Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Margaret Simwanza Sitta

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Urambo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na nichangie hoja iliyoko mezani. Kwanza ninamshukuru Mwenyezi Mungu; pili, ninawashukuru wapigakura wa Urambo pamoja na familia yangu kwa ushirikiano wanaonipa; na tatu, kipekee ninamshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia, Rais wetu, kwa miradi mikubwa aliyotupa Urambo, lakini kwa sababu ya muda sitapata nafasi ya kuitaja yote. Ninamshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishukuru Wizara, Waziri Mwenyewe Mheshimiwa Dkt. Pindi Chana, Mheshimiwa Dunstan kitandula, Katibu Mkuu Dkt. Abbas na wengine wote walioko ndani ya Wizara hiyo, Idara zote zinafanya kazi vizuri, hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, asubuhi nilikuwa ninapita nikitoka kwangu, nikapita pale Chinangali Park nikaona kaulimbiu nzuri sana, ninawapongeza Wizara ya Maliasili na Utalii. Inasema, “Nyuki ni Uhai na Uchumi Imara, Tuwahifadhi”. Nilikuwa nimepanga kuja kuchangia, kwa kweli hiyo kaulimbiu imenifurahisha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa, nyuki ni kwa uhai, uchumi imara, tuwahifadhi na ndicho ninachokizungumzia leo kwa niaba ya wananchi wa Urambo, hususan Kata Nne ambazo zimo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Mto Ugalla. Ninaomba niliweke wazi ndani ya Bunge hili kwamba, sisi kama wananchi wa Urambo tunaheshimu sana Hifadhi ya Taifa ya Mto Ugalla. Tunajua madhumuni yake kwa faida ya sasa na ya baadaye. Kwa hiyo, tunaunga mkono, tatizo letu sisi ni hilo moja tu ambalo linatokana na kaulimbiu hii hapa, kwamba nyuki ni uhai, hata ukisema nyuki kwa uhai na uchumi imara, tuwahifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ghafla tu tulisikia kwamba Serikali imegeuza sasa eneo lote lile la pale kwetu Urambo, ambalo ndani yake kuna Kata Nne ambazo ni Nsenda, Ukondamoyo, Kasisi na Ugalla. Ghafla limeshageuzwa lile umekuwa Msitu wa Hifadhi ya Taifa. Kimsingi wazo ni zuri, tatizo lilitokea tu kwamba, wazo zuri, lakini lilifikishwa kwa utaratibu usioeleweka, tulishtukia tu ghafla kwamba sasa wananchi hawawezi kuingia hapa kwa sababu tayari imeshakuwa Hifadhi ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa msingi huo, kitu kikubwa ambacho kilikosekana pale ni elimu kwa wananchi, kwamba maana ya Hifadhi ya Taifa ni nini? Wao watabaki na nini? Kitu gani watakuwa nacho, kitu gani watakosa, hapo ndiyo palipokosewa, elimu na ushirikishwaji wa wananchi. Wazo lilikuwa zuri, lakini utaratibu uliotumika ndiyo ninasema Mheshimiwa ulitakiwa ufanyie kazi vizuri kwa kuwaandaa wananchi waliomo mle ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizo Kata Nne zina maeneo mengi ambayo ninapenda niyataje ili wajue kwamba kwa kweli maeneo mengi sana yameguswa. Kuna eneo la Kangeme, Lunyeta yenyewe, Kangeme, Mpola, Mtakuja, Magimagi, Holongo, Itewe na Msumbiji. Ni maeneo mengi ambayo yameguswa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafikiria kwamba, kwa sababu tunatambua kwamba ni muhimu kuwa na Hifadhi ya Taifa, lakini wakati huo huo tunaamini kwamba kuna umuhimu wa ushirikishwaji wa wananchi, ninaomba nilete maombi manne kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi la kwanza, bado Wizara ya Maliasili na Utalii iandae utaratibu wa kukusanya hawa watu wanaohusika, wawe na kikao chao ili waone kweli Serikali inawathamini lakini wakati huo iwaelezee maana ya hifadhi na wao watabaki na nini na kitu gani kitakwenda kwenye Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ulivyosikia nilivyosema kaulimbiu, nyuki ni uhai. Kwanza asali yenyewe ni dawa, ni chakula, lakini ni uchumi imara tuwahifadhi, kwa miaka yote maeneo haya yalikuwa yanafuga nyuki. Ombi letu la pili, baada ya kuwashirikisha na kuwapa elimu, ombi letu la pili tugawiwe eneo hili angalau kilometa tano ili wananchi waendeleze huu uchumi imara wa asali ambao pia ni chakula, kwa hiyo, tunaomba angalau kilomita tano za eneo lile, Serikali itufikirie waturudishie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, tunaomba hapa hapa Bungeni, tunaomba tu tuikumbushe Wizara kwa nia nzuri tu, kwa kuwa waliamini na wao maneno yetu kwamba ni uchumi imara, wakaahidi huu humu Bungeni kupata mashine ya kuchenjua asali, tunaomba na sisi tuchenjue. Baada ya kupata mizinga, tufuge nyuki, tuchenjue asali ili na sisi tuuze asali kutoka Urambo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho katika haya maombi yangu makubwa manne, eneo la Lunyeta kuna lango ambalo lilikuwepo zamani tunaomba walifufue, kwa sababu kuna mindombinu ya umeme kuna miundombinu ya simu, kwa hiyo tunaomba nasi Urambo tuwe na lango ambalo watalii watapita huko kwa sababu eneo ni kubwa, kuna wanyama na kadhalika, tunaomba Serikali yetu na sisi ituwekee lango. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hivyo, Serikali yetu ni sikivu, Wizara Watendaji wazuri, ninaamini kabisa leo tutapata majibu mazuri ili na sisi wa Urambo tupate asali kwa ajili ya uhai, hatimaye uchumi imara na maendeleo oyeee! (Makofi)

WABUNGE FULANI: Oyee!