Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Hawa Subira Mwaifunga

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye Wizara hii ya Maliasili na Utalii. Kwanza kabisa, ninamshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunijalia afya na uzima, kuweza kusimama katika Bunge hili Tukufu, katika bajeti hii ya Maliasili ambayo ni ya mwisho katika Bunge hili la Kumi na Mbili12 na mimi kuchangia hoja hii ya Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Wizara watuambie, maana nilikuwa ninajaribu kupitia hotuba yao. Tangu baada ya Royal Tour sijaona Wizara ikija na mkakati wowote wa kuendeleza utalii. Baada ya Royal Tour sijaona jambo lolote jipya lenye kuvutia ambalo litatufanya tuondoke kwenye Royal Tour tuje tuingie kwenye jambo hilo lingine ambalo litavutia hata watalii wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni mapungufu makubwa sana kwa Wizara ambayo tayari ilikuwa imewekwa juu kabisa na Mheshimiwa Rais, katika suala zima la kutangaza utalii wetu. Sasa kama wao wenyewe bado wanasubiri tena mbeleko ya namna hiyo, sidhani kama tutafika tunapotakiwa kufika kwa sababu lazima tuongeze mapato kupitia utalii wetu nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku zote tunasema, Tanzania kwa masuala ya utalii vivutio vyetu ni vingi kweli kweli, lakini bado Wizara haijafanya kazi ya ziada kuhakikisha kwamba kwenye eneo hili tunapata fedha za kutosha kupitia utalii wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona nikumbushe hilo ili wenzetu hawa tuwaamshe kwamba jamani, sasa Royal Tour, Royal Tour, Royal Tour tena sasa hatuwezi kuendelea nayo miaka yote. Tutaisema ilikuwepo na imefanya vizuri kwelikweli kuliko kipindi kingine chochote, lakini mje sasa na mkakati mwingine au jambo lingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano nilikuwa ninajaribu kupitia hapa. Leo Tanzania na sisi ni sehemu ya watu ambao tutakuwa wenyeji wa mashindano ya AFCON na CHAN lakini Wizara ya Maliasili mpaka sasa mbona hatuoni nini ambacho wanataka kufanya katika masuala mazima ya ku-promote utalii wetu nchini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana labda wenzetu hawajui ama kwa sababu tumezoea mambo ya zima moto, tunataka sasa tuanze tena yale mambo yetu ya last minutes ndio tunaanza kukurupuka, tunaanza kufanya aje, tunaanza kuchezea hela tu bila sababu zozote. Twende polepole wakati tukielekea kwenye mashindano hayo ili tuweze kuutangaza utalii wetu sawasawa na utalii huu utaweza kutuingizia kipato kikubwa kuliko hata hiki ambacho tunakipata sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Mkoa wetu wa Tabora ni mkoa ambao una mapori mengi sana. Eneo ni kubwa la Tabora na Tabora ndio mkoa mkubwa nchini. Nchi hii ya Tanzania, Mkoa wa Tabora ndio mkoa mkubwa ambao una eneo kubwa, lakini eneo kubwa la mkoa wetu ni pori. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliomba wakati ule Kamati ya Mawaziri Nane inapita, tukasema tusaidiwe, watu wetu wameongezeka. Leo kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2022, sisi ni wa tatu kwa wingi wa watu katika nchi hii. Kutokana na hilo tusaidike basi kwenye maeneo yetu mbalimbali tuweze kuongezewa maeneo ya watu wetu kuishi na kufanya shughuli zao za kila siku na hii itapunguza migogoro ya hifadhi na wananchi kwenye hayo maeneo ambayo yapo karibu na mapori. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaona muda sio rafiki sana, lakini pamoja na kuwa tuna ukubwa wa mapori haya, lakini bado hata askari wetu wanaolinda mapori haya: moja; ni wachache na hawatoshi, pili; askari hawa wa TAWA bado hata vipato vyao haviridhishi. Hili jambo ninalirudia tena, ninasema; kwa nini kunakuwa na matabaka? Nawauliza Maliasili na Utalii kwa nini kunakuwa na matabaka?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwani haya majukumu hawayaoni ama hawayajui, kwamba hawa watu wanafanya kazi ya aina moja? Wanaolinda mapori na wanaolinda hifadhi, hawa wanafanya kazi ya aina moja, hawana kazi tofauti. Kwa hiyo ni lazima waangalie uwezekano wa kuweza kuwasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho lakini sio kwa umuhimu, ni kuhusu huu Mfuko wa Maendeleo ya Utalii. Nilikuwa ninajaribu kupitia baadhi ya viambatanisho, lakini ninaomba niseme jambo dogo kwa Wizara na huu ni ushauri. Baada ya kupitia hii na haya ambayo nimekutana nayo hapa, ninaomba nishauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii waunde chombo maalum ambacho kitasaidia kudhibiti matumizi ya fedha hizi; kwa sababu gani ninasema hivi? Sisi Wabunge nami nikiwa miongoni mwao, tulipambana kuiomba Serikali iweze kusaidia zipatikane fedha ili tuweze kusaidia hifadhi zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulisema hapa TANAPA imeongezewa hifadhi, kutoka zilizokuwepo zikaongezeka zaidi. Hawa wenye hifadhi zilizoongezeka hawana uwezo wa kujiendesha. Kwa hiyo, kukiwa na fedha ambayo itasaidia wataweza kufanya zile hifadhi nyingine zianze kufanya kazi zao bila kutegemea watu wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niwaombe na nimwambie Mheshimiwa Dkt. Pindi Chana, Waziri wa Maliasili na Utalii, unda chombo maalum. Wakati tutakapokuja kwenye bajeti ijayo, maana tutakuwepo wote (Inshallah, Inshallah tutakuwepo wote humu ndani Inshallah), tukute hiki chombo kimeundwa ili muweze kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima ya fedha hizi. Hizi fedha ni nyingi na zinakwenda bila utaratibu. Hili jambo si sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante ninakushukuru. (Makofi/Kicheko)