Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilwa Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia. Kwanza ninampongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kufanya kazi kubwa kupitia sinema ya Royal Tour na Amazing Tanzania ambayo imeweza kuchechemua Sekta hii ya Utalii na kuongeza mapato maradufu na idadi ya watalii maradufu katika nchi yetu (watalii wa ndani na wa nje).
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri na Wizara nzima ya Maliasili na Utalii kwa kazi kubwa wanayoifanya, sambamba na taasisi zilizo chini ya Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wilaya ya Kilwa tuna sehemu kubwa ya mafanikio ambayo yamepatikana. Tumepata GN Na. 163 na 166 zilizotambua mnara wa mashujaa wa Majimaji pamoja na mapango ya Nang’oma na Namaingo. Pia, tuliweza kuletewa boti ya kitalii pale Wilayani Kilwa Masoko ambayo imetumika kuongeza idadi kubwa ya watalii maradufu ya ilivyokuwa hapo kabla. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru pia juhudi zimefanywa na taasisi ya TAWA katika kutoa elimu ya uhifadhi kwa wananchi wetu. Wananchi wetu zaidi ya 2,000 wamepewa elimu ya uhifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona hapa Sekta ya Utalii imepanda kiwango cha uchangiaji baada ya kuwa mapato mengi yamepatikana hadi kufikia 21%. Ni imani yangu kuna mambo ambayo ninakwenda kuishauri sasa Serikali, ikiyatekeleza nina hakika tutapandisha sehemu ya pato la Taifa kufikia hadi 40% mpaka 50% kutokana na vivutio vya Utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ushauri wangu ni katika maeneo yafuatayo kwenye Kumbukizi za Majimaji sambamba na yale mapango yaliyopo Kilwa, ninashauri GN itolewe na uwekezaji ufanyike katika mapango 17 yaliyopo sambamba na yale matatu, ambayo tayari yametolewa GN Namba 163. Ninaomba pia, Serikali itekeleze ahadi na mkakati wake wa kujenga Nyumba ya Makumbusho, Nandete, ambayo inahusiana na Vita vya Majimaji, lakini pia, iweze kujenga ngazi kushuka kwenye pango kubwa kuliko yote la Nang’oma, ambalo limepewa GN Namba 163. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru Serikali yetu, kupitia Wizara hii ya Maliasili na Utalii, imeweza kuanza kutoa tuzo. Sisi Wanakilwa tulianza kutoa tuzo tangu Majimaji iliyopita, tulipotimiza miaka 119. Tulimtunukia Mheshimiwa Zakia Meghji, kama ambavyo mmefanya kwa sababu, yeye ndiye alikuwa Waziri wa kwanza wa Utalii kuingia katika pango kubwa kuliko yote la Nang’oma, mwaka 2001. Pia, tulitoa kwa Mashujaa wengine wa Majimaji na Waziri Mstaafu wa Utalii, dada yangu, Mheshimiwa Angellah Kairuki. Kwa hiyo, tunamkaribisha Mheshimiwa Waziri katika maadhimisho ya mwaka 2025 naye tuje tumpe tuzo yako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sasa nitoe ushauri kwa Serikali, pia, kule kuliko na Boma la Wajerumani, Kibata, kutolewe GN kuliko kuwa na shamba la pamba, pale Kikwetu. Ginnery ya pamba ilikuwepo pale enzi za Wajerumani, nako kutolewe GN. Kuna GN katika Mlima Imbiliya ambao mtu wa kwanza katika Vita vya Majimaji aliuawa pale, ninaomba pia GN itolewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende pia, kuzungumzia yale ambayo wamezungumza wenzangu kuhusiana na kadhia ya wanyama aina ya ndovu. Mheshimiwa Waziri, tuna vijiji zaidi ya 12 katika Wilaya ya Kilwa, ambavyo vinakumbwa mara kwa mara na vingine kila siku kila kukicha. Hivi, ninapozungumza muda huu, tayari kuna vijiji tembo wameshaingia toka alfajiri; kuna Kijiji cha Zinga Kibaoni, Mitole, Mtepera, Kikole, Ruhatwe, Nakiu, Mkarango, Kandawale, Ngarambi, Namatewa, Kipindimbi na Kisimamkika. Hivi vijiji watu wetu wamekuwa wakisumbuliwa sana na wanyama wakali na wasumbufu aina ya ndovu, ambao kila kukicha wamekuwa wakivamia katika hivyo vijiji. (Makofi)
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa, Mheshimiwa Ngassa.
