Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026


MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. Nianze kwa pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo yake mengi kwenye hii sekta na yana tija kubwa. Ninampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na timu yao yote ya Wizara kwa maandalizi mazuri ya hotuba na uwasilishaji mzuri ambao umeeleweka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ushauri katika maeneo mawili. Eneo la kwanza, umuhimu wa jumuiya za hifadhi zinazoshirikisha wananchi kuanzishwa katika maeneo mengi. Kwangu kule Sikonge kwa kweli kuna matatizo makubwa sana ya uhifadhi. Watumishi wa TAWA na TFS ni wachache mno kuweza kudhibiti maeneo waliyokabidhiwa. Kwa mfano, TFS Sikonge inatakiwa ihifadhi misitu minne. Msitu wa Itulu, Iswangala, Inyonga na Nyahua, ambapo maeneo yote haya yana kilometa za mraba 14,712 au hekta 1,479,208, eneo hilo ni kubwa sana, lakini watumishi ambao wameajiriwa na Serikali wako chini ya TFS, wako 17 tu na wengine 10 ni watumishi wa mikataba ya muda mfupi mfupi. Hivi hawa watu 27 ndiyo wanaweza wakadhibiti eneo lote hilo? Jibu ni kwamba haiwezekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge nayo ina misitu mitano ya hifadhi; Ipembampazi, Ugunda, Wala, Sikonge, na Goweko. Jumla ya kilometa za mraba 5,175 au hekta 517,560. Halmashauri nayo ina watumishi 17 tu wa Maliasili, kati ya hawa, watatu tu ndiyo Maafisa Wanyamapori. Hivi unategemea hawa watumishi wachache namna hiyo ndiyo wadhibiti eneo lote hilo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaishauri Wizara ianzishe jumuiya za hifadhi kwenye Kata za Kitunda na Kiloli, jumuiya moja; Kata za Kipili na Kilumbi jumuiya ya pili; na Kata za Nyahua, Igigwa, Kisanga mpaka Kiloleli nao wawe na jumuiya moja kubwa. Hizi jumuiya tatu ndiyo zitawasaidia hawa Maafisa wa Serikali Kuu, TAWA na TFS, pamoja na Maafisa wa Halmashauri kuweza kudhibiti na kutunza vizuri hizo hifadhi, vinginevyo encroachment ya wananchi itaendelea na hakutakuwa na udhibiti mzuri kwa sababu ya eneo kuwa kubwa na watumishi wachache. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, encroachment hii inaharibu mpaka mazalia ya nyuki na inaathiri mpaka Sekta ya Asali na Nta. Kwa hiyo, ninashauri Wizara ishirikiane na halmashauri kuanzisha hizi jumuiya za wananchi. Tunayo jumuiya moja kwenye Game Reserve ile ya Ipole, hiyo jumuiya moja ndiyo inasaidia hifadhi angalau kidogo, lakini kwingine kote kuna shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwenye eneo la pili, tunao Mradi wetu wa Umwagiliaji wa Uluwa, huu ni mradi ambao ulianzishwa na Mwalimu Nyerere mwenyewe. Mwaka 1972 Mwalimu Nyerere alikuja na Sera ya Siasa ni Kilimo ambayo ilikuwa ni sera rasmi ya TANU. Mwaka 1975 zilipatikana fedha za kuchimba mabwawa 1,000, miongoni mwa mabwawa 1,000 yaliyochimbwa ni Bwawa la Uluwa kule Kiloleli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hili bwawa kuchimbwa likakamilika, mwaka 1977 Mwalimu Nyerere mwenyewe ndiye alikuja akalizindua hili bwawa. Siku ya kuzindua hilo bwawa akatoa hotuba akisema Wizara ya Kilimo ikamilishe miundombinu ili wananchi waanze Kilimo cha Umwagiliaji wa Mashamba. Sasa, kilichotokea kwa nini hayakujengwa mwaka 1978? Fedha zote zilielekezwa kwenye vita baada ya kuzuka Vita ya Uganda, ndiyo maana mradi ule haukujengwa wakati wa Mwalimu Nyerere.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mradi ulikuja kuanza kujengwa mwaka 2007/2008, baada ya Wizara ya Kilimo kukumbuka maagizo ya Mheshimiwa Rais Nyerere kipindi kile, wamejenga mradi ule umekamilika....

Mheshimiwa Mwenyekiti, muda umeisha au ni kengele ya kwanza?

MWENYEKITI: Endelea.

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, aah bado bado!

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili bwawa limejengwa na miundombinu ikakamilika, wakati wanajiandaa kwa uzinduzi wa mradi tarehe 27 Januari, 2010 ilikuwa mradi uzinduliwe mwezi Februari, 2010, akaja Afisa Maliasili akatoa katazo la kuzuia. Hii Hifadhi ya Ipembampazi ni hifadhi ya Halmashauri, lakini sasa kwa nini Afisa Maliasili wa kutoka Wizarani amekuja akazuia ule mradi na mpaka leo haujawahi kufanya kazi? Serikali ndiyo iliwekeza na Serikali ndiyo imezuia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba, kwa sababu Afisa Maliasili yule alisema ipatikane ridhaa ya Waziri wa Maliasili na tumemfuatilia sana. Waziri Maige alikuja akatembelea pale akasema hakuna tatizo lolote, akaja Naibu Waziri Mheshimiwa Eng. Dkt. Ramo Makani akatembelea pale akasema hakuna tatizo. Akaja Waziri Mheshimiwa Profesa Magembe mwenyewe akafika pale akasema hakuna tatizo, akaja Waziri Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla akasema hakuna tatizo, tatizo ni kwamba, barua tu ya idhini ya Waziri ndiyo haijapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba leo Mheshimiwa Waziri atoe tamko la kuruhusu. Pale kinachochukuliwa ni hekta 550 tu, wakati mbuga yenyewe ya Ipembampazi ina hekta 133,000. Hebu angalia ukubwa wa mbuga hekta 133,000 na hawa wakulima watafaidika na hekta 550 tu. Kwa nini Wizara imekataa kuruhusu mradi huu kwa miaka yote hii; ambao ni mradi unaomuenzi Mwalimu Nyerere. Kwa hiyo, ninaomba Waziri atoe ufafanuzi wa kueleweka, vinginevyo tusije tukafika mpaka tunashika shilingi wakati wa kupitisha mafungu ndiyo tueleweke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. (Makofi)