Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Daimu Iddi Mpakate

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kupata nafasi jioni hii kuchangia juu ya hoja iliyopo mezani ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Kwanza kabisa ninamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ziara aliyoifanya Tunduru akishirikiana na Waziri Maliasili na Utalii, kwa maelekezo yake sasa angalau vurugu ya tembo imepungua kwa asilimia kubwa. Tunashukuru tumepata VGS 28 katika maeneo ya TAWA, TANAPA, pamoja na TFS, lakini tumeletea Ndege Nyuki wawili wanaosaidia kufukuza tembo, vilevile tumepata kituo kimoja cha kudumu na vituo viwili vya muda katika Kijiji cha Mbesa na kule Matemanga ambavyo vinasaidia kuwafukuza tembo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada hizo kubwa tunaomba sana tusaidiwe kuongeza Askari, Jimbo la Tunduru Kusini na Tunduru kwa ujumla tuna hifadhi nyingi na tembo wanasumbua kutoka Selous, wanasumbua kutoka Msumbiji, at least kila Tarafa ingepata camp moja kwa ajili ya kufukuzia tembo ingetusaidia sana, hasa Tarafa ya Nalasi, Tarafa ya Lukumbule na Tarafa ya Namasakata, ingeweza kutusaidia kufukuza hawa wanyama wakali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, katika Hifadhi yetu ya Mwambesi, ni ya muda refu sana, ni hifadhi ya kijamii. Mwanzo lilikuwa ni eneo la uwindaji, lakini sasa hivi limebaki kama hifadhi na hifadhi ile imekaribiana sana na wananchi wa vijiji 12 katika Tarafa ya Namasakata na Tarafa ya Lukumbule. Ni muda mrefu sana wananchi wa Vijiji vya Mchesi, Jiungeni, Kazamoyo, Imani, Angalia, Mwenge, pamoja na vijiji vingine 12 waliomba kupata maeneo ya kulima kutokana na idadi kubwa ya wananchi walioongezeka ili wapate namna ya kujikimu kwa njia ya kilimo. Kwa hiyo, tunaomba sana tufikiriwe mpango huu wa Mwambesi kugawa sehemu angalau watu wetu wapate maeneo ya kulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, niongelee kuhusu TAWA. Nimesikiliza hotuba ya Mwenyekiti katika mapendekezo aliyoyatoa ya kufanya retention ya pesa ya makusanyo yao, ninawaona TAWA wamesahaulika, lakini hawakusahaulika kwa bahati mbaya, TAWA tangu miaka ya nyuma kama sijasahau kwa sababu kipindi hiki si kipindi cha kumbukumbu sana. Ninakumbuka Kamati ilipendekeza iletwe sheria ya kuifanya TAWA iwe independent entity kama ilivyo TANAPA pamoja na Ngorongoro ili kuifanya TAWA iwe taasisi inayojitegemea na bodi yake iwe na mamlaka halisi ya kufanya maamuzi badala ya kushauri, mpaka kusubiri Mkurugenzi wa Wanyamapori apitishe then waende kutekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli TAWA wana matatizo mengi sana, moja ya matatizo ni eneo lao la operation ni kubwa ukilinganisha na Ngorongoro, ukilinganisha na TANAPA. Wanyama wote wakitoka TANAPA, wakitoka Ngorongoro, nje ya maeneo ya mipaka yao wanakuwa wanamilikiwa na TAWA. Kwa hiyo, TAWA nchi nzima hii wana maeneo makubwa ya operation kuliko TANAPA ilivyo na hawa wenzetu wa Ngorongoro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, jambo la kwanza wanatakiwa wafikiriwe kuwa taasisi kamili, jambo la pili waongezewe mishahara. Katika taasisi za hifadhi hawa watu wa TAWA ndiyo dhalili wana mshahara mdogo kuliko TANAPA, kuliko Ngorongoro. Kwa hiyo, hata TFS nao wamewazidi mishahara wakati wote wanaajiriwa katika mtindo mmoja, wote ni Askari USU ambao wanapaswa wale walioko kwenye rank moja, basi wapate mshahara kulingana na wenzao pia kazi kubwa ya uhifadhi ya kutunza wanyamapori wanao hawa TAWA. Kwa hiyo, ninaomba jambo hili la kisheria lifanyiwe kazi ili mapungufu haya ya mshahara na operation yaweze kufanya TAWA ifanye kama wanavyofanya wenzake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na changamoto za TAWA, kwa Jimbo letu la Tunduru Kusini kwa kweli ninawashukuru TAWA, kwa sababu ndiyo wanaosaidiana na Halmashauri yetu kwa asilimia kubwa kufukuza wanyama wakali ambao wanasumbua wananchi wetu. Juzi tu hapa Jumamosi kutokana na matumizi ya Ndege Nyuki, tembo walikimbia wakamwacha mtoto, mtoto yule akabaki anahangaika kwenda huku na kule, bahati nzuri akakutana na watu wakamfunga kamba tembo mtoto wakaondoka naye mpaka kijijini, kitu ambacho ni hatari, lakini watu wa TAWA wakamchukua yule tembo mtoto wakamrudisha kwenye hifahdi. Hili jambo linafanyika kwa sababu wale wako karibu, sasa, wakiwepo VGS kila eneo, itatusadia changamoto kama hizi kuzitatua kwa haraka iwezekanavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ambalo ninadhani ni suala la malipo ya fidia au kifuta jasho. Katikati hapa mlianzisha mtindo wa kutumiwa kwa mtandao. Kidogo lile jambo lilikuwa linaenda vizuri, lakini linachelewesha, wameamua kurudi kwenye mfumo ule wa zamani wa manual. Jambo hili linachelewesha malipo ya wananchi wetu, lakini kipekee ninaishukuru Serikali kuongeza kiwango cha kulipa kifuta jasho, kutoka shilingi laki moja mpaka shilingi laki mbili kwa hekta na mtu yeyote aliyeathirika kutokana na ukubwa wa shamba basi afanyiwe hesabu kulingana na ukubwa wa shamba kuliko ilivyokuwa zamani kwamba chini ya heka moja Serikali ilikuwa haiwezi kulipa fidia ya aina yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru tena kwa ile fidia ya wale ambao wameuawa na wanyama wakali au kudhurika, kwa malipo ya shilingi milioni mbili ingawa hayalingani na uhai wa binadamu, at least itaendelea kufuta jasho kwa hawa ndugu zetu ambao wanaathirika na hao wanyama wakali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa ninawashukuru Serikali wameona umuhimu wa kuondoa baadhi ya tozo ambazo zilikuwa zinazuia kuendeleza au wananchi wazawa kufanya shughuli za uwekezaji katika utalii. Ninaipongeza sana Serikali kuhusu jambo hili ninaomba lisiishie hapo, waangalie hata yale maeneo ambayo sisi wadogo tunaoanza kwenye Sekta ya Utalii wapunguze zaidi ili kuvutia Watanzania washiriki katika suala la utalii wa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuunga mkono hoja na ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)