Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ninaomba nimtangulize Mwenyezi Mungu katika mchango wangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nitoe pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu ambaye kupitia Royal Tour ameweza kuhakikisha kwamba ameongeza idadi ya watalii nchini, lakini pia pato limeongezeka kupitia utalii kutokana na Mheshimiwa Waziri alipotusomea hotuba yake. (Makofi) 
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri ambayo amekuwa akiifanya kusimamia Wizara hii. Vilevile, nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kazi nzuri anayoifanya katika Wizara hii, Katibu Mkuu Dkt. Abbas na Makatibu Wakuu wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanazozifanya na watendaji wote wa Wizara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaendelea kuipongeza Serikali kuhusu na Mradi wa REGROW. Kwanza, ujenzi wa barabara ile ya Msembe, inayokwenda Ruaha National Park; tunashukuru sana. Pia, ujenzi wa Kiwanja cha Ndege Iringa tunajua kwamba sasa utalii utakwenda kwa kasi kubwa lakini pia na ujenzi wa jengo la TAWIRI katika kituo cha Kihesa Kilolo, mimi nawapa maua yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, majengo mengine wanakamilisha lini? TTB, TFS, ISCC na Chuo cha Utalii cha Taifa lini sasa majengo yao wanakuja kuyajenga pale eneo la Kihesa Kilolo ili huu Utalii sasa hii REGROW iweze kwenda vizuri? Tutaomba majibu watakapokuwa wanajibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni elimu kiasi gani sasa wananchi wa Iringa au wa Nyanda za Juu Kusini wameweza kupata katika kuendeleza huu utalii ili pia waweze kujiajiri kupitia utalii? Kwa sababu mradi huu wa zaidi ya shilingi bilioni 23 ninafikiri ulitakiwa uishie Januari 25 mwaka huu, sasa tupo mwezi wa tano; je, ukiisha huu mradi tutapatiwa mradi mwingine kwa ajili ya kuendeleza utalii Kusini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nielezee kuhusu maonesho ya utalii Kusini. Tunatambua kuwa Mkoa wa Iringa ni kitovu cha utalii kwa Mikoa ya Iringa, Mbeya, Njombe, Rukwa, Ruvuma, Songwe, Katavi, Morogoro, Lindi na Mtwara.  Mwaka 2019 Wizara ikishirikiana na mikoa hii ilianzisha Maonesho pale katika eneo la Kihesa Kilolo na kumpatia heshima Spika, wetu Dkt. Tulia Ackson, ambaye alikuwa ndiye mgeni rasmi na Maonesho hayo yalihudhuriwa na zaidi ya wananchi 58 elfu. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninaomba niwaulize maswali yafuatayo: je, ni kwa nini Wizara imeiachia mikoa wakati ikijua bajeti yao haiwezi kukidhi maonesho hayo ya kitalii ya kimataifa, kwa sababu wao wanatumia OC tu kwa ajili ya maonesho hayo? Je, kwa nini Wizara isichukue jukumu la kusimamia maonesho hayo kama ilivyofanya mwaka 2019 wakati huo najua Katibu Mkuu alikuwa Profesa Mkenda? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, je kwa nini Bodi ya Utalii wasiratibu maonesho hayo ili hadhi ya kimataifa iweze kudumishwa na kurahisisha kuunganishwa Mikoa ya Kusini kuendeleza utalii wetu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, ninaomba nishauri kwamba, Wizara iyasajili hayo maonesho kama yalivyo CTITE ili iyape kipaumbele kuyasimamia ili Nyanda za Juu Kusini tuweze kufanya vizuri kupitia utalii. (Makofi)  
Mheshimiwa Mwenyekiti, nielezee kuhusu wanyamapori waharibifu. Hili tatizo la wanyamapori hasa tembo na mamba kwa kweli katika Mkoa wetu wa Iringa wananchi wanateseka sana. Kuna baadhi ya maeneo kama Mahenge, Magana, Msosa, Ikula, Udekwa, Utalisoli katika Wilaya ya Kilolo wananchi wanateseka mno. Mashamba yao yanaliwa, wameuawa na kuna watu karibu sita wameshapoteza maisha kwenye Kijiji cha Msosa na Kijiji cha Mtandika, lakini hawa wote bado hawajaweza kupata hata kifuta jasho wala kifuta machozi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliuliza swali juzi kwamba hawa wananchi walioharibiwa mashamba yao bado hawajalipwa kutoka mwaka 2020 mpaka 2025 na majina yao nimeomba wameshaniletea ninayo hapa na leo baada ya kuchangia nitakukabidhi ili wananchi hawa waweze kulipwa kifuta jasho na kifuta machozi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, katika maeneo mengine ya Idodi, Pawaga, Izazi na Migoli - Iringa vijijini na kwenyewe watu wanapata shida sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ilikuwa na mpango wa kuanzisha hizi WMA lakini ule mpango ukoje? Ninataka tujue kwamba, tulijua kwamba hizi jumuiya ndio zitasaidia uharibifu ambao unajitokeza lakini na ulinzi wa hawa wanyamapori. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kuuliza pia; hifadhi ya Udzungwa 75% ipo katika Milima ya Udzungwa katika Wilaya ya Kilolo na wananchi wanaoishi katika maeneo hayo wanaitwa Wazungwa lakini hii hifadhi inatajwa kutokea Morogoro. Sasa ninataka nijue; je, wananchi wa eneo hilo na halmashauri zinafaidikaje, zinapata nini kutokana na kuwepo 75% katika eneo hilo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa niombe sasa Wizara ijaribu kuangalia Nyanda za Juu Kusini tuna vivutio vingi sana ambavyo bado havina matangazo, havitangazwi kiasi cha kutosha. Mheshimiwa Sanga amesema, lakini pia miundombinu ya kwenda kwenye hivyo vivutio wala sio vizuri.  Kwa hiyo tunaomba Nyanda za Juu Kusini ukiwepo Mkoa wa Iringa sasa iangaliwe kwa ukaribu ili pia wananchi waweze kujiajiri kupitia utalii na vilevile tuweze kupata pesa nyingi kupitia utalii wa Nyanda za Juu Kusini ili na sisi tuchangie pato kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa ninaomba sasa Mkurugenzi wa Utalii au Waziri au Katibu au Naibu Waziri hebu waje watembelee Kihesa Kilolo, Kihesa Mgagao - Kata ya Ng’uruhe Wilaya ya Kilolo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi nilikuwa nimeelezea hapa kwamba kule kuna eneo zuri sana waliishi wale wapigania uhuru wakimbizi, ambapo katika eneo hilo kuna vyumba ambavyo waliishi maraisi. Lile eneo, kuna ambalo waliishi watu wa South Africa...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Dkt. Ritta Kabati, kengele ya pili ilikuwa umalizie.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Ninaomba waje waangalie kuna utalii mkubwa na wenzetu Gereza alilolala Nelson Mandela, limekuwa utalii mkubwa na wanaingiza pesa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)