Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bunda
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara maalumu katika nchi yetu. Ninamshukuru Waziri Mheshimiwa Pindi Chana, anafanya kazi nzuri sana tangu amepewa Wizara hii. Naibu wake Mheshimiwa Kitandula anafanya kazi nzuri, Abbas ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara anafanya kazi nzuri sana, Naibu Katibu Mkuu wake, Makamshina wote watatu wakubwa wale, Kamishna wa TAWA, Kamshina wa TANAPA na Kamishna wa TFS wanafanya kazi nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais; tumezungumza hapa sana mambo ya Royal Tour kwamba amefanya kazi vizuri na tumepata wawekezaji wengi kwenye maeneo yetu.  Ninajua, wakati fulani mtu anaweza kusema tuwekee Wizara iwe na fedha nyingi kwa ajili ya kujenga hoteli; hapana, wakati fulani ni kutengeneza mazingira mazuri ya nchi yetu ili watalii waje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa kwanza wa nchi ya utalii duniani ni kuweka amani, mkakati wa kwanza. Kwa hiyo pamoja na kwamba kuna Royal Tour ya Rais Samia, lakini kwa diplomasia yake ya nchi zote duniani ameleta watalii wengi kwenye nchi yetu. Ninampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa diplomasia hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana niliona, maana mimi sielewi, ni kweli au sio kweli. Hivi Profesa Janabi amekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani, ni kweli au sio kweli? Kama ni kweli kwani, Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani huwa tuna zamu? Kwamba zamu hii Kanda ya Afrika, kwamba zamu hii tuliweka Mkurugenzi ambaye anatoka Tanzania, Mungu akamchukua akaenda, kwa sababu ni zamu yao Watanzania tuwape tena? Hapana, maana yake ni kwamba diplomasia na Mama Samia imefanya uteuzi wake na Profesa Janabi ametokea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tukubali kwamba huyu mama katika makocha ni kocha bora duniani. Maana ukiteua mtu akaenda akafanya vizuri kwenye mechi maana yake unasifiwa kwamba ulifikiri vizuri zaidi. Kwa hiyo tunampongeza Profesa Janabi kwa cheo alichokipata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado ninamshukuru Waziri Pindi Chana kwa sababu mgogoro wa wafugaji na mapori ya akiba umepungua sana.  Nilikuwa ninajiuliza maswali mengi sana, hivi inatokeaje mimi kwa bahati mbaya nipo mpakani mwa hifadhi, ng’ombe wangu ameingia hifadhini, unawafilisi wote ng’ombe 500, 400, halafu mimi nimekaa nimerudi nyumbani, nikifika nyumbani ninaanza kukodisha ng’ombe wa kulimia, ninapata shamba ninalima, nikishalima heka kumi au tano, tembo anakuja anamaliza zote, hivi inakuwaje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachunga ng’ombe wangu, wewe unachunga tembo porini lakini wewe unaachia anamaliza mazao, mimi nikija unanifilisi, hivi inakuwaje? Sasa kwa diplomasia ya Mama Samia amefanya kumteua Mheshimiwa Pindi Chana, hii diplomasia sasa imeenea kwa wananchi, migogoro imepungua, tunawapongeza sana Serikali na iendelee kufanya hivyo. Ikiwezekana huko mbele tunakokwenda kuwe na sheria kwamba, kama ni ng’ombe mmoja anatozwa elfu 50 atozwe, kama ni elfu 30 atozwe, ili ng’ombe wakiingia porini tumalizane huko huko na sisi turudi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi inakuwaje unakuwa na ng’ombe, una kesi wanakaa pale ng’ombe 500, unakaa na kesi kwa miaka miwili, unakuta ng’ombe 20 wamebaki. Hivi tunamfilisi nani? Si Mtanzania huyu huyu? Tutengeneze mazingira, wewe uliyepeleka ng’ombe porini, tumalizane hapo hapo, lakini sio kumfilisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niipongeze diplomasia ya sasa hivi, naona wanafanya kazi nzuri na Makamshna wote, sasa hivi wana diplomasia, mambo yanakwenda vizuri, wanaweka huruma na mambo mengine yanaenda vizuri, niwashukuru sana kwa hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la fence. Suala la fence kama Grumeti Fund wamekubali kuweka fence, kama kuna maeneo yanachengachenga kutokuwekewa fence njooni Bunda. