Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mwanga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kupata nafasi ya kuchangia Wizara hii muhimu. Awali ya yote, kwa ridhaa na hisani yako, ninaomba uniruhusu kwa niaba ya Wana-Mwanga wote, kwa vile leo ninasimama mbele ya Bunge lako hili mara ya kwanza toka tumalize shughuli nzito ya kumsindikiza na kumuhifadhi Muasisi wa Wilaya yetu, Mzee Cleopa David Msuya, ninaomba uniruhusu nitumie fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa jinsi ambavyo alitusindikiza kuanzia Dar es Salaam, kwenye kumuaga mzee wetu mpaka Mwanga na Kijijini kabisa, nyumbani kule Usangi, kwenye kumhifadhi mzee wetu. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, lakini pia, tunamshukuru Mheshimiwa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, tunamshukuru sana Mheshimiwa Spika Dkt. Tulia Ackson, tunamshukuru sana Jaji Mkuu, Mheshimiwa Profesa Ibrahim Hamis Juma, pamoja na Mawaziri, Wabunge na wote ambao kwa kweli, walitukimbilia na kutupa faraja kubwa katika kipindi kile. Tunawashukuru sana, Mwenyezi Mungu awabariki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwahakikishie tu, Watanzania Wana-Mwanga pamoja na Chama Cha Mapinduzi kwamba, ni kweli tumepata pigo, lakini mzee wetu alituwekea misingi mizuri na hakuwa mchoyo katika kutufundisha jinsi ya kuendeleza mambo. Kwa hiyo, mimi bado ninaona mwanga mkubwa mbele ya Mwanga, sioni giza lolote, ninaamini mambo yatakuwa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maslahi ya muda niende haraka. Nieleze tu kwamba, kwa kweli, Jimbo langu la Mwanga ni moja kati ya wanufaika wakubwa wa miradi mbalimbali ya Wizara hii, pamoja na taasisi zake. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu na timu yako tunawashukuru sana kwa jinsi ambavyo mmeihudumia Wilaya yetu, wametupatia lango la Kaskazini la Hifadhi ya Mkomazi kwa heshima kubwa kabisa, alikuja kufungua Mheshimiwa Waziri Mkuu na sasa limeshaanza kufanya kazi. Ninaendelea kutoa wito kwa Wana-Mwanga kulitumia, kama fursa ya Uchumi, lakini pia, kuwaomba wadau wa utalii walitangaze sasa, ili liweze kupata wateja wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru pia, Wizara ya Maliasili, kupitia TANAPA kwamba, walitupatia bweni katika Shule ya Sekondari ya Kigonigoni na kuna mradi unaoendelea wa bweni katika Shule ya Sekondari ya Kwangu na kuna mradi wa madarasa mawili katika Shule Sikizi ya Mgigili, tunawashukuru sana. Maeneo yote haya, ambayo wametupatia miradi hii ni yale maeneo ambayo yana changamoto ya wanyama wakali. Kwa hiyo, tunasisitiza wanafunzi kupata mabweni na kuwa na shule shikizi, kwa ajili ya watoto wadogo wasiende mbali sana wakaathiriwa na hawa wanyama wakali. Kwa hiyo, tunawashukuru kwa kazi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wanamwanga ni wahifadhi wazuri sana, pamoja na changamoto zote za wanyama wakali, lakini wamekuwa wavumilivu, wametoa ushirikiano kwa Serikali kwa kutokuleta madhara wala hasara kubwa kwa wanyama hawa, wamekuwa wakiishi nao na kufuata masharti. Kwa hiyo, basi Mheshimiwa Waziri na timu yake, pamoja na yote mema sana ambayo wametutendea, bado niwasilishe kwako maombi matatu tu; la kwanza ni, Serikali imetujengea shule nzuri sana inaitwa Toloha Secondary School, ni Kata ambayo ilikuwa haijapata shule, lile eneo ni la wafugaji, tunaomba Mheshimiwa Waziri, kupitia taasisi yako nzuri sana ya TANAPA au nyingine yoyote, watusaidie tupate bweni kwenye ile Shule ya Toloha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shule ya Kivisini, Serikali imetujengea shule nzuri sana na mabweni ya kidato cha kwanza mpaka cha nne. Tunaomba TANAPA kwa vile eneo lile ni lenye changamoto ya wanyama, basi watuongezee bweni, kwa ajili ya kidato cha tano na cha sita, tunawaomba sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ule mradi wa ile Shule ya Msingi Mgigili, ambayo wametujengea madarasa mawili pamoja na vyoo, ikiwapendeza, basi watuongezee madarasa matano pale, ili tuweze kukamilisha darasa la kwanza mpaka la saba. Wale watoto wasome kwenye yale madarasa yenu bora kwa sababu, ukweli kabisa ni kwamba, madarasa waliyotujengea mabweni ni ya viwango vya hali ya juu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Mwanga imetunza mazingira vizuri na kwa namna moja au nyingine hiyo imesababisha matatizo ya wanyama. Eneo la tambarare, Tarafa ya Jipendea, yote ina tatizo la wanyama wakali ambao wanadhuru maisha na kuzuia uzalishaji, lakini maeneo ya milimani kuna wanyama wadogo sana, lakini nao wanaleta hasara kubwa, tumbili. Tunaomba mwongozo Mheshimiwa Waziri kwamba, ni namna gani watu wawa-treat wale wanyama kwa sababu, kwa kweli, sasa hivi hata kupika chakula inabidi ukae hapo na fimbo ushikilie kwa sababu, watakuja waipue sufuria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Mwongozo wa Serikali wa kitaalam jinsi ya ku-deal na hao Wanyama, ili watu waweze kuishi. Tunapata hofu sasa kwamba, inawezekana hata haya magonjwa ambayo, pengine yanabebwa na wanyama, kama haya, yasije kwetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni juu ya suala zima la kifuta jasho na kifuta machozi. Katika harakati hizi za wanyama wakali katika Tarafa hii ninayosema ya Jipendea, wapo watu wengi ambao wengine ndugu zao wamepoteza maisha na wengine wameharibiwa mazao yao na walishahakikiwa tayari, malipo yamefanyika mpaka mwaka 2023, baada ya hapo bado hawajalipwa. Tunaomba kipaumbele katika eneo hili, ili katika miaka iliyofuata, baada ya 2023 basi, yale madai yaweze kulipwa, wale watu waweze kuendelea vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, kwa kipindi hiki cha mvua changamoto ya tembo kule kwetu imepungua, hii inatudhihirishia kwamba, tatizo kubwa ni maji.  Ninadhani sasa ni wakati umefika, Serikali ichukue hatua ya kuhakikisha kule kwenye hifadhi tunapata mabwawa ya kutosha, hawa tembo wakae kwao na sisi tukae kwetu tuendelee na maisha yetu. Ninaunga mkono hoja, siyo tu kwa sababu nimependa, lakini kwa vile Wizara imefanya kazi nzuri. Pongezi sana Mheshimiwa Waziri na Naibu, wamemwakilisha sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Sekta hii ya Utalii. Ahsanteni sana. (Makofi)