu ya kutukwepa kwamba hakuna sifa ya kupita kule. Hotels nzuri za kitalii tumejenga tunazo wanaweza kulala barabara inapitika. Niombe sana watalii hawaji kuangalia lami, kinachowaleta ni kuangalia vitu vya asili ikiwemo na maisha halisi ya Wasukuma wanaokaa maeneo yale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninadhani warudishe ule mlango ili watu wangu wa Jimbo la Geita waweze kwenda kutalii, kuona watalii wanaenda wanapita Nkome maisha yanaendelea. Ninakushukuru sana Mheshimiwa kama hili atalizingatia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nami ninatoka Mkoa wa Geita kuna shamba linaitwa Silayo lipo pale Bwanga. Mheshimiwa Waziri shamba hili lina historia na Silayo nimemwona yumo humu. Mgogoro wa shamba lile, eneo la hifadhi lilimwondoa Waziri, Mheshimiwa Vuai Nahodha, anafahamu wale waliopo kwenye hifadhi operesheni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kile Kitongoji cha Nyakayondwa Kijiji cha Bwanga ni kikubwa Mheshimiwa Waziri kina watu karibu 40,000. Lile shamba hatuna tatizo nalo, watu wanalilinda vizuri miti ya Silayo imepandwa imeota vizuri shamba kubwa. Sasa, kadri wananchi wanavyoongezeka, sisi bahati moja mbaya ukienda kulia unaenda ziwani, ukija huku unakuja kwenye hifadhi. Sisi sifa yetu Wasukuma tunazaa sana na mtu anapozaa watu wanataka kujitegemea hamuwezi kurundikana kwa baba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri kama itampendeza baada ya bajeti yake hebu akatembelee hicho Kijiji kinaitwa Nyakayondwa Bwanga. Kumeenda operesheni, watu wanakata ng’ombe wa watu, wanachoma vyakula. Sasa, hii haiwezi kuwa sawa na haya mambo yote yanafanyika purukushani, tunajua kabisa tunaenda kwenye uchaguzi, halafu zinaanza operesheni za kwenda kufukuza watu, kukata ng’ombe wa watu na kunyang’anya watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, ikimpendeza aende pale akakutane na wale wanakijiji, aone namna ya kuumaliza ule mgogoro, ili wananchi waendelee kulilinda lile Shamba la Silayo. Kwa kweli ni shamba la kihistoria, tunahitaji kulilinda, lakini na sisi tunahitaji kuona kwamba tunaongezeka tunahitaji kuongezwa maeneo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni la Geita. Tumempelekea maombi Mheshimiwa Waziri ninadhani toka ameingia amekuta documents zipo mezani. Watu wa Geita kama ninavyosema sisi tuna bahati kubwa sana ya kuzaa na miji yetu inakua, tunaongezeka. Ukifika Geita Mjini katikati ya mji kulia ni Ofisi za Mkuu wa Mkoa, kushoto kuna Hifadhi inaitwa Usindagwe eneo ambalo lipo mjini huhifadhi chochote hata fisi hawezi kukaa mle, ni vichaka tu vinafuga vibaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulishamwomba muda mrefu atupatie baraka tuanze kujenga, watu wapime tupate viwanja. Katikati ya mji utahifadhi kitu gani? Sana sana tunahifadhi vibaka na mambo mengine. Kwa hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri hili suala la Usindagwe limechukua muda mrefu sana. Ninajua mwenye maamuzi ni Waziri, akitamka hata leo watu wapo tayari kuanza kugawa viwanja pale tujenge, ili na sisi miji yetu ifanane na miji mingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kuwa na miji inayoonyesha ghorofa halafu kulia inaonyesha vichaka vya vibaka. Kwa hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri alichukulie hili suala kwa uzito wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho ninampongeza Mheshimiwa Rais: Mheshimiwa Rais, wakati anafanya Filamu ya Royal Tour Watanzania wengi tulisikia maneno yaliyopita. Ikifika hapo ninaanza kuona faida ya shule, tunahitaji mawazo mapya na ubunifu. Hakuna mtu alitegemea, sisi watu wenye akili tulinyamaza, tukijua tusubiri tuone wazo litakapofikia mwisho, lakini watu waliponda; Rais anaenda ku-act filamu, anafaya kazi za wasanii. Leo hii tunaona faida yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hata Arusha kwa Mheshimiwa Gambo kumetulia kwa sababu ya Royal Tour ya Mama Samia. Huu utalii tunaojisifu leo tumeongeza mapato ni sababu ya ubunifu wa Rais wetu alioufanya kutengeneza filamu ya Royal Tour. Kwa hiyo, ninawaomba Watanzania, watu wazuri wanapokuja na mawazo mazuri, mawazo mapya, tusikatishane tamaa, tuunganane mkono, tumeona faida kwenye royal tour, tunamwomba Mama asikate tamaa, aendelee kuleta mawazo mapya na sehemu zingine ili tuweze kupata matunda zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)