Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon Abubakar Damian Asenga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilombero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa nafasi hii. Pia ninataka kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyoifanya mpaka tumepata matunda haya makubwa ya utalii; na muda mchache uliopita Mheshimiwa Rais ametoka kulihutubia Taifa na kusema kwamba tulinde amani yetu ili wageni katika dunia nzima waendelee kuikimbilia Tanzania. Mheshimiwa Rais ametoka kusema kwamba hatoruhusu watu hata wa nchi jirani ambao wamevuruga kwao waje wavuruge kwetu; na Mheshimiwa Rais amesema kwamba hapa Afrika Mashariki na Afrika ambao hatujavurugwa ni sisi peke yetu. Kwa hiyo ikikupendeza hii hoja ya Mheshimiwa Rais ambayo ameihutubia leo ni muhimu sana ikaja kwenye Bunge lako tukaiunga mkono ili iendelee kukuza utalii na kulinda maliasili za nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hongera sana kwa Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri na Watumishi wote wa Wizara pamoja na askari wetu, Wakuu wa Mikoa wetu na Waheshimiwa ma-DC; wanafanya kazi kubwa ya kulinda rasilimali zetu. Ninataka kusema Wizara hii ni kama wizara moja ya mfano kwa sababu imekusanya zaidi halafu inaomba fedha kidogo. Wamekusanya trilioni moja na bilioni moja nukta moja nane, lakini wanaomba bilioni 359. Ninaunga mkono hoja na ni imani yangu kwamba Wabunge wote wataunga mkono hoja; na tunapenda Wizara zote zingekuwa hivi, yaani anakusanya trilioni moja halafu yeye anaomba bilioni 359. Kwa kweli ni mfano mzuri sana ambao tunapaswa kuiga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Kilombero tuna Hifadhi ya Nyerere na Udzugwa; ninataka kuwa mmoja ya wahifadhi wazuri katika nchi yetu kwa sababu katika jimbo langu kuna mambo haya. Hata hivyo, ili tuendelee kuona kuwa tunanufaika na maliasili hizi watukumbuke sana sisi watu ambao tuna hifadhi. Kule kwenye Kata zangu za Mang’ula, Mwaya na Kisawasawa bado tembo ni tatizo kubwa sana tunaomba sana watusaidie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili tunaomba wawaangalie wavuvi wetu. Wanaingia wakiingia kuvua mtoni wanatozwa. Ninashukuru TAWA wamepunguza tozo; lakini baiskeli inatozwa, tenga linatozwa na mvuvi anatozwa. Tulikuwa tunaomba; kwa sababu hawawezi kwenda kukata miti tena, hawawezi kwenda kulima basi wapate nafuu kwenye kwenda kuvua kwa gharama ya chini zaidi ili iweze kupata matunda makubwa (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho na la msingi ambalo ninataka kusemea ni kuhusu mgogoro wa Kitula. Ninataka nimpongeze Mheshimiwa Waziri hapa alitutumia timu, kuna wananchi walikuja hapa wakaa muda mrefu; na juzi ile timu ambayo imekuja walipata ajali, ninataka nitoe pole kwa Mkurugenzi wa Kitengo cha Utatuzi wa Migogoro katika Wizara yake. Alipata ajali Mr. Kauzeni na sasa anaendelea vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepanda mpaka kwenye eneo la mgogoro kule Itula, mimi mwenyewe nimejionea; sijafika kabisa Itula lakini nimejionea na ninataka niseme kwa kifupi hapa kwa sababu kulikuwa na vyombo vya habari vya wananchi hapa. Sisi sote tunaunga mkono uhifadhi na ukienda kule unaona kabisa ni mazingira ambayo yanakusanya maji, lakini wananchi wana hoja zao. Ninaomba Mr. Kauzeni atakapopata nafuu na timu twende pale tukawaambie wananchi ukweli, tuwasikilize kutokana na ramani yao ya kijiji, tuwasikilize kutokana na hoja zao za kijiji ambazo zimewauzia maeneo, tukae kwa pamoja tuwaambie ukweli wale wananchi; kwamba kama hapa ni hifadhi na kama kweli kuna mazao kama wanavyosema kwa sababu hatujafika. Basi, Mheshimiwa Waziri amesema kwenye hotuba yake kuwa analipa fidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bonde la Kilombero wale watu ambao wanawatoa wana makaburi yao yapo kule na wanasema kwamba kokoa yao ipo kule. Kama ni lazima watoke basi walipwe fidia ili kuondoa nongwa wakati huu. Jambo hili ninalisema kwa ufupi sana, nimeona wananchi wameongea katika lugha kali, wanawasema askari wetu ambao wanafanya kazi ya kulinda kule kwa hali ya ukali, hawaamini tena Polisi wa TANAPA, wanazungumza mpaka wanawalazimisha kuimba nyimbo ambazo sio nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa unyenyekevu mkubwa, ninamwomba Mheshimiwa Waziri baada ya kupitishiwa bajeti yake hapa anipatie watu twende tufike hadi Itula. Wale wameomba mwezi mmoja waisome ramani, waitafsiri ramani, waweze kuweka mipaka. Tukawaambie ukweli wananchi wetu kama ni eneo la hifadhi basi kinachotakiwa kufanyika ni kwamba tuanze kuomba sasa kama linafaa kwa kilimo. Kama Serikali itatunyima basi wapewe fidia wale ili watoke, kuliko wanavyosema, kwamba mazao yao yamekatwa, wanasema kwamba kuna mazao yamepigwa dawa, wanasema wamepigwa mpaka alama huko mgongoni. Ninazungumza katika lugha ya kujenga kwa sababu tunataka Bonde la Kilombero lijaze maji Bwawa la Mwalimu Nyerere na pia tunataka tuendelee kulinda hifadhi yetu. Kama kweli tunataka kutoka kwenye hifadhi basi wananchi wetu walipwe fidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa muda huu mfupi wa dakika tano ulionipa na ninaunga mkono hoja. (Makofi)