TAARIFA
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana. Ninapenda kumpa Taarifa Mheshimiwa Ndulane, hata sisi pale Igunga, Maeneo ya Itumba, Mtunguru, kule tumekuwa tukisumbuliwa na tembo mara kwa mara na kusababisha maafa kwa wananchi, lakini tumeshatoa Taarifa Wizarani. Kwa hiyo, tunaona pia, na sisi tusaidiwe maeneo ya Mtunguru na Itumba. Ninampa Taarifa hiyo Mheshimiwa. Ahsante. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Ndulane, unaipokea Taarifa hiyo?
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na nimeipokea kwa mikono miwili kwa sababu, hilo ni tatizo la Kitaifa. Kwa hiyo, kumekuwa na shida kubwa na kwa bahati mbaya katika eneo letu sisi tembo huwa wanaingia jioni wanatoka alfajiri. Wamekuwa wakiharibu miundombinu mbalimbali ikiwemo nyumba za wananchi, mazao yao na pia, hata mazao yaliyohifadhiwa kwenye hifadhi nayo wamekuwa wakivunja nyumba wanakwenda kuchukua yale mazao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata wananchi wengi wamepata vilema, wengine wameuawa kwa nyakati tofauti, lakini tunashukuru Serikali imeanza kuchukua hatua. Vijana wetu 10 wameshafundishwa VGS katika ule mpango wa kila vijiji vitano kuweza kupelekwa kwenye mafunzo katika Chuo cha Likuyu kule Namtumbo na tumeshaletewa mabomu 125, lakini pia, tunatarajia kuletewa ndege nyuki mwaka ujao wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme hivi vyote ambavyo tumeletewa, sambamba na mafunzo ya uhifadhi, bado havijaleta tija ya kutosha kwa sababu, vimekuwa vichache. Kuna Kijiji kama Mkarango, Kijiji kama Kandawale, Kipindimbi na kule Mtepera yaani sasa hivi tembo wameshaingia tayari. Kwa hiyo, udhibiti wao umekuwa mdogo kwa sababu, hata VGS wamekuwa wachache, lakini pia, hayo mabomu bado hatujayaona, japokuwa yalizunduliwa tangu mwaka 2024. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali iongoze VGS kuwapeleka kwenye training kule Namtumbo, lakini pia, iweze kuleta ndege nyuki wanaoweza kukabiliana na hao wanyama aina ya ndovu hata usiku kwa sababu, nina mashaka kwamba, huenda hata… 
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kidogo la kumalizia. 
MWENYEKITI: Sawa, malizia.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningependa pia, kule Malinyi katika Kata za Itete kuna Pori la Akiba la Hifadhi ya Kilombero imezunduliwa, lakini kuna maeneo ya wananchi yamechukuliwa na mpaka wakati huu bado hawajalipwa fidia, lakini hawaruhusiwi kuingia kuhudumia mazao ya kudumu yaliyopo mle; kuna mazao kama miti ya mitiki na kakao.  Kwa hiyo, ningeomba Serikali iweze, aidha kuwaruhusu wananchi waingie kwenda kumalizia kulima yale mazao yao ili yakikomaa waweze kuvuna au waweze kulipa fidia kwa wale wananchi kwa sababu, hifadhi imefuata wananchi. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)