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kwenye vijiji vile vya Bunda ambavyo ni Vijiji vya Kunzugu, Nyamatoke, Mihale, Bukore, Hunyari, Mariwanda, Kihumbu, Sarakwa, Mugeta, Kyandege na Tingirime. Waje kwenye maeneo haya waweke fence, sisi tumekubali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri aende akaongee na watu wanaoweka fence, sisi mpaka wetu na Bunda ni Mto Rubana. Sasa ili fence ipite inatakiwa iwe zig zag, siyo wapige fence ndani ya mto sisi tukose pa kwenda, hapana! Twende tuweke zig zag ili wanyama wafaidi na sisi tufaidi. Tunaomba tukaweke hiyo fence. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Barabara ya Mugeta – Kilawila, nimeona TANAPA mmefanya kazi nzuri sana kwa kuilima Barabara ya Mugumu ambayo inakuja Maeneo ya Natta huku. Mmefanya kazi nzuri na sisi sasa tunaomba Barabara ya kutoka Mugeta kwenda Mto Rubana, kwenda Kilawila. Haiwezekani watu wetu wanalima mchicha, wana maziwa na wanalima chakula hawaendi porini kuuza mpaka wazunguke Serengeti au waende Lamadi. Tunaomba hiyo Barabara ya Mugeta muweze kuilima iwe nzuri. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la kifuta machozi na kifuta jasho. Sasa pale Bunda kuna Vijiji vya Hunyari, Kihumbu, Mariwanda, Sarakwa, Mugeta, Kyandege, na kuna Tingirime. Karibu watu 540 wanadai kiinua mgongo na wengine wale waliouwawa na tembo wapo wanadai, wako 11. (Makofi)
 Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba, kuanzia kesho nitakwenda ofisini kwa Mheshimiwa Waziri unisaidie hata hao ambao wanalipwa kifuta machozi wakalipwe. Haiwezekani jamani wameua, siku moja amenisaidia kazi nzuri sana, ninakukumbuka kazi nzuri ya Mheshimiwa Waziri. Mama mmoja aliuawa na mtoto na nini, akaamuru wakamlipa hapo hapo. Tunampongeza sana na Mungu ambariki. Kwa hiyo, hawa wengine waliobaki, tuje tuwalipe wafanye kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, TANAPA imejenga Kituo cha Afya kinaitwa Hunyari kwa 60%, asilimia nyingine Serikali ilimalizia. Sasa walijenga jengo la upasuaji (theatre), sasa limebakia madirisha na finishing. Tunaomba sasa waje walimalizie lile jengo ili kile kituo sasa kiweze kufunguliwa kifanye kazi vizuri sana. Ninawashukuru sana kwa moyo huo wa kujenga hicho kituo cha afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la njaa la Jimbo la Bunda lisiwe kwa wakulima wa Jimbo la Bunda. Tatizo linaletwa na tembo, haiwezekani watu wakawa wanalima kila mwaka chakula kinaliwa chote. Sasa watu wa TANAPA na watu wa Wizara ya Maliasili watusaidie, tunapokuwa tunaomba chakula Serikalini waingilie kati tupewe. Kwa sababu wanyama weo au wanyama wetu ambao sisi hatuwezi kuwalinda ambao ni tembo wanakuja kumaliza mazao. Watusaidie wakati tunaomba chakula kuja kusaidia watu wa Jimbo la Bunda wanaoathirika na tembo ili wale wananchi sasa waweze kupata chakula.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Getere, muda wako umekwisha, malizia. 
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, sina mbambamba na hii Wizara, ninaipenda sana, wanafanya kazi nzuri. Ninawaunga mkono na ahsante sana. (Makofi)