Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Taska Restituta Mbogo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ya Bajeti ya Maliasili na Utalii ya mwaka 2025. Kwanza ninapenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Dkt. Pindi Chana na Naibu wake Mheshimiwa Kitandula. Pia ninapenda nimpongeze Mheshimiwa Katibu Mkuu Mheshimiwa Abbas, Watendaji wote wa TANAPA, Ngorongoro, TFS na TAWA pamoja na wafanyakazi wa Wizara ya Maliasili na Utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda pia nichukue nafasi kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuboresha utalii Nchini Tanzania. Sisi wenyewe ni mashahidi, bila filamu ya Royal Tour nchi yetu ilikuwa bado haijafahamika huko ughaibuni. Kwa hiyo Mheshimiwa Rais alilichukua jambo hili kwa uwezo wake na kutoa ile filamu ya Royal Tour ambayo sasa hivi inatuuza huko nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo ambalo ninaliona hapa ni suala la upungufu wa hoteli. Watalii wengi wamekuwa wanakuja nchini kwetu Tanzania, lakini hatuna vitanda vya kutosha kwa sababu hoteli nyingi zilibinafsishwa. Kama mtakumbuka Serikali ilibinafsisha hoteli kwa mikataba mbalimbali lakini wapo wawekezaji ambao hawakutimiza masharti ya ubinafsishaji. Hoja hii imekuwa ni hoja ya Kamati tangu mwaka 2021, lakini Serikali haijaweza kuifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Azimio la Bunge ambalo lilipitishwa humu ndani ya Bunge, kwamba zile hoteli ambazo hazijatimiza masharti ya ubinafsishaji ziweze kurudishwa. Mfano mzuri ni hoteli ya Embassy Dar es Salaam, ina takribani miaka 17 haijaweza kufanya kazi. Zipo hoteli nyingine za Kunduchi Beach, Mikumi na kadhalika. Hoteli Hizi zilibinafsisha lakini hazifanyi kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ije kwenye hoja ya kuzichukua hoteli hizi. Hatuwezi kuwa tunalalamika hatuna vitanda vya watalii kuja kulala wakati tulibinafsisha hoteli zetu na sasa tunashindwa kuzirudisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hoja hiyo ningependa niende moja kwa moja kwenye suala la Maafisa Maliasili walioko kwenye halmashauri zetu nchini Tanzania. Ningemwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha atuambie hawa Maafisa Maliasili, Maafisa Wanyamapori waliopo kwenye halmashauri vitendea kazi vyao vinatakiwa kununuliwa na nani? Kwa sababu wengi waliopo kwenye halmashauri hawana magari, wengine hawana risasi na wengine hawana bunduki. Utakuta ofisi imewekwa Afisa Wanyamapori hana gari la kwenda kuangalia wale wanyama msituni, hana bunduki, hana risasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba, waje na ufafanuzi na watueleze; je, huyu Afisa Wanyamapori aliye halmashauri anatakiwa kuhudumiwa na nani? Anahudumiwa na halmashauri au anahudumiwa na Wizara? Ili tufahamu, kwa sababu jambo hili limekuwa likileta shida. Unakuta wanyama wakali wamevamia mahali halmashauri ina Afisa Wanyamapori lakini anashindwa kwenda kule kwa sababu hana gari, anashindwa kwenda kumpiga yule tembo au mnyama yeyote mkali kwa sababu hana risasi. Sasa tuombe ufafanuzi, risasi za hawa Maafisa Wanyamapori walioko kwenye halmashauri, ni nani anayepaswa kuzinunua? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, nimeona wanapokuja wanyama wakali na waharibifu kwenye vijiji vyetu tunatumia VGS. VGS ni temporary measure, hata hizi ndege nyuki ambazo zimevumbuliwa sasa is temporary measure, is not a permanent measure. Permanent measure ilikuwa ni kuchimba mabwawa kwenye hifadhi zetu. Hata hivyo, mpaka sasa TAWA wamechimba mabwawa nane tu kwenye hifadhi zetu, hifadhi nyingine hazina maji. Tembo wanatoka kwenye hifadhi wanakwenda kutafuta maji, wanakwenda kutafuta chakula kwa sababu kwenye zile hifadhi hakuna maji…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ninaomba umalizie, muda wako umekwisha.

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru na ninaunga mkono hoja zote za Kamati na ninaunga mkono hoja ya Maliasili na Utalii. (Makofi)